Halima Mdee: Kudai haki isiyotambuliwa na watawala ni gharama kubwa

Francis12

JF-Expert Member
Sep 30, 2016
7,533
22,276
HALIMA MDEE :KUDAI HAKI ISIYOTAMBULIWA NA WATAWALA NI GHARAMA KUBWA

Haikuwa haki kwa mwanamke kupiga kura ili kumchagua kiongozi wake nchini Marekani. Hii ilisababisha mtu yeyote mwenye kudai haki hiyo aonekane ni tatizo. Mashujaa Lucy Burns na Alice Paul waliitwa magaidi.

Hajawahi kubaki salama mtu yeyote mwenye kupaza sauti kudai haki ambayo watawala hawaitambui. Uwe msafi usiye na doa, ukijiingiza kwenye kudai haki isiyotakiwa na watawala, utatambulika ni gaidi.

Ukijifanya kumkumbusha mtawala kuhusu haki ambayo hakubaliani nayo lazima ukione cha moto hata kama unazungumza huku mikono umeifunga kwa nyuma kuashiria hutaki mapambano isipokuwa amani.

Kanuni ni moja; unapoamua kudai haki ambayo unaamini ni haki, endelea kuidai mpaka mwisho. Katikati kuna maumivu mengi, kuteswa, kudhalilishwa, kutwezwa na kadhalika, lakini heshima huchukua mkondo baada ya mafanikio.

Wakati ambao nchi za Magharibi hazikuamini kama Nelson Mandela alikuwa mtetezi wa haki ya mtu mweusi nchini Afrika Kusini, alipokuwa anapambana dhidi ya ubaguzi wa rangi, aliitwa gaidi.

Hata hivyo, baada ya mafanikio ya kuwashinda Makaburu Afrika Kusini na kushinda vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, Mandela alihusudiwa na ulimwengu mzima. Waliomwita gaidi waligeuka na kumtukuza. Mandela akawa shujaa wa dunia.

Mataifa ya Magharibi yaliyomtangaza Mandela kuwa gaidi wa dunia, yalibadilika na kumtangaza Mandela kuwa binadamu mstaarabu na mwenye kuheshimika zaidi ulimwenguni.

Ni Mandela gaidi, aliyeshikwa mkono na Malkia Elizabeth II, alipokwenda kuhutubia mama wa mabunge ulimwenguni, Bunge la Uingereza, ukumbi adhimu wa Westminster.

Ni Mandela gaidi ambaye kifo chake kiliombolezwa duniani kote. Waliomwita gaidi walisitisha shughuli zao na kwenda kumtolea heshima za mwisho, pale alipofariki dunia mwaka 2013.

Kipi unakielewa hapo? Ni kwamba nyakati watawala Afrika Kusini walipokuwa hawaitambui haki ya mtu mweusi nchini Afrika Kusini, walimuona Mandela na wenzake kuwa magaidi wenye kuhatarisha amani kutokana na madai yao.

Kwa msingi huo, mataifa yaliyokuwa yanaunga mkono utawala wa kibaguzi nchini Afrika Kusini, yalimuona Mandela ni gaidi. Ndiyo maana Mandela aliwekwa kwenye orodha ya magaidi wa dunia.

Muda ulipofika wa haki ya mtu mweusi Afrika Kusini kutambuliwa na nchi hiyo na ulimwenguni kote, ndipo hadhi ya Mandela ilipobadilika kutoka kuitwa gaidi daraja la Osama bin Laden mpaka kuwa shujaa na mtu mstaraabu wa mfano duniani.

Kumbe sasa, nyakati za kudai haki ni nyakati za mdai haki kudhalilika na kuteseka. Mandela alifungwa jela miaka 27. Muda wa haki unapowadia kuchukua nafasi yake, ni hapo mdai haki hupewa heshima yake.

ALICE PAUL NA LUCY BURNS

Alice Paul na Lucy Burns wakiwa wanawake vijana warembo, waliamua kutojali urembo wao na kuanzisha harakati za kuidai Serikali ya Marekani haki ya mwanamke kupiga kura na kuchagua kiongozi aliyemtaka.

Alice na Lucy waliwaongoza wanawake wenzao kuunda chama walichokiita National Woman's Party (NWP) ambacho kilibeba sauti za madai ya wanawake kuhusu haki zao za kimsingi lakini kikubwa zaidi ilikuwa haki ya kupiga kura na kuchagua viongozi (active suffrage).

Alice na Lucy ni alama kuu ya mateso makali katika Usiku wa Gaidi (Night of Terror), Novemba 14, 1917, katika Gereza la Lorton Reformatory (Occoquan Workhouse), Virginia.

Wanawake 33, akiwemo Alice na Lucy, waliokamatwa baada kuandamana mpaka kwenye geti kuu la Ikulu ya Marekani, White House, wakipaza sauti huku wakibeba mabango yenye ujumbe kuhusu haki ya mwanamke kupiga kura, waliteswa mno.

Lucy, Alice na wenzao walianza kukamatwa Juni 1917. Hata hivyo, kila walipoachiwa walirejea tena White House na mabango yao ya kudai haki ya mwanamke kupiga kura.

Waliendelea kukamatwa mara kwa mara mpaka Novemba 1917, ndipo Novemba 14, 1917, walipoteswa katika usiku wa kihistoria. Kosa lao likiwa kumsema Rais wa 28 wa Marekani, Woodrow Wilson kuwa ndiye alikuwa mpinga haki za wanawake.

Wanawake hao walipigwa na kudhalilishwa gerezani. Walipewa mateso makali na askari magereza. Kudai haki kama mtawala haitaki ni ugaidi. Haki ya mwanamke kupiga kura, kuidai ilihesabika ni ugaidi.

Baada ya mateso ya Night of Terror, Lucy na Alice waliwaongoza wanawake wenzao kufanya mgomo wa kula wakiwa gerezani. Hatua yao hiyo ndiyo ilishitua Serikali na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu.

Hakuna haki nyepesi kuidai kama mtawala hataki kuiruhusu. Lucy, Alice na wenzao kuna kipindi walionekana wasumbufu mpaka wakahukumiwa kifungo cha maisha jela.

Pamoja na mateso, vitisho na kila aina ya usumbufu waliopata, lakini kila walipotoka jela walipambana kudai haki ya mwanamke kupiga kura.

Ni mapambano hayo yakiambatana na ushawishi mkubwa, ndiyo yaliyochochea Mabadiliko ya 19 ya Katiba (Amendment XIX) nchini Marekani, Agosti 18, 1920. Ni mabadiliko hayo yaliyowapa wanawake Marekani haki ya kikatiba ya kupiga kura.

Utekelezaji wa mabadiliko hayo ya Katiba ulikwenda jimbo moja baada ya lingine. Tennessee lilikuwa jimbo la 36 kutekeleza mabadiliko hayo ya Katiba.

Baada ya kushuhudia Tennessee wakitekeleza mabadiliko hayo, Lucy aliamua kustaafu harakati. Alisema alichokifanya kilitosha kwa ajili ya kumtetea mwanamke. Kuanzia hapo alianza kufanya kazi za Kanisa Katoliki mpaka alipofariki dunia Desemba 22, 1966, Brooklyn, New York.

Alice aliendelea na harakati za kutetea haki za wanawake mpaka alipoanza kuugua kiharusi mwaka 1974. Alice alifariki dunia Julai 9, 1977, Moorestown, Jew Jersey.

Hata wakati Alice alipochochea muswada wa haki za kiraia na baadaye kupitishwa kuwa Sheria ya Haki za Raia mwaka 1964 (1964 Cilivil Rights Act), halikuwa jambo jepesi, ila lilipopita likampa heshima.

Civil Rights Act ya mwaka 1964 nchini Marekani ndiyo iliyowezesha wanawake kupata malipo sawa na wanaume katika kazi sawa.

Alice alifungwa Uingereza kwa kuonekana gaidi, alifungwa Marekani na kudhalilishwa mara kwa mara. Hata hivyo, Alice na Lucy wameibuka mashujaa wa Marekani kwa haki walizopigania.

Mwaka 2012, Marekani ilitoa sarafu mpya ya dhahabu ya dola 10, yenye picha ya Alice, kuonesha jinsi ambavyo taifa linakumbuka mchango wake. Alice kutoka gaidi mpaka nembo ya taifa.

Kipindi cha kudai haki lazima kusota, baada ya ushindi hadhi hubadilika. Wakati wa kudai haki ni kipindi cha dhiki, mateso na kudhalilishwa, haki ikishadhihirika ni wakati wa faraja, ushujaa na utukufu.

Mandela alichomoza kutoka kuitwa gaidi mpaka nembo ya ustaarabu duniani. Haki ya mtu mweusi Afrika Kusini isingetambuliwa, Mandela asingepaa kwa utukufu duniani. Hivyo, wakati mwingine ugaidi ni tafsiri ya kuuelekea ushujaa na utukufu.

NAZUNGUMZA NA HALIMA MDEE

Ujumbe kuhusu Lucy, Alice na Mandela ni mahsusi kwa Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ambaye ameingia matatizoni na dola kwa sababu ya kauli alizotoa wakati akitetea haki ya mwanafunzi mjamzito kurejea masomoni baada ya kujifungua.

Halima aliwekwa mahabusu kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi, aliyetaka mbunge huyo awekwe ndani saa 48. Saa 48 zilipokwisha, polisi waliendelea kumshikilia Halima.

Kwanza nieleze kusikitishwa matumizi ya sheria hiyo iliyotumika, kwani ni kati ya sheria kandamizi ambazo zinapaswa kufutwa. Tanzania yenye miaka 56 tangu ipate Uhuru, haiwezekani raia wake wawe wanakamatwa kwa amri za viongozi.

Hii ni sheria mbovu kwa sababu inakinzana na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu ya tatu inayozungumzia Haki ya Usawa, ibara ya 12 mpaka 17.

Tuachane na ubovu wa sheria, turudi kwenye mada. Halima anapaswa kufahamu kuwa gharama ya kudai haki ambayo mamlaka haikubaliani nayo ni kubwa mno.

Ni kweli kuwa Serikali ilishapitisha sera ya kumpokea mwanafunzi aliyejifungua ili aendelee na masomo. Hata hivyo, Rais Magufuli amesema hakubaliani na utaratibu huo.

Rais Magufuli amesema kuwa katika Serikali yake, mwanafunzi anapopata ujauzito ndiyo basi, akishajifungua hataruhusiwa kurejea shule. Alisema kuwa katika Serikali yake hatasomesha wazazi.

Halima anapingana na hilo, anataka mtoto wa kike anapopata ujauzito achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria kisha arudishwe shule ili aendelee na masomo.

Ni hapo pa kutambua kuwa gharama za kudai jambo ambalo mtawala analiona halipo sawa ni kubwa. Unaweza kuonekana mhalifu na kuvunjiwa heshima.

Unaweza kujenga hoja nzuri lakini kwa sababu tayari unachokizungumza kinapingana na msimamo wa mtawala, hapo lazima mvutano utokee na hata mwenye kudai kuonekana mhalifu.

Kama Alice na Lucy walivyoonekana magaidi kwa kudai haki ya mwanamke kupiga kura Marekani, kitendo cha kwenda White House na mabango kilitosha kuwafanya wahukumiwe kifungo cha maisha jela.

Unapoamua kuwa mtetea haki fulani, kama mtawala hakubaliani nayo itakugharimu tu. Unaweza kutetea haki ya watu kutazama Bunge, lakini kama utawala hautaki ni gharama.

Bunge la Bajeti mwaka jana, wabunge Zitto Kabwe, Ester Bulaya, Godbless Lema, John Heche, Pauline Gekul na Halima, walifungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa sababu walitaka Bunge lioneshwe moja kwa moja na Watanzania waone.

TURUDI KWA WANAFUNZI

Suala la wanafunzi na ujauzito halipaswi kuwa mjadala leo, maana miaka mingi iliyopita mwanamke shujaa wa elimu ya mtoto wa kike nchini, Dk Maria Kamm alishaonesha mwanga na mafanikio yalionekana.

Dk Kamm ambaye ni mwalimu mkuu wa kihistoria wa Shule ya Sekondari ya Wasichana, Weruweru, alifanya kazi kubwa kumuokoa mtoto wa kike aliyepata ujauzito.

Tangu akiwa mmoja wa wanawake wa mwanzo kabisa nchini kupata shahada za chuo kikuu, Dk Kamm aliamua kujielekeza kwenye uwekezaji wa elimu kwa watoto wa Kitanzania, hususan mtoto wa kike.

Dk Kamm akiwa mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana, Machame na baadaye Weruweru, aliumizwa na watoto wa kike waliokuwa wanapata ujauzito na kufukuzwa shule, hivyo kupoteza ndoto zao.

Hapa iwe wazi kuwa katika kila msichana anayepata ujauzito kuna kipaji kikubwa kinapotea. Wapo madaktari, mainjinia, marubani, wataalamu wa kompyuta, wahadhiri bora wa vyuo vikuu na kadhakika, huishia njiani na kupoteza uelekeo kwa sababu ya kupata mimba.

Dk Kamm alikataa kuona vipaji vya watoto wa kike vikipotezwa na mimba za umri mdogo, tena nyingi zikiingia kwa sababu ya uelewa mdogo wa watoto wa kike kuhusu elimu ya uzazi na ukuaji wao wa kimaumbile.

Utaona kuwa Dk Kamm alichotaka ni kumpa nafasi ya pili mtoto wa kike ili arudi shule na kusoma kwa bidii mpaka atimize ndoto zake. Mtoto kapata ujauzito kweli, hakika amefanya makosa. Je, kwa nini asipewe nafasi ya pili?

Pamoja na yote hayo Dk Kamm alisemwa kuwa anatetea umalaya shuleni. Hata Serikali ilimpinga Dk Kamm. Alionekana mwanamke wa ajabu kupita kiasi. Mwanamke mtetea umalaya, ndivyo alivyoitwa Dk Kamm.

Leo hii, kuna wanawake wasomi wakubwa, wakihudumia serikalini na hata taasisi za Kimataifa. Wamefika huko baada ya Dk Kamm kuwapa nafasi ya pili ya kurudi shule na kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

Dk Kamm aliwajenga watoto wa kike kifikra, aliwaandaa kuwa wanawake wazuri, wenye kujiamini na kuwafanya wasijione wakosefu kwa kupata ujauzito, badala yake washike matarajio yao ya baadaye kielimu. Hakika amewezesha wengi.

Kuna wanawake wakubwa nchini wamekuwa wenye hadhi kubwa kwa sababu walipita kwenye malezi bora ya Dk Kamm. Kumbuka kuwa awali aliitwa mtetezi wa umalaya.

Ni kawaida, mwanzoni katika harakati za kutetea haki ambayo jamii au watawala hawaitambui, lazima mtetezi atapokea kashfa na maneno yenye kuumiza, lakini baada ya mafanikio ni heshima.

Leo hii, Dk Kamm anatambulika kuwa mwanamke shujaa kwa sababu aliamua kutetea haki ya mtoto wa kike kupata elimu hata baada ya kujifungua. Ushujaa wake umekuja baada ya kufanikiwa. Awali alidhalilishwa. Aliitwa mtetea umalaya.

Hata Halima nyakati zijazo ataibuka shujaa pale Taifa litakapokuwa na wanawake wasomi wakubwa waliopewa nafasi ya pili baada ya kupata ujauzito. Watakapokuwa wakitolewa mfano wanawake hao na heshima ya Halima itachomoza vizuri.

ELLEN JOHNSON SIRLEAF

Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf alikuwa na watoto wanne akiwa na umri wa miaka 19. Wakati huo alikuwa mwanamke aliyechoka na mwenye kupoteza matumaini.

Ellen alipoamua kusoma, Serikali yake ilimuwezesha, akaenda Marekani, akaibuka kuwa mtaalamu wa fedha. Akaitumikia nchi yake katika nafasi za Waziri Mdogo wa Fedha, Gavana wa Benki Kuu na sasa ni Rais.

Liberia kama utawala wao ungesema hausomeshi wazazi, leo hii Ellen asingekuwa Rais. Ellen asingekuwa Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika.

Ni uhakika kuwa wapo wanawake wengi ambao wanaweza kufanya maajabu kama watapewa nafasi ya pili. Ni uhakika kuwa kuwanyima wanawake nafasi ya pili ya kurudi shule baada ya kupata ujauzito kuna vipaji vingi hupotea.

Aliyekuwa Seneta katika Seneti ya Texas, Marekani, Wendy Davis alipewa mimba na kukatisha masomo yake ya sekondari.

Wendy alipopata nafasi ya kurudi shule alifanya maajabu mpaka akafika Chuo Kikuu cha Harvard ambako alisoma sheria. Baada ya hapo, Wendy aliibuka mwanasiasa mwenye kuheshimika sana nchini Marekani.

Ujumbe ni mmoja tu; usimchukulie poa mtoto wa kike anayepata mimba mapema. Anayo mengi ya kuifaa nchi na dunia kama atapewa nafasi ya pili shuleni.
 
cc Bw John, Mwigulu Nchemba &co.
Hebu someni hayo maneno hapo juu, na kama hamuelewi basi jina analotumia BM mara kwa mara litakuwa linawahusu kabisa bila kumung'unya maneno.
 
Kama kuna dhambi kubwa isiyosameheka no ile ya wabuge wanawake was CCM ambao waliwahi kupata ujauzito shuleni kisha wazazi wao wafanikiwa kuwarudisha darasani, lakini leo hii wako mstari wa mbele wakishangilia amri ya watoto wasirudi darasani! Inauma, inauma, inauma, sijui wamelewa mafanikio yao sasa wanawaona wenzao ni malaya? Neno Malaya si sahihi kwa watoto hawa.
 
Ndefu mno summarise....

Sent from my SM-G900F using JamiiForums mobile app
 
Swala Lauelewa ni pana,ulivyopokea wewe usitake nasi tukusapoti na Huyo mdee wako.

Sent from my TECNO-W3LTE using JamiiForums mobile app
 
Vijana na wazee wa ccm wanavaa ovyo zaidi ya hapo! By the way unajua Halima alivaa hivyo katika mazingira gani? Acha chuki we kiumbe, pigana na umaskini wako!

Sent from my TECNO-J8 using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom