Nikajibu, ‘’Naam, nimethubutu. Sikiliza! Dakika hizi unazopoteza kwa ajili ya hasira zako za bure, zaweza kulipoteza taji lako, na maisha yetu pia.
Wapanda farasi wa Sorais wamekwisha kwenda kukusanya jeshi. Katika muda wa siku tatu. Nasta atajiamsha katika milima yake kama simba wakati wa jioni, na ngurumo zake zitasikika katika nchi ya kaskazini.
Sorais ana sauti tamu, naye hataitumia bure. Bendera yake itachukuliwa toka mlima mpaka mlima, na toka bonde mpaka bonde, na askari wataifuata kama mavumbi yanayofuata chamehela.
Nusu ya jeshi zima la nchi watamfuata na katika kila mji na kijiji makuhani watawasengenya wageni, nao watafanya vita hivi viwe vita vya kidini Nimesema Ee Malkia.’’
Nyleptha alikuwa ametulia sasa, hasira yake na wivu ulikuwa umitulia, akajibadili kabisa kwa haraka, na sasa si mwanamke Yule mwenye wivu tena ila ni Malkia mwenye kuweza kazi na matendo.
Akasema, ‘’Maneno yako, Ee Makumazahn, ni ya busara. Nisamehe upuuzi wangu mahaba ni kama umeme. Ni mzuri mno nao huunganisha dunia na mbingu, lakini ole wetu, namna unavyoyapofua macho. Nawe unafikiri kuwa dada yangu Sorais atafanya vita nami. Basi, na afanye.
Hatanishinda ng’o. mimi pia ninao rafiki zangu na wafuasi wangu. Wako wengi watakao ziinua sauti zao na kuita ‘Nyletpha’, bendera yangu itakapotwekwa, na mioto yangu itakapowashwa karibu milima usiku huu kuwajulisha habari za vita vyangu.
Nitazivunja nguvu zake na kuwatawanya askari zake, na sehemu ya Sorais, ‘bibi wa usiku’ itakuwa usiku wa milele. Nipe karatasi na wino.
Asante. Sasa mwite mkubwa wa zamu, najua ni mtu mwaminifu.’’
Nilifanya kama alivyo niambia, na mkubwa wa zamu, mzee mtulivu jina lake Kara aliingia, akajiinamisha kwa heshima.
Nyleptha akampa karatasi ile akamwambia, ‘’Twaa hati hii, ni nguvu zako, weka watu kulinda kila mahali pa kutokea na kuingilia vyumbani mwa dada yangu Sorais, ‘bibi wa usiku.’ Watu wasipewe ruhusa kutoka wala kuingia, au maisha yako yatatozwa.’’
Yule mtu alishangaa mno, lakini hakusema neno ila ‘’Neno la Malkia litimizwe .’’ Akaondoka. Kisha, Nyleptha akatuma mtu kumwita Sir Henry , akaja anaona haya nyingi. Nilifikiri labda Nyleptha ataanza tena maneno yake ya wivu, lakini hakumtaja.
Basi, halafu kidogo, Yule mkubwa wa zamu aliyetumwa, akarudi kupasha habari ya kuwa Sorais amekwisha ondoka. Alikuwa amekimbilia hekaluni. Basi, hapo tukaanza kufanya mashauri.
Majemadari waliojulikana kuwa ni waaminifu wakaitwa, wakaambiwa habari, si zote, ila zilizotosha kufahamu mambo jinsi yalivyo, wakaamrishwa kukusanya watu wa vikosi vyao kadiri walivyoweza.
Nyleptha akawaambia wakuu wengine alioweza kuwatumaini, na wengine wao walitoka siku ile ile kwenda mahali pa mbali kuwakusanya wafuasi wao na watu wa makabila yao.
Basi, mchana kutwa na jioni tulifanya kazi ya kutuma matarishi huko na huko, wala hatukurudi vyumbani mwetu mpaka saa mbili za usiku. Kabla ya kulala, Sir Henry akafikiri ni vizuri kumwambia Umslopogaas alinde zamu karibu na chumba cha Nyleptha.
Umslopogaas alikuwa anajuana na watu wote wa jumbani, na Malkia walikuwa wamekwisha toa amri aruhusiwe kwenda popote apendapo, akazoea kutembea tembea usiku, kwa hiyo, hata kama akionekana anatembea karibu na chumba cha Malkia, watu hawatashuku jambo.
Basi, alilitwaa shoka lake, akaondoka, na sisi tukalala.
Ilikuwa kama kwamba nimelala dakika chache tu, nikaamshwa kwa kuona kama mambo si sawasawa.
Niliona kama kwamba yumo mtu chumbani ananitazama, mara ile niliketi kitandani, nikastajabu kuona kumekwisha pambazuka, na karibu na kitanda changu, Umslopogaas amesimama kama kivuli.
Nikamuuliza, ‘’Je, umesimama hapa kwa muda gani?’’
Akajibu ‘’Kadiri ya nusu saa Makumazahn.. nataka kusema nawe.’’
Basi, mara ile nilikuwa macho kabisa, nikamwambia aseme maneno yake.
Akasema, ‘’Kama nilivyoambiwa usiku, nilikwenda kulinda zamu karibu na chumba cha Malkia, basi nilijificha nyuma ya nguzo katika chumba kilicho karibu na chumba cha kulala cha Malkia, nikangoja.
Bougwan (Bwana Good ) alikuwa peke yake katika chumba cha zamu, na nje ya chumba askari mmoja wa zamu alikuwa amesimama.
Nikataka kujua kama ninaweza kupita bila kuonekana, nikaweza, nikapita nyuma yao. Basi, hapo nilingoja saa kadha wa kadha, ndipo ghafla niliona mwanamke anakuja ameshika kisu mkonononi mwake.
Tena nilimwona Bougwan amevivua viatu vyake anamfuatia Yule mwanamke. Yule mwanamke alipita karibu nami, nikamwona alikuwa ‘Bibi wa Usiku,’ Basi, nikangoja, na Bougwan naye alinipita pia.
Basi, vivyo hivyo tuliendelea pole pole kimya kabisa. Wa kwanza Yule mwanamke, wa pili Bougwan na wa tatu mimi, ila Yule mwanamke hakumwona Bougwan, na Bougwan naye hakuniona mimi.
‘’Basi, ‘Bibi wa Usiku ‘ alifika mpaka katika pazia la chumba cha Malkia Nyleptha, akapita ndani na Bougwan alimfuatia, na mimi niliwafuatia.
Mwisho wa chumba ni kitanda cha malkia, na Malkia alikuwa amelala usingizi.
‘Bibi wa Usiku’ alijikunia hivi na huku ameshika kisu tayari, akanyemelea mpaka kitandani pa Malkia. Alipokikaribia sana, Bougwan akamgusa mkono, na mara ile aligeuka akampiga kisu.
Kwa bahati Bougwan alikuwa amevaa deraya chini ya nguo zake, ama sivyo angalimzuru. ndipo Bougwan alipomtambua Yule mwanamke yu nani, akarudi nyuma ameshangaa asiweze kusema neno.
‘Bibi wa Usiku’ naye alishangaa, asiseme neno ila alikiweka kidole chake midomoni pake, akarudi , akapita katika pazia, na Bougwan alimfuatia.
Basi, hivyo walipita, nikamsikia Yule mwanamke kama anamsihi, nayeye anajibu, Hapana! Hapana! Hapana.
Nikaona kuwa anataka kuwaita askari wa zamu, lakini Malkia Sorais aliacha kusema, akamkazia macho yake makubwa, nikaona ya kuwa Bougwan ameshindwa kujizuia kwa uzuri wake.
Kisha aliunyosha mkono wake na Boungwan aliubusu, nikajifanya tayari kumkamata, mara! Akatoweka.’
Nikasema, alitoweka?’’
Akajibu, ‘’Ndiyo, na Boungwan alisimama akimtizama ukutani kama kwamba ameshikwa na jinamizi la usingizi. Kisha, naye pia akaenda, na mimi nikaja hapa.’’
Nikamuuliza, ‘’Una hakika Umslopogaas ya kuwa hukua unaota ndoto ya mambo hayo?’’
Akaufumbua mkono wake, akanionyesha kipande cha chuma cha bapa la kisu, kadiri ya inchi tatu, akasema, ‘’Makumazahn, kama niliota ndoto, basi, tazama kitu nilichopewa kwenye hiyo ndoto.
Kisu kilivunjikia katika deraya za Bougwan, na nilipopita nilikiokota hiki katika chumba cha kulala cha Malkia Nyleptha.’’