Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 34,059
- 79,415
HISTORIA YA MAREHEMU
Na, Robert Heriel
Alikuwa rafiki yangu mkubwa, alipo nilikuwepo, alichopenda nilikipenda, alichochukia nilikichukia. Watu wengi walituona ndugu. Wengine walituita mapacha tusiofanana. Kumbukumbu zake mpaka leo hii zinaniumiza, zinaujaza moyo wangu huzuni kuu, ni rafiki mwema ambaye mpaka leo hii sijapata wa kuziba pengo lake.
Basi ilikuwa siku mbaya kwangu, siku ya majonzi na kilio, siku ambayo moyo wangu ulipasuka kwa simanzi. Siku ya msiba wa Rafiki yangu kipenzi, ndiye huyo JOHN FILIPATAI. Mimi nilipenda kumuita Filipatai yaani jina la ukoo wake.
Filipatai alikuwa amekufa, na leo hii ndio siku ya mazishi yake. Taratibu za kuuaga mwili ziliendelea kama ilivyodesturi ya jami ya Kiafrika kwa taratibu za dini ya Kikristo.
Watu walikusanyika makundi kwa makundi kuja kumuaga Shujaa Filipatai, ukumbi wote nyumbani kwa kina Filipatai ulikuwa umefurika pasiwepo nafasi ya kutemea mate. Watu walimpenda Filipatai mithili ya Baba wa taifa. Sikuona uso wa mtu asiye na huzuni, watu wote walikuwa na nyuso zenye majonzi, wakisikitikia kifo cha Rafiki yangu kipenzi.
Mimi nilikuwa nimekaa karibu na mama yake, mita chache kutoka lilipowekwa jeneza lake. Tulilizunguka Jeneza lake likiwa umbali wa mita tano hivi. Nililitazama Jeneza la Rafiki yangu, Loooh! Nilijikuta machozi yakizidi kulowesha mashavu yangu. Hapo nikakumbuka siku za nyuma tulipokuwa vijana wa dogo.
Enzi zile tukiwinda ndege porini, Filipatai alikuwa mashuhuri kwa uwindaji wa ndege, hakuna ndege ambaye hakuwahi kumlenga, ndege wote waliokuwa kijijini kwetu walionja joto ya jiwe la rafiki yangu. Pengine kama kuna waliofurahia msiba wa Rafiki yangu basi ni pamoja na ndege wa kijiji chetu. Walimchukia mno, walimuona kama adui yao.
Hata ndege aitwaye Pugi alikutwa na madhila ya Filipatai, Mbanja hakusalimika pia, Chorwe bwenzi yeye ndiye alikuwa kibonde kila siku idadi yao ilipungua sana kutokana na kuuawa na Filipatai. Njiwa, chokoribati, kwelea kwelea, Kunguru mkubwa na kunguru mdogo yule mweusi tii, Kwicho, na hata kipanga wote walipigwa na jemadari wa pori ndiye Filipatai.
Niliikumbuka Manati aliyokuwa anaitumia Rafiki yangu, ilikuwa manati kubwa yenye panda mbili nene, yenye mipira ya bomba nne. Kwenye kipago cha manati yake aliichora [picha ya ndege aitwaye tai. Sikujua ni kwa nini alichora picha hiyo kwenye Manati yake, pengine ni kwa sababu ya kumuona Tai kama mfalme wa ndege, lakini hayo ni mawazo yangu tuu.
Manati ile alikuwa akiiita IBWE LIKOMA ambapo ni lugha ya kipare akimaanisha Jiwe Liualo. Hakuna ndege aliyewahi kusalimika mbele ya Ibwe Likoma. Nakumbuka tukiwa porini nikiwa na Filipatai, kabla hajamlenga ndege alikuwa akiikamata Ibwe Likoma kisha analipenda kuiambia maneno haya: Rafiki yangu Ibwe Likoma, umeua ndege wengi, Nimeshindwa kuhesabu mpaka idadi. Haya jikuchulie kitoweo kingine tena.
Maneno hayo huyaongea akinongona huku macho yake akiwa kayafumba, baadaye huibusu Ibwe Likoma. Nakuambia ndege huyo lazima apigwe na kudondoka chini.
Filipatai pia alikuwa mahiri wa kutega mitego ya kunasia ndege kama Kanga, kware, njiwa na pugi. Alijua kutengereza urimbo bora sana. Kwa ujumla Filipatai alikuwa mashuhuri kwa uwindaji wa ndege.
Leo shujaa wa kuwinda ndege alikuwa kalala ndani ya Jeneza, shujaa kaumaliza mwendo wake.
Muda wa kusoma historia ya Marehemu ulifika, mzungumzaji ambaye alipewa nafasi ya kusherehesha katika msiba wa Filipatai alizungumza: Ratiba inayofuata ni Historia ya marehemu, wote tunajua kuwa Marehemu alikuwa mtu mashuhuri aliyefanya mambo mengi makubwa. Tunamkaribisha Taikon wa Fasihi, yeye ndiye alichaguliwa na Marehemu mwenyewe kuwa asome Historia yake. Na kwa vile tunamheshimu Ndugu yetu John Filipatai, tumeona tumpe Taikon kama alivyosema.
Hapo moyo wangu ukapasuka kusikia maneno hayo. Sikuwa nimejiandaa wala sikujua kama ningepewa nafasi kama hiyo siku ile. Kama hiyo haitoshi, sikuwahi kusoma historia ya Marehemu tangu kuzaliwa. Siku ile ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza. Hivyo nilikuwa naogopa sana.
Basi nikasimama na kupita mbele mpaka ilipo Maiki, Mshehereshaji akanipa maiki, kisha akanambia nikasimame karibu na Jeneza la Rafiki yangu, Nikaenda kusimama, kisha akaja mtu mmoja akafungua lile jeneza sehemu ya kichwani, Jamani! Nilimuona Filipatai, rafiki yangu kipenzi akiwa kafumba macho, uso wake ulikuwa kama mtu aliyelala, pengine nilifikiri angeamka lakini zilikuwa ndoto za mchana.
Sasa nikaambiwa nisome Historia ya Marehemu huku kila mara nikimtazama Marehemu. Ati hivyo ni kumuonyeshea upendo. Nikasema sawa.
Basi hivi ndivyo nilivyosoma Historia ya Marehemu Filipatai, Rafiki yangu kipenzi, siku ile ya msiba wake:
"HISTORIA YA JOHN FILIPATAI 22.2.2222, SAA 9.00 ALASIRI.
''John Filipatai alizaliwa miaka ishirini na tano iliyopita katika kijiji cha Muipo, wilayani Same, Mkoani Kilimanjaro. Ni Mtoto wa tatu katika Familia ya Filipatai. Katika utoto wake alipenda kuwinda ndege, na kucheza Gololi''
Hapo nikameza mate kisha nikamtazama Filapatai pale ndani ya Jeneza. Kumbe pembeni juu ya Jeneza iliwekwa Ibwe Likoma ndiyo ile Manati yake, Manati ya Mauaji.
Nikaendelea Kusoma;
"Alimaliza elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi Muipo, kisha akajiunga na shule ya Sekondari Muipo. Hapo akahitimu kidato cha nne na hakupata bahati ya kuendelea"
Nikamtazama kisha nikaendelea;
"Alianza harakati za siasa, alikuwa mtu apendaye haki, mwenye kutetea wananchi wa Muipo. Kazi aliyoifanya kwa Moyo wote. Hakupenda Dhuluma, na uonevu, alijipambanua kwa kupigana na wahalifu jambo ambalo lilifanya watu wabaya wote wamchukie"
"Kutokana na tabia hiyo, alipata misukosuko mingi ya kisiasa na kiuchumi. Kuna wakati aliwekwa gerezani kwa kesi za kubambikiziwa, ili mradi kumuzuia katika ndoto yake ya kuhakikisha wananchi wa Muipo wanaishi maisha mazuri"
Hapo nilipumzika, machozi yakinitoka tena. Nilimtazama Filipatai kwa uchungu sana. Historia hiyo nilikuwa naijua vyema, mimi ndiye nilikuwa rafikia yake wa karibu iweje nisijue harakati zake.
Nikaendelea;
"Filipatai mpaka anakutwa na mauti, hakuwahi kuwa na mtoto hata wa kusingiziwa, hakuwahi kuoa wala kuishi na mwanamke. Harakati zake zilikuwa ni kutetea haki"
"Filipatai alikutwa chumbani kwake alipokuwa amepanga akiwa ameuawa kwa kupigwa risasi. Uchunguzi bado unaendelea wa waliofanya unyama huo. Bwana ametoa, bwana ametwaa, Jina la Bwana lihimidiwe"
Nilimaliza kusoma Historia ya Marehemu, Kwikwi ilikuwa imenikaba sana. Uso wote ulikuwa umetepeta kwa machozi.
Labda niseme; mimi ndiye nilikuwa namfahamu Filipatai vizuri, pengine ningeambiwa niandike historia ya Marehemu ningeandika historia tofauti na niliyoisoma siku ile.
Filipatai hakuwa na Historia fupi kiasi kile, Filipatai hakufa kwa kupigwa Risasi. Filipatai alioa Mke na ana mtoto mmoja licha ya umri wake mdogo. Historia ile ilikuwa imepotoshwa kwa sehemu kubwa.
Kuhusu kucheza Gololi sikatai, Filipatai alikuwa mchezaji mashuhuri wa Gololi, alipenda kusema maneno kama ''No Fagi" akimaanisha usisafishe sehemu gololi yake ilipojificha. Alipenda pia kusema "No mtingisho" akimaanisha ukimlenga gololi yake ikitingishika kidogo basi haujamlenga, bali unapaswa umlenge kabisa. Pia alipenda kusema "Tili au doble Tili" akimaanisha anataka awalenge wote wawili aliokuwa akicheza naye. Maneno mengine ni kama "Double Kula" aliyatumia pia. Filipatai alikuwa bingwa haswa wa kucheza Gololi. Pengine historia hiyo isiwe ya maana kwani inahusu michezo ya watoto.
Lakini Historia yake ya kuoa mke ndio inayoibua hisia mpya za huzuni nafsini mwangu. Filipatai alikutana na Mesiando Lepuruka binti mzuri wa kimasai, ambaye alikuwa mrembo asiye na shaka. Mesiando ndiye aliyemzalia Filipatai mtoto wa kiume aliyeitwa Loishoki John Filipatai. Filipatai alimuita mwanaye jina la kimasai kwani alimpenda sana Mesiando.
Wakati huo Filipatai aliendelea na harakati zake za kisiasa huku akiwinda ndege na wanyama wadogo katika mapori ya Muipo, Mvungwe, Ruvu jitengeni, na Ruvu Jiungeni, Shughuli hiyo ya uwindaji ndiyo iliyokuwa ikilisha familia yake. Aliuza nyama za Kanga, Kware, digidigi, swala na wakati mwingine alibahatika kuwinda mbogo.
Nini kilimchopata Filipatai, nini kilimsibu rafiki yangu Filipatai. Kwa kweli ni swali nisilopenda kulijibu kwani ni swali lenye majibu ya kuhuzunisha.
Misukosuko ya kisiasa ilimshindwa, mizengwe na mizinguzi ya kisiasa ilinyosha mikono juu kwake. Sasa mahasimu wake waliona mbinu ya mwisho na salama ni kuondoa uhai wake.
Wangeondoaje sasa ikiwa Filipatai alikuwa mtu shujaa, mwenye kujua mbinu chafu za adui zake. Filipatai pia alikuwa na mazindiko ya Kihehe kwani asili yake ilikuwa ni mtu wa Iringa. Wengi wa mahasimu wake walisema anakingwa na mizimu ya kihehe.
Lakini walipata wazo lililokuwa pigo la mwisho kwake. Waliamua kumtumia Mke wake ndiye huyo Mesiando.
Walimrubuni Mesiando kwa kumuahidi endapo atamuacha Filipatai na kusema Loishoki sio mwanaye bali alimsingizia basi watampa ukuu wa Mkoa. Basi kwa tamaa za Mesiando akisaidiwa na rafiki yake aitwaye Nanyori akakubali. Na ndipo akamuacha Rafiki yangu solemba na kumsimanga kwa maneno ya dhihaka.
Pengine hilo lingekuwa ni afadhali, lakini wakaona haitoshi, Mesiando alimtumia majambazi usiku, wakamfanyia uovu mkuu, wakamlawiti rafiki yangu, wakamfanyia kila aina ya mateso mpaka pale alipokufa.
Filipatai hakupigwa risasi, ila aliumizwa na kulawitiwa.
Filipatai alioa na alikuwa na mtoto mmoja aliyeitwa Loishoki.
Hayo yote niliyakumbuka nikiwa naikunja ile karatasi iliyoandikwa Historia ya Marehemu rafiki yangu Filipatai.
Tulimsindikiza Shujaa Filipatai hadi kwenye kaburi lake, huku mimi nikiwa nimeibeba ile Ibwe Likoma naam ndiyo ile Manati yake ya Mauaji. Hiyo ndiyo Historia ya Marehemu John Filipatai rafiki yake Taikon wa Fasihi.
Kaburi linafukiwa, vumbi linatimuka, anga lote linazingirwa na vumbi la kaburi huku nyimbo za mazishi zikiendelea. Hatimaye kunakuwa kimya.
Niite Taikon wa Fasihi, niliyeachiwa Ibwe Likoma, manati ya kifo.
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa Sasa Nairobi, Kenya