Historia ya Zanzibar iliyofichwa

sinafungu

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
1,527
865
ZANZIBAR inaumwa; tena inaumwa ugonjwa unaoua hima (terminal disease) isipopata tiba makini, tiba yenye nguvu na kwa dozi kubwa.

Vipimo vya kitaaluma vinaonesha inasumbuliwa na mashetani, mizuka yenye kukalia kigoda cha mzimu wa watu wa kale. Mzimu huu unayumbisha Muungano wa Tanzania pia.

Juhudi za Serikali ya Muungano kutibu ugonjwa huu zimepwaya, kwamba badala ya kutibu ugonjwa wenyewe, mara nyingi zimeelekezwa kutibu dalili za ugonjwa pekee.

Mzimu wa ubaguzi kwa misingi ya rangi na uchama wa vyama mfu vya kale unaitafuna Zanzibar kwa kificho cha vyama vya siasa vya sasa – Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kwa staili ya mababu. Kwa vipi?.

Harakati za kisiasa za uhuru (modern independence struggles) Visiwani, ziliongozwa na vyama vikuu viwili: Zanzibar Nationalist Party (ZNP), kilichoundwa mwaka 1955; na Afro-Shirazi Party (ASP) kilichoanzishwa mwaka 1957.

Kipindi cha uchaguzi Mkuu wa mwisho, Julai 1963 kuelekea uhuru, kulijitokeza vyama viwili vibanzi (splinter parties) – Zanzibar and Pemba Peoples’ Party (ZPPP) cha waliojiengua kutoka ASP, na Chama cha Umma Party (UP) cha Abdulrahman Mohamed Babu na wenzake waliojiengua kutoka ZNP. UP hakikushiriki Uchaguzi Mkuu wa mwisho wa 1963, lakini kilishiriki kupanga na kuratibu kwa mafanikio, Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

ZPPP na ZNP viliunda umoja (Ukawa) dhidi ya ASP na kushinda uchaguzi na hivyo kukabidhiwa serikali chini ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte wa ZPPP. Siku 33 baadaye, serikali hiyo ilipinduliwa.

ASP ni muungano wa vyama viwili vya kijamii, “African Association” (AA) na “Shirazi Association” (SA), kufanya “Afro-Shirazi Party” (ASP).

Chama hiki kilijipambanua kuwa cha Waafrika zaidi, kama ambavyo tu Chama cha “Tanganyika African National Union” – TANU cha Tanzania Bara kilicholeta uhuru wa nchi hiyo mwaka 1961, kilivyojipambanua mwanzoni, lakini kikajisahihisha haraka kuachana na ubaguzi na kuwa cha watu wa rangi zote. Mapinduzi ya 1964 yalikiweka ASP madarakani, chini ya Serikali ya Mapinduzi iliyoongozwa na Abeid Amani Karume wa ASP. Hapo ndipo ugonjwa unaoitesa Zanzibar hadi sasa ulipoanzia.

Kwa kuanzia, Wazanzibari wote waliokuwa wanachama wa ZNP/ZPPP na ndugu zao walihesabiwa kama maadui wa Mapinduzi na kuvurumishwa nje ya Zanzibar, na waliobakia waliteswa kwa kutwezwa kwa ubaguzi mkubwa.

Mohamed Babu wa UP, aliyekuwa na asili ya Visiwa vya Ngazija, alitakiwa kuvunja Chama chake, naye akakubali ambapo yeye na baadhi ya vijana wake, kwa kutambuliwa mchango wao katika Mapinduzi ya 1964, walipewa Uwaziri katika Serikali ya Mapinduzi na baadaye katika Serikali ya Muungano.

Mwaka 1971, Karume aliwatuhumu Washirazi kuwa na asili ya Uarabu na hivyo kwamba Uzanzibari wao ulikuwa wa kutiliwa shaka nakuwataka waukane “Ushirazi”, vinginevyo waondoke Zanzibar. Washirazi walikuwepo Zanzibar kabla ya ukoloni wa Sultani mwaka 1828. Mmoja wa Viongozi wa SA, mwenye damu ya Kishirazi, Thabiti Kombo, alifanywa Katibu Mkuu wa ASP.

Kufuatia kifo cha Karume Aprili 7, 1972, mzimu wa ubaguzi ukakita kwa kishindo kikubwa zaidi. Kwanza, Wazanzibari wote waliokuwa wanachana wa ZNP, ZPPP na Umma Party na koo zao, walitiwa ndani ya kapu moja la mauaji ya Karume bila udadisi na hivyo kuitwa maadui wa Mapinduzi.

Kisha ikapitishwa amri kwamba, Wazanzibari wa kundi hilo wasipewe nafasi za uongozi Visiwani, wala kuruhusiwa kujiunga na Jeshi la Ulinzi na Polisi.

Pili, Zanzibar ilifanywa kuwa ya Wazanzibari weusi; suriama (chotara) na wahamiaji wengine wa rangi tofauti, bila kujali walifika lini Zanzibar, hawakustahili kuitwa Wazanzibari.

Ubaguzi huu na manyanyaso yalikuwa yalisimamiwa na Serikali ya Mapinduzi chini ya Usimamizi wa kundi katili, maarufu kama “Genge la watu 14” – (the Gang of fourteen), likiongozwa na Kanali Seif Bakari wa idara ya Usalama Zanzibar.

Hata pale Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964, ubaguzi huu uliendelea kwa chukizo kubwa kwa Mwalimu Nyerere, ukifanywa kwa jina la Serikali ya Mapinduzi chini ya ASP kilichokuwa juu ya Serikali ya Muungano; Karume akageuka kuwa mwiba kwa Mwalimu.

Ili kukomesha ukatili na ubaguzi huu, mwaka 1976, Mwalimu Nyerere (TANU) alibuni Muungano wa Vyama vya TANU na ASP (kama alivyobuni mapema Muungano wa nchi hizo mbili) kwa madhumuni ya kudhibiti maovu ya Zanzibar ndani ya Jamhuri ya Muungano, ili chaka la hayo yote (ASP) liweze kudhibitiwa na chama kipya chenye kushika hatamu za uongozi wa Jamhuri ya Muungano, Zanzibar ikiwa ndani.

Wazo hili lilipingwa vikali na Wahafidhina wa siasa za ubaguzi visiwani kiasi cha Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Aboud Jumbe, kulazimishwa aachane na “mbinu za Nyerere” za kutaka “kuimeza” Zanzibar; akatoa sababu za kutaka muda zaidi kufikiria.

Lakini baada ya vuta nikuvute, na kwa tishio la kuvunja Muungano, wahafidhina hao, waliojiita “Wakombozi” (Liberators), walikubali ASP na TANUviungane, lakini kwa masharti.

Sharti la kwanzalilikuwa kwamba, jina la Chama kipya lisiwe kwa lugha ya Kiingereza ili kutowakumbusha Wazanzibari enzi za ukoloni wa Mwingereza Visiwani; la pili, kwamba neno “Mapinduzi” lionekane na kusomeka bayana ndani ya jina la Chama kipya ili kutopoteza historia ya Mapinduzi ya 1964. Tatu, tarehe ya kuzaliwa kwa Chama kipya ioane na tarehe ya kuasisiwa kwa ASP, na kwamba angalau tarakimu moja ya mwaka 1957ionekane pia.

Potelea mbali, TANU ya Nyerere haikupoteza muda kwa hayo; ikakubali jina la Chama liwe “Chama cha Mapinduzi” (CCM) bila tafsiri ya Kizungu ambapo kingeitwa “Revolutionary Party of Tanzania” – RPT; na ikakubalika kianzishwe Februari 5, 1977, tarehe ya kuasisiwa ASP, 5 Februari 1957.

Kisha, CCM kikatangaza kushika hatamu za uongozi hivi kwamba kiongozi yeyote aliyekwenda kinyume na maagizo ya Chama, alikwenda kinyume na Muungano na hivyo mhaini, Mzanzibari kwa Mtanzania Bara.

Kwa hatua hiyo, wahafidhina wa siasa za ubaguzi na ukatili Visiwani walivurumishwa; Baraza la Mapinduzi na “the Gang of 14” likamalizwa nguvu kwa nafasi yake kuchukuliwa na Baraza la Wawakilishi; demokrasia ikamea Zanzibar.

Ukuu wa Chama (Party Supremacy), ndio uliomng’oa madarakani Rais wa awamu ya pili Visiwani, Aboud Jumbe, alipojaribu kuungana na Wahafidhina wa siasa za chuki, kuhoji uhalali wa Muungano, mwaka 1984.

Kurejea kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini mwaka 1992, kulifufua ubaguzi na chuki kwa misingi ile ile ya vyama vya kale kufanya Zanzibar kumeguka vipande vipande.

Kwamba wale ambao walitaka mabadiliko kwa kuona Zanzibar mpya (wanajiita “Frontliners”) na ambao hawako tayari hadi leo kuishi kwa “legacy” ya ukatili na ubaguzi wa kitabaka wa miaka 1950/1960, wanahesabiwa kuwa si Wazanzibari wa kweli na kuchukuliwa kama maadui wa Mapinduzi.

Baadhi ya waliojaribu kufanya hivyo mwaka 1986, akiwamo Kada wa CCM wa zamani na kipenzi cha Mwalimu Nyerere, aliyesaidia kung’olewa madarakani kwa Jumbe, Maalim Seif Sharrif Hamad; walifukuzwa uanachama wa CCM kwa kusaliti Mapinduzi.

Wengine waliofukuzwa pamoja na Hamad ni Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan, Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid (sasa yupo ADC) na mwingine mmoja.

Kufukuzwa kwa kundi hili, maarufu kama “The Magnificent Seven” (Waadhimu Saba), kulifanya waungane na kuanzisha upinzani kwa mwavuli wa “Kamati ya Mwelekeo wa Vyama Huru” – “KAMAHURU”, iliyozaa Chama cha “Zanzibar United Front” [ZUF] mwaka 1992. BaadayeZUF kiliungana na “Chama cha Wananchi” (CCW) cha Bara, kuunda Chama cha kitaifa cha sasa – “Civil United Front” (Chama cha Wananchi) – CUF.

Vyama hivi viwili, CCM na CUF vina nguvu sawa Visiwani kiasi kwamba hakuna aliye na uhakika wa ushindi kwa chaguzi zote. Kwa wahafidhina wa siasa za kale Visiwani, ASP hakijafa, kinaishi ndani ya kivuli cha CCM; na vivyo hivyo Baraza la Mapinduzi na nadharia zake.

Kwa wahafidhina hao, Chama chochote cha upinzani kwa CCM ni cha upinzani kwa ASP mfu na Baraza la Mapinduzi, “upinzani” wenye kuibua hisia za mzuka wa ZNP na ZPPP za kujitakia.

Wakati CCM Zanzibar kinaishi kwa hofu ya mzimu wa watu wa kale, CCM Bara kinasumbuliwa na hofu itokanayo na Katiba shaghalabagala ya Muungano, inayozua maswali mengi kuliko majibu kama vile: Je, iwapo, kwa mfano, CUF kitashinda uchaguzi Zanzibar na Seif Sharrif Hamad kuwa Rais wa Zanzibar, na Magufuli wa CCM kama Rais wa Tanzania; hali ya kisiasa itakuwaje kwa vyama viwili tofauti kutawala sehemu mbili tofauti za Tanzania?.

Kwa kuwa Rais wa Zanzibar ni Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano (Angalia Katiba, - ibara 54 (1) ambalo wajumbe wake ni pamoja na Rais wa Muungano, hali itakuwaje kama Seif Sharrif Hamad wa CUF atakuwa mjumbe wa Baraza hilo? Je, litaweza kufanya kazi ipasavyo?, wakahoji.

Kwa kuwa Baraza la Mawaziri linawajibika kwa Bunge la Muungano na kwa Rais katika ujumla wake, Je, Hamad naye atawajibika kwa Bunge hilo na kwa Rais wa Chama tawala Tanzania? Je, atawajibika pia kutekeleza uamuzi wa Baraza hilo la Mawaziri nchini Zanzibar? Kama nani?

Rais wa Zanzibar kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano kulitokana na hofu nyingine kubwa zaidi, juu ya uwezekano wa Hamad kuwa Rais wa Zanzibar na hivyo kuwa Makamu wa Rais wa Muungano, jambo ambalo halikuingia kichwani mwa CCM.

Hivyo, haraka haraka ikateuliwa Tume ya Jaji Mark Bomani mwaka 1994, kupendekeza marekebisho ya Katiba kama ilivyo sasa kwa kukiuka mmoja wa misingi ya Muungano, kama inavyofafanuliwa kwenye Mkataba wa Muungano [Articles of Union] wa mwaka 1964.

Tatizo ni upungufu katika Katiba ambao umeandikwa kana kwamba hapana uwezekano wa sehemu mbili za Tanzania kutawaliwa na vyama viwili tofauti, licha ya kufungua milango kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Inapofikia hapo, hofu ya wahafidhina wa siasa za ubaguzi Visiwani na hofu ya wenye uchu wa madaraka Bara, zinaungana kwa kivuli cha CCM kubaka demokrasia na umoja wa kitaifa kwa kusigina Katiba na Sheria tulizozitunga wenyewe.

Sheria zinazotakiwa kuzingatiwa na kuheshimiwa ni Katiba ya Zanzibar, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar, na kwa Wasimamizi wake kujiepusha na ushabiki wa vyama vya siasa.

Historia ya Zanzibar inaonesha kwamba, umwagaji damu wote uliowahi kutokea Visiwani ulitokana na machafuko yaliyosababishwa na chaguzi kuu zisizokuwa huru na za haki. Kwa mfano, uchaguzi wa kwanza, uliofanyika Januari 1961 haukutoa mshindi kati ya ASP na ZNP; ghasia zikazuka na watu kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Hata hivyo, chuki na uhasama wa kisiasa enzi hizo haukuwa mkubwa kama ilivyo sasa; wanasiasa waliongozwa na azma moja ya kuipatia nchi uhuru kutoka kwa Waingereza bila kuingiza ubaguzi wa aina yoyote miongoni mwa Wazanzibari. Ndiyo maana, baada ya Vyama vyote kukosa ushindi katika uchaguzi wa Januari 1961, iliundwa serikali ya mseto ya mpito ya vyama vya ASP, na ZNP/ZPPP kuelekea uchaguzi mwingine uliopangwa kufanyika Juni 1961.

Kabla ya uchaguzi huo, Karume alimwomba Kiongozi wa Chama cha ZPPP, Mohamed Shamte waunganishe vyama vyao (ASP na ZPPP) ili kukipiku, lakini Shamte alikataa.

Juni 1961 ilipowadia, ZNP na ZPPP viliunda mseto dhidi ya ASP; ghasia kubwa zikazuka, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kupinda kanuni za uchaguzi. Katika ghasia hizo, watu 70 waliuawa, 400 walijeruhiwa na wengine 1,002 kutiwa mahabusu na Serikali ya Uingereza. Hapo ndipo uhasama mkali wa kisiasa ambao umedumu hadi leo uliposhika kasi.

Uchaguzi wa tatu na wa mwisho kabla ya uhuru uliofanyika Julai 1963 ulilalamikiwa na Chama cha ASP kwamba haukuwa huru na wa haki. Hata hivyo, Karume aliamua kutupa karata yake ya mwisho kwa kutaka kuundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa kati ya ZNP/ZPPP na ASP ili kumaliza manung’uniko na uhasama wa kivyama.

Aliwatuma Viongozi wawili waandamizi wa ASP – Othman Sharrif na Hasnu Makame, kumwomba Shamte akubali kuundwa kwa serikali hiyo, ambapo Shamte angeongoza serikali akiwa na uhuru kamili wa kuteua mawaziri kutoka ZNP, ZPPP na ASP. Kwa mara ya pili, Shamte alikataa katakata na badala yake akashauri ASP kivunjwe na wanachama wake wajiunge na ZNP/ZPPP.

Sote tunafahamu kilichotokea; Serikali ya Shamte ilipinduliwa katika Mapinduzi ya umwagaji damu, yaliyopangwa na kuongozwa na vijana wenye itikadi za Kisoshalisti wa vyama vya ASP na UMMA, Januari 12, 1964. Siku 100 baadaye tangu Mapinduzi hayo kufanyika, Zanzibar na Tanganyika ziliungana kuunda Tanzania.

Wazanzibari bado wanabaguana kwa misingi ya vyama vya siasa hai na mfu, rangi na kwa nasaba za koo zao; ubaguzi ambao haupo Tanzania Bara. Haya yote ni ishara ya kuzorota kwa umoja wa kitaifa na chanzo cha ghasia. CUF Zanzibar kinahesabiwa kuchukua nafasi ya ZNP/ZPPP, na CCM Zanzibar nafasi ya ASP.

Tunayoshuhudia sasa ni vituko vya uhuru vinavyofanywa na Wazanzibari waliochoka na hali ya amani. Kwa nini hatujifunzi kutoka Darfur, Sudani, Rwanda na Burundi na kwingineko kwa yanayotokea Visiwani.

Mzee Karume hakukosea alipowataka wapinzani wake kuunda serikali ya mseto mwaka 1961 na 1963 kama njia ya kumaliza mgogoro; na pale waliposhindwa kumsikiliza, ghasia ziliendelea kuitafuna nchi hadi Mapinduzi.

Kwa hali ilivyo Visiwani Zanzibar, kuna kila dalili kuonesha kwamba historia inaweza kujirudia kama nguvu za CCM na CUF hazitaweza kushabihishwa (harmonize) ziweze kutumika kwa maendeleo ya Wazanzibari.

Ushabiki na unafiki wa kisiasa unaochochewa na maswali magumu tuliyoyataja mwanzo hautalifikisha mbali taifa hili, badala yake utaliangamiza. Ilivyo, sasa Zanzibar inaumwa; tena ni mahututi kitandani.

Kauli tata na hasi za baadhi ya viongozi kwamba “Uhuru wa Zanzibar hauwezi kukabidhiwa kwa yeyote kwa njia ya sanduku la kura”; au kwamba, “kama lolotelisilotarajiwa (kushindwa uchaguzi) litatokea, tuko tayari kutumia silaha za Mapinduzi ya 1964 kwani CCM Zanzibar wanazo funguo za sanduku la silaha hizo”, zinachochea chuki na kuvuruga umoja wa kitaifa Zanzibar na kuzua tufani kwa Muungano pia.

Kiongozi bora ni yule anayeweza kuchukua hatua, hata kama hatua hizo hazitakuwa za manufaa kwa Chama chake cha siasa, mradi tu ni za manufaa kwa nchi nzima; au kuchukua hatua zinazogongana na matakwa ya wengi kwenye Chama chake, lakini ni hatua sahihi kwa nchi. Hapa iwe ni nchi kwanza, siasa baadaye.

Kurudia Uchaguzi Mkuu wote kama ZEC ilivyoamua, kwa sababu tu CUF kimeonekana kushinda baada ya baadhi ya matokeo kutangazwa, hakutaifanyia mazuri Zanzibar, badala yake kutakaribisha mtafaruku, chuki, hasira na pengine kuvunjika kwa amani. Kwa utamaduni wa Kizanzibari ulivyo, haya si mambo magumu kuweza kuyang’amua.

Kwa mantiki hii, tunapenda kuamini kwamba viongozi wa CCM na CUF Zanzibar pamoja na ZEC ni watu wazima, wenye akili timamu kuweza kuiweka Zanzibar ya kwanza rohoni mwao badala ya matakwa yao binafsi au yale ya vyama vyao na marafiki zao.

Hatutaki umwagaji damu wa mwaka 1961 na 2001 ujirudie kwa kuziba masikio kukidhi matakwa, uchu na uroho wa madaraka wa “wateule” wachache Visiwani. Mungu ibariki Zanzibar na Wazanzibari wote.


Chanzo: Raia Mwema
 
Kumbe kama ni hivyo wasijaribu kuvunja muungano maana kuna hatari ya kumalizana wao kwa wao
 
Siasa za Zanzibar ni ngumu ukilinganisha na uku bara upinzani uko ndani ya damu.


Sent from my BlackBerry 9810 using JamiiForums
 
Kumbe kama ni hivyo wasijaribu kuvunja muungano maana kuna hatari ya kumalizana wao kwa wao
Pengine wangekuwa nje ya Muungano hata CCM Zanzibar wangetambua kuwa hawatoshi kuwa peke yao, so wangelazimika kuungana na wengine kuongoza nchi. Lakini kwa mazingira ya sasa, CCM Zanzibar wanapata kiburi kwamba hata wasipotosha, wataongezewa nguvu kutoka bara, iwe ya kisiasa au ya kijeshi
 
Back
Top Bottom