Hatua za kupata udhamini ughaibuni (4) - makulilo, jr. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Hatua za kupata udhamini ughaibuni (4) - makulilo, jr.

Discussion in 'Jukwaa la Elimu (Education Forum)' started by MAKULILO, Feb 6, 2012.

 1. MAKULILO

  MAKULILO Member

  #1
  Feb 6, 2012
  Joined: May 30, 2010
  Messages: 84
  Likes Received: 23
  Trophy Points: 15
  HATUA ZA KUPATA UDHAMINI UGHAIBUNI (4)

  NA: ERNEST BONIFACE MAKULILO (MAKULILO, JR.)
  CALIFORNIA, USA

  View attachment 46751
  Mfululizo wa hatua za kupata udhamini Ughaibuni unaendelea. Leo hii tunaangalia Sampuli ya Maandiko (Writing Sample). Kuna maswali mengi ya kujiuliza hapa; Hiki ndio kitu gani? Umuhimu wake ni upi? Nini kinatakiwa kuandikwa humo na kwa sababu gani? Je, ni lazima kuwasilisha sampuli hiyo? Mambo gani ya kuepuka katika uandaaji wake?

  Sampuli ya Maandiko katika uombaji wa udahili na udhamini wa elimu ya juu ughaibuni ni kitu cha msingi sana. Ofisi ya udahili inazingatia hili kama kigezo kikubwa lengo kuu ni kuhakikisha wanadahili mwanafunzi ambaye ataweza kusoma, kuandika vizuri insha zake, kufanya utafiti makini wa kielimu nk. Kumbuka kuwa chuo au taasisi fulani inapoamua kutoa udhamini wake tuchukulie wanakupa dola 30,000 kwa ajili ya ada ya masomo yako ya Shahada ya Uzamili, hicho ni kiasi kikubwa cha fedha. Hivyo mdhamini lazima ajiridhishe kuwa anayepewa hela hiyo ana uwezo wa kutosha na si mtu anapewa akifika shuleni anashindwa kuonesha viwango vitakiwavyo, matokeo yake ni kuleta hasara kwa mdhamini.

  Urefu wa andiko hili hutegemea masharti unayopewa na chuo husika. Unaweza kuambiwa uandike insha yoyote kama sampuli yenye idadi ya maneno kadhaa, au si chini ya kurasa kadhaa. Hivyo usiwe mgumu kubadilika kutokana na masharti upewayo, maana ukiweka kiburi unakuwa umejitoa mwenyewe kwenye ulingo wa ushindani. Kumbuka si wewe pekee ambaye anatafuta udhamini wa elimu ughaibuni.

  Sampuli ya maandiko ni LAZIMA iwe kazi yako mwenyewe uliyoiandika mwenyewe. Ni kosa kubwa sana kuchukua kazi ya mtu mwingine na kuiwasilisha kama ya kwako. Endapo itabainika kuwa umeiba, au umechukua kazi ya mwingine na kuiwasilisha utaweza kukosa nafasi hiyo na kitaaluma unaweza kuadhibiwa vibaya sana. Ni vyema ujipange na uandike kazi yako mwenyewe. Lakini pia unaweza kuwa ulishawahi kuandika insha wakati wa shahada yako ya kwanza, unaweza kuifanyia maboresho na kuiwasilisha hiyo. Endapo kazi ni yako, si lazima uandike kitu kipya kabisa.

  Sampuli ya maandiko ina lengo kuu la kutaka kutambua uwezo wa wako wa kuandika insha za kitaaluma, na/au kufanya utafiti wa kisayansi na kuuwasilisha kitaaluma. Hii itaweza kutoa ushawishi kuwa mtu wanayetarajia kumpa udhamini huo ni mtu makini na kamwe wadhamini hawatokuja kujuta kwa kukupa udhamini wewe kwani uwezo wako ni mzuri sana. Hivyo basi tumia muda wa kutosha kupanga mawazo yako, soma vitabu vihusuvyo mada unayoandika. Usiandike ili mradi, kumbuka upo kwenye ushindani mkubwa.

  Mada unayoandika ni vyema itumie lugha ya kitaaluma kuendana na fani unayotaka kusoma. Mfano tuseme mwombaji ana Shahada ya Udaktari, ni vyema matumizi ya lugha, uchaguzi wa misamiati na sarufi ziwe za kidaktari zaidi. Itakuwa ni kituko mwombaji ni daktari na katika sampuli ya maandiko yake ametumia lugha ya kawaida mno ambayo haioneshi udaktari wake, hilo litatia walakini kama kweli mwombaji anaweza kuhimiri masomo ya udaktari. Kama wewe ni mtu wa sheria, basi tumia lugha ya sheria, na kama wewe ni mtu wa sayansi ya siasa basi lugha lazima iendane na fani husika.

  Si kila chuo kinahitaji sampuli ya maandiko uliyoandika ili waweze kuona uwezo wako wa kitaaluma. Kama chuo kinahitaji, ni lazima kiandike ni vitu gani vinahitajika mwambaji kukamilisha maombi. Ushauri wangu ni kwamba uwe umeambiwa uwasilishe maandiko haya au hujaambiwa, ni vyema uwasilishe sampuli yako. Hili litakuongezea sifa na kuwa mshindani wa nguvu na wanaofanya udahili watajua unajiamini, na wao wanataka wanaojiamini na wenye uwezo.

  Kama mwombaji umeshawahi kuandika makala ya kitaaluma na kuchapishwa kwenye majarida ya kitaaluma, au umeshawahi kuandika kitabu, ni vyema uwasilishe nakala yake kama sampuli ya maandiko yako. Mfano, mimi nilipokuwa nafanya maombi ya udahili kwa Shahada ya Uzamivu (PhD), kila wakati aidha waombe au wasiombe sampuli ya maandiko yangu, nilikuwa nawasilisha MA Thesis/Dissertation yangu. Hii ilikuwa inanifanya nionekane mshindani kwani Thesis/Dissertation ni kazi ya utafiti wa kitaaluma.

  Unaweza kutembelea tovuti zifuatazo zina msaada wa jinsi ya kuandika, kuwasilisha sampuli ya maandiko yako. Tovuti hizo ni: Grad School Writing Sample: Tips on Content, Style, Structure, Writing Samples - Applying to Graduate School na pia unaweza kwenye google na kutafuta Writing Sample utapata maelezo na kujifunza zaidi.

  Tafadhali jiunge (SIGN UP) kwenye Scholarship Forum www.scholarshipnetwork.ning.com na uweze kupata habari zaidi kwenye barua pepe yako kila siku.

  Kwa maswali, niandikie Makulilo@makulilofoundation.org  MAKULILO
   
Loading...