Kaa la Moto
JF-Expert Member
- Apr 24, 2008
- 7,903
- 1,061
Hatimaye rais ataapishwa!
Edward Kinabo
Edward Kinabo
ENYI wana wa Tanzania, mnaolia kwa uchungu wa kupewa rais msiyemtaka, yule mnayemwita rais wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), nimetafakari sana jinsi ya kuzipoza hasira zenu, nimeshindwa!
Nimeshindwa kwa sababu naujua uchungu wenu, si rahisi sana kupozwa kwa wito wa kuweka mbele amani badala ya haki. Najua hasira za kila mmoja wenu ni nzito kuliko uzito wa taifa lolote ukilibeba pamoja na watu wake. Nani awezaye kupoza uchungu kama huo? Nani awezaye angalau kufariji mioyo inayokata tamaa kama hiyo?
Nakiri tena nilitamani kulitimiza jukumu hilo lakini nimeshindwa. Kitu pekee nilichoweza ni kuuchomoa ujumbe huu kutoka kwa mmoja wa vijana wazalendo wa taifa hili, Eric Ongara.
Yeye angalau amejaribu kutoa maneno yanayoweza kulifariji taifa linaloumia. Naitumia safu hii, kuwasilisha kile Ongara alichokiandika kwenu, kama ifuatavyo:
"Enyi watu mahiri na mashujaa wa wakati wenu na kwa kizazi chenu. Poleni sana kwa harakati za uchaguzi na hongereni sana kwa kujitoa katika kila hali katika kutetea na kusimamia kile mnachokiamini.
Mungu azidi kuwajaza nguvu, ujasiri na mafanikio katika maisha yenu, kwa maana nyinyi ni watu huru ambao mnakula vilivyo halali kutokana na jasho lenu. Misukumo yenu ya kisiasa ni uzalendo na mapenzi yenu kwa nchi yetu iliobarikiwa na wala si ufisadi kama walivyo washindani wetu waovu.
Ni kweli hatimaye walio waovu, mafedhuli, mafisadi na wahuni wamepoka ridhaa yenu, wameamua kufanya uteuzi badala ya kusimamia ridhaa yenu. Haya yasiwarudishe nyuma. Sisi ni dhaifu kiasi gani hata kukatishwa tamaa na uovu?
Historia inatufundisha siku zote wema hushinda uwovu, ukweli husimama juu ya uongo na haki ya mtu haipotei. Sisi kushinda na wao kukamata mamlaka ni changamoto za kawaida katika harakati za ukombozi. Wanaye mkuu wa mamlaka lakini katika mioyo yetu yupo kiongozi wetu tumembeba na kumhifadhi.
Wana wa Israeli kule Misri kiongozi wao alikuwa Musa lakini mwenye mamlaka alikuwa Farao, kwa shurti walitii maagizo ya kikatili ya Farao, pamoja na jeshi lake lakini uhalali wa kuwa kiongozi katika mioyo ya wana wa Israeli ulibaki kwa Musa.
Makaburu waliwatesa weusi wenzetu kule Afrika ya Kusini, Botha alikuwa na mamlaka makubwa lakini katika mioyo ya wazalendo kiongozi wao alikuwa Mandela pamoja na kuwa jela.
Wakoloni walikuwa na nguvu ya kupindukia lakini kamwe hawakuweza kuteka mioyo ya Watanganyika wazalendo, kiongozi wao alikuwa Nyerere. Huko Burma leo hii utawala dhalimu wa kijeshi unamnyanyasa mwanamama mpambanaji kwa vifungo vya ndani lakini pamoja na hayo ridhaa yake haijafutika katika mioyo ya wana wa ardhi. Je, sisi ni bora kuliko wao?
Tunajifunza kutoka katika historia hizi zilizotukuka kwa wazalendo kutochoka pamoja na mateso, unyanyasaji, ubabe na dhihaka. Hata siku moja hatuwezi kumchukia mama yetu, hatuwezi isusa nchi yetu tuliyopewa na aliye na mamlaka juu ya wahuni na mafisadi.
Natambua mna hasira, dhibitini hasira zenu, tujipange………ila msisahau muda wote kuwakumbusha kuwa tunajua uhuni wao na hatukubaliani na unajisi wao kwa taifa.
Watakuwa na kauli zao za kawaida za kuwaambia tugange yajayo, yaliyopita si ndwele! Cha msingi ni kuwakumbusha kuwa tunafahamu na hatuwezi kusahau kwamba tunapambana na wezi na waovu. Tunajipanga, tutawashinda karibuni bila kumwaga damu, wala hatuchukua miaka arobaini kuelekea nchi ya ahadi.
Mungu amewajalia maarifa na vipaji vya kuzaliwa akawabariki na upendo kwa wengi wanaowazunguka. Fanyeni kazi kwa bidii, imarisheni familia zenu, mfanikiwe katika kazi zenu, mzidishiwe rasilimali na mkumbuke kujiwekea akiba na kujipanga.
Malaika wa mbinguni wanapaza sauti kuimbia na kusifia majina yenu kwa maana mmesimama upande wa haki. Msichoke, Msinyong'onyee kuweni imara kwa maana tunajipanga, unabii u-karibu kutimia. Nawapenda kama aliye juu anavyowapenda", mwisho wa kunukuu. Ahsante sana Eric.
Na ikiwa kila mmoja wetu atabaki imara bila kukata tamaa, huku akitii nasaha za rais aliyetazamiwa, Dr.Willbrod Slaa, hatimaye siku si nyingi sana lolote linaweza kutokea. Rais wa kweli hatimaye ataapishwa!
Yaliyotokea yametupa njia, tunakaribia kufika. Tuunge mkono msimamo wa Dk. Slaa wa kuyapinga matokeo feki ya urais. Tushiriki kikamilifu katika vuguvugu la kudai kuundwa kwa tume huru ya kupitia matokeo ya uchaguzi.
Tujiandae kuwa sehemu ya kupigania katiba mpya mapema iwezekanavyo maana vuguvugu hilo ndilo litakalobeba matumaini mapya ya taifa hili.
Tuweke mbele amani ya taifa letu bila kutoa fursa ya kuendelea kuporwa haki zetu. Siku ya haki yafanya hima kuja na siku hiyo ikifika hatimaye rais wa kweli ataapishwa.
Aluta continua.
Source: Tanzania Daima