Gaddafi azikwa kwa siri jangwani

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
BAADA ya maiti ya aliyekuwa kiongozi wa nchini Libya, Kanali Muammar Gaddafi, kukaa kwa muda wa siku nne ndani ya bucha katika mji wa Misrata, hatimaye uongozi wa Serikali ya Mpito (NTC), umeamua kuizika kwenye jangwa moja la siri nchini hapa.
Mwili wa kiongozi huyo umezikwa sehemu moja na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi na mtoto wake mkubwa ambaye naye aliuawa katika mapambano yaliyofanyika nje kidogo ya jiji la Sirte, Mutassim.
Msemaji mmoja wa Baraza la Kitaifa la Mpito (NTC), Ibrahim Beitalmal, amelieleza Shirika la BBC kwamba miili ya watu hao imezikwa siku chache baada ya kutokea utata wa mahali sahihi palipofaa kuzikwa kiongozi huyo.
Kabla ya serikali hiyo kusimamia maziko ya kiongozi huyo mwili ulikuwa ukiombwa na jamaa zake kwa ajili ya kuuzika katika jiji la Sirte mahali alipozaliwa ombi ambalo lilipingwa na viongozi wa NTC.
Taarifa zingine zinamnukuu msemaji wa NTC, Beitalmal, akisema kuwa maziko hayo yalihusisha jamaa wachache wa familia ya Gaddafi ambao walimzika kwa utaratibu wa imani ya Kiislam ikiwa ni pamoja na kumuombea dua.
Baadhi ya mashuhuda wa mjini Misrata wanasema kuwa miili ya watu hao iliondolewa usiku wa juzi eneo iliyokuwa imehifadhiwa kwa ajili ya kupanga maziko yao.
Kabla ya kuzikwa raia wa Libya wamekuwa wakitembelea eneo hilo la Misrata kujionea mwili wa kiongozi huyo ili kuuaga kwa mara ya mwisho hali ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwenda kinyume na utaratibu wa imani ya dini ya Kiislam.
Sababu ya kuzikwa kwa kiongozi huyo katika sehemu ya maficho badala ya ile ya wazi ni viongozi wa NTC kuhofia kaburi lake kugeuzwa kuwa mahali patakatifu na wafuasi wake.
Pamoja na hilo mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza uongozi wa NTC kufanya uchunguzi kuhusu kifo cha Kanali Gaddafi kwani picha za awali zilionyesha alikamatwa akiwa hai.
Kiongozi wa NTC, Mustafa Abdul Jalil, ameahidi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kifo cha Gaddafi ingawa mara kadhaa amekuwa akipinga kutomtambua aliyemuua kiongozi huyo.
Hata hivyo wadadisi wa mambo wa mjini hapa wana wasiwasi wa kutofanyika uchunguzi huru kwani haujahusisha mashirika ya kujitegemea.
 
Back
Top Bottom