Hakimu akwamisha kesi ya ‘Scorpion’

Hakimu akwamisha kesi ya ‘Scorpion’

Donatila

JF-Expert Member
Joined
Oct 23, 2014
Posts
8,274
Reaction score
25,322
pic+scorpion.jpg


Dar Es Salaam. Kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi inayomkabili Salum Njwete (31) maarufu kama Scorpion, imeshindwa kuendelea baada ya hakimu anayesikiliza shauri hilo Flora Haule kuwa na udhuru.

Kesi hiyo iliyopo katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala ilipaswa kuendelea leo kwa upande wa utetezi kutoa ushahidi wao katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi.

Wakili Mwandamizi wa Serikali Nasoro Katuga , ameiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja leo kwa ajili ya upande wa utetezi kutoa ushahidi wao katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi, lakini Hakimu anayesikiliza shauri hilo amepata udhuru hivyo, hivyo aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea.

Mbali na Hakimu anayesikiliza kesi hiyo kutokuwepo Mahakamani hapo, pia wakili wa Utetezi Juma Nassoro naye hakuwepo mahakamani hapo kutokana na kuwa na kesi nyingine Mahakama kuu.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Adelf Sachore ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 28, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kuendelea.

Hata hivyo, Agosti 2 mwaka huu Shahidi wa tisa katika kesi ya hiyo, alieieleza Mahakama kuwa mshtakiwa huyo alikiri kosa la kumjeruhi Saidi Mrisho, wakati akihojiwa kituo cha Polisi Buguruni.

Akitoa ushahidi wake katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi, Shahidi huyo F 1092 D/CPL Brayson kutoka Kituo cha Polisi Buguruni , alidai kuwa licha ya kukiri shtaka la kumjeruhi Mrisho, Njwete alikana shtaka la unyanganyi wa kutumia silaha.

Hata hivyo, Mahakama hiyo iliamua kusikiliza kesi hiyo ndogo baada ya kuibuka ubishani wa kisheria kati ya upande wa mashtaka na utetezi, kuhusu uhalali wa maelezo ya onyo ya mshtakiwa.

Upande wa Mashtaka ukiongozwa na Katuga umeiiomba mahakama kupokea maelezo ya onyo kama kilelelezo, lakini wakili wa Scorpion, Juma Nassoro amepinga maelezo hayo kupokelewa Mahakamani hapo kwa madai kuwa mteja wake hakuyatoa kwa ridhaa yake.

Pia wakili huyo wa utetezi alidai maelezo hayo yamechukuliwa kinyume cha kifungu cha 57 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambacho kinaelekeza maelezo ya mshtakiwa yaandikwe kwa mfumo wa swali na jibu.

Akijibu hoja hizo za pingamizi, Wakili Katuga alidai kuwa utaratibu wa kuchukua maelezo ya mshtakiwa unapatikana katika kifungu cha 57 na 58 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai(CPA), hivyo maelezo ya mshtakiwa hayawezi kukataliwa kama yalichukuliwa chini ya kifungu cha 57.

“Askari ambaye ni mpelelezi anaweza kumhoji mshtakiwa kwa kutumia mfumo wa mtiririko au kwa njia ya maswali na majibu, kupitia kifungu cha 57 na 58 cha CPA”

Kutokana na mvutano huyo, Hakimu Haule alisema mahakama imepitia hoja za pande zote mbili na kuona kuwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa yalichukuliwa kwa kufuata sheri.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom