Habari wanajamii wote popote mlipo hapa duniani. natanguliza heshima za dhati kwenu nyote na itifaki imezingatiwa.
Napenda niwashirikishe wanajamii wenzangu kuhusu faida za kuwa mama wa nyumbani na naomba niseme kuwa kwa miaka ya hivi karibuni, jamii imekuwa ikimdharau sana mama wa nyumbani na kumuona mvivu na hana mchango wowote kwenye maendeleo ya familia yake eti kisa haingizi CASH. jamii imeenda mbali hata kudiriki kumtungia maneno ya kashfa na kejeli kwamba ni golikipa yani ni kama kandege kanakosubiria kufumbua mdomo na kupokea chakula kutoka kwa mama yake pasipokuwa na mchango wowote katika kutafuta chakula hicho.
Tukumbuke kwamba wamama zetu walio wengi waliweza kutulea na kutuwezesha kuwa na maadili mema kwa kuwa walikuwa karibu yetu masaa 24. kuanzia tulipozaliwa wamama zetu walio wengi;
1. wametunyonyesha si chini ya miaka 2
2. wametuogesha utoto wetu wote (mama anapokuogesha anahakikisha umetakata na anakukagua mwili mzima kama siku hiyo umeumia au una kidonda basi mama atajua mara moja na kukuhudumia ipasavyo)
3. kukupikia uji/chai na kuhakikisha amekunywesha kila siku. kama unaumwa atajua. ni furaha kubwa sana kwa mtoto kulishwa na mama yake.
4. kukuandaa kwenda shule huku akikusisitiza usome kwa bidii
5. kufuatilia kwa ukaribu masomo yako na kuhakikisha unaishi kwa adabu pale nyumbani maana yupo muda wote kufatilia mwenendo wako (bakora za kutosha).
Wakati huo baba yeye yuko bize kibaruani kuhakikisha analeta mahitaji yote ya familia yake na cha kushangaza maisha yalikuwa mazuri na matamu sana. kulikuwa hakuna dharau. Mama alikuwa anamuheshimu baba maana anajua mchango wake katika familia. Baba naye alikuwa anamuheshimu mkewe maana alikuwa anajua mchango wake katika familia. hivyo kila mtu alikuwa na wajibu wake na familia nyingi (sio zote) silizoishi kwa mfumo huu zimekuwa familia bora.
Je, kulikoni nyakati hizi???
- pesa imekuwa ndo kila kitu. kumekuwa na vita ya pesa kiasi kwamba si baba wala mama anayependa kupitwa na hii kitu
- pesa imekuwa ndio msingi wa familia... hapendwi mtu bali pesa. leo hii mwanamke ukijitolea kuwa mama wa nyumbani ili uwalee watoto wako ipasavyo, uwepo muda wote watoto watakapokuhitaji, unaonekana wa ajabu, jamii na hata mume wako hatokuelewa. lakini ukiondoka nyumbani saa 12 asubuhi na kurudi saa 4 usiku ukitokea kazini (kutafuta pesa), hapo unaonekana mjanja na mpambanaji wa kweli huku nyuma watoto wako wanaharibikiwa.
Hivi kweli hii ni sawa???
Mimi naamini kuwa tumeingia kichwa kichwa katika hii dhana ya usawa na tunakoelekea itatugharimu. Kwa nini?
1. Wanawake siku hizi hawana muda wa kunyonyesha watoto wao kisa wanawahi kazini. kumbuka maziwa ya mama ndio pekee yenye uwezo wa kujenga immunity ya mtoto kwa maisha yake yote. inashauriwa mtoto anyonyeshwe walau miaka miwili (jambo ambalo mama zetu walilijua na kulifanyia kazi japo hawakuwa wamesoma sana). huyu mtoto aliyenyonyeshwa kwa miezi miwili tu atakuwa salama kweli?
2. Dhana hii imewafanya wanaume kuwa wavivu na kukimbia majukumu yao. wanaogopa kubeba mzigo wa familia zao hivyo kutafuta wanawake wenye vipato tayari ili kukwepa majukumu. wake zao wasipokuwa na kazi huwanyanyasa na kuwaona tegemezi (golikipa).
3. Watoto wetu siku hizi wanaharibikiwa kwani wazazi wote wako bize kutafuta pesa, hakuna mwenye muda na mtoto. hakuna anayejua ameamka vipi, kama amekunywa chai ama la, ameenda shule ama la, huko shule maendeleo yake yapoje, labda kapigwa na mtu shule, au dada au kaka wa kazi kamfanyia kitu kibaya, hakuna anayejali.
4. Madhara makubwa ya hii dhana ni kwa wanawake kwani wanajikuta wamejiover-load na shughuli nyingi sana. mfano utakuta mtu ni mjamzito (tumbo kule) hapohapo anahaingaika na kazi kila siku ya Mungu mpaka anajifungua, bosi haelewi una kichefuchefu wala kizunguzungu anachotaka kazi iende.
ukijifungua unanyonyesha miezi 3 tu unakimbia kazini, katoto unakaachia hausigeli ambaye humwamini, unafanya kazi huku presha iko juu. mume naye haelewi. mtoto anakosa bonding na mama yake kitu ambacho ni muhimu sana kwa ustawi wa mwanadamu.
5. Na mengine mengi.....
Sisemi mwanamke asijishugulishe, nachosema mwanamke asiwe bize sana na kusaka pesa, awe na muda wa kulea familia yake (mume na watoto). hata kama ni ujasiriamali usiwe full time ili apate muda wa kulea watoto wake ipasavyo.
Tukubali tukatae, kazi ya kulea watoto na kuhakikiha wanakuwa na maadili mazuri ni ya mama kwa asilimia 90.
HITIMISHO;
-HESHIMA ZANGU ZA DHATI NA ZA KUTOKA MOYONI MWANGU ZIWAENDEE WANAUME WOTE WANAOTAMBUA KUWA JUKUMU LA KULETA MAHITAJI YA NYUMBANI NI LA KWAO NA WANAFANYA HIVYO KWA MOYO WAO WOTE
-WAHESHIMIWE PIA WANAUME WALIO NA WAKE AMBAO NI MAMA WA NYUMBANI NA WANATAMBUA MCHANGO WAO KATIKA FAMILIA NA WALA HAWAWADHARIRISHI WAKE ZAO KWA KUWAITA MAGOLIKIPA AU KUWANYIMA MAHITAJI
-WAHESHIMIWE WANAWAKE WOTE WANAOFANYA DOUBLE JOBS YAANI KUZAA KWA UCHUNGU NA KULA KWA JASHO (wakati wanaume wao wanafanya moja tu ya kula kwa jasho hiyo nyingine hawaielewi). MUNGU AWAFANYIE WEPESI WAMAMA HAO.
Kwa mtazamo wangu USAWA (Beijing) umeletwa kuwakandamiza wanawake na kuharibu familia na si kuwatetea na kuwainua wanawake.
AMANI KWENU WOTE.