Haya ndiyo maamuzi ya CHADEMA | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Haya ndiyo maamuzi ya CHADEMA

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Josh Michael, Dec 6, 2009.

 1. Josh Michael

  Josh Michael JF-Expert Member

  #1
  Dec 6, 2009
  Joined: Jun 12, 2009
  Messages: 2,525
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  Na Dk. Wilbroad Slaa

  NAANDIKA makala haya kuelezea maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) ambayo mengine yanahusiana na mambo ya kupotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari katika habari na hata makala.

  Kamati Kuu ya CHADEMA ilifanya kikao chake cha kawaida Jumatano, Desemba 2-3, 2009, jijini Dar es salaam, katika Hoteli ya Keys, Mbezi, kikiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe.

  Kikao hicho kilikuwa na ajenda zifuatazo: Yatokanayo na Muktasari wa Kikao Kilichopita; Hali ya Siasa Tanzania; Tathmini ya Uchaguzi wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji; Kupanga Shughuli za Kutekeleza Mpango Mkakati wa Chama Kuelekea Uchaguzi wa Mwaka 2010; Kuthibitisha Makatibu wa Wilaya/Mikoa na Sekretariati zao.

  Nyingine ni Taarifa za Rufaa Mbalimbali za Uchaguzi wa Ndani ya Chama; Taarifa ya Zanzibar; Taarifa Kuhusu Mfumo wa Uanachama kwa Njia ya Kieletroniki (E-Membership); Taarifa ya Fedha; Uteuzi wa Bodi ya Wadhamini; Tarehe za Mikutano ya Baraza Kuu na Mkutano Mkuu; na Mengineyo.

  Yafuatayo ni maamuzi ya kikao hicho ni ambayo chama kinapenda kuwataarifu wana CHADEMA na watanzania kwa ujumla kwa kila ajenda.
  Mihtasari ya vikao vya Agosti 30, 2009 na Septemba 6, 2009 iliwasilishwa kwa Kamati Kuu na kuidhiniswa.

  Yatokanayo na vikao hivyo yalijadiliwa na Kamati Kuu ambayo, mengine, ndiyo yaliyokuwa ajenda ya kikao cha Desemba 2-3, 2009 cha Kamati Kuu.
  Taarifa ya kina ya hali ya siasa Tanzania iliwasilishwa kwenye Kamati Kuu ikiwa na sehemu kuu mbili: taarifa ya hali ya siasa kwa ujumla na taarifa ya hali ya chama.

  Taarifa hiyo itasambazwa ngazi mbalimbali za chama kwa kuzingatia itifaki na mawasiliano ya ndani ya chama.

  Kamati Kuu iliipokea, kuitafakari, kuijadili na kufikia maamuzi yafuatayo ambayo CHADEMA ingependa wanachama na umma wayafahamu: katika kipindi husika taifa limeendelea kugubikwa na migogoro na malumbano inayosababishwa na uongozi mbovu na udhaifu wa kisera na kitaasisi wa serikali iliyoko madarakani.

  Chama cha Mapinduzi (CCM) nacho kimegubikwa na malumbano ya hali ya juu yanayoashiria kufilisika kwa hali ya juu kimaadili kama tulivyoelezea kwenye orodha ya mafisadi Septemba 15, 2007.

  Kamati Kuu imejadili taarifa ya sekretariati ya uamuzi wa kutengua uteuzi wa waliokuwa maafisa wawili wa chama (David Kafulila na Danda Juju) kutokana na utovu wa nidhamu wa kukiuka maadili ya chama.

  Kamati Kuu imeamua kuipongeza sekretariati na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa, kwa uamuzi makini wa kusimamia kwa uthabiti nidhamu na maadili ndani ya chama.

  Aidha, Kamati Kuu imemtaka Katibu Mkuu kila inapowezekana kupuuza propaganda za baadhi ya vyombo vya habari zinazoendelezwa juu ya maamuzi hayo zinazolenga kujenga hisia kwamba CHADEMA ina mgogoro na mpasuko ndani ya uongozi.

  Badala yake Katibu Mkuu na sekretariati yake wajikite katika kutekeleza mikakati ya chama ya kuendelea kueneza sera mbadala za CHADEMA kwa njia mbalimbali ikiwemo ziara na kuiwajibisha serikali iliyoko madarakani inayotawaliwa na CCM kama sehemu ya mpango endelevu wa chama wa kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa kwa manufaa ya Watanzania.

  Kamati Kuu ilipokea taarifa ya tathmini ya uchaguzi wa vitongoji, vijiji na mitaa; ikajadili na kufikia maamuzi yafuatayo ambayo CHADEMA ingependa wanachama na umma wayafahamu: Kamati Kuu imebaini kuwa uchaguzi wa serikali za vitongoji, vijiji na mitaa ulifanyika kwa utaratibu wa kihuni na uliolitia aibu taifa na serikali inayoongozwa na CCM kwa kuwa ulikwenda kinyume na kanuni za msingi za kidemokrasia na haki za binadamu na hivyo kuwa uchaguzi usiokuwa huru na haki.

  Kamati Kuu imeiagiza sekretariati kuandaa taarifa ya kina kuhusu mapungufu ya uchaguzi husika ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo juu ya hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na CHADEMA kwa kushirikiana na watu wengine kuibadili hali hii.

  Kamati Kuu imetafakari kuwa pamoja na uchaguzi kufanyika katika mazingira ya hovyo kikanuni na hata kiusimamizi, kutokana na uchaguzi kuandaliwa na serikali yenyewe kupitia waziri mwenye dhamana ya uchaguzi wa serikali za mitaa, bado CHADEMA imefanya vizuri zaidi katika uchaguzi huu ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2004.

  Aidha, idadi ya nafasi ambazo CHADEMA imezipata katika maeneo mbalimbali ya nchi imepanda ukilinganisha na vyama vingine.

  Hata katika maeneo ambayo CHADEMA imetangazwa kuwa haikushinda, bado wagombea wake wamepata wastani wa juu wa kura ukilinganisha na uchaguzi wa 2004.

  Hii ni ishara ya kuongezeka kwa wanachama na kukubalika kwa chama. Aidha, katika uchaguzi huu, CHADEMA imeweza kusimamisha wagombea wengi na wengine kuzuiwa ama kuenguliwa kwa sababu za kihuni.

  Mafanikio haya yaliyopatikana katika uchaguzi uliokuwa na changamoto nyingi, yanaonyesha kwamba Watanzania wameendelea kukikubali chama kuwa ni mbadala na tumaini jipya la Watanzania kuelekea uchaguzi wa 2010.
  Kamati Kuu imeamua kulaani hatua ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza matokeo bungeni kabla ya kuwa na taarifa yenye matokeo kamili ya uchaguzi nchi nzima.

  Kamati Kuu inaamini hatua hiyo ililenga kulipotosha Bunge na kuwapotosha wananchi kama sehemu ya propaganda za serikali ya CCM kutaka kuonyesha kwamba inakubalika na Watanzania. Hivyo, Kamati Kuu inayatilia shaka matokeo ambayo yanaendelea kujumuishwa hivi sasa; kwani yanaweza kubadilishwa ili kuendana na matokeo ambayo Waziri Mkuu alishayatangaza bungeni kabla ya kupokea matokeo ya nchi nzima.

  Hivyo, Kamati Kuu inaitaka serikali kuweka hadharani matokeo yote ikiwa ni pamoja na kuyaweka katika tovuti ya serikali; matokeo hayo yawekwe kwa kila kituo cha kupigia kura na kwa kila mgombea ili umma uweze kuyapitia na kuyajadili.

  Kwa mamlaka iliyokasimiwa na Baraza Kuu, Kamati Kuu imewateua wafuatao kuendelea kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini: Silvester Masinde, Mary Joackim na Muslim Hassanali.

  Aidha, Kamati Kuu imewatea wafuatao kuwa wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini: Balozi (Mstaafu) Chistopher Ngaiza na Chacha Kiguha.
  Kamati Kuu ilipokea taarifa na kuwathibitisha Makatibu wa Wilaya/Mikoa katika maeneo ambayo vigezo vya kikatiba, kikanuni na kiutendaji vimetimizwa.

  Aidha, Kamati Kuu iliahirisha kuteua makatibu katika baadhi ya maeneo ambayo vigezo havikutimizwa na kuelekeza hatua za kuchuliwa na sekretariati kuhakikisha uteuzi unakamilishwa.

  Taarifa kwa mikoa/wilaya, ambazo makatibu na sekretariati zao zimethibitishwa na ambazo hazijathibitishwa, zitatumwa kwa mujibu wa itifaki kupitia mawasiliano ya kichama.

  Kamati Kuu iliipokea na kuijadili taarifa ya rufaa kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama katika ngazi mbalimbali na kuelekeza sekretariati ifuatilie maelezo na vielelezo vya ziada ili maamuzi yaweze kufanywa katika kikao kijacho.
  Kamati Kuu iliipokea na kuijadili taarifa ya hali ya kisiasa Zanzibar kuanzia Septemba-Novemba, 2009 yenye sehemu mbili: Hali ya Kisiasa kwa Ujumla na Hali ya Chama.

  Kamati Kuu imeilekeza Kamati Maalum ya Kamati Kuu Zanzibar kuendelea kufuatilia na kutafakari mwelekeo wa mambo na kuwasilisha taarifa kwenye kikao.

  Kamati Kuu ilipokea na kuijadili taarifa ya fedha katika kipindi cha Mwezi Septemba mpaka Novemba 2009 na kufanya maamuzi yafuatayo na kuelekeza sekretariati ifuatilie kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) taratibu za mahesabu ya vyama kukaguliwa naye kwa kuzingatia sheria mpya ya vyama vya siasa ya mwaka 2009.

  Aidha, Kamati Kuu ilielekeza kwamba ukaguzi wa mahesabu ya chama katika mwaka wa fedha uliomalizika ambao ulikuwa ukitumia utaratibu wa zamani wa kukaguliwa na wakaguzi binafsi ukamilishwe.

  Kamati Kuu ilijadili taarifa zilizojitokeza kwenye magazeti kuhojiwa kwa maamuzi ya vikao vilivyopita vya chama kumteua Mwenyekiti Freeman Mbowe kuwa mmoja wa watia saini wa hundi za chama kwa mujibu wa taratibu za fedha.

  Kamati Kuu imeazimia kwamba Mwenyekiti Freeman Mbowe, kwa wadhifa wake, aendelee kuwa mtia saini kama sehemu za usimamizi wa kifedha uliopo kwenye taratibu za fedha za chama zilizopitishwa na vikao vya juu vya chama.

  Kamati Kuu ya chama ilipokea taarifa kuhusu maendeleo ya mfumo wa uanachama kwa njia za kielekroniki (e-membership).

  Pia Kamati Kuu ilitaarifiwa kwamba baada ya namba ya simu husika 15710 kutangazwa hadharani kupitia Mkutano Mkuu wa Chama mwezi Septemba 2009, kujiunga kwa wanachama hakukuanza mara moja kutokana na changamoto zilizokuwepo katika mfumo husika zilizokuwa nje ya uwezo wa chama zilizohusu zaidi masuala ya kiufundi.

  Kamati Kuu ilitaarifiwa rasmi kuwa mfumo umeshaanza kwa wateja wa simu za mkononi za Zain na Vodacom ambao wanaombwa kuchangia ama kujiunga CHADEMA kwa kutuma ujumbe mfupi (sms) wenye neno CHADEMA kwenda namba 15710.

  Waraka na. 5 wa Katibu Mkuu kuhusu utaratibu husika umetolewa na Kamati Kuu; waraka huo umeelekeza usambazwe kwa ngazi zote za chama na kwa wanachama kwa ujumla kwa njia mbalimbali za mawasiliano.

  Pia Kamati Kuu ilipokea taarifa kwamba hakuna akaunti iliyofunguliwa na chama kwa ajili hiyo, badala yake fedha hizo zinapokelewa kwa akaunti ya wadhamini.

  Hivyo taarifa kwamba Mwenyekiti Freeman Mbowe na Mkurugenzi wa Fedha wamefungua akaunti ya CHADEMA kwa ajili ya kupokea fedha za michango ya sms hazina ukweli wowote. Zinalenga kuwakatisha tamaa wasichangie ama kujiunga na CHADEMA kwa njia hii iliyoanzishwa kwa ubunifu mkubwa.

  Aidha, taarifa ilitolewa kuwa wanaowasiliana na makampuni ya CHADEMA kwa niaba ya CHADEMA wako kwenye majadiliano na Kampuni ya Tigo kwa muda mrefu ili nayo iweze kutoa huduma husika.

  Kamati Kuu imeazimia kwamba mawasiliano yafanyike ili kuhimiza kampuni husika itoe huduma mapema iwezekanavyo kwa kuwa wateja wengi wa kampuni yao nao wangependa kupata huduma ya kuchangia ama kujiunga CHADEMA kwa njia ya simu zao za Tigo.

  Kamati Kuu ilipanga ratiba ya kikao cha Baraza Kuu ambacho kimepangwa kufanyika mapema mwakani.

  Aidha, Kamati Kuu imeandaa mapendekezo ya tarehe za Mkutano Mkuu wa Chama ambazo zitawasilishwa kwenye Baraza Kuu la Chama na kutangazwa kwa umma baada ya kupitishwa na kikao husika.

  Kamati Kuu ilipokea na kujadili mapendekezo ya shughuli za kutekelezwa kama sehemu ya mpango mkakati wa chama kuelekea uchaguzi wa mwaka 2010; Kamati Kuu iliamua vipaumbele vya chama kuelekea uchaguzi husika.
  Mikakati hiyo itawasilishwa kwa ngazi nyingine za chama kupitia mawasiliano na vikao vya ndani vya chama.

  Na katika mengineyo, Kamati Kuu imepokea kwa mshangao taarifa ya uamuzi wa serikali, kwa kushirikiana na utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kukataa kuongeza mkataba wa aliyekuwa mhadhiri mwandamizi wa chuo hicho cha umma na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu.

  Kamati Kuu imelijadili suala hilo na kuamua kulaani uamuzi wa serikali na chuo hicho cha umma kwa kuwa una dalili zote za kufanyika kwa ajili ya kumkomoa kutokana na msimamo wake thabiti wa kuikosoa serikali, kutetea umma na kuiunga mkono CHADEMA.

  Kamati Kuu imelazimika kuamini hivyo kwa kuzingatia hali ya kisiasa nchini wakati maamuzi hayo yanafanyika na uhaba wa wahadhiri waandamizi kama yeye katika chuo hicho.

  Kamati Kuu ilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini na mmoja wa waasisi wa CHADEMA, Kanali (Mstaafu), Geofrey Marealle, kilichotokea jana usiku. CHADEMA inatuma salamu za pole kwa familia ya marehemu na wana CHADEMA wote duniani kutokana na msiba huo. Salamu za rambirambi zitatolewa na Mwenyekiti Freeman Mbowe mara baada ya kutaarifiwa utaratibu mzima wa mazishi toka kwa familia ya marehemu.


  Makala haya yametolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA anayepatikana kwa barua pepe: slaa@chadema.or.tz na simu/fax: 022-2668866
   
Loading...