Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Ilikuwa majira ya saa 11:15 jioni Inspekta wa polisi afande Kamazima alikuwa ndiyo amefika kwenye eneo la tukio. Ilikuwa ni maeneo ya Posta katika jengo la Bujibuji Plaza. Hapo ndipo zilipokuwa ofisi za kampuni ya Bima iliyokuwa ikimilikiwa na Bwana Mlaponi. Aliitwa baada ya kutokea mauaji ya Bwana Mlaponi, Mkurugenzi na mmiliki wa kampuni hiyo ya Mlaponi Insurance Agency
Hapo ofisini alikuwepo Katibu Muhtasi wa Bwana Mlaponi aitwaye Nshemele, ambaye alizungumziwa na watu wa ofisi za jirani waliohojiwa awali kama Katibu Muhtasi muadilifu wa Bwana Mlaponi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Nshemele alidai kwamba alitoka saa 9:45 jioni na kuwaacha bosi wake na mgeni wake aliyemtaja kwa jina la Makanyaga wakizungumza na yeye alitoka kwa ajili ya kwenda kufanya manunuzi ya vifaa vya ofisini katika duka la Msemo Printers ambapo alikuwa na risiti zinazoonyesha kwamba alifanya manunuzi hayo majira ya saa 10:15 jioni.
Kwa mujibu wa maelezo yake Nshemele alidai kwamba, aliporudi majira ya 10:30 ndipo alipokuta Bosi wake ameuawa kwa kuchomwa kisu mgongoni.
Muda alioutaja kwamba ndiyo aliyorudi kutoka Msemo Printers unaonyesha kwamba alikuwa nje ya ofisi kwa takriban muda wa dakika 45 ambazo zinatosha kutumika kwa mtu kwenda Msemo Printers na kurudi kutokana na umbali ilipo ofisi za Mlaponi Insurance Agency na ilipo Msemo Printers.
Pale mezani kulikutwa gloves, matone ya kahawa, na pia meza hiyo ilikuwa imevurugika huku baadhi ya mafaili yakiwa chini na hata baadhi ya mafaili mengine yaliyokuwa kwenye kabati nyuma ya kiti cha mkurugenzi huyo yakiwa yameanguka chini kuashiria kwamba kulikuwa na mapigano kati ya muuaji na mkurugenzi huyo na pia shubaka kubwa la kuhifadhia fedha lilikuwa wazi na ndani hapakuwa na fedha na pia funguo za shubaka hilo hazikujulikana zilipo.
Mkononi mwa mkurungenzi huyo alikuwa amevaa saa ambayo nayo pia ilikuwa imevunjika na ilikuwa imesimama kufanya kazi ikiwa imesimama katika muda wa saa 9:55.
Nshemele alipoulizwa kama bosi wake huwa ana kawaida ya kunywa kahawa, akasema hapana bali mgeni aliyemuacha na bosi wake yaani Bwana Makanyaga ndiye aliyekuja na kahawa ikiwa katika kikombe cha Karatasi ngumu cha take away na wakati wanazungumza Bwana Makanyaga alimaliza kunywa Kahawa yake na kukiweka kikombe chake juu ya meza yake (yeye Nshemele) ambapo alikitupa kwenye dust bin yake.
Askari wa upelelezi alipochunguza ndani ya ile dust bin aliona kikombe kile cha kahawa na kikachukuliwa kwa ajili ya kuchunguzwa alama za vidole.
Kwenye daftari la wageni kumbukumbu inaonyesha wageni watatu wa mwisho waliorekodiwa walikuwa ni Kiranga (8:35), Mkumbange (9:10) Makanyaga (9:40).
Kisu alichochomwa nacho Bwana Mlaponi hakikukutwa na alama za vidole, kikombe cha kahawa kilichokutwa kwenye dust bin kilikutwa na alama za vidole vya Makanyaga na shubaka la kuhifadhia fedha lilikutwa na alama za vidole za Bwana Mlaponi.
Baada ya kuchunguza eneo la tukio kwa makini Ispekta Kamazima alibaini muuaji aliyehusika na mauaji ya Bwana Mlaponi si mwingine ni Katibu Muhtasi wake Nshemele ambapo aliamuru akamatwe na kuhojiwa zaidi kwa kuhusika na mauaji ya Bosi wake.
Baada ya kuhojiwa kwa umakini mkubwa kwa kuangalia mazingira ya tukio zima hatimaye Nshemele alikiri kuhusika na mauaji ya Bosi wake.
Je ni kitu gani kilimfanya Inspekta Kamazima amjue muuaji kirahisi vile?
Hint: Ipo sababu moja ya msingi ambayo inaunganisha dot na ndiyo iliyopelekea kukamatwa kwake.
Sitaki majibu ya jumla jumla.