Hadithi fupi: Hadithi ya Wakurya wa Tanganyika

Hadithi fupi: Hadithi ya Wakurya wa Tanganyika

Lycaon pictus

JF-Expert Member
Joined
Jan 31, 2021
Posts
10,884
Reaction score
18,824
Na D. Kingdon.



HADITHI YA WAKURYA WA TANGANYIKA
WAKATI ule mvua ilikwishaanza; lakini majani yalikuwa yangali makavu, ingawa sehemu zingine zilikuwa na majani mabichi. Vivuli vya mawingu vilitanda juu ya miinuko ya nchi, na ukiangalia kwa mbali, utaona milima kama imefunikwa na moshi, kwa ajili watu hawajamaliza kuchoma mabua.

Makao ya watu yalionekana kando ya vilima, na mbugani, chini ya mteremuko mkubwa unaoingia katika nchi. Makao yao yalikuwa ni jumla ya vibanda na ghala za vyakula ambazo zilizunguuka zizi la ng'ombe; na vyote vilizungukwa na 'milangali'. Katika nchi hii, palikuwa msichana mmoja aitwaye Robi, ambaye aliolewa na Chacha. Huyu Chacha alikuwa mzee, na aliyekwisha oa wake wawili. Mzee Chacha aliweza kumwoa Robi kwa sababu alikuwa tajiri kuliko vijana. Ingawa Robi alikuwa ni mke wa tatu, alistarehe, na aliridhika kumzalia mtoto wa kiume wa kwanza.

Vibanda vyote vilifanana, na viliunganishwa na ua wa miti minene. Kila kibanda kilikuwa na ukuta uliotenga wanyama wagonjwa na ndama mbali na watu. Katika chumba cha watu kulikuwa giza, na pembeni palikuwa kitanda kilichotandikwa ngozi; upande wa miguuni, palikuwa na mafiga.

Mwezi ulipokuwa kamili, wazee walimshauri mganga wa mvua. Alifanya matambiko mengi ya siri, lakini alishindwa.

Akasema, 'Baba zetu wamekasirika, wamezuia mvua.' Walimpa kondoo na mbuzi wawili. Ikaja mvua ya manyunyu, lakini binadamu na wanyama walisubiri kupata mvua ya kutosha ili iondoe dhiki ile. Mwishowe, yakaja mawingu mengi yaliyokusanyika pamoja, yakipita angani. Kulikuwa mvumo wa upepo na mungurumo wa radi.

Sauti za kengele za ngombe zilizidi kwa uziri wakati wipwa wa Chama wakiwarudisha ngombe kwa haraka nyumbani kutoka machungani. Kundi la ng'ombe lilipoingizwa zizini, watoto walifunga mlango kwa magogo mazito. Magogo haya yalifungwa pamoja na mti mrefu ambao ulipita katikati ya jengo la banda upande wa kulia, na kufuata kitanda ili uwape ishara, kama kuna mtu ye yote anayejaribu kufungua mlango usiku. Mvua ilinyesha sana mpaka asubuhi, lakini upepo ulitulia mapema. Robi siku ile alichelewa kuamka, na alipooza sana. Moto ulififia kidogo, na mtoto Mwita alikuwa akilia. Alikuwa mtoto wake wa kwanza kama jina lake lilivyoonyesha; kwa sababu mtoto ye yote wa kiume wa kwanza kuzaliwa huko Kuria, lazima aitwe Chacha, Mwita, au Marwa.

Kwa desturi yao, humwacha mtoto wa kwanza akae na bibi yake, anapotazamiwa wa pili; kwa hiyo, ilimlazimu Mwita amwache mama yake. Basi, kwa masikitiko mengi, Robi alimlisha akamlaza. Kisha aliongeza kuni motoni, na ulipowaka, akakaa kuotea. Hapakuwa mwanga mwingine zaidi ya ule wa moto kibandani, ila ule uliopenya katika nyufa za mlango wa fito kutoka nje. Mionzi mikali ya mwanga iliang'aza ndani ya heleni za shaba ambazo Robi alivaa kujijulisha kuwa ni mwanamke aliyeolewa. Heleni hizi zilipembea katika ndewe kubwa za masikio yake. Bangili zake nzito ziling'aa sana. Alikuwa amezivaa bangili hizi kwa miaka mingi hata zikakata katika mikono yake na kuvimbisha pande zote mbili. Robi alipotoka nje, jamaa zake walikwisha kuamka mapema, wakishughulika na kazi. Ng'ombe walikwisha kukamuliwa na mbegu zilikuwa zimetolewa ghalani. Miti na majani yenye umande yalimeta-meta kwa mwanga wa jua, na Robi alichangamka.

Babu zake Mwita waliishi umbali wa mwendo wa siku nzima, upande wa magharibi. Chacha alimwambia Robi kuwa baada ya kumaliza kupanda, aende huko. Basi, siku moja alfajiri, baada ya kumaliza kupanda, aliiteremsha ngozi yake ya arusi. Ilitundikwa kwa ukanda mkuukuu kwenye pao la nyumba, na ilivaliwa wakati wa sherehe ya kumpeleka mtoto kwa babu zake au wakati wa arusi ya wanawe.

Alimbeba Mwita pamoja na hirizi na dawa zake, ambazo zilikuwa vijiti vidogo, vifuko vidogo vya kamba vilivyofungwa pamoja, shanga za rangi, senti, na kibuyu kidogo kilichopambwa ambacho alipewa na mpenzi wake kabla ya harusi yake.

Alipokuwa akitembea njiani, hali ya nchi ikawa inabadilika kidogo kidogo. Njia yake ilipitia kwenye miinuko na miteremko hata akafikia uwanda wa juu; na ilipofika jioni akateremka kwenye nchi yenye miti mingi. Aliona vilima vidogo vidogo vyenye majabali yaliyochongoka. Pengine alipita mahame ya watu. Hapa ilibaki milangali iliyosongwa na majani na mimea mingine, ambayo ilikuwa makao ya wanyama wadogo wa porini na pengine mizimu ya watu waliokaa hapo. Wakati huu wote jua lilikuwa likichwa na mbingu ilibadilika rangi.

Robi alipofika nyumbani kwa wazazi na ndugu zake, kulikuwa kumetulia. Vibanda vilifungwa na ng'ombe walikuwa zizini. Alibisha hodi, na mara alisikia mlio wa mlango ukivutwa toka kwa ndani ya kibanda. Wasichana wawili walichungulia nje huku wakitafuna makande. Walikuwa wakingojea chakula cha jioni, lakini waliposikia kuwa ni Robi aliyebisha hodi, walitoka nje wote na kumkaribisha kwa furaha. Baada ya kupeana mikono na kuongea kwa muda mrefu, aliingia kibanda cha wazee na kushirikiana chakula chao cha jioni. Alilala usiku ule tu, na asubuhi akarejea nyumbani, akimwacha Mwita katika hali ya ugenini.

Msichana mmoja mwenye umri wa miaka kama tisa, aliyekuwa amevaa kiunoni majani yaliyosukwa, mara ile alichukua daraka ya kumlea. Alimkorogea uji na kumlisha, lakini punde kidogo alimkumbuka mama yake na alianza kumlilia. Bibi yao alishughulika na kupiga mtama. Alikaa huku ameinyosha miguu, na mtama ulijirundika katika ngozi iliyokuwa katikati ya miguu yake. Ufito wa kupigia mtama ulitoa mlio hafifu. Pengine alimfukuza kuku, na wakati fulani aliwatazama watoto. Mwishowe aliwaita, akainyosha mikono yake kumchukua Mwita, akambembeleza kidogo na kumkumbatia. Alipoburudika, alipendezwa na bangili zake za shaba hata akalala.

Babu yake aliyekuwa akisinzia kivulini, akaja kumchukua mtoto aliyelala, na kamlaza taratibu karibu yake. Baada ya kumfunika ngozi, naye akajifunika blanketi lake, wakalala kwa utamu wa sauti za wadudu wakiimba na mvumo wa mtama ukipetwa. Kwahiyo wakati ulipitishwa kwa kulala, kula na michezo kidogo.

Ilikuwa ni wakati wa masika; mimea ilisitawi sana, na mtama ukachanua na kukomaa.

Baada ya mavuno, Robi akamzalia Chacha mtoto wa kike. Alfajiri ile baada ya mtoto kuzaliwa, mzee mzalishaji alitoka na kapu la unga na kijiko cha uji. Akasimama juu ya kisuguu nje ya kibanda, akaumwaga hewani, huku akiita kwa sauti kali mara nne. Jirani waliposikia, waliambizana' 'Robi mke wa Chacha amezaa Shoka na Kuni,' maana yake mtoto wa kike. Kama angeliita mara tano, wangejua kwamba ni mtoto wa kiume, na wangesema, 'Amezaa Ngao na Mkuki'. Robi alikaa ndani siku nne, kama ilivyo kawaida baada ya kuzaa mtoto wa kike. Kisha alimnyoa na kumwita Boke, kwani kila mtoto wa kwanza wa kike huitwa Boke, Robi, au Gati.

Mara baada ya haya, mtoto akaugua. Robi akamtafutia hirizi na madawa. Alishuku kuwa babu zake walikasirika. Ili kutaka kujua mzimu uliokasirika, alipiga bao. Aliyataja majina kadhaa ya mizimu ya ukoo wao, huku akisimamisha bangili yake juu ya jiwe dogo la mviringo ambalo lilitumika kwa kusagia mtama. Alipolitaja jina la Mirimo, bangili ilisimama sawa sawa juu ya jiwe, na toka pale Mirimo likawa jina la pili la mtoto. Kwa mastaajabu makubwa, homa ilimtoka, na alipoacha kunyonya, Mwita alirudishwa nyumbani kwa baba yake.

Alipokuwa na umri wa miaka mitatu, alivaa kipande cheupe cha ngozi ya mbuzi, na alikwenda kuchunga na ndugu zake. Hivi miaka ilipita, na Mwita alipata makamo na akawa mwenye nguvu.

Aliangushana mieleka na watoto wakubwa na kuwinda nao sungura kwa makundi ya mbwa wao. Wakati mwingine alitumwa kwenda kwa babu zake na huko alikaa muda kidogo kabla ya kurudi. Alipokwisha kuwa mtu mzima, alizikumbuka zaidi safari zake kuliko mambo mengine yote ya utotoni mwake.

Itaendelea. . . .
 
inaendelea....

Kando kando ya milima nyuma ya vibanda, kulijengwa safu za ngome za mawe makubwa, ambazo zimeachwa katika pori. Hapa walifanza michezo ya kutisha wakikumbuka hadithi walizosimuliwa na mzee Marwa juu ya vita vya zamani. Kila mara jirani walipokusanyika jioni na miraji yao mirefu, Marwa alikuwepo, akiyazungumza mambo ya zamani. Hakuna kati yao aliyemsikiza isipokuwa Mwita, kwa sababu walipendelea mambo ya kisasa. Lakini Marwa alizungumza mambo mengi ya zamani juu ya majengo ya mawe, wakati ambao ukoo wake walikuwa hodari zaidi kuliko ukoo mwingine katika Ukuria, na jinsi walivyoweza kujenga ngome imara milimani kuwazuia Wamasai. Wamasai walipoona vile, walishindwa na hawakurudi tena kuua vijana wao na kuteka ng'ombe wao. Pia alizungumza juu ya watoro walivyoomba amani kwa kumgusa adui yake kwa jani, au kukamata figa nyumbani kwa adui yake na kuliweka kitandani.

Hizi zilikuwa siku nzuri za zamani. Mambo yote ya zamani hayakufuatwa; ilikuwa ni bure tu kumtupia askari majani. Mwita alizipenda pia siku za kwenda sokoni kila juma, wanapoondoka wote kwenda Tarime, na kupumzika njiani kunawa mtoni. Walichukua vichwani mwao viazi vitamu, mihindi, vikapu vya mtama, na ndizi. Wakati mwingine walipeleka kondoo na mbuzi kuwauza. Hapa walifika kadiri ya Bakuria elfu mbili. Wengi wao walivaa shanga, bangili, heleni, na ngozi maridadi, au nguo mpya. Ng'ombe walichinjwa na vipande vikubwa vya nyama vilitundikwa juu ya matawi ya mrumba. Mahali pengine walikaa wasuka vikapu, katika vikundi, wakionyesha makapu yao marefu. Wafinyazi walikaa pamoja wakizunguukwa na mitungi mikubwa na midogo. Wauza ugoro walishughulika na biashara yao na huku wakisokota mishasha. Kulikuwapo vikapu vya tumbaku, na samaki wakavu waliletwa toka ziwani. Watu walipitapita huko na huko katika mavazi na mapambo ya kila aina vichwani na masikioni; pia walijipamba gurudumu za nyuzi, sazia, shaba, na vyuma vya namna mbali mbali, hata vijiti vilivyopakwa mafuta. Hewa ilichafuka kwa harufu ya moshi wa nyama, na mafuta ya ng'ombe. Wakati wa kiangazi zilichezwa ngoma nyingi; mashujaa na wasichana walivaa vizuri sana, na watoto wakiwaiga wakubwa wao. Hivi miaka mingi ilipita kwa furaha mpaka Mwita akawa na umri wa miaka kumi na nne, ndipo akatoja masikio; kwa sababu ni mila ya Bakuria kuyatoboa na kuyavuta masikio ya kila mvulana na msichana ili aweze kutundika mapambo ayapendayo. Masikio yaliyovutwa hivi, huwa ni kitu cha kujivunia sana, hata humlazimu mtu kumlipa mwenziwe ng'ombe iwapo amekikata kipande cha sikio hilo katika ugomvi.

Basi mara wazazi wa Mwita wakafanya mashauri ya kumwingiza jando. Wakuu walichagua siku fulani za mwezi unaofaa, wakati wa mavuno na wakawatahiri vijana wote waliochaguliwa. Iwapo mavuno si mema, mtemi huamuru jando isifanyike mpaka mwaka ufuatao. Lakini ilikuwa mwaka wa neema. Mwita alipewa ngao na mkuki na kwa muda wa miezi miwili, vikundi vya vijana hawa walipita huko na huko nchini katika mavazi ya vipande vya ngozi, kata za nyuzi za katani na kofia zilizopambwa manyoya ya jogoo.

Siku ilipowadia, watu walisafiri kwenda kwa ngariba ambaye aliwatahiri wale vijana alfajiri mapema wakati jua likichomoza. Mwita alivaa kivita. Aliitundika nguo begani na kuvaa kofia yenye manyoya ya simba. Alisindikizwa na ndugu zake. Walipofika, walisimama katika msitari, na walitishwa kwa fimbo na virungu na kuonywa wasiwe waoga. Ushujaa na uvumilivu yalikuwa ni mambo ya muhimu kwa kila anaye kuwa askari wa vita. Wakati jando ilipokwisha, watu walirudi majumbani kwao, mnamo saa tatu ya mchana.

Baada ya watoto kufanyiwa jando hiyo, baba yake huwa mzee wa kabila lao, na kufanya sherehe ya ngoma kwa cheo alichopata. Kwa hivi, hii ilikuwa tukio la pili nyumbani mwa Mwita. Wanawake walipika pombe kabla, na Chacha aliwaalika rafiki na ndugu zake kuhudhuria sherehe hizi. Ng'ombe watano walichinjwa kwa karamu hiyo, baada ya kila kitu kutayarishwa, Chacha alipewa na wazee kofia liyotengenezwa kwa manyoya ya simba. Vibuyu vitupu viliwekwa kwapani mwake, na mabegani walimvisha ngozi ya mbuzi. Kisha yeye pamoja na wazee watano, mkewe na mwanawe wa kwanza, walikwenda porini kwa siri. Na walipopata mahali pa faragha, kiongozi wa wale wazee aliwapa maziwa na asali, ambayo waliilamba na kuitema kama tambiko. Jua lilipotua, waliuzunguka pole pole na kwa utaratibu mti fulani waliouchagua. Usiku wote ule, Chacha alikaa zizini akinywa pombe na rafiki zake.

Siku ya pili wageni walifika. Mashujaa wakaja wamejipamba mavazi mazuri; kichwani walivaa vitambaa vyeupe virefu pamoja na shada nyeusi za manyoya ambayo yalining'inia pamoja na yale meupe ya mbuni. Nyuso zao walipaka rangi nyekundu na walivaa shanga shingoni na heleni nzito masikioni. Kifuani kila mmoja alivaa kitambaa cheupe ambacho kilifungwa na mkanda mweusi mpana na chini yake kipande cha ngozi ya chui kilifungwa kwa kuning'inia. Nyuma ya yule mtu, kulikuwa na ngozi ya sherehe iliyopakwa rangi nyekundu na ncha moja ilining'inia yenye shanga ndogo mkononi mwao. Kuanzia mabegani, walivaa ngozi nyeusi na nyeupe ya mbega.

Baada ya kusalimiana, mashujaa walivaa mitarawanda miguuni ambayo iliwafanya wawe warefu inchi tano zaidi. Kisha wakafanya duara huku njuga zikilizwa na mitarawanda yao iliyotiwa changarawe ilitowa sauti, na wote walivaa nguo za aina moja. Hapa walimkuta mkuu wa sherehe ambaye hakuvaa viatu wala manyoya. Alimkaribisha kila mgeni kwa wimbo na alitoa hotuba ya sifa huku ameshika vibuyu viwili mikononi vilivyo na changarawe na kuviliza. Kisha ngoma zikaanza kupigwa na michezo ikaanza upya. Mwanzo huwa pole pole, huku wachezaji wakizunguka kwa duara, na baadaye huinamisha manyoya na mavazi yao ya kipembea kama wenye wazimu, na mitarawanda ilitoa vishindo vikubwa ardhini.

