Hoja Sita za Kutaka Mabadiliko ya Mifumo ya Uchaguzi, Haki na Kulinda Rasilimali za Nchi

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
617
1,541
Uchambuzi wa ACT Wazalendo kuhusu mpango wa bajeti wa Wizara ya katiba na sheria kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Utangulizi.
Tarehe 29 April 2024 Wizara ya katiba na sheria iliwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Bunge liliijadili na kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 441.260 kwa ajili utekelezaji wa mpango huo.

ACT Wazalendo kupitia Wizara Kivuli ya Katiba na Sheria tumeupitia Mpango huo wa bajeti ambao umegusa taasisi zifuatazo zilizo chini yake; Tume ya Utumishi wa Mahakama (Fungu 12); Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Fungu 16); Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (Fungu 19); Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (Fungu 35); Mfuko wa Mahakama (Fungu 40); Wizara ya Katiba na Sheria_Wakala wa usajili ufilisi na udhamini; Taasisi ya Mafunzo ya uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Fungu 41). Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (Fungu 55); Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Fungu 59);

Aidha, katika uchambuzi wetu tumehusisha mapitio ya utekelezaji wa bajeti wa mwaka 2022/23 na kutuwezesha kutoa mapendekezo yetu kama chama juu ya vipaumbele au maeneo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kwa mwaka huu wa fedha.

Maeneo Sita (6) ya uchambuzi wa ACT Wazalendo kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/25.

1. Serikali ya imetupilia mbali madai ya Katiba Mpya.
Katika wasilisho la Bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2024/25 Waziri anasema Serikali imeweka mpango wa kutoa elimu ya katiba kwa wananchi ikiwa kama hatua ya kuelekea kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi. Hii ni mwendelezo wa kauli za Serikali kuanzia Agosti 28, 2023 aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) aliposema kuwa Serikali kabla ya kuanza mchakato huo itatoa elimu ya katiba kwa miaka mitatu.

Kurudiwa tena Bungeni kwa maelezo hayo ya Serikali tena katika hotuba ya bajeti ni wazi kuwa Serikali haina mpango wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya. Katika taifa letu kwa muda mrefu tangu siasa za mageuzi 1992 tayari kuna mwafaka wa wananchi kuhusu hitajio la kuwa na Katiba mpya. Kuanzia Tume ya Jaji Nyalali, Jaji Kisanga na hata Tume ya Jaji Warioba mchakato wa kifikra na mwelekeo ulifakiwa kujengwa nchini.

Serikali ya awamu ya Nne iliweka kipaumbele katika swala la katiba mpya, hata hivyo ni wazi kwamba mchakato ule uliharibiwa kwa makusudi na Wanaccm na kufanya mchakato kusimama kwa muda hadi sasa. Katika kipindi cha mwaka 2015-2020 Serikali ya awamu ya Tano haikuweka kipaumbele katika swala la katiba mpya kwakuwa halikuona umuhimu kwa maslahi ya kisiasa. Serikali ya awamu ya sita imekuwa ikisitasita katika kuweka kipaumbele kuhusu mchakato wa katiba mpya. Hiki kinachoendelea ni ujanja ujanja wa kukwepa kupatikana kwa Katiba mpya.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali iache mzaha na iachane na kutumia fedha za umma kwa ajili ya kuendelea kuiweka madarakani CCM. Tunataka fedha hizo zianze kutumika kukwamua mchakato wa Katiba mpya. Mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya uanze sasa.

Serikali ipeleke Bungeni Mswada wa marekebisho/mabadiliko ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Constitutional Review Act) na Sheria ya Kura ya Maoni (Referendum Act) katika bunge hili linaloendelea (Bunge lililoanza Aprili 2, 2024). Kisha tuendelee kwa hatua zingine za kupata mwafaka wa Kitaifa, kuundwa kwa Timu ya wataalamu na kura ya maoni.

2. Hasara za mikataba mibovu na uwezo mdogo katika usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji wa Kimataifa.
Wizara ya Katiba na Sheria ina wajibu wa kuishauri Serikali katika mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa. Katika uratibu huo tumeshuhudia Tanzania ikisaini mikataba ya uwekezaji ya aina mbalimbali hususani mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili (Bilateral Investment Treaties_BITs) ambayo shabaha yake ni kuhamasisha na kulinda uwekezaji unaofanywa na nchi mojawapo ndani ya nje nyingine (baina ya nchi hizo mbili).

Ingawa, tunatambua umuhimu na nafasi ya uwekezaji kwenye maendeleo ya uchumi wa taifa, hoja yetu kubwa kuhusu mikataba ya uwekezaji ya kimataifa ni kuongezeka kwa kasi kwa kesi, madai na fidia zinazopaswa kulipwa na Serikali ya Tanzania kwa Kampuni za Kimataifa. Ambapo mikataba ya namna hii imekuwa ikitumika kama nyenzo ya unyonyaji na uporaji wa utajiri wa maliasili na nguvu za Watanzania kinyume na madai yanayopigiwa chapuo.

Athari za mikataba mingi ya uwekezaji wa kimataifa ni nyingi sana lakini katika uchambuzi wetu tumetaja kipengele cha mikataba kinachoruhusu wawekezaji wa nje kuishataki Serikali katika mahakama za kimataifa. Hii ni kutokana na uzoefu ukionyesha kuwa mifumo mbalimbali ya kimataifa ya utatuzi wa migogoro ya biashara na uwekezaji ikiwa na changamoto zinazopelekea mzigo mkubwa wa gharama za kesi na fidia, kukosekana kwa uwazi katika Mwenendo wa mashauri. Aidha, athari kubwa zaidi ni kuminya uhuru wa nchi kujiamulia mambo yake kwenye matumizi ya rasilimali kwa kupunguzwa nguvu ya kudhibiti unyonyaji na uporaji wa rasilimali za nchi.

Katika uratibu unaofanywa na wizara ya mambo ya nje na baadaye wizara ya katiba na Sheria kuingia mikataba kwa miaka 17 (kuanzia 2005- 2022) Tanzania imesaini mikataba baina ya nchi mbili ipatayo 19. Ndani ya miaka hiyo, kuna kesi zaidi ya 10 zilizofunguliwa na wawekezaji dhidi ya Serikali ya Tanzania katika Kituo cha kimataifa cha usuluhishi kesi za uwekezaji (ICSID). Kesi hizi zinaigharimu sana nchi yetu kutokana na mapengo yaliyopo kwenye mikataba iliyoingia. Baadhi ya mashauri yaliyofunguliwa na Madai yao tumeyaonyesha kama ifuatavyo;

Kampuni ya Winshear Gold Corp (ICSID Na.Kesi.ARB/20/25); Inapeleka madai ya Sh. bilioni 223.8 kwa kutumia makataba kati ya Canada na TZ. Kesi bado inaendelea.

Kampuni ya Indiana Resources Ltd kupitia kampuni tanzu za Nachingwea U.K. Ltd, Ntaka Nickel Holding Ltd & Nachingwea na Nickel Ltd (ICSID Case No. ARB/20/38) nayo inataka kiasi cha Sh. bilioni 218.3 MIUMBI. Kesi bado inaendelea inaendelea.

Madai ya Shilingi trilioni 3.7 ($1.57bln) Kampuni ya Symbion Power Tanzania Ltd & wengine (ICSID kesi Na. ARB/19/17)

Standard Chatered Bank (Hong Kong) Ltd (ICSID Case No.ARB/15/41); Mkataba wa Uwekezaji kati ya IPTL na Tanzania. Tanzania iliamuriwa kuilipa SCB-HK dola za Marekani milioni 185.45 (sawa na Sh. bilioni 438.5) pamoja na riba ya 2% kila baada ya miezi 6 kuanzia Septemba 1, 2018

Kesi ya Standard Chartered Bank (Hong Kong) Ltd22 (ICSID Case No. ARB/10/20) Mkataba wa uwekezaji kati ya TANESCO na IPTL. TANESCO iliamuriwa kuilipa SCB–HK dola Marekani milioni 148.4 (sawa na bilioni 346) na riba ya 2% kila baada ya miezi 3 kuanzia Septemba 30, 2015.

Hizi ni baadhi ya kesi na madai yake pamoja na fidia kwa kesi zilizoamriwa. Orodha ni ndefu hivi karibu Novemba, 2022 ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) ilishikiliwa nchini Uholanzi kutokana na mwekezaji kutoka Swedeni kushinda kesi dola 165 milioni (Sh.380 bilioni) dhidi ya Tanzania na kuishawishi Mahakama ya uholanzi kushikilia ndege hiyo kama kigezo cha kushinikiza malipo yake.

Katika bajeti ya Wizara Katiba na Sheria kwenye masuala ya uwekezaji, mikataba na makubaliano mbalimbali hakuna taarifa iliyoelezwa kuhusu kesi na tahadhari ya Serikali kwenye mikataba mbalimbali ya kimaifa kwa faida ya nchi yetu.

Hofu na wasiwasi wetu ni kuwa mikataba hiyo ni hatari na kuhusu mashauri yaliyopo kwenye vituo vya kimataifa ambayo yanaikamua nchi kulipa kampuni hizo trilioni za shilingi sio tu kinatishia kupunguza uwezo wa Serikali kuwekeza kwenye huduma muhimu na ujenzi wa miundombinu bali hata juu ya uwezo wao wa kutunga sheria na sera, na kudhibiti uwekezaji kwa maslahi ya umma.

Hivyo, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali sio tu kupiga mapambio ya kuvutia uwekezaji iweke wazi mikataba yote ya uwekezaji inayoingia baina ya Tanzania na nchi nyingine.

Pili, tunatoa wito kwa Serikali kutathimini mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili kama ipo haja ya kuendelea nayo au kusitisha kabisa mikataba yenye vipengele vinavyopalilia uporaji wa rasilimali na unyonyaji wa nguvu kazi.

Tatu, ni wakati wa kuamua nafasi yetu ya kuendelea au kusitisha kwa kujiondoa kwenye vyombo vya kimataifa vya utatuzi wa migogoro ya kimataifa.

Mwisho, Wizara ya katiba na sheria kwa kushirikiana na wizara ya Mambo ya Nje inapaswa kuongeza umakini katika kubaini mapengo ya kisheria yanayotokana na uwekezaji yatakayoitia hasara zaidi nchi yetu.

3. Kutofuatwa kwa sheria za manunuzi na mikataba.
Serikali imekuwa ikipata hasara kila mwaka kutokana kutofuatwa kwa Sheria na taratibu katika Wizara, Idara, Wakala na taasisi za Serikali, Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) ameonesha kuna masuala ya Mikataba iliyosainiwa bila kupekuliwa na Wanasheria zaidi ya Bilioni 4.7, Ununuzi Uliofanyika bila Kutumia Mikataba wa Bilioni 2.16 pia CAG ameonesha kuwa Serikali bado ina orodha ya Mikataba ya Mikopo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.6 bila kupokea fedha za mikataba hiyo, hoja za ubadhilifu na upotevu tulizoziibua kwenye uchambuzi wetu ni zaidi ya shilingi Trilioni 3.14 lakini Waziri hajasema lolote katika hotuba yake kuhusu jambo hili.

Wizara ya Katiba na sheria ambayo ndani yake kuna Ofisi ya Mwanansheria mkuu na wakili mkuu wa serikali, haijaonesha mpango wa kukabiliana na ongezeko la upotevu na hasara ambayo serikali kupitia Wizara, Idara, Wakala na Mmalaka za Serikali inapata kwa kutofuata Sheria na mikataba mbalimbali, hili na jambo la kutowajibika kwa Wizara.

Fungu namba 35 Ofisi ya taifa ya Mashtaka halioneshi mpango wa kukabiliana na ubadhilifu hata baada ya CAG kuonesha makosa na ubadhilifu wa wazi haichukui hatua zozote za kisheria kwa taasisi mbalimbali ambazo zimtajwa kusababishia Serikali hasara kubwa kwa makosa mbalimbali.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kufanya kazi zake kwa weledi na uzalendo kwa kuchukua hatua za kisheria kwa watendaji wa taasisi zote zinazosababishia serikali hasara ya mabilioni.
Pili, Ofisi ya Mwanasheria mkuu na Ofisi ya Wakili mkuu ziweke nguvu katika kesi mbalimbali na mikataba ya kimataifa ili kuhakikisha serikali inashinda mashtaka mbalimbali.

4. Tume huru ya Uchaguzi bado giza.
Jitihada kubwa zilizofanywa na wadau wa Demokrasia kuhusu upatikanaji na kuundwa kwa Tume huru ya Uchaguzi itakayoratibu, kuendesha na kusimamia chaguzi zote nchini zinaenda kufifishwa. Katika jitihada hizo ni kuhakikisha kupatikana kwa Sheria mpya ya Tume huru ya uchaguzi ya mwaka 2024. Ingawa sheria hiyo kuwa na mapungufu kwa kutozingatia maoni yote ya wadau ili kuwa na msingi madhubuti wa chaguzi zetu.

Lakini tumeona Sheria mpya ya Tume huru ya Uchaguzi ya mwaka 2024 imeweka msingi wa kupatikana kwa Tume huru ya Uchaguzi kwa kutaka wajumbe wa tume wapatikane kwa mchakato wa ushindani badala ya kuteuliwa moja kwa moja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, sheria ya Tume huru ya Uchaguzi katika kifungu cha 10 (1) (c) kinaeleza majukumu ya Tume huru ya Uchaguzi ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Hata hivyo, inashangaza kuona Serikali ya CCM haijachukua hatua zozote za kutekeleza sheria hiyo ili kuhakikisha Tume huru ya Uchaguzi inaundwa kwa mujibu wa sheria waliyoipitisha wao wenyewe. Tayari tumeona Bunge limeshapitisha bajeti ya OR-TAMISEMI ili kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa na mchakato wa kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.

Katika hali ya mshangao, tumeona Tume ya taifa ya Uchaguzi kujibadili jina lake na kujiita ‘Tume huru ya Uchaguzi’. Kwa hiyo, hakuna muundo mpya (wajumbe wale wale wanaendelea), Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaendelea kusimamiwa na TAMISEMI. Hatua hizi zote zinaonyesha kuwa Serikali kutoheshimu maoni ya wadau na kukosekana kwa nia ya dhati ya kufanya mageuzi ya kisiasa nchini. Hii ni dalili mbaya kuelekea Oktoba 2024 kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Mitongoji na Uchaguzi Mkuu 2025.

Kubadili jina la tume bila kuiunda upya katika utaratibu utakaojenga Imani kwa wadau ni dhihaka kubwa kwa demokrasia ya nchi yetu. Na kuonesha kuwa kauli za maridhiano, ustahimilivu, kuponya majeraha na mwanzo mpya (4R) ni hadaa tupu.

Ushahidi wa unaonesha bado kuwepo kwa dosari, hujuma na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu vinavyojitokeza katika usimamizi na uendeshaji wa uchaguzi hata baada ya uchaguzi Mkuu wa 2020. Hii ni kutokana na wajumbe wa tume kuwa wateule na watumishi wa tume pia ngazi zote kutokuwa huru.
ACT Wazalendo tunawataka wajumbe wa sasa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wajiuzulu ili kupisha mchakato wa uuundwaji wa Tume huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria.

Pia, tunamtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusitisha mchakato wa usaili kwa mujibu wa sheria mpya.

Pili, Serikali ipeleke Bungeni mabadiliko ya sheria ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili Kuwezesha uchaguzi huo kusimamiwa na Tume huru ya Uchaguzi itakayoundwa chini ya sheria mpya.

5. Mfumo mbovu wa haki, uchelewashaji wa upelelezi na kutokamilika kwa kesi kwa muda mrefu.
Mfumo wa haki jinai nchini umekuwa na changamoto nyingi ambazo zinasababisha uonevu, ukandamizaji, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu. Maeneo makubwa yanayozaa madhila haya ni; Utaratibu wa ukamataji wa watuhumiwa; upelelezi wa makosa ya jinai; uendeshwaji na usikilizwaji wa mashauri mahakamani na utoaji wa adhabu. Changamoto za mifumo ya haki imesababisha kuchelewa kumalizika kwa kesi, kuwa na mlundikano wa mashauri, vyombo vya dola kuwashikilia watuhumiwa kwa muda mrefu hadi miaka 10 hadi 20.

Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Ofisi ya Mwendesha mashtaka inasimamia na kuendesha kesi zote za jinai nchini. Kulegalega kwa uendaji wa Ofisi hiyo kunazuia kwa sehemu kubwa mfumo mzima wa utoaji wa haki nchini. Mfano katika hotuba ya bajeti 2024/25 inaonyesha kupungua kwa kasi ya usikilizaji wa kesi kwa asilimia 5 kwa mahakama kuu, kushuka kwa asilimia 17 kwa mahaka za rufaa.

Ubovu na dosari za mfumo wa haki jinai unathibitishwa na ripoti ya tume ya kupitia mfumo wa haki jinai chini ya Jaji Mstaafu Prof. Othaman Chande iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Ripoti ya Tume hiyo imeelezea changamoto na namna ya kuboresha mfumo wa upelelezi na uchunguzi, Masuala ya dhamana, utitiri wa vyombo vyenye taswira ya kijeshi, usikilizwaji wa mashauri, na Tume ya Utumishi na Utawala Bora, dhana ya kifungo cha maisha, adhabu ya kunyongwa, malipo ya mafao ya mkupuo kwa wastaafu, masauala mahususi ya Jeshi la Polisi, Jeshi la magereza na mambo mengine.

Katika, kushindilia hoja hii; mwaka jana tulionyesha ushahidi wa malalamiko ya viongozi wa dini ya Kiislamu wakatika wa kuadhimisha Sherehe za Eid-fitri mwaka 2023 walielezea namna gani masheikh zaidi ya 151 ambao wanasota katika magereza mbalimbali nchini (Ukonga na Segerea 79; Gereza la Kisongo Arusha 27; Maweni Tanga 13; Butimba 11 na Gereza Kuu la Morogoro) kwa takribani miaka 11 tangu 2013.

ACT Wazalendo tunaitaka wizara ifanye maboresho ya mfumo wa upelelezi wa mashauri kwa kusimamia ukomo wa muda wa upelelezi na kuweka ukomo kwa makosa ambayo hayajawekewa ukomo ili kupunguza mlundikano wa kesi zinazochagizwa na upelelezi kutokamilika.

Pili, tunapendekeza kuwepo kwa dhamana kwa makosa yote na kuboresha utaratibu wa udhibiti wa dhamana kwa baadhi ya makosa. Ruhusa hii itaimarisha mfumo wetu wa haki jinai kwa kuondosha hila za kubambikiza kesi zisizo na dhamana ili kuwatesa na kuwakomoa wananchi.

Mwisho, Serikali ifanye mapitio ya Sheria zote kandamizi ili kuondoa vifungu vinavyotumika kuwaonea, kuwabagua na kuwanyanyasa wananchi.

6. Kushughulikia urejeshwaji wa Watanzania wanaoshikiliwa na waliokutwa na makosa ya jinai Nchi za nje.
Miongoni mwa majukumu ya Wizara ni pamoja na kuratibu kurejesha kwa Watanzania au raia wa nchi zingine wanaotuhumiwa na uhalifu ili kuimarisha ushirikiano wa kisheria na mataifa. Katika kufanya hivyo Wizara inapitia mikataba ya urejeshwaji wa wahalifu watoro kutoka nchi mbalimbali na kujadili namna bora ya kuboresha mikataba husika.

Zipo taarifa za uhakika za ukamatwa kwa Watanzania 37 kati yao 24 walikuwa wavuvi kutoka Zanzibar na 13 kutoka Tanzania Bara ambao walienda kwa shughuli mbalimbali. Wavuvi hao walipatiwa vibali mapema mwezi Septemba 2017 kwa ajili ya kufanya shughuli za uvuvi kupitia Bahari ya Hindi. Mwezi mmoja baadae, yaani Oktoba 2017 kulitokea machufuko Nchini Msumbiji, ndipo wavuvi 24 na Watanzania wengine (13) waliokuwa kwenye shughuli mbalimbali walikamatwa na kuwekwa magerezani. Hadi sasa zipo taarifa kuwa Watanzania 17 wamefariki wakiwa magerezani nchini Msumbiji na wengine kuendelea kushikiliwa bila msaada wowote.
Ukimya wa Serikali unaibua simanzi, sintofamu na kushusha imani za ndugu, jamaa na marafiki juu ya hatima ya Ndugu zao waliopo vizuizini.

ACT wazalendo tunaitaka Serikali kupitia Wizara ya katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wizara ya Mahusiano ya Kimataifa na Mahusiano ya Afrika Mashariki Kufatilia mashtaka yote yanayowakabili Watanzania waliopo Nchini Msumbiji na Afrika ya Kusini na nchi nyengine kuhakikisha wanatendewa haki, na wanarudishwa nyumbani.

Hitimisho
Falsafa ya Serikali ya awamu ya sita ya 4R ya Maridhiano, Mageuzi, Ustahamilivu na kujenga upya ni falsafa ya maneno tu, ni falsafa isiyounganishwa na mifumo ya kisheria, falsafa hiyo haiwezi kuhojiwa popote, kama taifa hatuwezi kuongozwa kwa hisia na matamanio ya mtu mmoja. Taifa linahitaji Katiba Mpya ambayo itaondoa mtanziko wa kiutawala na kisiasa nchini, sambamba na hilo, wakati tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Serikali kuu 2025 Tume huru ya Uchaguzi isimamie chaguzi hizo, hicho ndio kipimo halisi cha Utawala wa Sheria.

Imetolewa na;
Ndg. Mbarala Maharagande,
Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria
ACT Wazalendo.
30 April 2024.
 
Ccm wanashinda kwa nguvu ya vyombo vya ulinzi na usalama (polisi, jeshi na usalama), hao ndio wanachakachua uchaguzi na kuiba kura. Siku vyombo vya ulinzi na usalama vikiamua kukataa kuiba kura kwenye uchaguzi, ccm watatoka mapema tu.Vyama vya upinzani wapeni elimu maaskari wa vyombo vya ulinzi na usalama waache kutumika kuiba kura.
 
Back
Top Bottom