Harakati za mdukuzi

dawa yenu

JF-Expert Member
Jan 7, 2014
2,825
3,673
Kichwa kiliwaka moto, kikachemka hasa. Vipele vya baridi vikamtoka huku kijasho chembamba kikimtiririka usoni, akatetemeka mwili na nafsi, mkono mmoja kiunoni mwingine mdomoni, ameduwaa! Alikuwa kwenye tafrani. Katikati ya uwanja wa medani akipambana dhidi yake mwenyewe. Akili iligoma kupokea kile ambacho macho yake yalikiona. Aliamini hata tisa huwa sita kutegemea na vile unavyoitazama, sasa alichokiona ni kipi? Ni tisa au ni sita? Huenda sio namba ni herufi, ni herufi au ni namba? Na wala haitashangaza kama haya yote ni maruweruwe tu, yote yawezekana. Tukio hili lilikuwa zito zaidi ya lile la mfanyakazi mwenzake kufukuzwa kazi takribani masaa mawili yaliyopita.

Taratibu sana kwa tahadhari kubwa akakata hatua fupi na kusogea karibu zaidi kisha akaegemea meza kubwa iliyokuwa imetandikwa kitambaa cheupe chenye maandishi mekundu, “BWANA WA MAJESHI”. Juu ya meza hiyo iliyokuwa imepambwa kwa maua ya kila aina kulikuwa na biblia ndogo ya agano la kale na pembeni yake kulikuwa na miwani ikiwa imepasuka lensi ya upande mmoja. Kwanini imepasuka? Wakati inapasuka Patrick alikuwa wapi? Ni nani kaiweka hapa? Kwanini ameiweka hapa? Ni mjadala mkali uliokuwa ukiendelea ndani ya nafsi yake. Akanyoosha mkono kivivu na kuichukua halafu akaitazama kidadisi huku akikumbuka siku ile amemsindikiza Patrick Ngome kuinunua maeneo ya Posta mpya jijini Da es Salaam. Ni miaka miwili sasa, hakika wakati unaenda kasi mno. Huku akionekana kufadhaika sana akairudisha ile miwani alipoichukua kisha akawatazama askari waliokuwa wakiranda randa huku na kule ndani ya kanisa lile. Haikuhitaji uwe mtaalamu wa saikolojia ili kujua askari wale waliongozwa na mihemko.

Katika hili Steven hakutaka kuongozwa na hisia kama wale askari bali fikra, umakini ulihitajika. Moyo wake ulikuwa mzito kusadiki kuwa alichokuwa akikiona mahali pale ni mwili wa Patrick Ngome ukining’inia kwenye kitanzi. Ni msiba ambao haukuwa rahisi kwake kuuhimili, alihisi dunia imemuangikia juu ya mabega. Muda wote akili yake ilikuwa katikati ya dhoruba kali ya maswali yasiyo na majibu. Patrick kajinyonga au kanyongwa? Vyovyote iwavyo swali litabaki kuwa kwanini iwe kanisani? Ni rahisi zaidi kujinyonga ukiwa chumbani, porini au sehemu nyingine yoyote ile lakini sio hapa. Kwanini iwe ndani ya nyumba ya ibada? Kwanini iwe ndani ya hekalu takatifu la bwana? Labda ni kweli amejinyonga lakini kwanini iwe sasa, kwanini iwe leo? Endapo kanyongwa ni nani mwenye ushahidi zaidi ya yeye mwenyewe Patrick?

Waandishi wa habari wa kitaifa na kimataifa waliendelea kumiminika eneo lile, nyuso zao zikisawiri kile kilichopo nafsini mwao, huzuni na hofu isiyomithilika. BBC, CNN, TBC, ITV, KBC hakuna herufi ambayo ilikosekana mahali pale. Walipiga picha kila tukio lililoendelea huku wakitafakari nini kimempata mwandishi mwenzao hata aamue kujiondoa uhai kwa mtindo ule wenye kuogofya. Angalau wao walisadiki walichokiona kuliko Steven ambaye hakujua kile ni nini, ni filamu? Au ni ndoto? Ni mazingaombwe? Ni nini basi? Ni wazi alikuwa vitani. Mtu aliyetoka kuongea nae kwenye simu dakika thelathini zilizopita akiwa mwenye siha njema kimwili na kiakili hivi sasa ananing’inia kwenye kitanzi, eti amekufa! Ni ajabu!

Gazeti la Darubini limepoteza mwandishi makini na hodari wa habari za uchunguzi, alikuwa ni mwandishi wa kutumainiwa katika taifa hili. Patrick Ngome, hakuwahi kuwa kasuku, alilimulika taifa kwa marefu na mapana. Kama hukumfahamu kwenye ishu ya EPA, basi ulimsoma kwenye mambo ya Escrow, au hata kwenye skandali ya Kiwira na kama bado hujamfahamu nadhani tunapaswa kutilia shaka uraia wako, lazima utakuwa Mserbia wewe. Patrick alikuwa ni zaidi ya B52 kwa mafisadi, walimuona kama kirusi cha ebola kwenye harakati zao. Uchafu wote unaofanyika jikoni aliunyaka pasipo shida yoyote na mara kadhaa aliwaacha mawaziri na uchi na kumfanya aonekane ni kibaraka wa maadui wa Taifa hili.

Ndani ya uvungu wa moyo wangu wa moyo wa Steven aliamini kuna kitu nyuma ya pazia, huenda ni kibaya kuliko hiki anachokishuhudia hapa. Wazungu wanasema, “No research, no right to talk” hakuwahi kusikia, “No research, no right to think” ndiyo, alikuwa na kila haki ya kufikiri nje ya mazoea na kwa wakati ule aliamini kuna mchezo mchafu nyuma ya ile tamthiliya! Yote haya ni mchezo wa kuigiza tu. Ndiyo hii ni bongo movie tu na siku zote Steven hakuamini katika michezo ya aina hiyo. Hata ile barua inayosemekana iliandikwa na marehemu dakika chache kabla hajajiondoa uhai nayo pia hakuiamini. Barua ni barua tu, inaweza kuandikwa na yeyote wakati wowote kwa malengo yoyote.

Niliishika kamera yake kwa umakini nikiwa ameridhika na idadi ya picha alizopiga. Kwake ile ilikuwa ni zaidi ya habari. Alitaka kuichimba kama ambavyo Patrick Ngome alikuwa akichimba katika habari zake, aliona hiyo ndiyo njia pekee ya kumuenzi.

“Steven….” Sauti nzito iliyoshiba ilimuita Seven akageuza shingo haraka. Dr Pengo akiwa ndani ya suti nyeusi alikuwa amesimama umbali usiozidi hatua tatu akimuangalia Steven kwa jicho ambalo Steven alishindwa kulitafsiri. Dr Pengo alikuwa ni mmiliki wa gazeti la Harakati ambalo Steven alikuwa ndiye mwandishi tumainiwa kwa wakati huo. Dr Pengo alikuwa ni miongoni mwa matajiri wakubwa ndani ya nchi hii akimiliki hisa katika kampuni kadha wa kadha. Alikuwa na mtandao wake mkubwa sana serikalini jambo lililopelekea aogopwe mithili ya ukoma na washindani wake kibiashara. Dr pengo hakuwa mtu safi jambo ambalo hata Steven alilijua fika. Miongoni mwa maadui wakubwa kabisa wad r Pengo alikuwa ni Patrick Ngome.

“Steven” aliita tena Dr Pengo kwa sauti ya utulivu, Steven akaongeza umakini katika kusikiliza, “Pole kwa msiba wa rafiki yako, japo ni msiba wetu wote kama taifa ila naamini umekugusa katika namna ya pekee zaidi” Aliongea Patrick huku akiweka miwani yake vizuri.

“Ahsante Doctor, asante sana” Alijibu Steven huku akijiweka vizuri zaidi.

“Aaah Steven….” Aliongea DR Pengo huku akikata hatua fupi fupi kumuelekea Steven kisha akakohoa kidogo na kuendelea, “Kutokana na ukaribu uliokuwepo baina yako na Patrick tumeona ni busara tukikupa likizo ya miezi miwili hivyo ningependa uje ofisini kuchukua barua yako ya likizo”

“Aaah ila doctor, ningependa kuendelea na kazi msiba huu hauwezi kuniathiri kiasi hicho”

“nafahamu ila maamuzi tayari yamefanyika Steven” aliongea Dr Pengo kwa mamlaka na kumuacha Steven njia panda akihisi kichwa kinamuuma. Masaa mawili yaliyopitwa kuna mwenzake kaachishwa kazi, saa hizi yeye anapewa likizo ya ghafla. Kuna nini nyuma ya haya yote?

ITAENDELEA JUMATATU.
 
Back
Top Bottom