Wanawake pia walijipaka rangi ile ile na miili yao iling'aa kwa mafuta. Walikuwa maridadi kwa shanga walizovaa, zenye rangi mbali mbali; mbele walivaa mlembe na nyuma ngozi ndefu iliyofungwa kiunoni na mkanda ulioshonelewa na majani. Bangili nzito za shaba zilibana mikono yao na kuivimbisha kuliko umbo la kawaida; walikuwa wenye furaha na hawakujali.

Baina yao Gati alikuwepo. Alivaa shanga kidogo kichwani mwake, na chini ya mdomo wake. Wakati Mwita amtupiapo jicho, alitazama chini kwa haya; lakini baadaye, wakati vijana waliposimama kwa safu ili wachaguliwe na wasichana kucheza nao, alikuja na akamgusa, lakini pia aliangalia chini. Bila ya kusema neno lolote alimfuata na kusimama mbele yake. Ngoma zilipigwa, mwanzo kwa taratibu, baadaye kwa upesi upesi, mpaka kwa ghafula zi lizimishwa, na yule mtu aliyekuwa na njuga ambaye aliimba kati ya wachezaji, aliwaita Mwita na Gati, na aliimba wimbo wa hatari Mwita alizopambana nazo, na jinsi alivyoonekana kama simba, alikuwa mwerevu na mwenye nguvu. Kisha wote waliimba, 'Muringa kurobe,' maana yake, 'Rudini kwenye safu zenu.' Wakati mwingine walipokuwa wakicheza, Mwita aliuchomeka mkuki wake ardhini mbele ya Gati ili asiondoke, na alimwimbia mambo yote ya ajabu aliyoyaona, na yote atakayofanya ya kumfurahisha.

Wakati huu wote, Chacha alikuwa akitembelea wageni wake amevaa joho na kibuyu na kofia ya ngozi ya simba. Baada ya siku kumi kupita aliruhusiwa kuyavua na akashika cheo chake kati ya wazee wa kabila lile.

Wakati michezo na karamu zilipokwisha, Mwita alipendezwa zaidi kumwona Gati, na alipoteza wakati mwingi kumtengenezea zawadi ndogo ndogo. Alimpelekea kibuyu kilichorembwa vizuri chenye mafuta; halafu alimtengenezea mkanda wa ngozi na baadaye alimchongea fimbo. Kwa hivi, baada ya muda, iliku- sudiwa kuwa Gati na Mwita waowane: lakini kabla ya kuwa hivyo ilitokea msiba nyumbani mwa Chacha. Usiku moja, wakati watu wote nyumbani wamelala, Mwita alishtuka usingizini akasikia sauti huko nje ya kibanda chake alikolala. Akamwamsha ndugu yake, wakachungulia nje kwenye mbalamwezi. Watu wawili walikuwa wakijaribu kufungua mlango wa zizi la ng'ombe. Wale vijana wawili walichukua virungu na wakatoka nje, wakatokea kwa nyuma ya wale wezi, kwa kuwa kibanda chao kilikuwa nje ya boma, wakawakamata kwa urahisi. Lakini yule Matiko, ndugu yake alipoanza kumshambulia mmoja wa wale wezi, yule mwizi aliushika mkuki wake na kumchoma yule kijana begani Mara wote mle nyumbani wakaamka kwa ghasia zile, wale wezi wakakamatwa na yule mtoto alipelekwa kibandani mwa mama yake. Siku ya pili wale wezi waliapishwa kiapo cha kimila, walilazimishwa kunywa damu ya makhsai wakinywea fuu la kichwa cha mtu aliye kufa kwa ugonjwa wa ukoma. Walipokuwa wakinywa, waliapa kwamba hawatarudia tena kuiba ng'ombe za wenzao.

Itaendelea...
 
Baada ya siku si nyingi, jeraha lile la Matiko halikuweza kupona, na siku moja jioni alipata homa kali, akafa. Kifo kisicho cha kawaida mara nyingi huwaogofya wenyeji wa Ukuria. Ndugu zake walimlilia halafu kilio chao kikabadilika kuwa mchezo wa kifo na wakaimba wimbo wa ukatili mtu anapouawa namna ile, "Tutakutupa kwa ndugu zako fisi.' Alitupwa porini akaliwa na fisi na hakuonekana hata mfupa mmoja, kwa sababu fisi hula mizoga ya namna yoyote.

Ingawa hivyo, pale nyumbani kulikuwa na huzuni na hofu kwa siku nyingi. Maiti yake yalitolewa nje kwenye tundu la uwa la boma ili mizimu isirudi kupitia mlangoni na kuwasumbua.

Baada ya muda, ule msiba ulisahauliwa na wakawa na mafikira ya kumwoza Mwita. Baada ya yote kukubaliwa, Mwita alichagua mbuzi kupeleka kwa mchumba wake. Rafiki zake walipofika na yule mbuzi nyumbani kwa msichana, walimjulisha kuwa mchumba wako yuko njiani anakuja. Hapo ikawa furaha kubwa kati ya wale vijana na wasichana, walijipaka mafuta na rangi na wakamvisha Gati nguo kwa umaridadi wake wote. Mara wakasikia sauti ya njuga za Mwita zikilia kwa mbali, alizovaa magotini, wote walitoka nje kwenda kumlaki, huku wakiimba na kucheza. Usiku ule Mwita alilala nyumbani kwa Gati, na asubuhi alirudi nyumbani kwake. Gati alimsindikiza, lakini alipoufikia mto wa kwanza alirudi, nyumbani kwa wazazi wake. Chacha na Robi walipomwona mtoto wao anarudi, nao wakafanya safari ya sherehe kwenda kwa wazazi wa mtoto wa kike. Lakini safari hii Mwita alibaki nyumbani. Kulikuwa sherehe kubwa nyumbani kwa bibi arusi. Mbuzi wa Mwita alichinjwa na kuchunwa vizuri. Ngozi ile ikafanywa kuwa vazi la bibi arusi, ngozi ya kichwani iliwekwa kando.

Kulikuwa na karamu kubwa ya nyama za mbuzi usiku ule, na wale wazee hawakurudi nyumbani mpaka asubuhi, walipomchukua Gati kwenda naye kwa bwana arusi. Wakati ule Mwita alikwisha waalika rafiki zake, wamkaribishe bibi arusi wake nyumbani, na walifika na kukaa nyumbani kwa baba yake. Wazazi wake walipofika pamoja na bibi arusi, Mwita alimkaribisha aingie ndani, lakini alikataa akijua ya kwamba lazima akaribishwe na mzee wa ukoo. Kisha Chacha alimkamata mkono na kumwingiza ndani.

Katikati ya shangwe walichukua kile kigozi cha kichwani na kukitoboa tundu. Walikitia ndani ya unga, halafu wakampa mgeni wa kwanza, huyu alijaribu kumvisha bibi arusi mkononi na kumwahidi kuwa atapata kondoo. Lakini aliweka mikono yake nyuma, 'Mbuzi je?' mgeni akamwuliza. Pia akakataa. 'Shillingi kumi basi'; hapo alimruhusu amvishe mkononi mara tano na akampa zawadi ya arusi.

Kile kigozi akapewa mgeni wa pili, ambaye alimtajia zawadi nyingi kila mara alikataa mpaka zawadi aliyoitaka alipotajiwa ndipo alimvisha kile kigozi vidoleni mara tano.

Ile ngozi iliachwa kwa wazazi wa Gati na ilipokauka walimpelekea Mwita ambaye alitumia siku nyingi kuitengeneza. Alipokwisha ilainisha na kutoa manyoya yote, aliirudisha kwa wakweze ambao waliipaka rangi nyeusi.

Vazi la Gati la arusi likawa tayari, na wazazi wake walipoondoka kwenda nyumbani kwa Chacha kufanya sherehe, Gati aliivaa, na arusi yake ikamalizika.

Mwita na ndugu zake wangali bado hai, lakini mwisho wa mwaka ule, mzee Chacha alikufa. Kwa maombolezo mengi walimzika ndani ya zizi la ng'ombe kama ilivyo desturi yao. Mwita na Gati sasa wana mtoto wa kiume, jina lake Chacha.

MWISHO​

Unaweza kuisoma hadithi hii na nyingine zaidi ya 100 bure ndani ya app ya Maktaba Sauti, inapatikana playstore
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom