Haki na utu zimefukiwa, ubinafsi unatamalaki taifa likitapatapa

kindikwili

JF-Expert Member
Oct 5, 2016
1,862
2,871
Wakuu kwa heshima na taadhima nawasalimu wote kwa unyenyekevu mkubwa sana!

Ndugu zangu kama umewahi kumuona mtu anayetaka kufa kwenye maji , mtu aliyezidiwa na maji unaweza kujua maana ya neno kutapatapa. Kama tunavyojua mtu akitaka kufa lazima ajitahidi kujitetea lakini ndani ya maji hilo ni sawa na bure maana maji hayashikiki.

Utajiri na maendeleo makubwa katika familia na nchi bila UTU ni sawa na bure, familia au nchi ambayo watu wake hawana utu ni familia au taifa la watu wanaotapatapa inayokaribia kuzama. Mtu asiye na utu ni mtu hatari sana, ni mtu asiyejali maisha na uhai wa mwingine, yuko tayari kumbaka mtoto, kulawiti, kula rushwa, kuiba, kuua, kutumia madaraka yake vibaya kuumiza wengine, kutesa wengine, kufunga watu bila makosa, kuonea masikini, wajane na yatima. Mtu asiye na utu na mnyama wanatofautiana umbile tu ila tabia yao ni moja.

Cha kunishangaza ni kwamba makanisani injili imebadilika sana, waamini huubiriwa mafanikio, utoaji na maendelea ya kimwili kuliko utu. Huko siku hizi ni kushindanisha sadaka kati ya jumuia na jumuia, kigango na kigango au parokia na parokia. Kwa wenye usharika nako hivo hivo ni kushindanisha usharika, wamama na wababa na kule kwenye MINISTRIES hali ni mbaya zaidi.

Huko somo la matoleo limepewa kipaumbele kuliko hata injili yenyewe ikifuatiwa na uponyaji, upako iambatanayo na chumvi, vitambaa, maji , keki na chochote kinachoweza kutumika kuleta upako. Utu ,uadilifu na uungwana hufundishwa kwa uchache sana kanisani. Madhehebu yanashindana kujenga shule, hospitali na uwekezaji wa kila aina, si kwamba kufanya hivyo ni vibaya ila WITO NAMBA MOJA WA KANISA NI KUVUA WATU KUTOKA KWENYE DHAMBI NA MAUTI KWENDA KWA MUNGU.

Katika kuvua watu elimu, afya na mengineyo ni mambo muhimu ila injili inapaswa kupewa nafasi ya kwanza. Makanisa yakemee dhambi kwa nguvu na sauti isiyochoka bila kujali inatendwa na nani mwenye nafasi gani katika jamii. Utu, haki na ubidamu usisitizwe na anayefanya kinyume na hayo aonywe hata akiwa anatisha kama shetani.

Familia zetu kwasasa hawafundishi watoto kuwa na utu, upendo kwa watu na kuheshimu kila mtu badala yake wazazi ndiyo hufundisha watoto ubinafsi na kujijali wao kwanza. Si jambo la kushangaza kwa sasa mama mjamzito wa miezi 9, mlemavu, mzee au mama mwenye mtoto mchanga mngongoni kusimama kwenye gari umbali mrefu huku vijana wa kike na kiume wakiwa wanachati wakiwa wamekaa kwenye seat hawana muda.

Utu umeisha katika jamii zetu maana mtoto wa mwenye uwezo anachukuliwa na gari yeye na dereva tu kwenda shule halafu kuna mtoto wa masikini pembeni yake anaenda kung'ang'ania dala dala hata lift hawezi kupewa. Familia zimekuwa sehemu hatari ambako watoto hulawitiwa, hubakwa, huteswa, wazazi wako busy na kazi na kutafuta maisha kuliko familia.

Kwingineko viongozi wa kisiasa nao nafsi zao zinawasuta kuhubiri kuhusu haki, utu, upendo, uvumilivu kwasababu wako mbali na hayo wamebaki kuhubiria watu kulinda amani. Wameona wapi asiye na utu akijali kuhusu amani ya nchi? amani ya nchi itatoka wapi kama hakuna haki, kama hakuna usawa na kama watu wanaungua ndani ya roho zao?

Hata wanaopata ujasiri wa kusema kuhusu utu nafsi zao zinaungua moto maana matendo yao ni mbali sana na maneo yao. Wako radhi kufanya chochote ili watimize malengo yao, wameweka uongo na hadaa mbele wakijifanya wenye haki mbele za watu wanaojua fika tabia na mienendo yao sema kwa unafiki watu wanawachekea.

Ndugu zangu huwezi kwenda mbinguni kwa meneno tu kama ambavyo huwezi kuwa mzalendo kwa maneno au kuwa na amani kwa maombi tu. Lazima familia zetu, madhehebu na viongozi wa dini pamoja na wanasiasa kuonesha utu kwa wengine, kuwa waadilifu na kuwa wazalendo wa kweli. Bila haki, bila uadilifu, bila utu na bila uzalendo wa dhati nchi yetu, familia zetu na taifa letu litaangamia.

NB: Motivational speakers, viongozi wa dini, wazazi na wanasiasa, waalimu fundisheni watu kujua utu ni nini, faida zake na hasara za kukosa utu katika jamii. Mali, madaraka na mafanikio bila utu ni sawa na bure. Fundisheni watu kuheshimu haki za wengine ili amani ijengwe kwenye msingi imara.

Kindikwili
 
Back
Top Bottom