UHALISIA: Wanga ni Rafiki au Adui wa afya yako?

UHALISIA: Wanga ni Rafiki au Adui wa afya yako?

JamiiCheck

JF-Expert Member
Joined
Nov 3, 2023
Posts
245
Reaction score
266
Katika ulimwengu wa kisasa wa lishe, kumekuwepo na mijadala mingi kuhusu ulaji wa wanga. Watu wengi, hasa watoa mada za mtandaoni na watu wenye ushawishi kwa kiasi kikubwa hutoa elimu inayopinga matumizi ya aina hii ya chakula, wengine wakienda mbali zaidi kwa kuiita takataka.

Hii imefanya watu wengi waanze kuogopa kula wanga wakiamini kuwa ndio chanzo kikuu cha kuongezeka uzito na magonjwa. Lakini je, ni kweli kuwa kula wanga ni vibaya na hairuhusiwi? Ukweli ni kwamba wanga ni kirutubisho muhimu ambacho mwili hauwezi kufanya kazi vizuri bila hicho.

Wanga ni nini na kwa nini tunauhitaji?
Wanga (Carbohydrates) ni chanzo kikuu cha nishati mwilini. Unapokula vyakula vya wanga, mwili huvivunja na kuwa sukari (glucose), ambayo husafirishwa kwenye damu ili kutoa nguvu kwenye seli, tishu, na viungo vyako.

Ubongo wa binadamu pekee unategemea takriban asilimia 20 ya nishati inayotokana na wanga ili kuweza kuratibu kumbukumbu na umakini. Bila wanga, mwili hulazimika kutumia protini na mafuta kama chanzo mbadala, jambo ambalo huuchosha mwili na kupunguza ufanisi wa kinga.

Kosa kubwa wanalofanya watu wengi ni kuweka kila aina ya wanga kwenye kundi moja. Ili kulinda afya yako, unapaswa kutofautisha kati ya makundi haya mawili:
  • Wanga tata (Complex Carbohydrates): Huu ndio wanga "mzuri." Hupatikana kwenye vyakula ambavyo havijapita kiwandani sana kama vile ugali wa dona, viazi vitamu, ndizi mbichi, mtama, na maharage. Vyakula hivi vina nyuzinyuzi (fiber) ambazo husaidia sukari kuingia mwilini taratibu, hivyo kukupa nguvu ya muda mrefu na kusaidia mfumo wa mmeng'enyo.
  • Wanga mwepesi (Simple Carbohydrates): Huu ni wanga uliosindikwa kama vile sukari nyeupe, soda, mikate meupe, keki, na unga uliokobolewa sana. Huu huingia mwilini kwa kasi sana na kusababisha mrundikano wa sukari, ambao usipotumiwa hubadilika kuwa mafuta na kusababisha vitambi na magonjwa ya moyo.
Kula wanga si kosa, bali kiasi unachokula ndicho huamua matokeo. Mtu anayefanya kazi nzito zenye kuhitaji nishati nyingi anahitaji wanga mwingi zaidi kuliko mtu anayeshinda ameketi ofisini siku nzima.

Tatizo huanza pale tunapojaza sahani nzima kwa wanga (mathalani wali au ugali mkubwa) huku tukisahau mbogamboga na protini. Kanuni bora ya afya ni kuhakikisha wanga unachukua robo tu ya sahani yako, huku robo nyingine ikiwa protini na nusu ya sahani ikijazwa na mbogamboga.

Kula wanga si vibaya na ni jambo linaloruhusiwa kabisa katika mpango wowote wa lishe bora. Muhimu ni kuchagua wanga asilia na kuepuka vyakula vyenye sukari nyingi na vilivyokobolewa. Ukila wanga kwa kiasi na kufanya mazoezi ya kutosha, utaupa mwili wako nishati unayohitaji bila kuhatarisha afya yako.
 
ADE14D66-9E2A-4761-84A6-1BBB49632B9C.jpeg

Aww 🥰
 
Back
Top Bottom