BAKOI
JF-Expert Member
- Jan 31, 2016
- 1,211
- 2,330
HITLER ALIKUFA LAKINI AKINA HITLER WAMEENDELEA KUZALIWA.
By Luqman Maloto
Kansela wa zamani wa Ujerumani na Kiongozi (Fuhrer) wa Ujerumani chini ya Chama cha Nazi, Adolph Hitler, alijipiga risasi pamoja na mkewe, Eva Braun, Aprili 29, 1945.
Ngoja kwanza hapa uone watu na matukio yao; Hitler na Eva walianza kuwa wapenzi mwaka 1929. Wakadumu kwenye mapenzi yao miaka 16 bila kufunga ndoa.
Baada ya kuona hali ni mbaya kutokana na Ujerumani chini ya Nazi kuzidiwa nguvu na majeshi ya Magharibi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, 'wazimu wa kifo' ukawatuma Hitler na Eva kufunga ndoa.
Kweli, Hitler na Eva walioana katika ndoa iliyodumu kwa siku moja tu, kwani walifunga ndoa rasmi Aprili 29 kisha Aprili 30, 1945, walijiua kwa risasi. Hapo kama ni filamu, unasoma maandishi The End!
Hitler hakutaka kuwapa watu kazi ya kumuua, alirahisisha jukumu kwa kujiua yeye mwenyewe. Hakutaka majeshi ya Magharibi yamtie nguvuni na kumtesa, aliamua iwe nusu shari. Naam, angengoja shari kamili angekiona cha mtema kuni cha kihistoria.
Hitler ni nani? Swali hilo majibu yake ni mengi. Kwanza Hitler ni mtawala wa zamani wa Ujerumani na ndiye chanzo kikuu cha kutokea kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kuanzia Septemba 1939 mpaka 1945.
Hitler alikuwa fashisti, aliyebeba mamlaka yote ya utawala wa nchi kwenye mabega yake. Ujerumani ya Nazi chini ya Hitler, sauti ya Hitler ndiyo ilikuwa Katiba na sheria.
Hitler alikuwa kiongozi mwongo na mchonganishi. Alikuwa mpandikiza chuki na mbaguzi. Aliigawa Ujerumani kwa matabaka akijifanya mtu wa watu wa chini.
Hitler aliua demokrasia Ujerumani, aliifanya nchi kama taasisi yake binafsi. Alihakikisha wapinzani wake wanaangamia. Alijitengeneza kuwa mtu pendwa zaidi Ujerumani.
Pamoja na athari nyingi ambazo Hitler aliwasababishia Wajerumani na dunia yote, je, alipokufa hakuacha masalia? Swali hilo linaleta kicheko kidogo halafu tafakari kwa mshangao; masalia ya Hitler!
Ukitaka kujua kama Hitler aliacha masalia au la, lazima kwanza ujue u-Hitler ni nini? Ukishaujua u-Hitler ndipo utaelewa ili mtu aonekane ni masalia ya Hitler sharti awe na sifa zipi.
Je, unaujua u-Hitler? Jawabu la swali hilo limo kwenye nadharia inayoitwa demagogue. Ukishaijua demagogue, utamuona vizuri Hitler. Baada ya hapo utabaini kuwa akina Hitler walikuwepo kabla ya Hitler na wameendelea kuzaliwa hata baada ya Hitler.
Kwa mantiki hiyo, masalia ya Hitler bado yapo. Wapo akina Hitler wanaoongoza Serikali. Akina Hitler wengine wanatamani wapate nafasi ya kuongoza nchi. Kuna akina Hitler wafanyabishara. Ma-Hitler ni mengi kweli.
DEMAGOGUE NI NINI?
Nadharia hii inampambanua kiongozi dikteta anayecheza na hisia za watu anaowaongoza ili kutimiza makusudio yake. Demagogue ni kiongozi ambaye hutumia ghiliba ili kupendwa.
Demagogue ni kiongozi ambaye hupandikiza chuki kwa watu. Mara nyingi huegemea kundi kubwa kisha kuwachonganisha na kundi dogo ili kuwatenganisha.
Watawala wengi ambao wapo kwenye kundi la demagogue, hujipatia umaarufu kwa kujifanya watetezi wa watu maskini na kujipambanua kuwa wanapambana dhidi ya matajiri.
Demagogue hutumia njia ya mkato kujenga chuki kwa wananchi maskini, kwa kuwaambia kuwa sababu ya umaskini wao ni kunyonywa na matajiri au jamii fulani.
