CHAMA cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimetoa wito wa kuachiwa mara moja na bila masharti yoyote kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Wakili Tundu A. Lissu na kubainisha kuwa kukamatwa kwake kunadhoofisha heshima ya taaluma ya sheria na misingi ya haki.
Taarifa ya leo Aprili 12, 2025 iliyotolewa na Rais wa TLS, Wakiili Boniface Mwabukusi imeeleza kuwa kuendelea kushikiliwa kwake kunaashiria vitisho kwa Wanasheria na washiriki wa siasa nchini.
“Iwapo wito huo hautazingatiwa, TLS inahifadhi haki ya kupendekeza kusitishwa kwa huduma za uwakilishi wa kesi za msaada wa kisheria (dock brief) na huduma nyingine za kisheria za kujitolea zinazotolewa na TLS na Wanachama wake, kama njia ya amani ya kupinga vitendo vya unyanyasaji na mashtaka yenye mlengo wa kisiasa"——imesema taarifa hiyo
TLS imemtaka pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuhakikisha kuwa mashtaka mazito kama ya uasi yanaungwa mkono na ushahidi madhubuti na hoja za kisheria na kwamba Uongozi wa kisiasa pekee hauwezi kuchukuliwa kuwa ni kitendo cha uasi kwa mujibu wa sheria zilizopo.
"Kukamatwa kwa Wanasiasa kinyume na sheria kunaweza kusababisha upinzani na machafuko, Mamlaka zinapaswa kuchukua hatua za kisheria na za tahadhari ili kudumisha amani na umoja wa kitaifa, na kuepusha hali ya hofu miongoni mwa wanasiasa kuelekea uchaguzi mkuu”
#KitengeUpdates