Hadithi ya umslopagaas

Naaam
 
SURA YA KUMI NA MBILI


Kile chombo kilichoendeshwa kwa makasia kilikuwa kinakimbia sana hadi kufika karibu na chini ya ile ngazi kuu.

Hapo Yule mzee aliteremka pwani akatuashiria tuteremke.
Hatukuwa na njia nyingine ila kutii, tena kwa kuwa tulikuwa nusura kufa kwa njaa, tulimtii bila kusita, lakini tulizichukua bunduki zetu pamoja nasi.

Tulipokuwa tukiteremka, Yule kiongozi wetu alijiinamisha na kuweka vidole viwili juu pa mdomo wake ili kutusalimu, na huku akawaamrisha watu wote waliokusanyika kututazama warudi nyuma watuachie nafasi.


Aliyekuwa wa mwisho kutoka katika mtumbwi ni Yule mwanamke tuliyemtoa katika maji, ambaye mwenzake alikuwa anamngojea, kabla hajaondoka alikuja akanibusu mkono yangu, nikafahamu anataka kunishukuru kwa kumwokoa katika hatari ya Yule kiboko. Ikaoneka kwamba hofu imekwisha mwondokea.


Mara tulipoteremka kando ya ziwa, mabaharia wengine katika wale waliopiga makasia ya chombo kile, waliibeba mizigo yetu, wakaanza kupanda nayo katika ngazi ile kubwa, na kiongozi wetu alituashiria ya kuwa tupo salama.

Kisha aligeuka upande wa kuume akatuongoza katika nyumba, ambayo baadaye tulipata kujua ni nyumba ya wageni.

Tuliingia katika chumba kikubwa tukaona chakula kimeandaliwa tayari. Basi, kiongozi alituashiria tukae mezani.

Wala hatukungoja atukaribishe tena, ila tulikaa tukaanza kula kama watu wenye njaa walavyo, Chakula kilipakuliwa, katika sahani za mbao.

Tulikula nyama baridi ya mbuzi iliyofungwa katika majani ya namna yaliyoifanya iwe na ladha nzuri sana, na mboga ya namna, na mkate mweusi; tena tulikunywa divai katika vikombe vilivyotengenezwa kwa pembe za wanyama.


Basi, baada ya kukaa na kula kwa muda wa dakika ishirini tuliondoka kama kwamba tu watu wapya.

Baada ya mambo yaliyotupata, tulikuwa na haja mbili, ndizo chakula na kupumzika, na chakula peke yake kilikuwa kama Baraka kwetu.

Vijana wawili wanawake wazuri walitungojea mezani, nao walituhudumia vizuri sana.
Wote wawili walivaa mavazi ya namna ile niliyokwisha eleza.

Basi, mara tulipokwisha kula, mzee kiongozi wetu ambaye wakati huo wote alikuwa amesimama, alitutazama akamwashiria Bwana Good ambaye alimfikiria ni mkubwa wetu kwa ajili ya mavazi yake mazuri, akatuongoza chini ya ngazi ile kubwa.


Hapo tulisimama kidogo ili kustaajabia sanamu mbili za simba zilizochorwa kwa mapande makubwa ya marumaru nyeusi, moja upande huu wa chini ya ngazi na moja upande huu, Sanamu hizo za simba ni kazi ya ustadi mno, husemwa zilichorwa na Yule mfalme mkuu Rademas aliyeijenga ile ngazi kuu.


Kisha tuliipanda ile ngazi ya ajabu na huku tunaishangilia. Hata Umslopogaas ambaye amezoea kutodhihirisha ushangao wake, alishtuka akauliza kama ‘’ngazi hii ilijengwa na wanadamu ama mashetani.’’

Basi, tulipanda sehemu ya kwanza ya ngazi, yaani vipangalio mia moja na ishirini na vitano, tukapita katika daraja kubwa kidogo lililoziunganisha sehemu zake mbili, tukasimama kidogo kustajabia nchi tuliyoiona chini yetu imepakana na kando ya ziwa la maji yenye rangi ya samawati.

Kisha tulipanda sehemu ya pili mpaka kufika juu kabisa, huko tuliona kiwanja chenye milango mitatu.

Milango miwili ilikuwa ya kuingilia njia nyembamba iliyozunguka nje ya ukuta wa jumba na kuteremkia mjini.

Njia hiyo hutumiwa na watu waendao bandarini. Milango hii ni ya shaba nyeusi, na sehemu ya njia iliyo karibu nayo inaweza kuteremshwa na kuacha nafasi wazi, ili kuzuia adui wasipite.

Mbele ya mlango wa tatu, ambao ulikuwa wa kuingilia ukuta wa jumba, palikuwa na ngazi nyingine yenye vipandio kumi vya marumaru nyeusi.

Ukuta wa jumba ulikuwa kazi ya sanaa kabisa, Ulijengwa kwa mapande makubwa ya mawe magumu na kimo chake kilipata futi arobaini na uso wake ulikuwa na uvungu, kwa hiyo haukuweza kupandika.

Basi, kiongozi wetu alituongoza mpaka mlango huo wa tatu, Mlango huu ni wa mbao nzito sana, na mbele yake uko mlango mwingine wa shaba nyeusi, ambao ulikuwa umefungwa lakini tulipoukaribia mara ulifunguliwa wazi, tukakuta askari wa zamu amesimama.

Silaha zake zilikuwa mkuki mzito uliofanana kidogo na singe, na upanga, naye alikuwa amevaa vipande vya ngozi ya kiboko vilivyotengenezwa vizuri, kifuani na mgongoni, tena, alikuwa ameshika ngao ya ngozi ya namna ile ile.

Upanga wake ulituvuta macho yetu, maana ulikuwa wa namna ile ile ya ule alioupata Bwana Mackenzie kwa Yule maskini msafiri.

Basi, ilidhihirika ya kuwa Yule mtu alikuwa amesema kweli. Kiongozi wetu alitaja neno ili aruhusiwe kupita mlangoni, na Yule askari aiitikia kwa kupiga mpini wa mkuki wake chini kwa kishindo, tukapita mlangoni tukaingia katika ua wa jumba.


Ua ulipata kadiri ya upana na urefu wa yadi arobaini, nao ulikuwa umetengenezwa kama bustani nzuri ya miti midogo na maua.

Njia pana ilipita katikati ya ua, tukaifuata njia hiyo mpaka tukafikia mlango mwingine wenye tao juu lililotundikwa pazia zito, tukapita katika kichochoro kifupi tukaingi katika sebule kubwa ya jumba.

Tukastajabu tena kuona jinsi ilivyo nzuri ajabu, urefu wa sebule ni futi mia moja na hamsini, na upana wake ni futi themanini, na dari yake ni kuba la mbao zilizotiwa nakshi.

Mwisho wa sebule iko sanamu ile niliyotaja iliyotengenezwa kuwa ukumbusho wa kazi aliyofanya mfalme Rademas kuijenga ile ngazi kuu, na tulipopata nafasi kuitazama vizuri, uzuri wake ulitufanya kuwa kama mabubu.

Katikati kabisa ya sebule kulikuwa na mwamba wa marumaru nyeusi uliofanana kidogo na kiti.

Baadaye tulipata habari kuwa mwamba huu ni mwamba mtakatifu wa taifa hilo la ajabu, na wafalme huweka mkono juu yake waishapo kutawazwa, na kuapa kwa jua kuulinda ufalme na kuzihifadhi desturi na mapokeo na sheria zake.

Tuliambiwa habari za ubashiri wa kigeni juu ya mwamba huo, yaani utakapovunjiliwa mbali, mfalme wa taifa geni ataitawala nchi.

Mwisho wa sebule kulikuwa kuna namna ya jukwaa lililotandazwa mazulia mazuri, na viti viwili vya kifalme vya dhahabu tupu vilikuwa vimewekwa pamoja juu yake.

Viti hivyo vilikuwa vimetiwa matakia mazuri, na sehemu za kuegemeza migongo zilizochorwa sanamu ya jua linalotoa miali yake huko na huko kila upande.

Sehemu ya chini ya kuwekea miguu ni sanamu mbili za simba waliolala, na macho yao ni vito vyenye rangi ya kimanjano.
 
Sebule iliangazwa kwa madirisha membamba mengi yaliyokuwa juu sana ukutani, lakini hayakutiwa vioo.

Basi, ndivyo ilivyokuwa ile sebule kubwa ya jumba tuliyoiona, lakini hatukujua mambo hayo yote mpaka baadaye, maana hatukupata nafasi nyingi kuiangalia wakati huo, kwa sababu tulipoingia tuliona wanaume wengi wamekusanyika mbele ya viti vile vya kifalme ambavyo vilikuwa vitupu.

Watu wakuu katika hao walikuwa wamekaa katika viti vya nakshi vilivyowekwa vingine upande wa kuume na vingine upande wa kushoto, lakini viti havikuwekwa mbele ya viti vile vya kifalme.

Watu hao walikuwa wamevaa namna ya magwanda meupe yenye nakshi za rangi mbalimbali, na walikuwa na panga zilizotiwa temsi za namna ya ule nilioutaja.

Wote walioneka kama ni watu wenye maraja ya juu na nyuma yao wafuasi wachache walisimama wawangojee.

Kwa upande wa kushoto wa viti vya kifalme watu sita wa namna nyingine walikuwa wamekaa pekee yao.

Nao badala ya kuvaa shuka walikuwa wamevaa namna ya kanzu ndefu nyeupe za katani na kifuani zilipambwa kwa sanamu ya jua kwa nakshi ya zari, kama zile zilizochorwa katika viti vya kifalme.

Kila mmoja wao alikuwa amevaa mahazamu yenye vipande vya dhahabu kama magamba ya samaki vilivyoning’inia, vikang’aa katika mwangaza wa jua na kufanya sauti kila walipojongea.

Watu hao wote walikuwa wazee kidogo walionekana kuwa ni wenye fikra, na nyuso zao zilikuwa za namna nyingine, na tofauti baina yao na watu wengine ilizidi kwa sababu walikuwa na ndevu ndefu sana.

Lakini mtu mmoja katika watu hao aliyevuta macho yetu kuliko wengine. Alikuwa mzee sana, apata miaka themanini au zaidi, mrefu sana na ndevu zake zilikuwa nyeupe kabisa zilizofika mpaka tumboni.

Uso wake ulikuwa mkali, na macho yake yalikuwa ya kijivu na baridi sana tena yana sisimua kabisa.

Watu wote wengine walikuwa vichwa wazi, ila yeye alikuwa amevaa kofia iliyonakshiwa kwa zari, na kwa hiyo tulifikiri haikosi ni mtu mwenye cheo kikubwa.

Na baadaye tulipata kujua ya kuwa ni Agon, kuhani mkuu wa nchi hii. Tulipokaribia wote na makuhani pia, waliondoka katika viti vyao wakajiinamisha kwa adabu, na huku wameweka vidole viwili mbele ya midomo yao kutusalimu.

Kisha watu wengine walitoka nyuma ya nguzo za sebule, wakaleta viti wakavipanga mstari mmoja mbele ya viti vya kifalme.

Tukakaa katika viti hivyo, ila Umslopogaas alisimama nyuma yetu. Mara tulipokaa tulisikia sauti ya panda ikitoka upande wa kuume, kisha sauti nyingine ya panda ikatoka upande wa kushoto.

Kisha mtu mmoja aliyeshika fimbo ya pembe nyeupe alisimama mbele ya kiti cha kifalme cha upande wa kuume.

Akasema maneno kwa sauti kubwa, na neno la mwisho ni Nyleptha, akalitaja mara tatu; kisha, mtu mwingine kama Yule akasimama mbele ya kiti cha kifalme cha upande wa kushoto, akasema maneno kama hayo, ile neno la mwisho lilikuwa Sorais, akalitaja mara tatu.

Ndipo tuliposikia vishindo vya watu wanaokuja toka upande huu na upande huu, na skari ishirini wenye silala waliingia toka upande wa kuume, na ishirini wakaingia toka upande wa kushoto, wakajipanga kuvizunguka viti vile vya kifalme, wakaikita mikuki yao chini kwa kishindo.

Kisha, tulisikia sauti mbili za panda tena, na Malkia wa Zuvendi waliingia, mmoja kutoka upande wa kuume na mmoja kutoka upande wa kushoto, kila mmoja amefuatana na mabibi sita, na watu wote sebuleni walisimama kama heshima kwao.


Nimeona wanawake wazuri katika maisha yangu, lakini maneno yangu hayawezi kabisa kuueleza uzuri wa maumbu Malkia hawa.

Wote wawili walikuwa vijana labda walikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano wote wawili walikuwa warefu na wenye maumbo mazuri sana, lakini hapo basi, waliachana kabisa kwa namna uzuri wao ulivyo.

Mmoja wao, yaani Nyleptha alikuwa mweupe sana mwenye nywele za rangi ya dhahabu zilizoviringana kichwani, lakini ndugu pacha aitwaye Sorais alikuwa mzuri kwa namna nyingine, maana nywele zake zilikuwa nyeusi kabisa, na ngozi yake haikuwa nyeupe sana ila nyeusi kidogo.


Basi, wote wawili walipita kuviendea viti vyao vya kifalme, na walipokuwa wakipita nilifikiri jinsi walivyoonekana kuwa Malkia halisi.

Lakini hata hivyo, walikuwa wanawake zaidi ya Malkia, nao waliona udadisi, maana walipokuwa wakipita niliona ya kuwa wanayatupa macho yao upesi kututazama. Niliona macho yao hayakunitazama mimi sana, labda hawakupendezwa kuona mzee kama mimi.
 
Kisha, walimtazama Umslopogaas kwa ushangao! Naye akaliinua shoka lake kuwasalimu.

Kisha walimtazama Bwana Good, wakavutwa na mavazi yake mazuri, kisha walimtazama Sir Henry aliyesimama na huku mwangaza wa jua unazing’arisha nywele na ndevu zake.

Sir Henry aliyainua macho yake yakakutana na macho ya Nyleptha, na hivyo kwa mara ya kwanza mwanaume mzuri kupita wote na mwanamke mzuri kupita wote niliopata kuwaona walionana.

Nikafikiri moyoni, ‘’Sasa nadhali wanawake wameyaingilia matata yetu, basi pengine mambo yataenda vizuri zaidi,’’ Nikaguna kimya nikijua ya kuwa uzuri wa mwanamke ni kama uzuri wa umeme kitu kinachoharibu na kufanya ukiwa.

Basi nilipokwisha kufikiri hivyo, Malkia wote wawili walikuwa wamekwisha kaa vitini mwao, na panda zililia tena, na watu wote walikaa, na Malkia Sorais alituashiria tufanye vile vile.

Kisha, Yule mtu aliyetuongoza ambaye alikuwa amerudi nyuma katika kundi la watu, alijitokeza amemshika mkono Yule mwanamke tuliyemtoa katika hatari ya kiboko.

Alijiinamisha mbele ya Malkia, kisha alianza kusema. Hakosi alikuwa anasimulia habari za namna walivyotukuta.

Lilikuwa jambo la kuchekesha kuzitazama nyuso za Malkia walipokuwa wakisikiliza habari hizo, na namna zilivyoonyesha ushangao na hofu.

Ikawa dhahiri kuwa hawakufahamu namna tulivyolifikia ziwa lile na kuonekana tunaelea juu yake, wakaelekea kusadiki kuwa hatukufika kwa njia za kibinadamu.

Basi, Yule kiongozi aliendelea kusimulia habari, na kwa jinsi alivyomuuliza Yule mwanamke mara kwa mara nilitambua ya kuwa anasimulia habari za jinsi tulivyowapiga viboko wale.

Nikaona ya kuwa mambo yamekwenda upande wa habari za viboko, maana wale makuhani walidakiza maneno mara kwa mara kama kwamba wameudhika sana, na wale Malkia wawili walisikiliza na huku nyuso zao zimejaa ushangao, na hasa Yule kiongozi alipowaonyesha bunduki zetu na kueleza ya kuwa ndizo zilizowaua wale viboko.


Basi, ni afadhali nieleze hapa ya kuwa Wazuvendi huliabudu jua, naya kuwa viboko ni mwiko kwao, wanahifadhiwa nao.

Si kwamba hawawauwi viboko, bali pengine huwaua wengi sana nao hutumia ngozi zao kufanyia ngao za askari.

Basi, kwa bahati mbaya, wale viboko tuliowaua walikuwa wamefungwa, nao walikaa mlangoni mwa bandari na kulishwa kila mara na makuhani ambao ulikuwa wajibu wao kuwaangalia.

Tulipokuwa tuna wapiga niliona kuwa walionekana kama kwamba ni wakufugwa, basi hii ndiyo iliyokuwa sababu yake.

Hivyo katika matendo yetu ya kuwaonyesha wenyeji nguvu zetu, kumbe , tumefanya jambo la kufukuru kuu kabisa.

Basi, kiongozi wetu alipokwisha simulia habari, Yule kuhani mkuu Agon alisimama akatoa hotuba ndefu ya hasira.

Sikupenda namna alivyotukazia macho yake baridi ya kijivu, na kwakweli ningalimchukia zaidi kama ningalifahamu ya kuwa anadai kwa jina la Mungu wao, ya kuwa lazima tutolewe kafara kwa kuchomwa moto tungali hai.

Alipokwisha sema, Malkia Sorais alisema naye kwa sauti nzuri ya upole ikawa kama kwamba anashindana naye na kumweleza upande mwingine wa jambo.

Kisha Nyleptha, akasema kwa sauti nzuri, lakini hatukujua ya kuwa anasihi kwa ajili ya maisha yetu, ndipo pale alipo akasema na mtu mrefu mwenye umbo la kiaskari, ana ndevu nyeusi na upanga mrefu, ambaye tulipata kujua baadaye jina lake ni Nasta.

Naye ni mkuu wa nchi kubwa, akawa kama anamsihi amsaidie. Lakini ilitokea ya kuwa Sir Henry alipomtazama Nyleptha rangi ya uso wake iligeuka, na Nasta aliliona jambo hilo, akajiuma mdomo akaushika upanga wake imara zaidi.

Baadaye tulipata habari ya kuwa Nasta anataka kumwoa Yule Malkia. Basi, ni dhahiri si mtu wa kumwomba msaada, na alipojibu alisema kwa sauti nzito kama kwamba anakubali shauri la kuhani mkuu Agon.

Alipokuwa akisema, Sorais alikuwa amekaa na huku ameshika tama, akamtazama Nasta na huku anacheka kidogo kama kwamba anazijua fikira zake, naye amekaza nia asishindwe naye.

Lakini Nyleptha alikasirika, na uso wake ulibadilika, na macho yake yaling’aa. Kisha aligeuka akamtazama Agon, ikaonekana kwamba anayakubali kidogo maneno yake, maana alikiinamisha kichwa chake; na alipokuwa akisema alipunga mikono yake ili kuyakaza zaidi maneno yake, na huku Sorais amekaa vile vile anacheka kidogo.

Kisha, Nyleptha alifanya ishara ghafla na panda zililia tena, na watu wote walisimama wakatoka sebuleni isipokuwa sisi na askari walinzi, maana alifanya ishara sisi tukae.

Walipokwisha toka, alijiinamisha mbele akacheka vizuri na kwa sauti na ishara alitufahamisha kwamba anataka kujua mahali tulipotoka.

Shida ilikuwa namna ya kuelezana, lakini nilipata akili. Katika mfuko wangu nilikuwa na kitabu cha kuandikia na kalamu, nikavitoa, nikachora ramani ya ziwa, na kwa namna nilivyoweza nilichora picha ya mto chini ya ardhi na ziwa upande mwingine wa mlima.

Basi, nilipofanya hivyo alifahamu, akapiga makofi kwa furaha, akashuka katika kiti chake akakipeleka kitabu kwa dada yake Sorais, na yeye pia alifahamu.

Kisha, akaitwaa kalamu na baada ya kuitazama kwa udadisi, alianza kuchora picha ndogo ndogo.

Picha ya kwanza ilifanana na yeye mwenyewe ameinyosha mikono yake kutupokea, na mtu mwingine aliyefanana na Sir Henry, anaipokea mikono yake.

Kisha, alichora picha ya kiboko anagaagaa majini kama anakufa, na ya mtu aliyefanana na kuhani mkuu Agon ameiinua mikono yake kwa ghadhabu amesimama kando ya ziwa.

Kisha, alichora picha ya moto mkubwa unaowaka, na ya Yule Agon anatuchochea katika moto kwa fimbo.

Basi, picha hizo zilitujaza kihoro, lakini nilitulia kidogo alipoanza kuchora picha nyingine ya mtu kama Sir Henry, na ya wanawake wawili niliowatambua kuwa ni yeye mwenyewe na dada yake Sorais.

Na kila mmoja ameuweka mkono mmoja kumkumbatia Bwana Henry, na kwa mkono mwingine wameushika upanga ili kumlinda.

Basi, Sorais aliyekuwa akituangalia sote, na hata Sir Henry, akafanya ishara kuonyesha kuwa fikira zake zinapatana na zile za dada yake.

Nyleptha alichora picha ya jua linaloanza kuchomoza, akafanya ishara ya kuwa sasa lazima aende, na ya kuwa tutaonana tena asubuhi.

Basi, hapo uso wa Sir Henry ulikunjamana, na Nyleptha alimpa mkono wake aubusu ili kumfariji akaubusu kwa heshima.

Basi, huku Sorais ambaye Bwana Good alikuwa anamtazama tokea mwanzo, alimpa mkono wake aubusu, lakini macho yake, yalikuwa yanamtazama Sir Henry tu.

Nafurahi kusema ya kuwa mimi sikuwamo katika mambo hayo, wala hakuna mmojawapo aliyenipa mkono wake niubusu.

Kisha, Nyleptha aligeuka akasema na Yule mkubwa wa askari walinzi, ikaonekana kwa namna alivyopokea maneno kwa heshima, ya kuwa anatoa amri yenye nguvu; kisha, alituchekea akatoka sebuleni amefuatana na Sorais na wengine wa askari wa zamu.

Malkia walipokuwa wamekwisha toka, Yule askari mkubwa aliyepewa amri za Nyleptha alikuja mbele na kwa ishara nyingi za heshima alituongoza kutoka sebuleni, na katika vichochoro vinginevyo mpaka katika vyumba vingine vyenye vyombo vizuri sana na mazulia na vitanda vizuri vizuri.

Vyakula vilikuwa vimeandaliwa mezani katikati ya chumba, na meza ilipambwa kwa maua.

Watumishi wanaume na wanawake walikuwapo kutuhudumia na huku kinanda kilikuwa kinapigwa mahali nje, tukajiona kama kwamba tu katika pepo ya duniani, na jambo tu lililotuudhi ni kufikiri ya kuwa Yule kuhani mkuu anataka kukutupa motoni.

Lakini tulikuwa tumechoka sana hata tuliona shida tusishikwe na usingizi wakati tunapokula, na mara tulipokwisha kula tulifanya ishara ya kuwa tunataka kulala.

Basi, walituongoza wakataka kutupa kila mtu chumba chake peke yake, lakini tuliwaashiria ya kuwa tulala wote chumba kimoja.

Tena ili tusije tukashambuliwa ghafla, Umslopogaas alilala pamoja na shoka lake katika chumba kilichokuwa jirani.

Basi tulivua nguo zetu isipokuwa deraya za chuma tulizokuwa tumevaa ndani ya nguo zetu, tukajitupa vitandani tukajifunika kwa mashuka ya Hariri yenye nakshi.

Nilikuwa karibu kupata usingizi nilipoamshwa na sauti ya Bwana Good akasema, ‘’Je, Quatermain, ulipata kuyaona macho kama yale’’ nikajibu kwa haraka, ‘’Mcho! Macho gani’’ akajibu, ‘’Macho ya Malkia. Macho ya Sorais!’’ nikapiga miayo nikasema, ‘’Sijui mimi, sikuyaangalia sana, abda ni macho mazuri.’’

Basi, baada ya dakika tano hivi niliamshwa tena kwa sauti yake, ananiita tena.
Nikasema, na sasa nimekasirika sana kuamshwa hivi, ‘’Je, unataka nini sasa’’
Akajibu, ‘’Je, ulipata kuona visigino vya miguu yake namna vilivyo vizuri .''

Basi, hapa upuuzi wake ulinichosha kabisa. Nilikuwa nimeviweka viatu vyangu vizito karibu na kitanda nilicholalia, basi nilivitwaa nikavitupa vikampiga Bwana Good baraabara. Baada ya hayo nililala sana.

Sijui habari za Bwana Good, sijui kama alilala au kama aliendelea kuota habari za uzuri wa Sorais.
 
Basi, baada ya dakika tano hivi niliamshwa tena kwa sauti yake, ananiita tena.
Nikasema, na sasa nimekasirika sana kuamshwa hivi, ‘’Je, unataka nini sasa’’
Akajibu, ‘’Je, ulipata kuona visigino vya miguu yake namna vilivyo vizuri .''

Basi, hapa upuuzi wake ulinichosha kabisa. Nilikuwa nimeviweka viatu vyangu vizito karibu na kitanda nilicholalia, basi nilivitwaa nikavitupa vikampiga Bwana Good baraabara. Baada ya hayo nililala sana.

Sijui habari za Bwana Good, sijui kama alilala au kama aliendelea kuota habari za uzuri wa Sorais.


 
nimekupenda wewe sana bi dada kama bwana Good kwa sorais
 
Let's learn kwa wahenga huku
Sisi wa juzi hatuzijui na upatikanaji wake mdogo
Mkuu shukran kunipa kitabu hiki nami nisome
 
Safi sana mkuu, wacha niirarue taratiiibu
 
Salute Sir Henry



Shukran Sir blackstarline
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…