Hatari ya Kuruhusu Mikopo Kwenye Biashara Changa

Hatari ya Kuruhusu Mikopo Kwenye Biashara Changa

VN Warehouse Limited

JF-Expert Member
Joined
Apr 13, 2023
Posts
763
Reaction score
985
Biashara inapokua bado changa inahitaji uangalizi mkubwa sana kuliko kipindi chochote kingine. Hiki ndio kipindi ambacho mmiliki wa biashara anajifunza mambo mengi kwa vitendo. Unaanza kutengeneza mtandao wako wa wateja, unaanza kuelewa ni bidhaa zipi zinatoka kwa kasi zaidi, na pia unapata picha halisi ya biashara yako tofauti na vile ulivyokuwa unaifikiria kabla ya kuanza.

Kwa kifupi, hiki ni kipindi cha kujenga msingi wa biashara.

Katika hatua hii, moja ya mambo yanayoweza kuathiri sana ukuaji wa biashara ni kuruhusu watu kuchukua bidhaa kwa mkopo.

Biashara changa inahitaji kuhakikisha kwamba pesa yoyote inayopatikana inarudi haraka kwenye mzunguko wa biashara. Hii inasaidia kuongeza stock, kuboresha huduma, na kuhakikisha biashara inaendelea kukua hatua kwa hatua.

Unapoanza kuruhusu watu wachukue bidhaa kwa mkopo, tafsiri yake ni kwamba unapunguza mzunguko wa fedha ndani ya biashara yako. Fedha ambayo ilipaswa kurudi haraka ili kununua bidhaa nyingine au kuendesha shughuli za kila siku inabaki mikononi mwa watu wengine kwa muda ambao hauko chini ya udhibiti wako.

Kwa maneno mengine, unajikuta unabeba mzigo wa watu wengine wakati wewe mwenyewe bado uko kwenye hatua ya kujijenga.

Athari za kuruhusu mikopo kwenye biashara changa zinaweza kuwa nyingi, mfano:

1. Kupungua kwa mzunguko wa fedha (Cash Flow).
Biashara nyingi ndogo hufa si kwa sababu hazipati faida, bali kwa sababu zinakosa mzunguko mzuri wa fedha. Ukiuza kwa mkopo sana, unaweza kuwa na mauzo mengi kwenye makaratasi lakini ukose pesa taslimu ya kuendesha biashara.

2. Kushindwa kuongeza stock kwa wakati.
Wakati wateja wengine wanakuja kununua kwa pesa taslimu, unaweza kujikuta huna bidhaa kwa sababu pesa nyingi ziko nje kwa wadaiwa.

3. Kuongezeka kwa madeni yasiyorudi.
Sio kila mtu anayechukua mkopo analipa kwa wakati, na wengine hawalipi kabisa. Hii inaweza kupelekea biashara kupoteza sehemu ya mtaji wake bila hata kutarajia.

4. Kuathiri mahusiano na watu wa karibu.
Mara nyingi wanaokopa huwa ni marafiki, ndugu au watu wanaokufahamu. Wanapochelewa kulipa au kukwepa deni, mahusiano yanaweza kuharibika.

5. Kupoteza nidhamu ya biashara.
Biashara inapokuwa changa inahitaji kuweka misingi na taratibu madhubuti. Ukianza kuruhusu mikopo hovyo, inaweza kuwa tabia ambayo baadaye itakuwa vigumu kuisimamia.

Hii haimaanishi kwamba mikopo haifai kabisa kwenye biashara. Biashara nyingi kubwa hutumia mfumo wa mikopo kama sehemu ya mkakati wa biashara.

Lakini tofauti ni kwamba biashara hizo tayari zina mtaji, mfumo mzuri wa kufuatilia madeni, na uwezo wa kuvumilia kuchelewa kwa malipo.

Kwa biashara changa, mara nyingi ni salama zaidi kuanza na mauzo ya pesa taslimu mpaka pale biashara itakapokuwa imeimarika na kupata uwezo wa kusimamia mikopo bila kuathiri uendeshaji wake.

Wadau mnaonaje hili?
Je, ni sahihi kwa biashara changa kuruhusu mikopo au ni bora kuanza na mfumo wa cash kwanza? Karibuni tushirikishane uzoefu.
 
Sio biashara changa tu.... biashara yoyote kwa hali ya sasa ya uchumi ukiendekeza mikopo ni sawa na kujichimbia kaburi ! Watu hawalipi madeni yani, wanaolipa wachache !!!!!

Bora ionekane mzigo upo, biashara ni mbaya, kuliko kukopesha uonekane unakimbiza kumbe hewa mikopo tu na si kingine... mzigo ukikata hela ya kufata mwingine huna
 
Msg sent umetoa madini muhimu cha kuongeza kidogo lazima uwe nizamu ya pesa unaweza unalipwa cash lakini mauzo na manunuzi yakawa hayalingani mwisho wa siku biashara inakuwa inashuka
 
Back
Top Bottom