Kiongozi demagogue hutumia maneno yenye kuamsha hasia za watu, halafu naye kujifanya yumo ndani ya chuki hiyo. Hujipambanua kama mpingaji mkuu wa kundi analolitengenezea uhasama.
Mathalan, kiongozi demagogue anajiweka wazi kuwa yeye yupo kwa ajili ya maskini, kwa hiyo anajipambanua kama kamanda mkuu wa vita dhidi ya matajiri.
Mafanikio ya kiongozi demagogue ni uelewa mdogo wa watu. Kwamba kiongozi anapowadanganya watu, nao kwa vile uwezo wao wa kuchanganua mambo ni mdogo, huamini kauli hizo za chuki na uchonganishi.
Kwa kawaida kiongozi demagogue ni mwoga. Huhofia mamlaka yake, ndiyo maana huhakikisha anawapeleka puta matajiri au tabaka lolote lenye nguvu ili awadhoofishe na kutawala watu dhaifu. Demagogue huogopa wapinzani.
Hivyo, kelele za kiongozi demagogue siyo kwamba lengo ni kuwainua maskini kiuchumi, bali hutaka matajiri wadhoofike ili aongoze taifa lenye watu dhaifu wasio na nguvu ya kuutikisa utawala wake.
Kiongozi demagogue huogopa matajiri lakini hujifanya hawaogopi, badala yake hujionesha anapambana nao. Hata hivyo, mapambano yake huegemea kwa watu maskini ili wamuunge mkono.
Kiongozi demagogue baada ya kufanikiwa kuwaweka taabani matajiri au lile kundi ambalo huamini ni hatarishi katika utawala wake, ndipo raia wote huanza kukiona cha moto.
Kimsingi kiongozi demagogue hutaka aogopwe na asipingwe. Hufahamu kuwa ili afanikiwe katika hayo mawili ni lazima utawala wake uwe na nguvu kubwa halafu watu wote wawe dhaifu, ndiyo maana kiongozi demagogue hajawahi kuwaacha salama matajiri na wapinzani wake wa kisiasa.
Kiongozi demagogue anapoanza harakati zake ni vigumu kumwelewa anapoelekea. Akianza kushughulika na matajiri watu hudhani ataishia kwao. Hata hivyo, safari moja ya kiongozi demagogue huanzisha nyingine.
Anapomalizana na matajiri hugeuka kwa kundi lingine ambalo huona ni tishio, mwisho kabisa huhakikisha watu wote wanakuwa dhaifu. Baada ya hapo kiongozi demagogue hugeuka dikteta kamili kwa kuongoza nchi jinsi anavyotaka yeye.
Kiongozi demagogue anapoanza kujipambanua kuwa fashisti kamili, Katiba na sheria huviweka kando. Ni hapo kiongozi huamua kujigeuza yeye ndiye Katiba na sheria, amri zake huongoza nchi na hata kuadhibu anaowakusudia bila kuheshimu utaratibu wa sheria za nchi.
U-HITLER UPO TANGU KALE
Hitler ni maarufu zaidi kwa sababu ya athari alizozisababisha kwa kuanzisha Vita Kuu ya Pili ya Dunia mnamo muongo wa nne na wa tano katika Karne ya 20. Hata hivyo, u-Hitler kama tabia zao la demagogue, upo kabla Yesu hajazaliwa.
Miaka 2300 kabla Hitler hajatawala Ujerumani na kudhihirisha u-Hitler (u-demagogue) wake, alishakuwepo Cleon wa Athens ambaye alitekeleza u-Hitler kwa kiwango chenye rekodi ya historia.
Mwaka wa 422 Kabla ya Kalenda ndipo Cleon alifariki dunia. Kuanzia mwaka 429 Kabla ya Kalenda mpaka mauti yalipomfika, Cleon aliweka historia kuwa kiongozi demagogue wa kuogopwa kuwahi kutokea.
Maandishi ya wanahistoria wa Ugiriki ya kale, Thucydides na Aristophanes, yamewezesha ulimwengu kutambua hulka na vitendo vya Cleon, hivyo kuonesha kuwa u-Hitler ulikuwepo kabla ya ujio wa kalenda.
Wakati Athens ikiwa chini ya uongozi wa Jenerali Pericles, Cleon aliibuka kama mpinzani hasa wa watawala. Cleon alikuwa mkosoaji wa utawala na jinsi uongozi wa Pericles ulivyotumia rasilimali za Waathens.
Ni asili ya kiongozi demagogue kuwajengea wananchi hofu kuhusu usalama wa rasilimali zao au hata amani yao. Cleon alijipambanua kuwa sauti ya wanyonge na alitaka wananchi maskini wamuunge mkono ili kutetea mali zao.
Mwaka 429 Kabla ya Kristo, Pericles alifariki dunia. Nafasi ikawa wazi kwa Cleon maana alipendwa hasa na wananchi wengi mafukara. Kweli, Cleon akawa Kiongozi wa Athens.
Kama kawaida ya viongozi demagogue, Cleon alianza kuwajengea chuki Waathens dhidi ya majirani, vilevile Waathens wenyewe kwa wenyewe. Cleon aliwashambulia watu waliokuwepo madarakani kuwa walikuwa wakijinufaisha kwa jasho la maskini.
Cleon aliwaambia Waathens maskini kuwa wamekuwa wakinyonywa kwa muda mrefu na tabaka la watawala. Maneno hayo yalizusha chuki kati ya wananchi maskini dhidi ya matajiri na vigogo.
Baadaye Cleon aliwajaza upepo Waathens dhidi ya majirani zao wa mji wa Mytilene. Cleon aliwashawishi Waathens kuamini kuwa uwepo wa Mytilene ni hatari kwa usalama wao.
Mwaka 427 Kabla ya Kalenda, Waathens walitwangana na majirani zao wa Mytilene. Cleon alisema kuwa kila mwanaume katika mji wa Mytilene auawe, wanawake na watoto wauzwe kama watumwa.
Inakadiriwa kuwa viongozi wa Mytilene na wananchi wa kawaida wanaozidi 1,000, waliuawa na Waathens. Agizo la kutaka kila mwanaume wa Mytilene auawe halikutekelezeka baada ya Waathens kuishtukia nia mbaya ya Cleon.
Aliyefanya Waathens wagome kutekeleza mpango wa kuuangamiza mji wa Mytilene ni Diodotus ambaye alikuwa mtiifu wa sera za amani na maridhiano. Wananchi walipokutana kwa pamoja kwenye Bunge la Athens, Diodotus alijenga hoja ya kupinga mpango wa kuua kila mwanaume wa Mytilene.
Waathens walimkubalia Diodotus na hapo wakawa wamemshtukia Cleon kuwa alikuwa anawajaza chuki dhidi ya majirani zao.
Kiongozi demagogue huwaaminisha wananchi kwa kuwaambia uongo wenye kupenya kwenye hisia kuhusu matarajio ya ustawi wa maisha yao baada ya kufanya jambo fulani.
Mathalan, Cleon aliwahakikishia Waathens maisha bora kwa ustawi wa kiuchumi na amani baada ya kuwaangamiza watu wa Mytilene. Aliwaambia hawapo salama kama watu wa Mytilene wataendelea kuwepo.
Miaka miwili baada ya Waathens kuamua kutoendelea na vita dhidi ya Mytilene, Cleon alilizua lingine. Ilikuwa mwaka 425 Kabla ya Kalenda, alipowajaza upepo Waathens kupigana na watu wa mji wa Sparta.
Pamoja na watu wa Sparta kuomba mazungumzo ya amani, Cleon alikataa na kulazimisha mapigano. Alitaka kuona watu wa Sparta wanakuwa wanyenyekevu kwa utawala wake.
Wakati vita kati ya Athens na Sparta ikipamba moto, Cleon aliwalaumu makamanda wa vikosi vyake kwa usaliti, kwa hiyo akaomba yeye mwenyewe ndiye aongoze mapambano.
Aliyekuwa mkuu wa jeshi la Athens, Demosthenes alikubali kumwachia bosi wake uwanja. Alijua asingeweza lakini ikawa kinyume, Cleon aliongoza mapambano na kwa vile Sparta walishakuwa dhaifu, aliwashinda kirahisi. Cleon akavimba kichwa.
Miaka mitatu baadaye, yaani 422 Kabla ya Kalenda, Cleon alilizua lingine dhidi ya Mji ya Amphipolis. Alishajiona anaweza vita, lakini awamu hiyo kifo kikamfika eneo la tukio.
Cleon alizingirwa na vikosi vya Amphipolis chini ya Jenerali Brasidas. Hata hivyo, mwisho, Cleon na Brasidas wote waliuawa, hivyo kuruhusu mazungumzo ya amani kati ya Athens na Amphipolis.
Mazungumzo hayo yalifanikisha mkataba wa amani kati ya Athens na Sparta yote. Mkataba huo hufahamika kama Amani ya Nicias au Amani ya Miaka 50.
Hivyo, Cleon ni demagogue wa kale zaidi. Unapouchukua u-Hitler kama hulka ya akina demagogue, unapata uthibitisho kuwa u-Hitler haukuanza kwa Hitler, isipokuwa Hitler aliufanya u-Hitler upate umashuhuri mkubwa.
Baada ya Cleon na kabla ya Hitler, viongozi demagogue walikuwepo. Baada ya Hitler mpaka huu muongo wa pili wa Karne ya 21, demagogues (akina Hitler) wameendelea kuwepo, japo ni kwa kung'ata na kupuliza.
Alikuwepo Alcibiades wa Athens baada ya Cleon, Roma ikawa na Gaius Flaminius Nepos, wote hao walitikisa kwa uzushi na kupandikiza chuki kwa wananchi.
MTAMBUE HITLER
Jambo moja ambalo si la kusahau ni kuwa kiongozi akiwa demagogue hutaka aonekane yeye tu. Hii ndiyo sababu demagogue ni kiongozi dikteta lakini mwenye kujifanya mwana demokrasia na kipenzi cha watu.
Hitler alichomoza kwenye siasa za Ujerumani kama mtetezi wa wanyonge na maskini, aliyepambana na matajiri pamoja na tabaka la watawala.
Hitler alipandikiza sumu ya chuki kwa Wajerumani, alipokuwa mshereheshaji wa hoja kwamba Wayahudi ni wavamizi na walikuwa wakiwanyonya raia wengine wa Ujerumani.
Uzuri wa demagogues tabia zao zinafanana. Ni wepesi kujitetea wanapokosolewa kwa dhamira na vitendo vyao viovu. Utetezi wao huwa wa kipuuzi lakini ndiyo huushikilia.
Mfano, Hitler alipokuwa akikosolewa tabia yake ya ubaguzi na siasa za chuki zenye kuwagawa watu, alikuwa akijitetea: "Mimi napingana na mfumo unaokandamiza wananchi maskini, ukipingana na mimi, maana yake wewe ni mnyonyaji."
Hitler alisema kuwa sababu ya Ujerumani kushindwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1914-1918 ni Wayahudi. Hitler pia aliwashambulia Wayahudi kuwa sababu ya uchumi wa Ujerumani kuwa taabani baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Katika hoja hiyo, mtu yeyote aliyejitokeza kumpinga, Hitler alimshambulia: "Mimi napambana na usaliti wa Wayahudi kwa Wajerumani. Ukipingana na mimi maana yake wewe ni sehemu ya walionufaika na usaliti huo."
Ni mtindo huohuo alioutumia aliyekuwa Seneta wa Wisconsin, Joseph McCarthy, alipobuka na kuishambulia Serikali Kuu ya Marekani kuwa ilikuwa imeingiliwa na Komunisti na kwamba Urusi ndiyo ilikuwa inaiongoza Marekani.
McCarthy alipobanwa athibitishe, hoja zake zilikuwa nyepesi. Halafu akawa anajitetea: "Mimi napingana na Ukomunisti. Wewe unapingana na mimi. Kwa hiyo wewe ni Mkomunisti."
Baada ya vyombo vya usalama kujiridhisha kuwa McCarthy ni muongo, waliamua kuunakshi u-demagogue (u-Hitler) wake, kwa kuanzisha msamiati unaoitwa McCarthyism, wenye maana ya uzushi usio na mashiko.
Turudi kwa Hitler; ni kwamba kiongozi muongo, anayejitoa ufahamu na kusema mambo yasiyo na ukweli ili kuteka hisia za kundi kubwa la watu, huyo ni masalia ya Hitler. Huyo ni masalia ya Cleon. Huyo ni mfuasi wa McCarthyism.
Kiongozi sampuli ya Hitler huzungumza zaidi kuliko vitendo. Hutoa matarajio makubwa ambayo hawezi kutekeleza. Akipewa nafasi hukimbilia kusingizia watu.
Mathalan, Hitler alipokuwa anakinadi chama chake cha Nazi, alisema kuwa kila Mjerumani lazima awe na ajira na alipwe mshahara.
Baada ya Nazi kushinda majimbo mengi hivyo yeye kuwa Kansela wa Ujerumani, aliamua kujipa na cheo cha kuwa kiongozi (mtawala mkuu) wa Ujerumani, yaani Fuhrer.
Pamoja na nguvu kubwa aliyojipa, bado hakuweza kutimiza ahadi. Matokeo yake Hitler alitengeneza visingizio kuwa Wayahudi na watawala kabla yake waliharibu nchi ndiyo maana alikuwa akishindwa kutimiza ahadi.
Hitler pia aliwalaumu Wayahudi na wapinzani wake kuwa walikuwa wakimhujumu. Akatumia kigezo hicho kufuta shughuli za kisiasa.
