Six Man
JF-Expert Member
- Dec 19, 2017
- 254
- 892
Sehemu ya kwanza
ILIKUWA ni majira ya saa nane na dakika kumi usiku. Mitaani, kulikuwa na giza la kutisha. Hali ya hewa ilikuwa ya baridi sana katika jiji la Birmingham nchini Uingereza.
Ni saa nne zilikuwa zimepita tangu kijana Alexander Norman apate usingizi katika nyumba yao ndogo iliyopo kaskazini mwa jiji la Birmingham.
Ilipofika saa nane na dakika kumi usiku, hali ya hewa ilibadilika, ulianza kuvuma upepo ambao ulikuwa unaongezeka kila sekunde zilivyokuwa zinayoyoma. Ndani ya dakika ishirini upepo huo wa ajabu haukukoma.
Saa nane na dakika thelathini usiku, upepo ulioshika hatamu ulisindikizwa na radi kali. Mishale mikale ya radi ilikuwa inamulika kwa sekunde chache anga la jiji la Birmingham na kufanya nje kuonekane kama mchana. Baada ya sekunde chache za mimuliko ya miale ya radi hali ya giza totoro ilirejea.
Katika chumba alipokuwa amelala Alexander kulikuwa patulivu sana. Ukiacha zile bughudha za upepo na radi zilizokuwa zinatokea huko nje, ndani ya chumba hiki kulikuwa patulivu.
Alexander alikuwa amelala fofofo juu ya kitanda cha futi sita kwa sita. Blanketi safi la rangi ya hudhurungi lilikuwa limemfunika juu yake. Alikuwa ametopea katika lindi la usingizi, usingizi uliokuja kirahisi tu kwakuwa alikuwa amechoka sana siku hiyo.
Saa nane na dakika thelathini na tano usiku, pembeni, katika kuta moja ya chumba hiko kati ya kuta nne zilizomo mle chumbani, ulitokea ufa mdogo. Ufa ulikuwa umeanzia chini kabisa karibu na sakafu hadi juu karibu na rinta. Ufa ule wa ajabu uliongezeka ukubwa kila sekunde, na kufikia ukubwa wa kuwezesha kupita mtu ingawa kwa shida. Mara, moshi mweupe ulitokea nje ya ufa ule na kuingia ndani ya chumba alicholala Alexander kupitia ule ufa. Kitendo hiko kilidumu kama dakika tano na ule moshi ulikoma. Ile kuta ilijiziba ukiuacha ule moshi mle chumbani.
Moshi ulisogea hadi katika kuta nyingine ya chumba cha Alexander. Ulizungukazunguka kama dakika tano zingine na kutengeneza umbo la mtu. Ulianza kusogea taratibu kuelekea pale kitandani alipolala Alexander. Ulisogea hadi upande wa kichwa cha Alexander. Kwa namna ya ajabu ulilifunua blanketi alilojifunika Alexander upande wa kichwa. Ule moshi uliinamia kichwa cha Alexander.
Na kutoa sauti.
"Alexander, nenda Milton Keynes, nyumba namba MK131402, kamuue Mr Robbin Thomas"
Baada ya ule moshi kusema maneno hayo, ulirejea kule ukutani ulipoingilia. Ukuta ulijitengeneza tena ufa kama awali na kuuruhusu moshi ule kupita. Baada ya moshi wote kutoka nje, ule ukuta ulijifunga kama awali.
Na dakika hiyohiyo kule nje upepo na radi zilizokuwa zimeshamiri zilikoma mara moja.
Je nini kitatokea?
Tukutane kesho hapahapa...
Sent using Jamii Forums mobile app