Ghadafi ni kiongozi Mujarabu

Ghadafi ni kiongozi Mujarabu

Comred Mbwana Allyamtu

JF-Expert Member
Joined
Jun 28, 2016
Posts
362
Reaction score
909
d02f2e3e3c5f21df80c75229516e47da.jpg


"NI--Blaise Compaore, Gaddafi na Charles Taylor
NA NI--Kiu ya mabadiliko iliwaingiza Ikulu kishujaa
NA NI--Ulafi wa madaraka ukawang’oa kwa fedheha"

Na: Comred Mbwana Allyamtu

OKTOBA ni mwezi wa kihistoria kwa aliyekuwa Rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore. Ni mwezi huo huo alipoingia madarakani mwaka 1987 na mwezi huo huo, kwa tofauti ya siku 15 tu, alipong’oka madarakani mwaka huu, 2014.
Compaore ni rafiki wa Charles Taylor na Muammar Gaddafi, wote wameingia madarakani kwa mapinduzi ingawa yale yaliyomwingiza Gaddafi hayakuwa ya umwagaji damu tofauti na marafiki zake hao.

*BLAISE COMPAORE NI NANI*

Blaise Compaoré alizaliwa Februari 3, mwaka 1951 na amekuwa Rais wa Burkina Faso kuanzia mwaka 1987 hadi alipojiuzulu kwa shinikizo Oktoba 31, 2014.
Huyu alikuwa mshirika na rafiki wa karibu wa Rais aliyekuwa madarakani miaka ya 1980 nchini Burkina Faso, Thomas Sankara na Oktoba, mwaka 1987, Compaore aliongoza mapinduzi yaliyosababisha mauaji ya Sankara. Baada ya mauaji hayo, Compaore aliingia madarakani na baadaye kushinda chaguzi zilizofanyika nchini humo; mwaka 1991, 1998, 2005 na 2010.

Kilichosababisha kulazimika kujiuzulu kwa Compaore ni tamaa ya kuendelea kubaki madarakani, kama ilivyokuwa kwa Gaddafi aliyedumu Ikulu ya Tripoli kwa miaka 42, lakini Compaore yeye akidumu kwa miaka 27 ingawa inawezekana alilenga kukaa zaidi ya hapo hata kuvunja rekodi ya Gaddafi.
Compaore pengine kutokana na utamu wa Ikulu, alidaiwa kuanza mchakato wa kubadilisha Katiba ya nchi yake ili aweze kudumu madarakani.
Kuna jambo moja la kukariri hapa, kama ilivyoelezwa awali, ni kwamba mwezi huo huo wa Oktoba pale alipoongoza mapinduzi yaliyomng’oa na kumuua mshirika wake wa awali, Sankara, ndio mwezi huo huo naye alishinikizwa kujiuzulu madarakani. Kwa Sankara ilikuwa Oktoba 15 mwaka 1987 lakini kwake ni Oktoba 31, 2014, yaani miaka 27 baadaye.

Compaoré alizaliwa katika mji wa Ziniaré, uliopo umbali wa kilomita 43 kutoka Jiji la Ouagadougou, ambao ndiyo mji mkuu wa Burkina Faso, alipitia mafunzo ya kijeshi akiwa amefikia cheo cha kapteni.
Alikutana na Thomas Sankara mwaka 1976 katika mafunzo ya kijeshi Morocco na hapo walianza urafiki wao uliokuwa wazi kwa karibu watu wote waliokuwa wakiwafahamu.
Compaoré ni gwiji wa kung’oa watu madarakani na ugwiji wake huo unathibitishwa na mchango wake mkubwa katika kuwang’oa kwa mapinduzi ya kijeshi Saye Zerbo na Jean-Baptiste Ouedraogo. Ni gwiji wa kung’oa watu madarakani ambaye hakusahau maisha ya ndoa, akiwa amefunga ndoa na Chantal Terrasson, mwaka 1985.
Katika utawala wa rafiki yake (Sankara), ulioanza mwaka 1983 hadi mwaka 1987, Compaoré aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, akiwa amepata kutumikia cheo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Naibu Waziri wa Sheria.
Ni mwanzilishi wa chama chake cha Congress for Democracy and Progress, akihusika katika mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1983 na yale ya mwaka 1987. Miaka mitatu baada ya kufanya mapinduzi na kuingia Ikulu, alichaguliwa rasmi Rais wa Burkina Faso kwa kura mwaka 1991, katika uchaguzi uliosusiwa na upinzani na kisha alichaguliwa tena kwa njia hiyo ya kura katika chaguzi za mwaka 1998, 2005 na 2010.
Alikuwa gwiji wa kushiriki mapinduzi ya kung’oa na kupachika watu madarakani na katika kuthibitisha hilo, akiwa na umri wa miaka 33, Blaise Compaoré aliratibu mapinduzi ya kijeshi yaliyomng’oa madarakani Meja Jean-Baptiste Ouedraogo nchini Liberia, hiyo ilikuwa Agosti 4 mwaka 1983. Wakati huo Burkina Faso ilikuwa ikiitwa Upper Volta.

Mapinduzi hayo ya kijeshi yaliungwa mkono na Libya chini ya Muammar Gaddafi rafiki wa Compaore, kwa wakati huo, Libya ikiwa katika msuguano na Ufaransa kuhusu Chad.
Washirika wengine wa mapinduzi hayo ya Agosti 4, mwaka 1983 ni Kapteni Henri Zongo, Meja Jean-Baptiste Boukary Lingani na Kapteni Thomas Sankara— aliyetangazwa Rais kuwa katika mapinduzi hayo ya kijeshi.
Compaore aliingia madarakani Oktoba 15 mwaka 1987 na ameondoka madarakani Oktoba 31, 2014. Kwa vyovyote vile, mwezi wa Oktoba ni mwezi muhimu katika historia ya maisha yake na hata familia yake, bila kusahau historia ya taifa lake.
Compaoré wakati huo alipofanya tena mapinduzi ya kijeshi mwaka 1987, alizungumzia mauaji ya rafiki yake wa jeshini zamani (Rais Sankara) ambaye alimsaidia kuingia Ikulu (mwaka 1983) akisema ilikuwa ajali tu.
Hata hivyo licha ya kuongoza mapinduzi ambayo si tu yalimng’oa rafiki yake huyo madarakani bali hata kumuua, licha ya kukaa kwake Ikulu kwa miaka 27, Compaore hakuwahi kuchunguza sababu za mauaji hayo ya Sankara, jambo linalozua hisia kwamba alishiriki kuhakikisha Sankara anauawa ili mapinduzi yatimie bila kauli za lawama kutoka kwa swahiba wake huyo.
Lakini mambo hayakuishia tu kwa Sankara, Compaore pia aliwahi kuwatia msukosuko makomredi wenzake wa mapinduzi ya 1983, yaani Henri Zongo na Jean-Baptiste Boukary Lingani, ambao Septemba 1989 aliwatia nguvuni na kuwashitaki kwa madai ya kutaka kuipindua serikali yake.
Baada ya chaguzi za mwaka 1991 na 1998 alizochaguliwa kuwa Rais, baadaye Agosti mwaka 2005, alitangaza nia yake ya kutaka kuwania urais katika uchaguzi uliokuwa ukifuata.

Hapo, wanasiasa wa upinzani walitafsiri kwamba nia yake hiyo ni kinyume cha matakwa ya Katiba ambayo ilikuwa imekwishafanyiwa marekebisho mwaka 2000, ikiweka ukomo wa urais kwamba ni mihula miwili yenye urefu wa miaka mitano kutoka saba ya awali.
Hali hii ni kama ile iliyotaka kutokea Zanzibar wakati wa utawala wa Rais Dk. Salmin Amour kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2000, sababu ni zile zile, kwamba wapambe wa Compaore walifanya walichoweza na Oktoba mwaka 2005 Baraza la Katiba Burkina Faso lilifanya uamuzi kwamba, kwa sababu Compaoré alikuwa rais aliyekuwa madarakani mwaka 2000 (wakati Katiba inafanyiwa mabadiliko), mabadiliko hayo yaanze kutumika pindi atakapomaliza muhula wake wa pili na kisha ataweza kushiriki uchaguzi unaofuatia kwa Katiba mpya, mwaka 2005.
Novemba 13 mwaka 2005, Compaoré alichaguliwa tena kuwa Rais akiwashinda wagombea wengine 12 akipata kura kwa kiwango cha asilimia 80.35 ya kura zilizopigwa.
Kati ya mambo ambayo hawezi kuyasahau licha ya utamu wa Ikulu ni tukio la Aprili 14 mwaka 2011, alipolazimika kutoroka Jiji la Ouagadougou kwenda mji wake wa asili wa Ziniare, baada ya askari kufanya uasi kutokana na kutolipwa posho zao. Fujo hizo za askari zilifika hadi Ikulu na katika baadhi ya kambi za jeshi, Compaore hakuwa na namna licha ya uaskari wake na ugwiji wa kung’oa watu madarakani, isipokuwa kutoroka.

Utamu wa Ikulu si haba, Juni mwaka huu wa 2014 chama tawala cha Compaoré, CDP, kilimshawishi kiongozi huyo aitishe kura ya maoni itakayotoa matokeo yatakayomwezesha kufanya mabadiliko ya Katiba ili aweze kuwania tena urais mwakani (2015), kinyume cha hapo, kwa mujibu wa matakwa ya Katiba alipaswa kuondoka madarakani kwa kuwa mihula ya urais kikatiba imetimia miwili.
Hakujua kuwa huo ndio uliokuwa mwisho wake Ikulu na pengine hakuwa na kumbukumbu nzuri kwamba Oktoba ni mwezi wake wa kihistoria, naam, ilipofika Oktoba 30, 2014 Bunge la Burkina Faso lilipanga kufanya vikao kwa ajili ya mabadiliko ya Katiba kwa lengo la kumwezesha Compaore agombee tena katika Uchaguzi Mkuu wa urais, 2015.

Wapinzani wake walifanya maandamano, wakirusha mawe na kufanya mashambulizi mengine dhidi ya majengo ya Bunge jijini Ouagadougou, uvamizi wa ofisi na wizi ni vitendo vilivyochukua nafasi kubwa katika tukio hilo la maandamano.
Kwa mtazamo wake Msemaji wa Upinzani, Pargui Emile Paré, kutoka Chama cha Federal alitafsiri tukio hilo ni Vuguvugu la Jeusi Burkina Faso (Burkina Faso’s black spring).
Kwa kumbukumbu Arab Spring ndilo vuguvugu lililouangusha utawala wa Zine El Abidine Ben Ali wa Tunisia, Rais wa pili wa nchi hiyo aliyeongoza kati ya mwaka 1987 hadi 2011 alipoangushwa. Pia ni vuguvugu lililomng’oa Rais wa Nne wa Misri, Muhammad Hosni El Sayed Mubarak, aliyeongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1981 hadi 2011.
Kwa hiyo, Compaoré alijitutumua katika mazingira ya kutapatapa, akavunja serikali na hata kufikia hatua ya kutangaza hali ya hatari, akiahidi kutaka kushirikiana na upinzani kutafuta ufumbuzi lakini vyote havikufua dafu.
Hakuna marefu yasiyo na nchi. Oktoba 31, 2014 Compaoré alitangaza mwenyewe kwamba anaondoka madarakani, akisema Ikulu iko wazi na uitishwe uchaguzi huru na wa haki ndani ya siku 90.

*Urafiki wa Compaore, Taylor na Gaddafi*

Ni Compaoré ndiye aliyemtambulisha Charles Taylor kwa rafiki yake mwingine kipenzi, aitwaye Muammar Gaddafi. Compaoré huyu ndiye aliyempa msaada mkubwa Taylor mwanzoni mwa miaka ya 1990.

*CHARLES TAYLOR NI NANI*

Charles McArthur Ghankay Taylor, ni mkubwa kwa Compaore kwa miaka 3, akiwa amezaliwa Januari 28, mwaka 1948. Taylor ni Rais wa 22 wa Liberia, akiwa ametumikia nchi hiyo kuanzia Agosti 2 mwaka 1997 hadi alipojiuzulu Agosti 11, mwaka 2003.
Utaona kwamba kwa Compaore na Taylor hawakuwa tu marafiki wa kawaida bali pia miezi yao ya kuingia katika Ikulu za nchi yao inafanana na miezi yao ya kung’oka Ikulu, Compaore aliingia OKTOBA 15 (1987) na kung’oka OKTOBA 31 (2014), Taylor naye aliingia AGOSTI 2 (1997) akang’oka AGOSTI 11 (2003).
Taylor alizaliwa Arthington, Jimbo la Montserrado nchini Liberia, ni msomi aliyepata shahada yake ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Bentley Marekani na alipata kufanya kazi katika Serikali ya Samuel Doe.

Baada ya kung’olewa katika serikali hiyo kwa tuhuma za ubadhirifu alikwenda Libya ambako alipata mafunzo ya kuwa mpiganaji wa msituni.
Alirudi Liberia mwaka 1989 akiongoza kundi la upinzani lililoitwa National Patriotic Front of Liberia, lililokuwa na lengo la kuung’oa utawala Samuel Doe, Taylor akawa mwanzilishi wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya kwanza nchini Liberia, kati ya mwaka 1989 hadi 1996.

Baada ya mauaji ya Samuel Doe, Taylor akawa na nguvu katika eneo kubwa la Liberia, akitambulika kuwa miongoni mwa wababe wa kivita vinara Afrika. Kutokana na kuwapo kwa mpango wa amani uliolenga kukomesha mapigano Liberia, Taylor akiwa na umaarufu wa kutosha hatimaye akachaguliwa kuwa Rais wa Liberia, mwaka 1997.
Akiwa ofisini, Taylor alikumbwa na kashfa mbalimbali za uhalifu wa kivita na hata ukatili dhidi ya binadamu, akitajwa kuhusika katika uchochezi wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone, mwaka 1991 hadi 2002.
Ndani ya nchi yake, upinzani dhidi yake ulishamiri na kuzusha vita nyingine ya wenyewe kwa wenyewe ya pili kati ya mwaka 1999 hadi 2003. Lakini katika mwaka huo wa 2003, Taylor alikuwa amepoteza sehemu kubwa ya nguvu zake pembezoni mwa nchi na mwaka huo huo alijiuzulu baada ya kuwapo kwa shinikizo kubwa la kimataifa na akatoroka kwenda uhamishoni nchini Nigeria.
Alikutwa na hatia katika Mahakama ya Kimataifa Aprili mwaka 2012, kwa makosa 11, yakiwamo ugaidi, mauaji na ubakaji. Mei mwaka 2012, Taylor alihukumiwa kifungo cha miaka 50 jela.
Kama ilivyo kwa Compaore aliyesaidia mapinduzi yaliyomweka madarakani Sankara, Taylor naye alisaidia mapinduzi ya kijeshi ya Aprili 12, mwaka 1980 yaliyokuwa yakiongozwa na Samuel Doe, ambayo hatimaye yalisababisha mauaji ya Rais wa wakati huo wa Liberia, William R. Tolbert na Doe akaingia Ikulu.

Kwa kumbukumbu tu ni kwamba, Rais Tolbert aliwahi kutoa mhadhara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wasomi wa wakati ule wa ujana wao, akina Profesa Issa Shivji na wengine wengi wanafahamu hili, kimsingi Tolbert alikuwa rafiki wa Tanzania pamoja na Rais Julius Nyerere.

Baada ya Doe kuingia madarakani, Taylor aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Jumla wa Huduma (GSA), akiwa na mamlaka ya kufanya ununuzi unaohitajika kwa Serikali ya Liberia. Alifukuzwa kwa ubadhirifu Mei mwaka 1983 akitajwa kufuja dola za Marekani takriban 1,000,000 na kuzituma katika akaunti yake katika moja ya benki zilizoko Marekani.
Baada ya ubadhirifu, Taylor alitorokea Marekani lakini alikamatwa Mei 21 mwaka 1984 na kurudishwa Liberia kujibu mashtaka ya ubadhirifu wa fedha za serikali dola za Marekani milioni moja, alipokuwa bosi wa GSA.
Septemba 15 mwaka 1985, Taylor na wafungwa wenzake wengine wanne walitoroka jela. Desemba 1989, Gaddafi, mbali na kumwezesha Taylor kupata mafunzo kama mpiganaji wa msituni pia alisaidia upatikanaji wa fedha kupitia mfuko maalumu ulioratibiwa nchini Ivory Coast ambao fedha zake ndizo zilizompa nguvu Taylor kumng’oa Samuel Doe, na kupitia vita ya kwanza ya wenyewe kwa wenyewe Liberia.
Kati ya mambo ya kukumbukwa ni pale mara baada ya kuhimitishwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Liberia (ya kwanza) mwaka 1996, Taylor akiwa anagombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 1997. Alikuwa akifanya kampeni akitumia kaulimbiu mashuhuri kwamba “..amemuua mama, amemuua baba lakini nitampigia kura.
Kama ambavyo Gaddafi alimsaidia Taylor kumng’oa Samue Doe kwa kuanzisha vita ya wenyewe kwa wenyewe, ndivyo hivyo pia Taylor naye akiwa Rais anadaiwa kusaidia kuanzishwa kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone, akitajwa kuwasaidia waasi wa Revolutionary United Front (RUF) kwa kuwauzia silaha.
Katika harakati zake na hasa pale alipokuwa akituhumiwa kwa kufanya mauaji, Taylor amekuwa akitamka kwamba; “...hata Yesu alituhumiwa kwa mauaji nyakati zake.”
Kwa shinikizo kama ilivyo kwa Compaore, Taylor naye alijitokeza kwenye televisheni Agosti 10, akitangaza kwamba ataachia madaraka siku inayofuata kwa Makamu wa Rais Blah.

*KANAL GADDAF NI NANI*

Gaddaf; rafiki yao wa maarifa

Kama ilivyo kwa wenzake, Compaore na Taylor, Muammar Muhammad Abu Minyar al-Gaddafi naye aliingia madarakani baada ya mapinduzi ya kijeshi, ni maarufu kama Kanali Gaddafi, hata hivyo, wakati Compaore akiwa amebweteka madarakani miaka 27, Gaddafi yeye alikaa madarakani akiwa kiongozi wa Libya kwa karibu miaka 42.
Kwa ujumla marafiki hawa watatu, Gaddafi, Compaore na Taylor wameondoka madarakani si kwa mapenzi yao bali shinikizo ambalo kwa namna fulani chimbuko lake ni umma ingawa ndani yake kuna mikono mingine ya kidola na ya nje (Gaddafi) isiyohusiana na umma wa nchi husika moja kwa moja.
Tofauti na wenzake hao, Gaddafi aliingia madarakani kwa mapinduzi yasiyokuwa ya umwagaji damu, akitwaa madaraka hayo kutoka kwa utawala wa kifalme wa Mfalme Idris na moja kwa moja kujitawaza kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (Revolutionary Command Council - RCC). Aliufutilia mbali utawala wa kifalme na kugeuza nchi yake kuwa Jamhuri, akitawala kwa kutoa amri ya rais (decree), akiiweka nchi yake karibu zaidi na mataifa ya kiarabu.

Muammar Gaddafi alizaliwa kijijini Qasr Abu Hadi, nje ya mji wa Sirte, magharibi mwa Libya. Hadi leo haijulikani tarehe na mwaka rasmi ambao kiongozi huyo alizaliwa kutokana na wazazi wake, Baba yake Mohammad Abdul Salam bin Hamed bin Mohammad, maarufu kwa jina la Abu Meniar na Mama yake, Aisha, kutotunza kumbukumbu za kuzaliwa kwa mtoto wao huyo, ni wazazi ambao hawakuwa na elimu, inadhaniwa alizaliwa kama si mwaka 1942 basi 1943, lakini zikiwamo taarifa nyingine kwamba alizaliwa kabla ya 1940.

Maisha ya Gaddafi hayakuwa ya mteremko, familia yake haikuwa na uwezo wala elimu lakini baba yake aliona umuhimu wa elimu na hivyo alijitahidi kugharimia elimu ya mwanawe, katika siku za wiki Gaddafi alikuwa akilala msikitini na siku za mwisho wa wiki alilazimika kutembea mwendo wa maili 20 kuwatembelea wazazi wake.
Walimu wengi katika moja ya shule alizosoma Gaddafi, Sabha, walikuwa wenye asili ya Misri na akiwa shuleni hapo kwa mara ya kwanza Gaddafi aliweza kupata nakala za magazeti na kusikiliza matangazo ya redio hasa kutoka Cairo. Gaddafi alivutiwa na mabadiliko ya kisiasa yaliyokuwa yakifanyika katika Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, akimtambua Rais Gamal Abdel Nasser wa taifa hilo kuwa ndiye shujaa wake. Nasser alikuwa akipigania kuundwa kwa taifa la Kiarabu; akipinga ukoloni wa Magharibi na ukoloni mamboleo na mabadiliko kutoka kwenye ubepari hadi ujamaa.
Kitabu cha Nasser, Falsafa ya Mapinduzi, ni kati ya mwongozo uliomshawishi Gaddafi; kupanga mapinduzi nchini mwake.
Gaddafi aliratibu maandamano na kusambaza waraka huko na huko kupinga utawala wa kifalme Libya.

Gaddafi alipata mafunzo ya kijeshi mwaka 1963, Benghazi. Jeshi la Libya lilikuwa likipewa mafunzo na wanajeshi wa Uingereza, Gaddafi alikuwa akiwaona Waingereza kuwa ni mabwanyenye tu na kwa hiyo, alikataa kujifunza Kiingereza, akijenga tabia ya ugaidi kwa maofisa wa kijeshi wa Uingereza na akafeli mtihani wa kijeshi.
Agosti mwaka 1965, Gaddafi alihitimu mafunzo yake ya kijeshi. Aprili mwaka 1966, alitakiwa kwenda Uingereza kwa ajili ya mafunzo zaidi ya kijeshi, ilibidi afanye kwanza kozi ya Kiingereza kwa zaidi ya miezi tisa.

Hatimaye akafanikiwa kujua lugha ya Kiingereza na akapewa mafunzo ya kijeshi katika kitengo cha mawasiliano. Maofisa wa kijeshi waliokuwa wakimfundisha walipata kuweka wazi kwamba Gaddafi ni kati ya watu wanaochukia Kiingereza.
Kwa asili unaweza kusema Gaddafi alikuwa ni mpenda vita (ukombozi?), akipata kusaidia makundi mbalimbali ya kijeshi katika nchi kadhaa duniani..................... Mendelezo wake utaupata kwenye kitabu changu ambacho kiko kwenye mchakato wa kukamilika.........

Kwa leo ngoja niitue chini kalam na niishie hapa kwa chakula cha ubongo zaidi endelea kufatilia makala zangu ujue nini kitakacho endelea juu ya kitabu changu.

" Mungu ibariki Afrika mungu baliki fikra huru za waafrika"

Ndimi.
Comred Mbwana Allyamtu

b940e29001585338509fc950f7ccbebc.jpg
 
Back
Top Bottom