Kiongozi mpenda kulalamika na kusingizia matajiri au viongozi waliomtangulia kuwa wameifilisi nchi au wanamhujumu, huyo ni masalia ya Hitler. Ni demagogue.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amejaribu mara kadhaa kuingiza sera za Hitler nchini humo lakini inashindikana kwa sababu ya uelewa wa Wamarekani kuwa mkubwa na mfumo wao wa dola una nguvu sana.
Siku alipoapishwa, Januari 20, mwaka huu, Trump alisema kuwa miaka yote utawala ulikuwa Washington DC palipo na Ikulu ya nchi hiyo, White House na kuwatawala Wamarekani bila wao wenyewe kuwa na sauti.
Trump alisema kuwa kuanzia siku hiyo, utawala ulikuwa unahama kutoka Washington DC na kwenda kwa watu. Kauli hiyo ya Trump ndiyo ya aina ya viongozi demagogues, viongozi wenye chembechembe za u-Hitler. Viongozi wenye kujenga matumaini makubwa ya kiini macho.
Trump anapopata upinzani kutoka idara za itelijensia na vyombo vya habari, husema anahujumiwa. Hujitambulisha kuwa yeye ni mtetezi wa Wamarekani, kwa hiyo vyombo vya habari Marekani ni maadui wa Wamarekani.
Hivyo, viongozi sampuli ya Hitler wapo na wanaendelea kutokeza kila mara kwenye wodi za wazazi katika nchi mbalimbali. Wanazaliwa kila leo.
Hatari ni kuwa viongozi wengi wanaupenda u-Hitler lakini hawajui madhara yake. Wapo viongozi wanaongoza ki-Hitler huku katika hotuba zao wakimlaani Hitler. Viongozi wengi humuenzi Hitler huku wakijiita walezi wa demokrasia.
Dunia ya Karne ya 21 haipaswi kuwa na akina Hitler. Mafashisti wenye kubeba njia zote za uchumi Serikali Kuu ili wawe na sauti ya mzunguko wote wa kifedha katika nchi.
Hitler aliwadanganya Wajerumani kuwa kila familia itamiliki gari. Kampuni ya Volkswagen ikatengeneza magari aina ya beetle. U-Hitler ni kuzungumza na kuahidi bila kupima matamshi na ahadi. U-Hitler ni kujitoa ufahamu.
U-Hitler ni uzuzu. Kwa vile huongopa, hutokea kuamini uongo ambao wao wenyewe huuanzisha na kuusimamia mpaka mwisho.
U-Hitler ni kupenda vurugu, visasi na uonevu. Kiongozi mwenye kupenda kulipa visasi, mshari na mchokozi wa wapinzani wake. Kiongozi anayetumia mamlaka yake kukandamiza asiowapenda huyo ni demagogue. Ni masalia ya Hitler.
Ukisikia kiongozi anasema: "Ninyi ni matajiri ila mmekuwa maskini kwa sababu ya akina fulani." Huyo mwogope, anamuenzi Hitler na siasa zake za chuki dhidi ya Wayahudi.
Ukimbishia atakwambia: "Unatetea wezi." Akina demagogue wapo hivyo. Hitler aliwaambia waliomkosoa: "Mnatetea wanyonyaji?"
Trump ni vigumu sana kutekeleza u-Hitler Marekani. Vladimir Putin amefanikiwa Urusi. Waliokuwa matajiri wamemkoma. Wapinzani wameshika adabu. Waandishi wa habari wanaomkosoa hukiona cha moto.
Samaki mkunje angali mbichi. U-Hitler hudhibitiwa ukiwa haujakomaa. U-Hitler unapoanza, anapoguswa mmoja, wengine hudhani watabaki salama.
Wakiguswa matajiri, wanasiasa hudhani wapo salama. Wanapoguswa wanasiasa wa upinzani, wale wa chama chake hudhani wapo salama. Hitler alipoanza safishasafisha yake, viongozi na wafuasi wa Nazi walijiona wapo salama. Hata hivyo, mwisho Ujerumani yote ililia kilio kimoja.
Putin alipoanza kuwashughulikia matajiri Urusi na kuwaondoa relini waliokuwepo na kusimika wapya, waandishi wa habari na wanasiasa walijiona wapo salama. Mwisho wapenda demokrasia wote wanalia kilio kimoja Urusi.
Aghalabu, kiongozi demagogue huanza kidogo na kusikilizia. Anapoachwa na kufuzu u-demagogue wake, hugeuka dikteta kamili, hivyo kuvaa vazi kamili la Mnazi Adolph Hitler. Ni hapo sasa Taifa zima hujuta.
Ndimi Luqman MALOTO.
06/07/2017.