Hawa ni wachukuaji, si wawekezaji – Jenerali Ulimwengu | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hawa ni wachukuaji, si wawekezaji – Jenerali Ulimwengu

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Magezi, Dec 4, 2009.

 1. M

  Magezi JF-Expert Member

  #1
  Dec 4, 2009
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  Hawa ni wachukuaji, si wawekezaji – Jenerali Ulimwengu

  KWAMBA sekta muhimu kama kilimo inaweza kusahaulika, watawala wakaiweka kando, na bado wakaendelea kuwa watawala, ni jambo linaloendana na mantiki ya jumla ya mahusiano kati ya watawala na watawaliwa na pia mahusiano kati ya nchi zetu na maslahi ya wakubwa wa uchumi wa dunia. Nitaeleza.

  Kwa muda mrefu sasa, nchi zetu zimekuwa zikielekezwa nini zifanye ili zipate maendeleo ya kiuchumi. Tanzania, ambayo kwa kipindi fulani huko nyuma iliwahi kufurukuta ikitafuta njia ya kuleta maendeleo bila kulazimika kufuata maagizo ya wakubwa hao, sasa imekuwa msitari wa mbele katika kukubali kila agizo tunaloletewa kutoka Washington na London.

  Ule uhuru kidogo wa kufikiri tuliokuwa tumeujenga, hata kama ulikuwa bado haujakomaa vilivyo, sasa haupo tena. Tumeruhusu asasi za nje zifikiri kwa niaba yetu, kisha zituletee maelekezo nasi tuyatekeleze. Kwa jinsi hii uwezo wetu wa kufikiri umevizwa, na tumekubali kuhasiwa kisaikolojia kiasi kwamba hatuamini uwezo wetu wa kufikiri wala kutenda.

  Kwa njia ya kusikitisha sana, watu weupe, ambao si zamani sana tuliwaona kama watu wa kawaida na wenye akili sawa na zetu, sasa tunawaona kama miungu. Nilikwisha kueleza katika makala zangu za nyuma jinsi vitoto vidogo, ambavyo vinaonekana kama vinahitaji kuwa shuleni bado, vilivyoketi katika ofisi zetu muhimu vikiitwa “washauri wa kiufundi,” vikiwashauri mawaziri wetu na makatibu wakuu wao. Tumehasiwa kisaikolojia, na baada ya hapo kila kitu kinakuwa rahisi kwa ye yote anayetaka kututawala.

  Kuhasiwa huko kumetufanya tufike hatua ya kushindwa kutambua kilicho na thamani nchini mwetu, tukianzia na watu wetu, ambao ndiyo hazina kubwa kuliko zote: watu wanaoweza kufikiri, kupanga na kutenda, alimradi wapewe mwanya wa kufanya hivyo. Badala ya kubuni njia za kuimarisha mawasiliano baina ya watawala na watu wao ili kuchakata fikra za kitaifa kwa lengo la kupata mwafaka kuhusu masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa nchi yetu, sasa imekuwa rahisi zaidi kwa watawala wetu kupokea maagizo kutoka nje na kuwalazimisha wananchi wayatekeleze.

  Hili ninalolisema si jipya, sote tunalijua, na wala si la hapa kwetu pekee, kwani nchi takriban zote za Kiafrika zimeingizwa katika utaratibu huo. Katika mijadala na mihadhara mingi katika ujana wa rika langu tulijadili sana masuala yanayohusu ukoloni mamboleo na ubeberu. Wakati ule mijadala ile ilikuwa ni ya kinadharia zaidi; sasa ndiyo tunaona ile nadharia ndani ya matendo halisi. Tumegubikwa na ukoloni mamboleo.

  Kama kawaida, mtu aliye na nia ya kukutawala huanzia kwa kukuteka akili, na akiisha kuiteka akili yako kila anachotaka umfanyie utamfanyia, tena kwa moyo mkunjufu. Kama anachotaka ni rasilimali zako, utazitoa, tena kwa hiari, na kisha utakwenda kwake kuomba akupe misaada. Kwa jinsi hii utampa dhahabu yako yenye thamani ya mabilioni ya dola za Kimarekani naye atakupa “msaada” wenye thamani ya shilingi milioni chache tu, nawe utaridhika na kushangilia na kutangaza kwa fahari.

  Baadhi yetu tunakumbuka jinsi serikali yetu ilivyotangaza kwa furaha kubwa taarifa kwamba tumekubaliwa kuwa miongoni mwa HIPC, au kwa Kiswahili kisicho rasmi, Nchi Masikini za Kutupwa zenye Madeni Makubwa. Eti tunashangilia sifa kama hiyo, na serikali yetu inajiona imefanya kazi kubwa!
  Yote haya yanahusiana vipi na jinsi tunavyoendesha utawala wetu? Uhusiano mkubwa hapa ni kwamba wananchi wetu hawana mamlaka yo yote juu ya maisha yao na juu ya rasilimali zao. Hili nalo si jipya, na wala si la nchi yetu pekee; ni ukweli usipingika katika nchi nyingi za Kiafrika.

  Maamuzi ya kiutawala na ya kiuchumi yanafanyika katika miji mikuu, hata pale maamuzi hayo yanapohusu maisha ya watu walio kilomita elfu na zaidi kutoka miji hiyo. Mara nyingi maamuzi hayo hutokana na shinikizo la wakubwa niliowataja hapo mapema, ambao wana maslahi yao mahsusi, ambayo karibu mara zote yanakinzana na maslahi ya watu wetu.

  Aidha, mara nyingi wanaofanya maamuzi hayo yanayopora rasilimali za nchi watarubuniwa kwa kupewa “kitu kidogo”, fedha, gari au karo ya mtoto. Lakini si lazima, kwa sababu watawala waliokwisha kutekwa akili na “wazungu” watafanya wanavyoagizwa kwa sababu utaahira waliopandikizwa nao unawafanya waamini kwamba asemacho “mzungu” ndicho sahihi.

  Kadri maamuzi yanavyozidi kufanywa katika miji mikuu bila kuwahusisha wananchi wa maeneo yanayoathiriwa na maamuzi hayo ndivyo maslahi ya nchi yanavyozidi kuhujumiwa na watawala wenye ajenda za hovyo. Kimsingi watawala hawana sababu ya kuumiza vichwa vyao wakihangaika na matatizo yanayoelekea yatachukua muda mrefu mno kupata utatuzi. Nitaeleza.

  Ni kwa nini mkuu wa nchi anadiriki “kusahau” kilimo. Kilimo ni kazi ngumu, hasa kama mtawala anataka kuwaongoza watu wake waondokane na kilimo duni cha jembe la mkono na walime kwa mbinu na nyenzo za kisasa.

  Shughuli yake ni nzito. Itabidi aweke mifumo ya elimu ya kilimo cha kisasa; aandae pembejeo zilizo bora; awe na viwanda vya kutengeneza zana za kilimo za kisasa; aweke mtandao wa huduma za ugani; ahakikishe pambejeo zinafika zinakohitajiwa kwa muda mwafaka; apambane na hali ya hewa inayobadilika kila mara; akae chonjo dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu, ahakikishe mazao ya wakulima wake yana soko lenye tija, na kadhalika. Ni mambo mengi, na baadhi yake hayatabiriki.

  Taabu yote ya nini kwa mtawala anayetaka kula raha na kufurahia neema ya ukubwa? Inakuwa ni rahisi zaidi kwake kukaribisha “wawekezaji” kutoka nje, kuwasabilia migodi yenye thamani kubwa, kuwaruhusu wachimbe wanavyotaka na wakadirie wenyewe ni kiasi gani watakulipa kama pango, na siku akitindikiwa anaweza kuziendea serikali zao kuomba “msaada” wa chakula kwa sababu watu wake wana njaa kutokana na kwamba mwaka uliopita hakusimamia kilimo kwa sababu alizidiwa na shughuli ya kutia saini mikataba ya uchimbaji. Kama huo si ujuha niambie ni nini.

  Tumefikia mahali pabaya, hivyo kwamba sasa wageni wanaweza kuingia nchini mwetu na kuzungumza na watawala wawili au watatu jijini Dar es Salaam na kisha wakamegewa kipande cha ardhi ya watu bila wahusika kushiriki, na kisha tukaambiwa kwamba hao waachwe kwani ni wageni ‘spesheli”. Kuna mtu anataka kuchokoza vita, lakini ukimwambia atakwambia wewe ndiye mchokozi.

  Labda ni muhimu kuwakumbusha watawala wetu yale baadhi yetu tuliyomwambia Benjamin Mkapa akiwa Rais. Kilimo ni shughuli nzito iliyojaa ngwamba na suluba. Inahenyesha, inachosha, na wakati mwingine ni tombola, kwani hujui kama utapata ama utakosa. Lakini ndiyo shughuli ya watu wako kwa kiwango cha asilimia 80. Huwezi “ukaisahau,” na kukimbilia kwenye madini.

  Sekta ya madini haina “wawekezaji” bali ina “wachukuaji.”
  Njia moja thabiti ya kuhakikisha kwamba watawala “hawasahau” sekta muhimu kama kilimo na maeneo mengine yanayobeba maslahi makuu ya wananchi ni kuondokana na utaratibu unaotoa madaraka ya maamuzi yote makubwa na muhimu mikononi mwa watawala wa serikali kuu, na kuwapa wananchi mamlaka makubwa zaidi katika maamuzi yanayowahusu.

  Source: Raia Mwema

  Sijui kama watawala wetu wanasoma maoni kama haya na je wanachukua hatua gani??
   
 2. M

  Magezi JF-Expert Member

  #2
  Dec 5, 2009
  Joined: Oct 26, 2008
  Messages: 2,827
  Likes Received: 87
  Trophy Points: 145
  CCM ikimaliza kuuza madini na mbuga za wanyama kwa ufisadi itahamia wapi?
   
Loading...