Gwaride la uhuru lakosesha wanafunzi masomo! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Gwaride la uhuru lakosesha wanafunzi masomo!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by FJM, Nov 25, 2011.

 1. F

  FJM JF-Expert Member

  #1
  Nov 25, 2011
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 8,088
  Likes Received: 90
  Trophy Points: 145
  WANAFUNZI zaidi ya 5000 wa shule za msingi jijini Dar es Salaam, watakosa masomo kwa muda wa siku 40 kutokana na maandalizi ya sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Tanzania. Uchunguzi wa Tanzania Daima umebaini kuwa watoto hao ambao watalipwa kiasi kidogo cha sh 80,000 siku ya mwisho ya sherehe hizo kama posho ni wale wanaosoma darasa la tatu hadi la sita na wamechaguliwa kushiriki mazoezi ya gwaride la chipukizi yanayoendelea katika Uwanja wa Taifa na vituo vingine vilivyoko sehemu tofauti jijini Dar es Salaam. Mazoezi hayo yaliyoanza tangu Novemba Mosi, mwaka huu, yatahitimishwa siku ya kilele cha uhuru Desemba 9.

  Akizungumza na Tanzania Daima uwanjani hapo, mmoja wa waalimu anayesimamia mazoezi hayo alisema kuwa kituo hicho cha Uwanja wa Taifa ni moja ya vituo sita vilivyoko jijini kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi hao wa chipukizi.

  “Hilo la malipo mimi silijui wala kiasi wanachopewa, ila ninachojua mimi ni kwamba hawa wa hapa wanafika asubuhi ya saa 12 na saa sita wanapatiwa chakula kisha wanaondoka kurudi majumbani mwao na zoezi hili litaendelea hadi siku ya kilele cha nchi kutimiza miaka 50 ya uhuru,” alisema mwalimu huyo.

  Alibainisha kuwa suala la kusoma kwa wanafunzi hao lipo mikononi mwa Wizara ya Elimu pamoja na ile ya Tamisemi kwa kile alichoeleza ndiyo waratibu wa shughuli hizo kwa wanafunzi hao. Hata hivyo Tanzania Daima lilishuhudia wanafunzi hao wakipatiwa chakula majira ya saa nane mchana tofauti na maelezo ya saa sita aliyosema mwalimu huyo.

  Aidha maelezo ya mwalimu huyo kuwa wanafunzi wanaoshiriki gwaride hilo ni wa darasa la tano na la sita yalitofautiana na baadhi ya wanafunzi waliosema wanasoma darasa la tatu katika shule ya msingi Mgulani. Wanafunzi hao waliokuwa wakiongea na mwandishi wa habari hizi kabla hawajaondolewa na ofisa wa jeshi la polisi aliyekuwepo uwanjani hapo walisema kuwa wameahidiwa kiasi cha shilingi 35000 baada ya sherehe na kwa sasa wanajitegemea nauli ya kwenda na kurudi majumbani mwao kwa kuwa bado hawajapewa fedha hizo.

  Wakati wanafunzi hao wakiwa katika hatari hiyo ya kukosa masomo, walimu wanaosimamia zoezi hilo, wamelalamikia usiri unaofanywa na waratibu wa zoezi hilo katika suala zima la malipo kwa kile walichodai wanalipwa viwango tofauti wakati kazi wanayoifanya ni ya aina moja.

  “Tumeanza kulipwa jana sisi na wanafunzi, walimu tumelipwa kwa viwango tofauti wapo waliolipwa kwa hesabu za shilingi 20,000 kwa siku na wengine 50,000 kwa siku ila wanafunzi wanapewa hesabu ya 2000 tu kwa siku na jana ndiyo tumeanza kulipwa hela za siku 20 tokea tumeanza zoezi hili Novemba mosi,” alisema mwalimu huyo.

  Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Meck Sadiky alipotakiwa kulitolea ufafanuzi suala hilo, alisema atafutwe mratibu wa shughuli hizi kimkoa aliyemtaja kwa jina moja la Ngali. Ngali alipopigiwa simu alikataa kuongea na kumtaka mwandishi amtajie mtu aliyempa namba zake, licha ya kutoa idadi ya wanafunzi 5000 kuwa ndiyo wanaoshiriki.
  SOURCE TANZANIA DAIMA

  Maoni yangu:
  Kwa nini hawa watoto wasifanye mazoezi kwa nusu siku ili waweze kuhudhuria masomo walao ya asubuhi? Nina hakika hizi ni shule za wakina sisi, watoto wa wakubwa watakuwa wanaendelea na masomo kama kawaida kwenye shule zao za international!

   
Loading...