Hatutapata suluhu ya kweli mpaka turidhiane kwanza

Hatutapata suluhu ya kweli mpaka turidhiane kwanza

Mpita Njia

Platinum Member
Joined
Mar 3, 2008
Posts
6,999
Reaction score
1,189
Wanaoshangilia siku 100 za rais Samia madarakani wasishangilie sana.

Wasishangilie sana kwa sababu kwanza kinachotajwa kuwa ni mafanikio kwa hakika ni sehemu ya utekelezaji wa mambo ambayo serikali inaoaswa kuyatekeleza.

Unashangiliaje kuwa hivi sasa watu wanapewa maiti bila kudaiwa bili hospitali wakati walioanzisha utaratibu wa kuzuia maiti wakidai bili ni hao hao ambao sasa wameamua kuziachia maiti bila kudai bili! Yaani wamelitengenexza tatizo na sasa wanatulaghai kuwa wamelitatua tatizo hilo! Na baadhi wanakuwa mazuzu na kuanza kushangilia!

Tukianza utamaduni wa kushangilia kiongozi anapotekeleza majukumu yake, kwa hakika tunaifanya kazi ya uongozi kuwa fadhila kwa wananchi. Hivi kama Serikali isingeyafanya haya yanayoshangiliwa kama mafanikio ingeonekana kuwa imefanya chochote cha maana? Tushangilie pale kiongozi anapofanya jambo la ziada.

Pili, hiki kinachoonekana kama mafanikio siku moja kinaweza kuja kuonekana kuwa ni kiini macho. Hivi sasa inaonekana kama mafanikio lakini yanaweza kutokea ya kutokea na haya yakaonekana kuwa kiini macho.

Chukulia mfano wa kilichotokea Oktoba 29. Hivi kuna mtu alijua kuwa kile tulichoringia kwa muda mrefu kama umoja na mshikamano wa taifa ni kiini macho? Kama kisingekuwa kiini macho basi tusingeshuhudia kundi fulani la watu katika nchi yenye umoja na mshikamano wakiinuka kupinga uchaguzi. Kama kisingekuwa kiini macho tusingeshuhudia kundi jingine likishika silaha na kuanza kumimina risasi kwa wananchi.

Kama umoja na mshikamano usingekuwa kiini macho tusingemsikia kiongozi akikiri hadharani kuwa “ililazimu kufanya kile kilichofanyika ili kutuliza hali ya mambo.”

Nchi yenye umoja na mshikamano haiwezi kushuhudia kilichotokea Oktoba 29.

Kwa hakika Oktoba 29 ilikua ni mvua kubwa ambayo imetuonyesha wapi dari letu linavuja. Mwanzoni tulidhani kuwa sisi ni wamoja, Oktoba 29 ikatuonyesha kuwa kuna mgawanyiko na msigano mkubwa kati yetu.

Kwa bahati mbaya, madhara ya Oktoba 29 yanazidi kuligawa taifa. Hii ni kwa sababu viongozi wameacha kutumia Oktoba 29 kama funzo na wameamua kuifanya kuwa fursa ya kisiasa.

Ukisikiliza kauli za baadhi ya viongozi utabaini kuwa kwao wao Oktoba 29 ni suala la kisiasa zaidi. Bado mpaka leo wana mawazo ya kutafuta mchawi na wanaonyesha dhahiri kuwa mpinzani wao kisiasa ndiye mchawi wao.

Baada ya Oktoba 29, pamoja na kauli hizo za kukatisha tamaa lakini tuliambiwa kuwa kuna dhamira ya kujenga upya - si majengo yaliyokuwa yamechomwa moto, bali umoja wa kitaifa uliovunjika.

Tukasikia kauli kuhusu maridhiano. Baadhi tukadhani kuwa kwa yale tuliyoshuhudia Oktoba 29, kauli hiyo ni ya dhati. Lakini miezi minne leo baada ya Oktoba 29, inazidi kudhihirika kuwa kumbe ile kauli ya maridhiano ilikuwa ni geresha tu – funika kombe mwanaharamu apite.

Leo hii bado watawala wako busy kutafuta nani alifanya nini Oktoba 29 kupitia Tume iliyoundwa.

Hivi wakimjua nani aliyefanya nini Oktoba 29 watamfanya nini? Hivi kujua nani alifanya nini au hakufanya nini Oktoba 29, itasaidia vipi kuleta maridhiano?

Mimi kwa akili yangu finyu nilidhani kuwa kabla ya kuanza kutafuta mchawi, tulipaswa kwanza kuridhiana. Tungekaa pamoja na kufanya mapatano kama taifa. Tungetoa fursa ya kila mmoja kutoa dukuduku lake, wasi wasi wake, majonzi yake, manung’uniko yake, malalamiko yake. Yote yakawekwa mezani.

Baada ya hapo mnakubaliana kuwa yaliyotokea si mazuri, bila kuanza kunyoosheana vidole mnakubaliana kuwa kuanzia sasa ebu tukubaliane kama Taifa tunapaswa kwendaje mbele.

Kama utaratibu huu utafanyika kwa dhati utabaini kuwa baada ya hapo hakuna ambaye atatembea akiwa na hofu kuwa akigeuka mwenzake atampiga rungu kisogoni – tungejenga taifa lenye kuaminiana.

Katika mazingira kama hayo hata pale ambapo hamkubaliani basi mnakubaliana kiungwana kuwa hamkubaliani na sababu za kutokubaliana zinajulikana wazi.

Njia tiliyopitia ya kuweka suala la maridhiano kwenye kabati ili kwanza tumjue nani alisababisha taifa kufikia Oktoba 29, haitatufikisha kokote kwenye mustakabali mwema. Sana sana njia hiyo itaongeza wigo kati ya pande zianzokinzana.

Bonde lililopo kuelekea maridhiani linazidi kukua wakati huu tukitafuta mchawi aliyesababisha Oktoba 29.

Hivyo, itakapofika wakati ambao viongozi wamepanga tufanye maridhiano, watabaini kuwa wogo kati ya pande kinzani umek,uwa mkubwa kuliko ulivyokuwa awali.

Kwa upande mwingine, kama tungeamua kuanza na maridhiano kwanza, serikali isingehangaika sana kutafuta uungwaji mkono kutoka nje kwani pande zote nchini zingekuwa zinazungumza lugha moja kuelekea nje ya nchi. Lakini nadhani hii ni mada ya siku nyingine.

Alamsiki…
 
Njia tiliyopitia ya kuweka suala la maridhiano kwenye kabati ili kwanza tumjue nani alisababisha taifa kufikia Oktoba 29, haitatufikisha kokote kwenye mustakabali mwema. Sana sana njia hiyo itaongeza wigo kati ya pande zianzokinzana.

Bonde lililopo kuelekea maridhiani linazidi kukua wakati huu tukitafuta mchawi aliyesababisha Oktoba 29.

Hivyo, itakapofika wakati ambao viongozi wamepanga tufanye maridhiano, watabaini kuwa wogo kati ya pande kinzani umek,uwa mkubwa kuliko ulivyokuwa awali.

Kwa upande mwingine, kama tungeamua kuanza na maridhiano kwanza, serikali isingehangaika sana kutafuta uungwaji mkono kutoka nje kwani pande zote nchini zingekuwa zinazungumza lugha moja kuelekea nje ya nchi. Lakini nadhani hii ni mada ya siku nyingine.

Alamsiki…
Kuna jambo sielewi au linanitatiza. Nimekazia neno maridhiano mara 4
Ni nini sababu ya kuwa na mardhiano?
 
Back
Top Bottom