Hoja za Wafanyakazi

Felixonfellix

JF-Expert Member
Feb 16, 2010
1,672
182
Wafanyakazi wamejenga hoja kadha wa kadha za kudai maslahi zaidi ambayo wanaamini kuwa zikiangaliwa kwa ukaribu, zina mantiki na kuwa serikali ina uwezo wa kuzishughulikia na kutimiza.
Kwa wafanyakazi wa Tanzania, hoja ni zaidi ya kima cha chini. Ni mfumo mzima wa ajira, mapato, mafao na hali nzima ya maisha ambayo imeathiriwa sana na uwepo wa mfumo wa kifisadi.
Kosa kubwa la wafanyakazi waliowakilishwa na TUCTA ni kuwa hadi sasa hawajawa tayari kuhusisha matatizo yao na utawala wa CCM! Wanafikiri matatizo na hali ngumu ya maisha imetokana na agizo la shetani au na njama kutoka kuzimu!
Ukweli ni kuwa hali ya maisha ya wafanyakazi inaendana na sera zilizoshindwa za utawala wa CCM. Kutokulielewa hili na kutarajia kuwa kuna mtu anaweza kuwashawishi CCM wabadili sera zao za Ubepari ili hatimaye ziwe nzuri kwa mfanyakazi, ni kuota njozi mchana na kuombea paka wasiwinde panya! Hilo halitatokea.
Hivyo, hoja za wafanyakazi kimsingi haziwezi kamwe kukubalika na CCM na serikali yake. Mafao yanayodaiwa na wafanyakazi yatagongana kabisa na waajiri (ambao Kikwete ni mwakilishi wao mkuu).
Njia pekee kwa wafanyakazi ni kuamua kuunga mkono chama kingine ambacho kitabeba matamanio yao na kitakuwa tayari kushughulikia matatizo yao na kufanyia kazi mapendekezo yao.
Ni kutokana na hilo Kikwete asingeweza kujibu hoja za wafanyakazi kwa namna yoyote ya kuridhisha. Yeye mwenyewe alikuwa katika msukumo mkubwa kwa makampuni mbalimbali ya kibepari nchini ambayo kimsingi kabisa ni lazima yamnyonye mfanyakazi ili yatengeneza faida ya hali ya juu kabisa. Hii ndiyo asili ya Ubepari mahali pote duniani.
Inashangaza akili zangu kuona eti waajiri wanazungumza kutoa baraka zao kwa mgomo au kutokutoa; inashangaza mwajiri mkuu (kama alivyojiita mwenyewe) alitarajiwa akubali wafanyakazi wagome dhidi yake! Hata mabepari waliokubuhu wa Marekani, Uingereza na Ujerumani hawana ujasiri huo kwao.
Udhaifu wa hoja za Rais Kikwete ni kutokana na kuzidiwa hoja na kutokuwa na nafasi au hata upenyo wa kuweza kuzijibu. Kikwete alibakiwa na njia moja tu inayoeleweka; nayo ni kutumia vitisho.
Lakini kabla ya kutoa vitisho vyake, alijaribu kutoa majibu ya hoja za wafanyakazi kwa kujaribu kugusa hisia zaidi kuliko mantiki. Akijaribu kuelezea kwa nini serikali haiwezi kulipa kima cha chini cha Sh. 315,000, alisema:
Kuwalipa mishahara wanayodai viongozi wa TUCTA inamaanisha kwamba serikali isitishe kutoa huduma yoyote ile kwa wananchi; madawa hospitalini yasiwepo, ruzuku za mbegu, mbolea na madawa ya kuulia wadudu visiwepo, ujenzi wa majosho, barabara, zahanati, mashule, maji na umeme usitishwe, shuguli za ulinzi na usalama wa raia pia zisimamishwe.
Jibu hilo kijuu juu linamfanya mtu aionee huruma serikali kuwa kweli ikianza kulipa kima cha chini cha kiasi hicho, basi, huduma “nyingine zote” zitasimamishwa. Lakini kwa mtu mwenye kufikiria japo kidogo tu ataona ukweli ni kuwa tayari inalipa fedha nyingi sana na haionekani kujali hizo huduma nyingine.

Majuzi tu tumepigia kelele ujenzi wa jumba la gavana wa BOT kwa Shilingi bilioni tatu, na gavana huyo huyo analipwa mshahara wa karibu dola 15,000. Shilingi bilioni 3 za nyumba ya mtu mmoja zingeweza kulipa kwa miezi 12, kiwango cha kima cha chini tu cha Sh. 315,000 watu karibu 700!
Kumbuka tumeangalia kigogo mmoja tu, hatujaenda kwa watu wa NSSF, NHC, na kwingine! Yaani; nyumba ya mtu mmoja inatosha kuwafanya Watanzania 700 wawe na kima cha chini kinachopendekezwa na TUCTA! Kama hilo halitoshi, mshahara wa Gavana huyo (kumbuka natumia mfano wa mtu mmoja tu, unaweza kujaribu kwa kuangalia vigogo wengine na kuona jinsi hoja za Rais hazina nguvu) ambao ni dola 15,000 ambao tuliambiwa kuwa “anastahili” na kuwa “mkataba” wake unasema anastahili ukilinganisha kima cha chini kilichoongezwa sasa ambacho nikikiweka kwenye dola ni sawa tu na dola kama 80 hivi, ni mara 187 ya mshahara wa Gavana!
Itamchukua mfanyakazi wa kima cha chini cha sasa miaka 15.6 kuweza kupita kiasi cha dola 15,000 anazolipwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa mwezi!! Na bado Kikwete anasema serikali haiwezi, haina fedha!
Nikitumia mfano huo wa Gavana mnaweza kusema ninamuonea wivu, na ninaleta ‘unafiki na uzandiki’. Hebu tuangalia wakubwa wengine. Naomba mniruhusu tu nitumie mifano ya wabunge na wakuu wa mikoa.
Mbunge wa Tanzania amepata nyongeza ya mshahara karibuni na sasa, kwa ajili ya hoja yetu, tuweke kiwango kimoja tu ambacho ni Shilingi 1,921,000. Tukichukulia wabunge 320 tu kwa mwezi tunatumia Sh. 614,720,000 kuwalipa (na hapa nimeondoa posho zote, naangalia mshahara tu!).
Mshahara wa mbunge ni mara 18 ya kima cha chini kipya! Tukiwalipa posho na marupurupu mengine, mbunge wa Tanzania ‘anatafuna’ fedha nyingi tu ya walipa kodi; lakini wananchi kudai nyongeza ya kima cha chini tunaambiwa haiwezekani.
Lakini Kikwete akaenda mbele zaidi na kuonyesha kuwa hakuzielewa hoja za wafanyakazi vizuri. Kuhusu mgomo Rais alisema:
Viongozi wamejitwalia mamlaka ya kisheria kutangaza mgomo bila kuzihusisha mamlaka za kazi jambo ambalo kwa kweli siyo zuri wala la kistaarabu. Kutokana na kushindwa kutekeleza masharti haya ya Sheria ya Ajira na mahusiano kazini, mgomo huu ni kuvunja sheria za nchi, ni haramu. Hatuwezi kukubali jeuri ya watu wanaovunja sheria za nchi.
Sasa kwa haraka haraka mtu anaweza kusema kuwa alisema jambo muhimu na la maana. Lakini kuna tatizo. Yeye mwenyewe ndiye alijitangaza kuwa ni mwajiri mkuu. Kwa maneno mengine, ndiye mlengwa wa mgomo huo. Hivi ni nchi gani ambapo mwajiri alisimama kuunga mkono mgomo wa wafanyakazi wake?
Itakuwa ni vichekesho kuona waajiri wakisimama na kusema “mgomo ni halali”; kwani watakuwa ni waajiri wa ajabu kabisa duniani. Kikwete, kama mwajiri na kama serikali, alikuwa na haki ya kuupinga mgomo, lakini uhalali wa mgomo hautokani na baraka za serikali au Ikulu!
Uhalali wa mgomo unatokana na kupitishwa na vikao halali vya vyama vya wafanyakazi na uzito wa madai yao. Mfanyakazi anayeonewa na kuona kuwa haki zake zinaminywa hawezi kusubiri serikali imuwekee mkono wa baraka ili adai haki hizo!
Ni kweli, hata hivyo, kuwa mgomo ni lazima uwe unatokea pale ambapo njia zote za kutatua matatizo zimeshindikana. Nakubaliana na Rais kwamba hadi wakati mgomo unaitishwa njia zote zilikuwa hazijaisha na milango ya majadiliano ilikuwa haijafungwa.
Hata hivyo, serikali isitarajie kuwa wafanyakazi wa Tanzania wataendelea kusubiri huruma ya serikali kusikiliza kilio chao. Siku yaja ambapo vitisho na kejeli havitazuia wananchi kudai kile wanachoamini kuwa ni haki yao.
Ni lazima niseme tena kuwa katika majibu yake Rais Kikwete hakuonyesha mpango wowote wa serikali yake kubana matumizi ili kuweza kumudu kuinua kima cha chini. Kuna maeneo mengi ambayo yangeweza kukatwa matumizi ili kuboresha mishahara ya wafanyakazi.
 
]............................uhalali wa mgomo hautokani na baraka za serikali au Ikulu!
Uhalali wa mgomo unatokana na kupitishwa na vikao halali vya vyama vya wafanyakazi na uzito wa madai yao. Mfanyakazi anayeonewa na kuona kuwa haki zake zinaminywa hawezi kusubiri serikali imuwekee mkono wa baraka ili adai haki hizo!
[/SIZE]Ni lazima niseme tena kuwa katika majibu yake Rais Kikwete hakuonyesha mpango wowote wa serikali yake kubana matumizi ili kuweza kumudu kuinua kima cha chini. Kuna maeneo mengi ambayo yangeweza kukatwa matumizi ili kuboresha mishahara ya wafanyakazi.

you are damn right! TUCTA watch that!
 
Back
Top Bottom