Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

Ndiye mwenyewe mkuu
bora umekuja mwenyewe ,kuna hadithi zako nyingi tu humu walileta wadau wa jf
tutapata wasaa wa kuuliza maswali moja kwa moja, ila uwe mvumilivu, kuna watu humu wana maswali mpaka ulivyoweka nukta,,
ushauli wangu we ni mwandishi mkubwa VERIFYING account yako itumie jina lako halisi
 
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA.
IMEANDIKWA: NYEMO CHILONGANI.
0756362035

Sehemu ya 05.

Ilikuwa kazi ngumu, kila aliponunua kilo mia moja, alipoondoka, alikaa nusu saa, mchele ulikwisha na kurudia kilo mia moja.
Ni ndani ya saa tatu tu, zile tani moja za mchele kwenye gari lile zilimalizika, zote aliuza Bazoka kitu kilichokuwa kimemshangaza sana.
“Bazoka!” aliita Hamisi.
“Niambie mshikaji wangu!”
“Umeanza lini kuuza mchele?”
“Leo! Yaani mpaka nimeshangaa, mchele umekwisha fasta sana,” alisema Bazoka.
“Kila mtu ameshangaa, imekuwaje?” aliuliza Hamisi.
Alipouliza hivyo ndipo alipokumbuka kile alichoambiwa usiku uliopita, ule utajiri alioambiwa ndiyo ambao ulikuwa ukimnyemelea. Hakujibu swali hilo, akajifanya akipuuzia na kuondoka sokoni hapo na kurudi nyumbani.
Alikuwa na kiasi kikubwa cha pesa, alijishangaa, katika maisha yake hakuwahi kushika kiasi kikubwa kama kile alichokuwanacho. Alipofika nyumbani, akamgawia Asha ile pesa aliyoazimwa na baba yake na kumpelekea.
Asha alishangaa, hakuamini alichokiona, hakujua mahali ambapo mpenzi wake alizipata pesa nyingi kiasi kile, alimuuliza na kitu pekee alichoweza kujibu Bazoka ni kwamba alifanya biashara.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa utajiri wake, akawa mfanyabiashara wa mchele, kila siku aliuza kiasi kikubwa mno, alipata pesa kupita kawaida, kila mtu alikuwa akimshangaa huku wengine wakimwambia alikuwa na kismati kuliko hata wao walioanza.
Baada ya mwezi mzima, akaamua kukodi gari ambapo akawa na kazi ya kuufuata mchele yeye mwenyewe mkoani Mbeya. Hilo likampa mafanikio makubwa, akaingiza kiasi kikubwa cha pesa na hivyo kuhama Kwa Ally Maua na kuhamia Mwenge ambapo bado aliendelea kufanya biashara zake kama kawaida.
Maisha yalibadilika, akapanga nyumba nzima, akaanzisha biashara nyingine, mafanikio yake yalikuja kwa kasi sana kiasi kwamba akawa anashangaa tu.
Akanunua gari la kwanza katika maisha yake. Aliyafurahia maisha yake, hakutaka kuishi peke yake, alichokifanya ni kumchukua Asha ambaye alibakiza mwezi mmoja kabla ya kujifungua.
Mara kwa mara alikuwa akikutana na marafiki zake, Sultani na Bonge na kwenda kuabudu kama kawaida yao. Maisha yake aliyakabidhi kwa shetani, hakutaka kurudi nyuma kwani kumuabudu shetani kulimpa mafanikio makubwa ambayo hakuwa akitegemea kuyapata.
Baada ya mwaka mmoja wa mafanikio makubwa huku akiwa ametengeneza jina kubwa nchini Tanzania, akapata kipele katika mguu wake wa kushoto. Kilikuwa kidogo na kilichokuwa kikiwasha sana.
Alikikuna, kadiri alivyokuwa akikikuna ndivyo kilivyokuwa kikiongezeka. Kiliendelea kuwa hivyo mpaka alipoamua kwenda hospitalini kuangalia tatizo lilikuwa nini.
“Ni kipele, inaonekana damu imechafuka eneo hili, chukua hizi dawa zitakusaidia,” alisema nesi huku akimpa dawa.
“Nashukuru sana!” alisema Bazoka na kuondoka.
Alipofika nyumbani, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumwambia Asha kilichokuwa kimetokea hospitalini kwamba alipewa dawa na hivyo kuanza kuzitumia.
Wakati huo alikuwa na mtoto wa kiume aliyempa jina la Edward, mtoto mzuri ambaye alichukua sura yake, alimpenda, kwake, mtoto huyo alikuwa kila kitu na kila alipokuwa akimuona, alizidi kupambana zaidi na zaidi.
Siku ziliendelea kukatika, kipele kile hakikuacha kuuma, kilimpa maumivu makali, alipewa dawa mbalimbali kwa ajili ya kukitibu lakini hakikuacha kuwasha na kuuma.
Aliendelea kwenda katika hospitali mbalimbali lakini bado matokeo yalikuwa yaleyale, alichokifanya ni kusafiri mpaka nchini Kenya lakini napo huko kukagonga mwamba, kipele kikaiva na kupasuka, kukatokea kidonda kilichokuwa na maumivu makali.
“Tatizo nini lakini?” alijiuliza lakini hakuwa na jibu lolote lile.
Baada ya mwezi mmoja wa maumivu, akaamua kumwambia Sultani kile kilichokuwa kikiendelea, mwanaume huyo akamuita Bonge na kuanza kumwambia kidonda kile kilitokana na utajiri aliokuwanao.
“Unasemaje?” aliuliza Bazoka huku akionekana kushtuka.
“Kadiri kinavyozidi kuongezeka na kuuma ndivyo utajiri wako utakavyokuwa ukiongezeka,” alisema Bonge.
“Kwa maana hiyo hakitopona?”
“Mpaka unaingia kaburini!”
“Kwa nini?”
“Unakumbuka ulivyoambiwa utajiri huo utaambatana na maumivu makali?” aliuliza Sultan.
“Ndiyo! Nakumbuka niliambiwa na mungu wetu!”
“Hayo ndiyo maumivu yenyewe. Hautoweza kupona, kitaendelea kuuma mpaka kifo chako,” alisema Bonge huku akimwangalia Bazoka.
Bazoka alihuzunika, hakuamini kama yale maneno aliyoambiwa na mungu wake ndiyo yangekuwa maumivu ya namna ile.
Ili kumuonyesha hakuwa peke yake, Bonge akavua shati lake, alikuwa na kidonda kikubwa chini ya kwapa lake, kilikuwa kidonda kilichotisha kuliko hata alichokuwanacho.
Bazoka akashtuka, hakutegemea kuona mtu akiwa na kidonda kile halafu akawa mzima na kuzungumza kana kwamba hakukuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Alimwangalia mwanaume huyo, kwake, alionekana kuwa jasiri kuliko wanaume wote ndani ya dunia hii.
“Na wewe Sultan?” aliuliza Bazoka huku akimwangalia Sultan.
“Mimi sina kidonda!”
“Una nini?”
“Sitoweza kupata mtoto maisha yangu yote!” alijibu Sultan huku akimwangalia Bazoka.
Hapo ndipo akagundua utajiri ule ulikuwa na maumivu makali mno. Ulikuwa mtamu, alifanya kitu chochote alichokitaka lakini kila siku alipokiangalia kidonda chake, moyo wake ulimuuma mno.
Asha alimpeleka katika hospitali mbalimbali kutibiwa, Bazoka hakuwa akikataa, alikubaliana na Asha lakini hakuwa radhi kumwambia ukweli kile kilichokuwa kikiendelea.
“Kidonda chako kinaonekana kuwa na bakteria wakali ambao kitaalamu wanaitwa Bicorture,” alisema daktari mmoja baada ya kukiangalia kidonda cha Bazoka.
“Na dawa yake?” aliuliza Asha.
“Naomba akatumie hii, nadhani anaweza kupata nafuu na kupona kabisa,” alisema daktari na kuwapa dawa.
Wakaichukua na kuondoka mahali hapo, moyoni mwa Asha aliamini mpenzi wake angeweza kupona kidonda kile lakini Bazooka alifahamu kila kitu na hakutaka kuweka wazi hata kidogo.
Wakarudi nyumbani na kuanza tiba kama alivyoambiwa lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale. Siku ziliendelea kukatika kama kawaida
Biashara zake ziliendelea kumuingizia kiasi kikubwa cha pesa. Akawa bilionea mkubwa na mwenye makamuni mengi, alikuwa na kazi ya kuuza nafaka ambazo alikuwa akizitoa vijijini na kuzipeleka katika masoko makubwa jijini Dar es Salaam.
Alifanikiwa, akanunua nyumba nyingi jijini Dar es Salaam. Yalikuwa ni mafanikio makubwa na ya haraka sana lakini cha ajabu hapakuwa na mtu aliyetilia shaka kwa kile kilichokuwa kikiendelea.
Walimuona mwanaume huyo kuwa mpambanaji, alijua kupambana kwa ajili ya mafanikio yake. Kila siku aliamka asubuhi na mapema na kuwahi kazini hata kabla ya wafanyakazi wake. Hilo likawafanya watu wengi kuona mafanikio yote aliyokuwa akiyapata ni kwa sababu alijitolea kupambana.
Baada ya miaka miwili, akaitwa katika nyumba ile ya ibada na kuambiwa huo ulikuwa muda wa kutoa kafara kwa mungu wao. Kwanza hakuamini, alichojua walimalizana baada ya kupewa kile kidonda.
Aliogopa, hakujua ni kafara ya aina gani alitakiwa kuitoa. Alikuwa radhi kutoa damu ya mnyama au kitu chochote kile lakini si kuua. Hakuona kama kweli mungu wao angewaambia watoe kafara ya mnyama, alichokiona walitakiwa kutoa kafara ya damu ya mtu.
Alikuwa na hofu, alitetemeka kiasi kwamba kijasho chembamba kikaanza kumtoka. Alikuwa na hofu moyoni mwake na kuhisi kabisa huo haukuwa muda mzuri, piga ua kulikuwa na tatizo mbele yake.
“Inakuwaje tena kutoa kafara,” alimuuliza Sultani huku akionekana kushangaa.
“Huo ndiyo utaratibu tuliyowekewa, kila baada ya miaka miwili, kafara inahitajika,” alisema Sultani huku akimwangalia Bazoka, uso wake ulikuwa na tabasamu pana kana kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile.
“Lakini si tuna vidonda?”
“Bado haitoshi, suala la kafara lipo palepale,” alijibu mwanaume huyo.
Jibu hilo lilimchosha, alimwangalia Sultani kwa kumkazia macho, alitamani kumsikia akimwambia alikuwa akimtania. Hakutaka kutoa kafara yoyote ile, moyo wake ulimwambia kile kidonda alichokuwanacho ndiyo kilikuwa kafara yenyewe.

Je, nini kitaendelea?
 
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
IMEANDIKWA: NYEMO CHILONGANI
0718069269

Sehemu ya 06

“Lakini si tuna vidonda?”
“Bado haitoshi, suala la kafara lipo palepale,” alijibu mwanaume huyo.
Jibu hilo lilimchosha, alimwangalia Sultani kwa kumkazia macho, alitamani kumsikia akimwambia alikuwa akimtania. Hakutaka kutoa kafara yoyote ile, moyo wake ulimwambia kile kidonda alichokuwanacho ndiyo kilikuwa kafara yenyewe.
Akakosa raha, furaha yote aliyokuwanayo moyoni ikatoweka. Kila siku alikuwa mtu wa mawazo tele kiasi kwamba hata Asha alishangaa. Hakuzoea kumuona mpenzi wake akiwa kwenye hali ile, alijaribu kumuuliza lakini mwanaume huyo alimwambia hakuwa na tatizo lolote lile.
Asha hakukubali, alijua kabisa alidanganywa, kama mwanamke alitumia ushawishi wake wote kwa mume wake lakini hakuwa radhi kumwambia ukweli kile kilichokuwa kikiendelea, alichomwambia ni kwamba hakukuwa na tatizo hata kidogo.
“Lakini umebadilika!” alisema Asha.
“Labda mawazo juu ya biashara zangu mpenzi,” alisema Bazoka.
“Una uhakika hakuna tatizo?”
“Kabisa!”
“Kweli?”
“Ndiyo mpenzi! Usijali kipenzi changu,” alisema Bazoka na kuachia tabasamu pana ambalo aliamini lingemuaminisha Asha kwamba hakukuwa na tatizo lolote lile.
Siku ziliendelea kukatika, baada ya siku kadhaa hatimaye siku ya ibada ya kutoa kafara ikawadia. Siku hiyo ndiyo ambayo Bazoka alikosa furaha kwa kiasi kikubwa, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alitamani hata kutokuhudhuria ibada hiyo lakini hilo lilishindikana.
Watu wengi, mabilionea walikusanyika katika chumba kikubwa cha kufanyia ibada. Mavazi yao yalikuwa makubwa, meusi kama majambazi waliokuwa wakienda kuiba sehemu fulani nyakati za usiku.
Nyuso zao waliziinamisha chini kama kawaida yao, hawakutakiwa kuziinua mpaka pale ambapo mungu wao angefika mahali hapo. Palikuwa panatisha, kulikuwa na mishumaa iliyokuwa ikitoa harufu mbaya kupita kawaida.
Baada ya kusimama kwa dakika kadhaa ndipo mungu wao akaanza kuingia mahali hapo. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kusujudu, wakafanya hivyo na kisha kuinuka.
Hapo ndipo wakaanza kupewa majukumu yao katika utoaji wa kafara uliotakiwa kufanyika. Kwa kuwa Bazoka alikuwa mgeni katika ibada ya kafara, akapewa jukumu la kuwatoa kafara watu wawili, albino na bibi kizee.
“Mmh!” aliguna moyoni mwake.
Kwake ulikuwa mtihani mkubwa kupita kawaida, hakuamini kama angepewa jukumu kubwa kulifanya kama hilo. Wenzake walipewa nafasi ya kutoa kafara kwa mtu mmojammoja tu lakini kwake, alitakiwa kuwatoa kafara watu wawili.
Moyoni mwake hakuona kama angeweza, alihisi kabisa angeshindwa lakini hakutaka kuwaambia watu hao mahali hapo. Kutoa kafara hizo zilitakiwa kufanyika ndani ya miezi mitatu tu.
Hakuamini kama angeweza kufanya hivyo. Wakati akifikiria kuhusu kushindwa kwake, yule mungu wake ni kama alijua alichokiwaza na hivyo kumwambia kama angeshindwa kufanya hivyo, angepokonywa utajiri na mwisho wa siku kumuua katika kifo cha mateso makali.
Mungu huyo akamwambia angempa nguvu za kufanikisha kile alichotakiwa kufanya hivyo hakutakiwa kuogopa kwa chochote kile. Aliamini hilo na baada ya ibada kumalizika, akaitwa mbele, akapakwa damu katika utosi wake na paji la uso na kuwekewa unga katika mashavu yake.
Aliona ni jambo la kawaida lakini baada ya mungu yule kutamka maneno fulani, akahisi mwili wake ukianza kupata nguvu ya ajabu, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipata nguvu hizo alizoanza kuzipata.
Hofu aliyokuwanayo moyoni ikatoweka na kuona kulikuwa na urahisi mkubwa wa kufanikisha kile alichotakiwa kukifanya baada ya kuondoka hapo.
Akapewa kisu kilichokuwa na makali pande zote, kisu kile kilikuwa na damu huku kikiwa kimefungwa kitambaa cheusi kilichochakaa na kuambiwa alitakiwa kukitumia kuhakikisha anafanya mauaji kwa wale watu alioambiwa.
“Niwachinje?” aliuliza kwa sauti ya chini.
“Vyovyote vile lakini kinachotakiwa ni kuona wakifa kwa kutumia kisu hicho,” alisema mungu huyo huku akimwangalia Bazoka.
Moyo wake ukaridhika na kwa asilimia mia moja akakubaliana na mungu yule na hivyo kuruhusiwa kuondoka ambapo akafumba macho, alipoyafumbua akajikuta akiwa ndani ya gari lake, hivyo kuliwasha na kuondoka.
Kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, hakuwahi kuua lakini mungu wake alimsisitizia lazima aue kama tu alitamani kuendelea kuwa na utajiri aliokuwanao.
Aliupenda, alikuwa tayari kupoteza kila kitu maishani mwake lakini si utajiri. Ulikuwa mtamu, aliutumia kwa kufanya mambo mengi japokuwa bado mwili wake ulikuwa na maumivu kutokana na kidonda alichokuwanacho katika mguu wake.
Aliendesha gari mpaka nyumbani kwake, akateremka na kuelekea ndani. Akamkuta Aisha akiwa sebuleni akimsubiri, alipomuona, akainuka na kuanza kumsogelea huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Pole sana mume wangu,” alisema Aisha huku akimwangalia Bazoka.
“Nashukuru sana. Nimechoka, nadhani natakiwa kupumzika!” alisema Bazoka huku akivua shati lake.
“Naomba ule japo kidogo,” alisema mkewe.
“Haina shida, niwekee chakula nakuja kula sasa hivi!” alisema na kuelekea chumbani.
Mawazo yake hayakutulia, kila wakati alifikiria kile alichoambiwa. Hakuona ugumu wa kufanya kile alichotakiwa kufanya ila ugumu aliouona mbele yake ulikuwa ni kuwapata wale watu ambao alitakiwa kuwamaliza.
“Nitakwenda kwenye kituo cha watoto yatima,” alisema wakati alipokuwa akioga.
Hilo ndilo lililomjia kichwani mwake, aliona kabisa kama angekwenda katika kituo chochote cha watoto yatima ingekuwa rahisi kwake kumpata mtoto na kummaliza.
Wakati akifikiria hilo, pia akauona ugumu katika kazi hiyo, aliona jinsi ambavyo ingekuwa rahisi kwa watu kugundua yeye ndiye aliyekuwa amefanya mauaji hayo.
Hilo likamtia hofu na kuamua kuchukua uamuzi mwingine kabisa. Kwa sababu aliambiwa alihitajika mtoto kwa ajili ya kumuua, alichokifanya ni kufikiria idadi ya watoto wengi waliokuwa mitaani.
Kulikuwa na watoto wengi mno ambao walikuwa wakizurura tu, watoto ambao hata wazazi wao hawakuwa wakijua walikuwa wapi, yaani walirudi nyumbani usiku au jioni. Hao ndiyo watoto ambao alitakiwa kuwatumia kutekeleza mpango wake alioutaka.
Hakutaka kuchelewa, siku iliyofuata akaanza kuelekea katika Mtaa wa Manzese ambapo aliamini kulikuwa na watoto wengi waliokuwa wakizurura. Siku hiyo alikuwa na kazi ya kusoma ramani, alitakiwa kugundua ni sehemu gani ilikuwa na watoto wengi ambapo kungekuwa na urahisi kwake kumchukua mtoto mmoja.
Kama alivyohisi ndivyo alivyokuta, kulikuwa na watoto wengi waliokuwa wakizurura kana kwamba hawakuwa na kwao. Alifurahi, moyo wake ukawa na uhakika wa kufanya kile alichohitaji kukifanya.
Kwa kuwa aligundua ni sehemu gani kulikuwa na watoto wengi na namna ya kumpata hata mmoja, akaondoka kurudi nyumbani. Moyo wake ukawa na hofu, alijua kabisa kile alichokuwa akienda kukifanya hakikuwa kizuri, kungekuwa na damu za watoto ambazo zingekuwa zinalia mikononi mwake lakini hakuwa na jinsi, ili aendelee kuwa na utajiri ilikuwa ni lazima kufanya kile alichotakiwa kufanya.
Aisha aligundua Bazoka hakuwa sawa, akamuuliza tatizo lilikuwa nini lakini hakumwambia ukweli, alimdanganya kulikuwa na mambo mengine ya biashara ambayo yalikuwa yakimtatiza.
“Kwa hiyo hakuna kitu?” aliuliza Aisha.
“Ndiyo! Ni mambo machache tu ndiyo yananichanganya,” alisema Bazoka huku akimwangalia Aisha.
Alipata kila kitu alichokihitaji, kilichokuwa kimebaki kilikuwa ni kufanya kile alichoambiwa tu. Kila alipoiangalia familia yake, alijikuta akisema ni lazima afanye alichoambiwa kwani vinginevyo utajiri wote aliokuwanao ungepotea na hivyo kurudi katika maisha ya shida kama ilivyokuwa zamani.
Alikaa kwa wiki nzima huku akiwasiliana na wenzake, Bonge na Sultani ambao walimwambia kuwa kutoa kafara halikuwa jambo gumu, katika kipindi cha kwanza kama hicho angeona kuna ugumu lakini baada ya kuzoea, kusingekuwa na ugumu wowote ule.
Walimtia moyo ili aone kile alichokuwa akienda kukifanya ni cha kawaida sana. Maneno yao yakamuingia, hofu aliyokuwanayo ikaanza kupungua na kujiaminisha kweli kile alichotakiwa kukifanya kilikuwa cha kawaida sana.

Je, nini kitaendelea?
 
Siwezi kuposti hadithi kila siku...na siwezi kuposti hadithi kila baada ya siku mbili. Apart from kuposti hadithi bado kuna mambo mengine ya maisha ya kuniingizia pesa inabidi yafanyike.
Sawa mkuu hila unatutesa sisi wasomaji bora Atuwekee hata tatu tatu Afadhali sio ka episode kamoja
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom