KWELI Graca Machel ni mwanamke aliyewahi kuolewa na marais wa nchi mbili za Msumbiji na Afrika Kusini

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Graca-Machel-m.jpg


Graca Machel ni mwanamke anayetajwa kuwa na historia ya kuolewa na marais wa nchi mbili tofauti za Msumbiji na Afrika Kusini. Madai haya yanafafanua zaidi kuwa huyu ni mwanamke pekee aliyewahi kupata bahati hiyo.
 
Tunachokijua
Taarifa zinazomhusisha Graca Machel kama mwanamke aliyewahi kuolewa na marais wa nchi mbili tofauti (Msumbiji na Afrika Kusini) zimekuwepo wa muda mrefu.

Mathalani, Julai 25, 2023, mtumiaji wa mtandao wa twitter anayefahamika kwa jina la Getrude Mligo aliweka ujumbe unaosimulia furaha ya kutimiza ndoto yake ya kukutana na Graca Machel, mwanamke aliyemtaja kuwa mke wa marais wa nchi mbili tofauti,

Getrude aliandika;

"Moja ya ndoto yangu kubwa sana jana imetimizwa. I finally met mama Graca Machel. Akiwa na miaka 29, alikua Waziri wa Elimu, na Utamaduni Mozambique kwa muda wa miaka 14. First Lady wa marehemu, Samora Machel. First Lady wa marehemu, Nelson Mandela. I also Learnt a lot"

Mtumiaji mwingine wa mtandao huo anayefahamika kwa jina la Bonge la Afya aliweka mkazo kwa kuandika;

"Amekua first lady wa nchi mbili Msumbiji na Afrika kusiki."

Bila shaka alimaanisha Afrika Kusini na sio Afrika Kusiki.

Watumiaji wengine pia wa mitandao ya kijamii ikiwemo Polymath Thread, Julai 19, 2023 aliweka ujumbe wenye dokezo la mwanamke huyu kuolewa na marais wawili tofauti.

JamiiForums imeduatilia suala hili kwa undani wake na imekuja na taarifa za kina zinazomhusu mwanamke huyu.

Historia yake
Graça Simbine Machel alizaliwa Oktoba 17, 1945, huko Gaza, Msumbiji , akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto sita. Baba yake, mhudumu wa Kanisa la Kimethodisti ambaye alifariki wiki tatu kabla ya yeye kuzaliwa, aliacha maagizo ya wazi kwamba ndugu zake wakubwa walipaswa kuhakikisha wanamhudumia na kumsaidia hadi afikie elimu ya upili.

Baada ya hapo, ufadhiri wa kanisa ulimwezesha kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Lisbon (Ureno) mnamo 1968.

Akiwa chini ya uangalizi wa polisi wa siri wa Ureno, alilazimika kuacha masomo yake na kukimbilia Uswizi ili kuepuka kifungo ambacho kwa hakika kilikuwa kinamngoja kutokana na shughuli zake za kisiasa alipokuwa mwanafunzi.

Mnamo 1973, alipokuwa Ulaya alijiunga na Chama cha Ukombozi cha Msumbiji (FRELIMO), vuguvugu lililolenga kuendeleza mapambano dhidi ya ukoloni wa Wareno.

Kuolewa na marais wawili tofauti
JamiiForums imebaini kuwa madai ya Graca kuolewa na marais wa nchi mbili tofauti yana ukweli. Hata hivyo, ndoa ya pili ilitokea baada ya kufariki kwa mume wa kwanza mnamo mwaka 1986.

Katika harakati za kupigania uhuru zilizoongozwa na chama cha FRELIMO, Graca alikutana na Samora Machel, kamanda wa FRELIMO ambaye baadae alikuja kuwa mume wake na Rais wa kwanza wa Msumbiji huru.

20060629111717Machel_Nkomati.original.jpg

Graca Machel akiwa na Samora Machel
Msumbiji ilipopata uhuru na FRELIMO kuunda Serikali ya kwanza ya nchi hiyo mwaka 1975, Machel akawa mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho na Waziri wa Elimu na Utamaduni hadi mwaka 1989.

Kufuatia kifo cha Rais Machel katika ajali ya ndege tarehe Oktoba 19, 1986, Graca alijiuzulu wadhifa wake kama Waziri wa Elimu, na kuacha nyuma rekodi bora ya watoto milioni 1.5 shuleni, dhidi ya 400,000 alipokuwa amechukua wadhifa huo. Kama Waziri wa Elimu kwa serikali mpya, aliweza kupunguza kiwango cha kutojua kusoma na kuandika kwa 72%.

Mhoje_mbuzini_photo_jpg.jpg

Ajali ya Ndege iliyoondoa uhai wa Samora Machel
Urafiki kati ya Graca na Nelson Mandela, Rais wa zamani wa Afrika Kusini unatajwa kuanza mwaka 1992 wakati Graca akiwa Afrika Kusini kupokea tuzo ya Udaktari wa heshima, kisha kuoana mnamo Julai 18, 1998 wakati Mandela akisherekea miaka 90 ya kuzaliwa kwake.

Katika mahojiano na CNN mwaka 2008 ,Graca Machel alisisitiza kuwa tofauti ya umri wa miaka 25 haijawahi kuwa tatizo kati yake na Nelson Mandela.

"Yeye ni mume mzuri. "Tulikutana katika maisha wakati wote tulikuwa tumetulia. Tulikuwa watu wazima, tulikuwa tumekaa, tulijua thamani ya mwenza, ya mpenzi. Kwa sababu hiyo, tumefurahia uhusiano huu kwa namna ya pekee.

"Sio kama ukiwa bado mdogo, unadai sana. Hapana, hapana. Tunakubalina tu jinsi tulivyo. Na tunafurahia kila siku kana kwamba ni siku ya mwisho. Kwa sababu hiyo, imekuwa nzuri kuwa naye kama mume."


100802486-76482679.jpg

Graca Machel akiwa na Nelson Mandela
Mnamo 2018 alitunukiwa tuzo ya juu zaidi ya Shirika la Afya Duniani, Medali ya Dhahabu ya WHO, kwa mchango wake mkubwa kwa afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana.

Graça Machel amejitolea maisha yake kuboresha hali za wanawake na watoto, kuwapa matumaini na kuwatia moyo, na kujenga ulimwengu wenye haki na usawa kwa wote.
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom