Nimefungua JF ili nione wenzangu mnasemaje juu ya kitabu nilichoandika nikijaribu kuweka kumbukumbu ya yale niliyofanya na ninayoyafahamu. Nawashukuru wote wanaonipongeza kwa kukiandika.
Hata hivyo, kila mtu ana uhuru wa kueleza maoni yake, na sioni ni ajabu wanaJF kadhaa kunilaumu. Lakini nikiri kwamba siwaelewi wanaonilaumu kwa kuandika historia hii. Nawashauri watulie na wapate wasaa wa kukisoma hiki kitabu, na ikiwezekana nao waandike upande wao katika kushiriki kuendeleza hili taifa.
Wanaosema Mwalimu Nyerere alinibeba kunipa nyadhifa nilizoshika ktk utumishi wangu, wasome kitabu na historia ya Tanzania kwa jumla. Nilibahatika kuwa miongoni mwa wananchi wachache tuliopata Shahada ya Chuo Kikuu na Nyerere hakutaka kuteua Mzungu aongoze uundaji wa Benki Kuu. Ninavyosema kitabuni, angeweza kumchagua Mtanzania mwingine, na mimi nilijitahidi kwa uwezo wangu kutekeleza majukumu kwa uadilifu na kwa uzalendo kama Mwalimu alivyonuia mambo yafanyike.
Ni upuuzi mtupu kusema Mwalimu alipendelea Chadema eti kwa vile binti yangu aliolewa na mwanae. Huu ni oungo usiothibitika. Wanaosema hivyo wamechanganyikiwa kwa vile Mwalimu alisifu Chadema mwaka wa 1994, mimi nikiwa mwenyekiti. Mbowe alikuwa hajulikani na alikuwa tu ni kijana ktk chama.
Tulitofautiana na Mwalimu, na nakiri kwamba kushindwa kwangu kum persuade kuwa yale niliyokuwa napendekeza yangesaidia Tz, ndiyo weakness yangu kubwa. Kama ningefaulu, historia ya nchi yangu ingekuwa tofauti, na wakina kanda mbili wangekuwa wachache nchini sasa.
Najivunia kuacha BoT ikiwa imara na uchumi ukinoga. US $ 1.00 = Tsh 7.14 wakati niliondoka BoT, 1974. Najivunia pia kwamba niliweza kuchaguliwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa IMF na Benki ya Dunia, 1979/80. Hakuna aliyenibeba hapo. Nilichangia pia katika mchakato w Reform of Monetary system nilipokuwa Deputy katika the Committee of Twenty. Soma kitabu.
Wanaolaumu kuwa nimebaka demokrasia licha ya kuwa najivunia kuasisi Chadema, nawashauri wazungumze na viongozi wa sasa wa chama. Naamini chama kiko imara kutokana na ushauri wangu, na siku muafaka itafika wakati vijana shupavu, jasiri, wabunifu, waadilifu na wazalendo wanaojali maslahi ya wanyonge na ya nchi yao, kama Freeman na Zitto, wataridhisha WaTz. kwamba chama chao kinaweza. Subiri. Iko siku.
Mwishowe nikiri sijui ningefanya nini katika kuzindua kitabu changu ili nijivue uChagga. Ndugu zangu wamezaliwa hivyo na Mchapishaji wa kitabu aliwaalika. Nilikuwa nimwemwalika mrithi wangu BoT, Profesa Ndulu awe mgeni rasmi lakini akapata safari ya ghafla. Hakuweza kuja.
Reginald Mengi akakubali, dakika za mwisho, kuwa mgeni rasmi, na hata haikuwezekana kumtaja ktk card kuwa ni Mgeni rasmi. Watanzania wa nyadhifa za juu, wanaonifahamu vizuri, kama Jenerali Ulimwengu na Ibrahim Kaduma wakakubali kusema machache ktk ile sherehe. Wao sio Wachagga! Ningefanya nini nionekane mimi ni Mtanzania wa kweli?
Nashauri JF wasiwe na prejudice. Tutaweza kufanya makubwa tukiacha prejudice.
Edwin Mtei