Fundisheni watoto wenu uzalendo, msiwafundishe chuki

Mhaya

JF-Expert Member
Aug 20, 2023
1,658
4,861
Ukiwa mfanyabiashara, kitu cha kwanza ni kuongeza thamani yako, uweke mazingira mazuri ya wateja kukipenda kitu chako. Ni sawa na nchi, ni lazima viongozi waweke mazingira rafiki kwa ajili ya kuwavutia watu wa nje.

Ni lazima usimamie amani, hata kama kuna vita, simama na kusema nchi yetu ni ya amani. Hata kama kuna mazingira mabovu, basi ruhusu picha zinazopigwa ni zile zenye mazingira mazuri tu.

Ukiangalia filamu za Kimarekani, mazingira yanayoonyeshwa kwa hapa Afrika ni yale mabovu, wakionyesha mapigano basi watawaonyesha watoto wakiwa wameshika silaha. Hawawezi kuionyesha Mlimani City kwenye muvi zao, hawawezi kuonyesha majengo mazuri ya kule Osterbay.

Ukienda Uarabuni, wao wanaonyesha majangwa, yaani wanatuaminisha kwamba Ukienda Uarabuni, kitu cha kwanza utapigwa na upepo wa mchanga na ujae vumbi kama umetoka Bonyokwa. Uarabuni si sehemu salama kuishi (Kulingana na muvi zao) na ndiyo maana leo mtu anatetea Waarabu, ukimwambia twende Iraq japo ukatembee hataki kwenda, kwa nini? Tayari amekwishaambiwa kwamba ukikaa huko, muda wowote ule unalipuliwa.

Watanzania wengi wanaogopa kwenda Kongo na Burundi, kwa nini? Ni kwa sababu tu tunasikia kuna mapigano, watu wanachinjana sana, kila kona milio ya risasi inasikia kumbe si hivyo. Taarifa za habari zimetuaminisha hivyo, muvi zinatuaminisha hivyo.

Tuliambiwa Iddi Amini Dada alikuwa anakula nyama za watu, tukaaminishwa hivyo na Wazungu, sababu kubwa ni kwa sababu hakuwa akiwafagilia wao. Kwenye filamu walizotengeneza kuhusu jamaa walimuweka akiwa anakula nyama za watu, tukaamini hivyo kumbe halikuwa kweli.

Hii ni dunia ya propaganda. Leo mtu anakwambia Marekani na Ulaya ni nchi za mashoga, lakini kutwa anatamani kwenda huko. Kwa nini? Wao wameweka mazingira rafiki ya kuishi. Kuna ugumu sana kuishi Marekani ila ugumu huo huwezi kuuona ukiwa Bongo, ila ukienda huko ndipo unaanza kugundua kumbe Marekani kugumu kuishi, bora Bongo yetu.

Maisha ya kule ni magumu kwa kuishi ila ukiishi kwa muda fulani na ukazoea, unaanza kuona maisha yanakuwa mepesi. Huwezi kuishi huko kama hufanyi kazi, ni lazima ufanye kazi ili uishi. Hapa Bongo unaishi bila kufanya kazi, utakula, utashiba, utalala na kesho asubuhi utatakata kupiga kimoja.

Pamoja na hayo yote wenzetu wameweka mbele haki za binadamu. Usione ni rahisi kwa Mwarabu kukimbilia Marekani, kwake anaona ni sehemu salama kuishi kuliko nchini mwake. Akitoka Iraq na kukimbilia Syria, ni sawa na kutoka chumbani kwenda sebuleni, bado utakuwa ndani ya nyumba hiyohiyo.

Waarabu hawanaga mambo ya kusaidiana, si wao tu hata Waarabu wa Bongo huwa wapo hivyo. Ni watu wanaochukiana kutoka moyoni. Ni rahisi leo Mwarabu kumsaidia Mzungu kumpa hifadhi lakini si Mwarabu mwenzake. Labda awe ndugu yake.

Osama alisalitiwa na Waarabu wenzake, Ghadafi naye alisalitiwa na Waarabu wenzake. Saddam Hussein naye alisalitiwa na Waarabu wenzake. Unapoona watu wa mataifa mengine wanakuja na kuingiza mkono nyumbani kwenu na kushinda, basi jua nyie wenyewe hamna umoja.

Mbona hatusikii Wazungu wakiwasaliti wenzao kwa ajili ya mgeni? Kitu cha kwanza ambacho Wamarekani huwa cha kwanza kufundishwa ni uzalendo wa nchi yao. Hiyo wameichukua mpaka Israel ndio maana si ajabu kuwaona Israel wakielekea nyumbani kwao kupambana vita, ni kwa sababu wamezaliwa nchi zilizofundishwa uzalendo. Ushaona Wapalestina waliokuwa nchi nyingine wakienda nyumbani kupigana vita?

Mwarabu akizaliwa, kitu cha kwanza anachofundishwa si uzalendo bali chuki. Ataambiwa tu kwamba kamwe hutakiwi kumpenda Mzungu. Mzungu ni adui namba moja kwenye maisha yako, yule ni kafiri. Wanakwenda mbali mpaka kusema ukimuua kafiri mmoja unakwenda peponi. Kweli kuna Mungu anaweza kuendekeza ujinga huo? Labda mungu wa maboksi.

Nchi za Kiafrika zimekosa uzalendo. Ulaya, Marekani na China, jambo la kwanza mtoto anafundishwa uzalendo na ndiyo maana unapoonekana huna uzalendo unaonekana kuwa mtu wa ajabu sana.

Sisi Waafrika na Waarabu tutafundishwa chuki kwanza. Muislamu ataambiwa Mkristo ni kafiri, kamwe usiolewe naye. Mkristo ataambiwa Muislamu na mchawi, hawajielewi, kamwe usiolewe naye. Yaani sisi hatuanzi kuwajengea watoto wetu uzalendo ama upendo, kitu cha kwanza tunawajengea chuki.

Chuki hizo zinakua. Mkristo hapendani na Muislamu japokuwa wanakaa na kuongea. Mtu wa kabila fulani anaambiwa tu kamwe usimuoe mtu wa kabila fulani kwa sababu hii na ile. Kwa wenzetu, jambo la kwanza kufundishwa ni uzalendo.

Watu weusi wanabaguliwa Marekani na Ulaya lakini siku zote wamekuwa wakisimama na nchi zao. Wanasema kabisa sisi ni Wamarekani, hii ni nchi yetu na tutaipambania. Uzalendo unajengwa tangu wakiwa wadogo, chuki nazo zinajengwa tangu tukiwa wadogo.

Baada ya kujazwa chuki sasa tunaanza kujazwa na unafiki. Tunasimama na kusema PRAY FOR ISRAEL, PRAY FOR PALESTINE na wakati huohuo hapo Kongo wanauana kila siku na hakuna anayesema chochote kile.

Huu unafiki nao huwa unajengwa tangu utotoni, ukitengenezewa chuki ni rahisi sana kujazwa unafiki moyoni mwako. Unakuta Waafrika wanaandamana kwa mapigano ya Israel na wakati huohuo kuna Wakongo 1500 wanauawa kila siku.

Unafiki wetu tunaugeuza na kuupamba kwa upande wa dini. Yaani sisi tunajifanya kushikilia sana dini kuliko Waisrael, tunashikilia sana dini kuliko Wapalestina. Yaani ni unafiki kila kona.

Ndugu yangu. Ukipata mtoto, jambo la kwanza kabisa mtengenezee upendo zaidi. Kwa kawaida mtoto anapozaliwa huwa na upendo, huo usiuondoe, usimwambie aache urafiki na Wakristo ama Waislamu. Hakikisha sana unaondoa chuki ambazo sisi tulijengewa sana miaka ya nyuma.

Leo kampuni zenye wakurugenzi Wakristo, wafanyakazi wengi ni Wakristo. Kampuni zenye wakurugenzi wengi Waislamu, wafanyakazi wengi ni Waislamu. Kwa nini? Hiki ni kitu kilichojengwa tangu zamani,

Yaani wazazi walikuwa bize kutengeneza chuki mioyoni mwa watoto kuliko upendo.

The same chuki ndiyo inawatafuna Waarabu. Leo Waarabu hawapendani, wapo radhi kumsaidia Mzungu kuliko wenzao. Leo wanaona Marekani ni sehemu salama kuliko nchi za Waarabu wenzao.

Wanajua hilo. Ili wawe salama ni lazima waondoke kwenye ardhi za Kiarabu, vinginevyo, unaweza kukuta Mwarabu wa Misri anakumaliza wewe wa Palestina.

Au hujui chuki kubwa baina ya Misri na Algeria? Misri wapo radhi wamsaidie Mtanzania mweusi lakini si Mwarabu mwenzao Algeria. Wazungu hawajafika hatua hiyo.

Utakuta mzungu anamsaidia Mzungu mwenzake kumpiga Mzungu mwenzake ila si Mzungu kumsaidia Mwarabu ama mwafrika kumpiga Mzungu mwenzake.

Fundisheni watoto wenu uzalendo, msiwafundishe chuki. Hususani sisi waafrika kwa waafrika tushikamane, tuache chuki miongoni mwetu, chuki ya kidini, chuki ya kisiasa, chuki ya ukabila.
 
Back
Top Bottom