Historia ya Kweli ya Mwanamalundi

Manyanza

JF-Expert Member
Nov 4, 2010
9,506
14,369
👉Hii ndio historia halisi iliyoibwa na watu weupe Kisha kuitengeneza na kuifanya yao na kuitumia kwenye vitabu vyao.Kisha wakawaaminisha kwamba mtu wao alizaliwa miaka ya zamani sana,kumbe ni fake story,sasa soma hapa kisha mwambie ukweli mwanao kwamba huyu ndiye yeye,aliyekuwepo,na atayekuwepo.

👉Mwanamalundi alizaliwa kijiji cha Ng'wakwibilinga, wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza mwaka 1892. Baba yake aliitwa Bugomola na mama yake aliitwa Ngolo.

KUZALIWA KWAKE KULIKUWA HIVI

📢 Mtaalamu mmoja WA mambo ya kiroho akawaambia Bugomola na Ngolo(yusufu na mariamu) kuwa Ngolo (mariamu ) atashika mimba na atazaa mtoto wa kiume ambae atakuja kuwa mashuhuri siku za hapo baadae lakini kwa bahati mbaya Bugomola (baba/mume) hatoweza kumuona mwanaye kwani atafariki kabla mtoto hajazaliwa.

📢Habari hii ilimfurahisha sana Bugomola (yusufu)pamoja na kwamba aliambiwa atakufa bila kumuona mtoto. Mkewe pia alifurahi kusikia kuwa atashika mimba. Bugomola hakujali kifo chake sababu hata umri wake ulikuwa umeenda kidogo. Furaha yake kubwa ilikuwa ni kumpata mrithi wake.

📢Baada ya wiki kadhaa Ngolo(mariamu) alishika mimba. Mimba ilipotimiza miezi mitatu tu, Bwana Bugomola aliaga dunia bila hata kuugua. Ngolo ambae alikuwa mjane wakati huo aliilea mimba hiyo hadi ilipofikisha miezi 9.

📢Siku moja kabla Ngolo hajajifungua mtoto, wingu kubwa lilitanda angani. Mvua kubwa na yenye radi kali ikaanza kunyesha. Mtoto aliyekuwa tumboni akaruka mruko usio wa kawaida na kisha ikasikika sauti ya kitoto kutoka tumboni ikisema, "máyù nibyalage, yaani mama nizae!" Ngolo akashtuka na kuingiwa hofu baada ya kusikia sauti hiyo, hivyo akamuita mama mkwe wake na baadhi ya majirani ili nao waweze kuwa mashahidi wa sauti hiyo. Kwa bahati nzuri sauti ile ikajirudia tena na ghafla uchungu ukamshika Ngolo. Ilikuwa ni mwaka 1892 Ngolo alipojifungua mtoto wa kiume mwenye maajabu tangu akiwa tumboni mwake. Mtoto huyo akaitwa Igulu, yaani Mbingu.

📢Igulu (Mwanamalundi) alizaliwa akiwa mwenye afya njema kabisa isipokuwa tu miguu yake ilikuwa myembamba na yenye nyayo kubwa tangu alipozaliwa. Kutokana na wembamba wa miguu yake, jamii ikampa jina la utani "Mamilundi" likimaanisha "mamiguu membamba".

MIUJIZA YAKE

👉 Mwanamalundi alishafanya miujiza kwa kujirefusha kama ngongoti asiye na magongo yoyote yale na kisha akaanza kucheza huku akiwa ameficha uso wake kwa kitambaa cheusi kama kawaida yake. Wakati anacheza ngoma akiwa ana urefu wa ngongoti, baadhi ya watu walijaribu kugusa na kuifunua miguu yake ili wajue kulikuwa kuna nini. Wote waliothubutu kuigusa walikufa baada ya muda mfupi.

👉 Mwanamalundi alishawahi kunyoosha kidole kwenye pori fulani na kuwaambia wapishi waende wakakate kuni alikonyooshea kidole. Kwa bahati mbaya wakati ananyoosha kidole hicho hakujua kama ndani ya pori hilo kulikuwa kuna mifugo na wachungaji kadhaa ambao wote walikufa na kukauka kama kuni.

👉Tukio hili la kukausha miti na kuua ng'ombe na wachungaji wake lilimuudhi sana Mtemi Masanja wa III ambae aliamuru askari wake waende kumkamata Mwanamalundi haraka iwezekanavyo ili awajibishwe. Askari wa Mtemi Masanja waliogopa sana kumkamata Mwanamalundi wakihofia kufa. Iliwalazimu kumkamata tu sababu walimuogopa zaidi mtemi kuliko Mwanamalundi.

👉Kabla Mwanamalundi hajakamatwa, alijua jambo hilo lingetokea. Hivyo akaenda haraka kumuaga mama yake mzazi na kumuachia maagizo. Mwanamalundi alikamua maziwa kiasi fulani kwenye kikombe na kisha akampa mama yake na kumwambia, "Iwapo maziwa haya yataanza kuganda, ujue kuwa nipo katika hali mbaya, iwapo yataganda kabisa, ujue kuwa nimekufa!", Mwanamalundi akachukua shoka isiyo na mpini kisha akaiegamisha ukutani na kumwambia mama yake, "Iwapo nitakamatwa na kupelekwa kuuliwa, shoka hii itakuwa ikipanda ukutani nikiwa napelekwa kuuliwa, tukifika eneo nitakalouliwa, basi hii shoka itapandisha hadi mwisho wa ukuta kuonesha kuwa tumefika mwisho wa safari!" Mama yake alipokea maagizo hayo na haikuchukua muda Mwanamalundi akakamatwa na askari wa Mtemi Masanja.

👉Mtemi Masanja III aliamua kupeleka shauri hilo kwa watawala wa kizungu (Wajerumani) ili wamchukulie hatua Mwanamalundi. Uchunguzi ukafanyika na Mwanamalundi akaonekana ana hatia ya mauaji ya watu wasio na hatia. Adhabu ya kosa hili ilikuwa ni kunyongwa.

👉Katika safari hii ya kunyongwa, Mwanamalundi aliambatana na Makongoro Igana ambae alikuwa ni Mtemi wa Ilemela. Mtemi huyu alikuwa ana hatia ya kuwachapa fimbo wajerumani baada ya kupita upande usio sahihi katika njia kadiri ya utaratibu wa utawala wake.

👉Mtemi Makongoro Igana kila alipokuwa akisafiri juu ya punda, mkono wake wa kuume ulikuwa umeshika fimbo ndefu. Fimbo hiyo hutumika kumchapia kila atakaepita upande wa kuume katika safari zake. Kwa bahati mbaya wajerumani hawakujua utaratibu huo wa Mtemi Makongoro. Siku wajerumani walipopishana safarini na Mtemi Makongoro, walipita upande wa kuume wenye fimbo. Mtemi Makongoro akawachapa fimbo wazungu hao kama ilivyo jadi yake. Wazungu hao walishindwa kumvumilia, wakamkamata na kumfungulia mashtaka yaliyoamuru Mtemi anyongwe.

👉Kaliyaya ni mtu wa pili alieambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa. Huyu Kaliyaya alikuwa ni mtu alieonekana ni mwenye ushawishi mkubwa kwa watu wa jamii yake. Kukubalika kwake kulimfanya apate wafuasi wengi ambao walihofiwa kumpindua mjerumani. Hivyo wajerumani wakaona ni bora wamfungulie mashtaka ili wamnyonge kabla hajawapindua. Kaliyaya alikuwa ni mtu wa kawaida tu ila ni mwenye ushawishi na kipenzi cha watu wengi.

👉Mtu wa tatu alieambatana na Mwanamalundi katika safari ya kunyongwa ni Mtemi Italange wa Bugando. Mtemi huyu aliingia mgogoro na Wajerumani baada ya kuhodhi eneo kubwa la pwani ya ziwa Victoria na bandari zake kisha akakataa kuwapa Wajerumani. Ili kumnyang'anya utajiri huo, wajerumani wakaamua kumfungulia mashtaka ili wamnyonge.

👉Zoezi la kunyongwa lilipofika, Mwanamalundi alikuwa ndio mtu wa kwanza kuvishwa kitanzi. Kamba ilipofyatuliwa tu ili kumuua, kamba ikakatika yenyewe. Zoezi la kumuua likaahirishwa, badala ya kunyongwa akabadilishiwa adhabu.

👉Ikaja zamu ya Mtemi Makongoro Igana. Mtemi alipowekewa tu kitanzi shingoni na kisha kuifyatua kamba hiyo ili kumuua, ghafla kukatokea mfano wa sinema kwenye ukuta. Ni sinema ya kimiujiza iliyoonesha matukio ya kivita miaka ya nyuma. Askari wakageuka kuitazama sinema hiyo. Sinema haikuchukua zaidi ya dakika moja, ikaisha. Walipomgeukia yeye (Mtemi Makongoro Igana) wakaona hana kamba shingoni. Huyu nae akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu.

👉Akaja Mtemi Italange. Huyu alipowekewa kitanzi shingoni, nae pia kamba ilifyatuka. Akawekwa pembeni na kubadilishiwa adhabu. Ilipofika zamu ya Bwana Kaliyaya, kitanzi kilipofyatuliwa ili kumnyonga, hakika kitanzi kilimuua. Huyu hakuwa mwenye ulinzi wowote ule kishirikina; yaani alikuwa ni mtu wa kawaida tu.

👉Ndipo mamlaka za mjerumani zikaamuru askari wawapeleke watu hao watatu Tabora. Wakiwa njiani kuelekea Tabora, walifika Nzega na kuamua kupumzika kidogo chini ya mti mkubwa nje ya Shule ya Sekondari Chama.

👉 Askari wakijerumani wakawa wakimuuliza maswali Mwanamalundi kuhusu nguvu zake na kisha wakamuomba afanye muujiza wa mwisho kabla hajafikishwa gerezani. Mwanamalundi akawaambia askari kuwa bado ana uwezo mkubwa, hata huo mti waliopumzikia anaweza kuukausha. Aliongea maneno hayo huku akiupigapiga mti huo. Kabla hajamalizia sentensi yake kuwa anaweza kuukausha, mti ulikauka palepale na majani makavu yakaanza kudondoka. Askari wa kijerumani waliogopa sana tukio hilo.

👉Walipofika Tabora mjini, Mwanamalundi na wale watemi wawili waliunganishwa na watu wengine wenye makosa ya uhaini na uhujumu uchumi na kisha kupelekwa kisiwa cha Mafia kutumikia kifungo cha miaka mitatu.

👉Akiwa gerezani, Mwanamalundi aliwekwa chumba kimoja na mtemi Makongoro Igana. Mtemi Makongoro akamuuliza Mwanamalundi, "Hivi huna namna ya kujiokoa mahali hapa?" Mwanamalundi akamjibu kuwa kwa wakati huo hangeweza kujiokoa, ila kuna miujiza ya shoka na maziwa amemuachia mama yake nyumbani.

👉 Mtemi akamuuliza, "Una miujiza mingine yoyote?" Mwanamalundi akamwambia Mtemi Makongoro kuwa yeye (Mwanamalundi) anaweza kupanda viazi na mihogo na ikavunwa ndani ya dakika kadhaa tu na ikawa tayari kabisa kwa chakula.

👉Wakiwa kisiwani hapo, wakakubaliana kwenda ng'ambo ya kisiwa (bara) kisha wakachukue mbegu za viazi na mihogo ili washuhudie miujiza hiyo ya kupanda na kuvuna ndani ya dakika kadhaa.

👉Kwa kuwa nyakati hizo wafungwa wa visiwani walikuwa wakiachwa huru sababu hawataweza kutoroka, Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walienda mpaka baharini ndani ya kisiwa hicho. Makongoro akiwa ameshika jiwe na Mwanamalundi akiwa ameshika fimbo. Makongoro aliporusha jiwe umbali mrefu baharini, Mwanamalundi aliyapiga maji kwa fimbo na kisha maji yakajitenga na kuacha njia mpaka pale lilipotua jiwe. Walifanya hivyo mpaka walivyofika bara (mainland). Wakatafuta mbegu za mihogo na viazi na kuonesheana miujiza.

👉Kila walipokuwa wakitoroka gerezani, waliacha vivuli vyao vilivyoonekana kama watu halisi. Kuna nyakati Mwanamalundi na Mtemi Makongoro walionekana wakiwa Mwanza au Shinyanga na gerezani pia muda huohuo. Jambo hili liliwachanganya sana wajerumani.

👉Walipomaliza kifungo chao walirudishwa nyumbani kwao kwa ndege. Jamii ya Mwanamalundi ilipoona ndugu yao amerudishwa kwa ndege wakaamua kumpa jina jipya, "Ng'wenhwandege", wakimaanisha "aliyerudishwa kwa ndege". Mwanamalundi anaaminika kuwa ndie msukuma wa kwanza kupanda ndege.

👉Wakati anarudishwa nyumbani baada ya kumaliza kifungo chake, mama yake alifurahi sana. Mama yake alifurahi kwa sababu maziwa hayakuganda kwa miaka mitatu jambo ambalo lilionesha kuwa huko aliko alikuwa hai. Maziwa yalibaki katika ubora uleule kwa miaka mitatu. Shoka ilianza kuteremka taratibu kwenye ukuta kadiri Mwanamalundi alivyokuwa akikaribia kufika nyumbani. Alivyofika tu, shoka ilikuwa tayari imefika ardhini kuashiri kuwa muda wowote Mwanamalundi atafika hapo. Na ndivyo ilivyokuwa.

👉Aliporudi mtaani, Mwanamalundi hakuacha asili yake. Aliendelea kucheza ngoma maeneo mbalimbali. Mtemi Masanja ambae ndie aliesababisha Mwanamalundi kunusurika kunyongwa na hatimae kufungwa, aliamua kumfukuza Mwanamalundi katika himaya ya utawala wake. Mwanamaundi akaamua kuhamia kijiji kiitwacho Seke kwa Mtemi Mahizi ambako akiendelea kucheza ngoma na kufanya miujiza yake.

👉Akiwa Seke wilayani Kishapu ,mkoani Shinyanga; Mwanamalundi alifanya muujiza uliomuongezea heshima kijijini Seke. Wanakijiji cha Seke waliibiwa ng'ombe wengi sana na Wamasai kutoka Tabora. Wanakijiji wakataka kwenda kufuatilia ng'ombe hao usiku huo huo jambo ambalo Mwanamalundi alikataa. Mwanamalundi aliwahakikishia wanakijiji kuwa ng'ombe hao wapo salama na watarudishwa salama tu kesho asubuhi na sio usiku huo. Wanakijiji walikubali kutokana na kumuamini Mwanamalundi.

👉Usiku wa siku hiyo, Mwanamalundi akatuma nguvu zake zilizowazingira Wamasai na kisha kuwafanya wasinzie na mifugo hiyo. Hata walipofuatwa asubuhi, walikutwa wamelala fofofo. Wanakijiji wakawaua Wamasai hao na kisha wakarudi na mifugo yao. Mwanamalundi akapewa jina jingine ugenini na kuitwa "Kishosha mang'ombe nga Seke", ikimaanisha "Alierudisha ng'ombe za Seke".

👉Kuna kipindi, Mwanamalundi alivamia pori la Mtemi wa Ng'hung'hu aitwae Chalya ili achimbe mizizi fulani ya dawa. Mtemi Chalya alipata machale kuwa kuna mvamizi katika mapori yake anachimba mizizi ya dawa. Mtemi akaondoka na kuelekea kule ambako machale yalimuelekeza. Ni kweli, akamkuta Mwanamalundi akichimba mizizi ya dawa fulani. Mtemi akamuuliza Mwanamalundi, "ni kwanini umeingia katika utemi wangu bila kunijulisha?" Mwanamalundi akajibu, "Wewe ni mtemi wa watu wote ila mimi ndie mtemi wa miti yote!" Jibu hilo lilimkwaza Mtemi Chalya ambae aliamua kurudi kwenye himaya yake kwa ghadhabu na kuwaamuru askari wake wamkamate Mwanamalundi ili aadhibiwe.

👉Askari wakiwa wameambatana na Mtemi Chalya walipofika porini eneo alilokuwepo Mwanamalundi, hawakumkuta. Badala yake waliwakuta simba wengi wakiwa wamelala eneo hilo. Ilibidi watimue mbio kujiokoa wenyewe dhidi ya simba hao walioanza kuwafukuza. Walipofika kwenye himaya ya Mtemi wakiwa salama, walimkuta Mwanamalundi amemaliza kula chakula chao na anaondoka. Ilibidi mtemi amuache tu Mwanamalundi aondoke bila kumbughudhi kwa lolote.

👉Mwanamalundi alifariki mwaka 1936 kwa maradhi ya kawaida na kuzikwa Ididí Jihū huko kijiji cha Seke wilaya Kishapu mkoa wa Shinyanga akiwa ana umri wa miaka 44. Tukio la kifo chake liliitwa "hang'witulo gwa shigela" ikimaanisha "Vita ya kuwakimbia wamasai". Hii ni kwa sababu wakati Mwanamalundi anakata roho, kulitokea kishindo kikubwa kama tetemeko la ardhi. Watu wengi walikimbia ovyo kwa hofu kuwa labda wamasai wamevamia eneo lao ili kuwaua. Baada ya kishindo hicho, giza likaingia ghafla, giza ambalo hata kuku wakaanza kurudi nyumbani, fisi wakaanza kutembea mitaani wakidhani ni usiku. Hata baada ya mazishi yake, kaburi lake lilifuka moshi mwingi sana uliopanda mpaka juu mawinguni na kutengeneza giza la muda mfupi. Mwanamalundi anakumbukwa pia kwa kuweza kutembea hewani bila kukanyaga ardhi, kujibadili na kuwa kiumbe tofauti kama mnyama, ndege, majani, mti au jiwe na uwezo wake wa kutembea juu ya maji au kuwa ndani ya maji kwa muda mrefu. Mwanamalundi ni mmoja tu wa watu mashuhuri katika tawala za Kisukuma. Kuna watu mashuhuri kabla yake kama akina Níndwa, Italange na Sïta. Hawa wote walikuwa ni watu wa miujiza kama alivyokuwa Mwanamalundi.
 
Akina Moses hata Africa walikuwepo, sema tulichoshindwa ni ku document vitu tu.
Sasa mtu anakausha mti hio miujiza ni next level.
 
Hivi hizi nguvu walizokuwa nazo walizipata wapi? Na je mpaka sasa mtu ukitaka kupata nguvu za namba hii zinawezekana ama waliondoka na elimu zao zote wakatuacha mambumbumbu?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom