sehemu ya 04
Kwa mbwembwe, mwanaume huyo akaanza kujisifia, aliamini ili kumpata Aisha, kwa jinsi alivyokuwa mrembo wa sura ilikuwa ni lazima uanze kujisifia kwamba una pesa, una biashara nyingi na mambo mengine.
Wakati akiendelea kujisifia Aisha alikuwa akimsikiliza tu, kuna wakati alikuwa akicheka, akitabasamu na hata kujifanya kujishtuka, yote hayo aliyafanya kwa kuwa alihitaji kuziteka hisia za mwanaume huyo.
“Tangu nizaliwe nimeona wanawake wengi sana,” alisema Curry huku akimuita mhudumu na kumuagiza pombe kali.
“Ooh! Hongera kwa macho yako makali!” alisema Aisha na kuangalia chini.
“Ila sijawahi kumuona mwanamke mrembo kama wewe,” alisema Curry.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Nashukuru sana!” alisema Aisha.
Curry akanyamaza, alichanganyikiwa, alihitaji kulala na mwanamke huyo ila hakujua ni kwa jinsi gani angeanza. Alimwangalia kwa makini huku akijaribu kumsoma, naye Aisha alijifanya kuwa mgumu, haingiliki kirahisi hata kidogo, alijipanga kupangua mashambulizi kwani kwa kufanya hivyo aiamini mwanaume huyo angeendelea kuongeza dau.
“Naomba nikalale nawe leo,” alisema Curry huku akimwangalia Aisha.
Msichana huyo akajifanya kushtuka, akayainua macho yake na kumwangalia Curry, akajifanya kuwa na hasira kali, kumbe yote hayo zilikuwa ni mbinu za kuonekana kuwa mkazaji kumbe hakuwa hivyo.
Curry akashtuka, akahisi alikosea kwenda moja kwa moja kwani inawezekana kabisa Aisha hakuwa malaya aliyekuwa akijiuza na ndiyo maana alionekana kukasirika.
“Unanichukulia mimi malaya?” aliuliza Aisha kwa hasira.
“Naomba unisamehe mrembo!” alisema Curry.
“Au kwa sababu nimekukubalia kukalia hicho kiti?”
“Naomba unisamehe! Punguza sauti kidogo!” alisema mwanaume huyo huku akionekana kuogopa.
Aisha akanyamaza, Curry akaanza kumbembeleza sana, alizungumza maneno yote matamu, alimuomba msamaha mno kiasi kwamba mpaka wakati mwingine Aisha alijiona kuwa mtu bora, mwenye bahati kukutana na mwanaume aliyejua kuomba msamaha kama alivyokuwa Caurry.
Baada ya mazungumzo kama ya saa moja, wakawa marafiki na kuanza kuongea mambo mbalimbali na hata Curry alipomuomba tena kwenda kulala naye, Aisha hakuwa na jinsi, akakubali na hivyo kwenda chumbani huku ikiwa ni saa saba usiku.