SoC03 Hivi ni kweli mbuyu huu umeshindwa kung'olewa?

Stories of Change - 2023 Competition

Mrs Samambo

New Member
Jul 25, 2023
2
3
Miaka takribani kumi iliyopita nilipoteza ndugu ambaye alikuwa ni mhanga wa madawa ya kulevya na kilichotokea ni kuwa aliugua ghafla na alipofika hospitali walimpatia matibabu bila kujua kuwa alikuwa ametoka kutumia madawa ya kulevya Jambo lililopelekea kifo chake. Kama familiya tuliumia mno, na toka kipindi hicho kila ninapokutana na wahanga wa madawa nimekuwa nikiumia Sana na kumkumbuka ndugu yangu yule aliyepotea. Nimewahi pia kuwa na rafiki ambaye mdogo wake amekuwa teja na hana msaada wowote kwenye jamii zaidi ya kuishia kuishi maisha ya hovyo na kufanya vitendo vya wizi wa hapa na pale.

Kiukweli tatizo hili lisikie kwa mwenzako tu ila likikugusa ndo utatambua ni kiasi gani linaumiza. Siku zote nimekuwa nikitamani kuona serikali yetu ikifanya Jambo kubwa kupambana na wanaofanya Biashara hii haramu lakini suala la madawa limekuwa ni Kama mbuyu ambao umeshindwa kung'olewa miaka na miaka. Mara kadhaa tumewahi kushuhudia wanaojitokeza kuwa mstari wa mbele kupambana na madawa ya kulevya wakipotezwa au kunyamazishwa ghafla na harakati zao kuishia njiani. Kuna nini nyuma ya pazia kuhusiana na Biashara hii?

Ikumbukwe kuwa mnamo mwaka 2017 ilianziashwa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya ikichukua nafasi ya iliyokuwa Tume ya kuratibu udhibiti wa dawa za kulevya ambayo ilianza kazi miaka ya 1997. Uwepo wa Tume Pamoja na Mamlaka bado hazijaweza kudhibiti uingizaji wa madawa ya kulevya nchini Jambo linalosababisha ongezeko kubwa ya wahanga wa madawa ya kulevya.

Taarifa mbalimbali zimekuwa zikitolewa na Mamlaka kuonesha mafanikio yao juu ya mapambano dhidi ya madawa lakini itoshe kusema mapambano yao yamefanikiwa zaidi kwenye kukamata bangi na mirungi tofauti na haya madawa mengine kama “cocaine” na heroini ambayo ndiyo yana madhara makubwa zaidi. Sambamba na hilo hata wauzaji wanaokamatwa ni wale wauzaji wa mwisho kabisa Pamoja na watumiaji huku waingizaji wakubwa wa madawa wakiwa bado wanapeta mitaani wakiendelea na Biashara hiyo. Kuna nini nyuma ya pazia kuhusiana na Biashara hii?? Ni kwanini serikali inashindwa kuwakamata waingizaji wakubwa wa madawa ya kulevya nchini??

Ifahamike kuwa serikali Ina mkono mrefu sana lakini kwenye suala la madawa ya kulevya itoshe kusema kuwa mkono wa serikali umekuwa mfupi tena butu (hauna vidole) kiasi cha kushindwa kukamata waalifu wakubwa. Inasikitisha sana kuona Taarifa ya Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya ikitoa Taarifa ya kufanikiwa kukamata madawa ya kulevya lakini ukisoma Taarifa hizo kwa undani unagundua madawa yanayozungumziwa ni bangi na Mirungi. Inaumiza sana hasa kwa sisi ambao ndugu zetu ni wahanga wa tatizo hili.

Nini kifanyike??
Ni matamanio ya wananchi wengi kuona mbuyu huu ukiangushwa na serikali yetu ili kuweza kukinusuru kizazi chetu ambacho kinazidi kuangamia kila iitwapo leo. Mamlaka isimame imara kupambana na waingizaji wakubwa wa madawa. Mbuyu ung'olewe kuanzia kwenye mizizi ili tuweze kuuangusha kabisa siyo kuishia kukata matawi na kuuacha ukiendelea kuchipua majani mapya kila siku. Serikali ituoneshe mkono wake mrefu kwenye suala hili na isiwe propaganda tu. Tunatamani kuona kwa vitendo mapambano dhidi ya madawa ya kulevya na siyo maneno mengi alafu vitendo sifuri. Hao wachache wanaofaidika na Biashara hii watokomezwe ili kuweza kunusuru maisha ya wengi ambayo yanazidi kupotea kila leo.

Tumeshuhudia vijana wengi hasa wasanii ambao walikuwa vizuri kwenye tasnia zao wakiharibika kabisa na kuishia kuwa mateja wasiokuwa na msaada wowote kwenye jamii. Tuna Malamka, tuna vyombo vya usalama hivi ni kweli wameushindwa mbuyu huu?? Nina Imani kubwa kuwa Kama wauzaji wadogo wanafahamika ni rahisi mno kuwafahamu waingizaji wakubwa kwa kuwa vyombo vya usalama vipo na Wana mbinu chungu nzima za kukamata wahalifu. Taifa linaangamia tuachane na maneno maneno mengi tuoneshe vitendo.

Jeshi la polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya kupambana na kudhibiti madawa ya kulevya simameni kiume muweze kuung'oa mbuyu huu. Wananchi tunakosa Imani na serikali yetu kila tunapoona mapambano yanaishia njiani. Nirudie kusema Jambo hili likikukuta ndo utatambua ni kiasi gani linaumiza. Nimepoteza ndugu na Kuna wengine wameshaathirika na madawa ya kulevya, maumivu niliyonayo ni makubwa mno.

Baraza la Taifa la Udhibiti wa madawa ya kulevya chini ya Mwenyekiti wake ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, liangalie na kufanya tathmini ya kina juu ya utendaji wa Sera ya Taifa ya Udhibiti wa madawa ya kulevya ili kuweza kujiridhisha na utekelezaji wake

HITIMISHO
Vita dhidi ya madawa ya kulevya ni kubwa na inahitaji wapambanaji kujivika silaha madhubuti ili kuweza kuishinda. Wananchi tunatamani kuona mizizi ya mbuyu huu iking'olewa kabisa na kufanya mbuyu usiweze kuchipuka matawi mapya. Tumechoka na Taarifa za kukamata “nyokaa” wa Biashara hizi na kuacha CHATU wakiendelea kuneemeka huku Taifa likiangamia. Ifike mahali hawa Chatu wakamatwe ili nyoka wadogo wapotee.
 
Back
Top Bottom