EWURA yafafanua kutoshuka bei ya mafuta nchini

N'yadikwa

JF-Expert Member
Aug 10, 2014
7,121
10,233
Yasema kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei hapa nchini LAKINI sio kwa wakati huohuo KWA SABABU hiyo bei watu wanayolalama ni ya mafuta ghafi na zaidi stock inayouzwa wakati husika siyo ile inayotajwa kwenye news break CNN, BBC kwamba imeshuka.www.ewura.go.tz
================

EWURA.PNG


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI ZA MAFUTA KATIKA SOKO LA DUNIA NA LA HAPA NCHINI


1. UTANGULIZI

Mamlaka ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inapenda kutoa taarifa halisi kuhusiana na mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia na la hapa nchini. Kati ya majukumu ambayo EWURA imepewa ni kuweka bei KIKOMO za mafuta aina ya petroli katika soko la hapa nchini, utaratibu ulioanza rasmi Januari 6, mwaka 2009 baada ya kutokea hali ya kukosekana uhalisia wa bei za mafuta katika soko la ndani ikilinganishwa na mwenendo wa bei katika soko la dunia. Matokeo yake ni kuwa watumiaji mafuta walikuwa wakinunua mafuta kwa bei isiyo halisi (2,200/= kwa lita) katika miezi ya mwisho mwaka 2008, na pia uchumi wa nchi uliathirika na mwenendo huu wa bei. EWURA ilishusha bei hizo hadi kufikia 1,140/= baada ya kuanza kupanga bei mwezi Januari 2009.


Pamoja na kwamba bei za mafuta katika soko la dunia ndicho kigezo kikubwa cha upangaji wa bei katika soko la ndani, kuna gharama zinazoambatana na uagizaji mafuta hayo hapa nchini, kama vile gharama za usafirishaji, faida za waagizaji mafuta, kodi za Serikali, gharama za bandari na tozo za mamlaka mbalimbali nk. Kwa bei za Januari 2016, kwa mfano, mchango wa bei hizi za ndani unaochangiwa na bei za mafuta masafi katika soko la dunia ni: Petroli 46.60%, Dizeli 47.82% na Mafuta ya Taa 49.83%. Lazima ifahamike kuwa bei zinazooneshwa kwenye mitandao mbalimbali ni bei za Mafuta GHAFI (Crude Oil) ambayo yakisafishwa hutoa petroli, dizeli, mafuta ya taa na ndege, gesi ya kupikia (LPG), oil, lami n.k. EWURA inaweka bei hizi kwa kuangalia bei halisia ya mafuta yaliyosafishwa na si mafuta ghafi.

2. UHUSIANO WA BEI ZA MAFUTA GHAFI KATIKA SOKO LA DUNIA NA BEI ZA HAPA NCHINI

Mafuta ghafi (crude oil) yanaponunuliwa katika soko la Dunia inabidi yapelekwe kwenye viwanda vya kusafishia mafuta (refineries) ili kupata mafuta safi. Hatua hii huchukua takriban miezi miwili mafuta hayo kutufikia sisi kama walaji hapa Tanzania.

Bei za mafuta katika soko la ndani hukokotolewa kwa kutumia gharama halisi za uagizaji mafuta nchini ambazo hutokana na meli za mafuta yaliyopokelewa katika mwezi husika, ambayo huwa yamenunuliwa mwezi wa nyuma yake. Hivyo uhusiano wa bei za soko la dunia kwa mafuta masafi na za soko la ndani huwa ni kwa kupishana kwa miezi miwili kama inavyoainishwa na Jedwali Na. 1.0. Aidha, uhusiano wa bei za mafuta ghafi katika soko la dunia na bei za hapa nchini huwa ni kwa wastani wa miezi mitatu au zaidi.

Jedwali Na.1 Uhusiano wa bei za mafuta masafi katika soko la dunia na soko la ndani
Jedwali 1.PNG


Bei za mafuta hapa nchini hupangwa na Mamlaka ya EWURA kwa kutumia kanuni (formula) maalum ambayo inatayarishwa kwa kuzingatia uhalisia wa vigezo husika. Aidha, utayarishaji wa kanuni hii huhusisha wadau wote na kisha kuchapishwa katika gazeti la Serikali baada ya kupitishwa na Bodi ya EWURA.

3. MWENENDO WA BEI ZA MAFUTA KWA SASA
Katika kipindi cha mwaka 2014 hadi Januari 2016 bei za mafuta katika soko la Dunia zimeendelea kushuka. Kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei hapa nchini japo si wakati ule ule. Aidha ni muhimu kuzingatia kuwa bei za mafuta masafi katika soko la dunia huchangia takriban asilimia 46 mpaka 49 ya bei katika soko la ndani (kwa bei za Januari 2016), hivyo kushuka huko hakuwezi kuwa na uwiano wa asilimia mia na kushuka kwa bei

katika soko la ndani. EWURA itaendelea kutimiza wajibu wake kisheria katika sekta ndogo ya mafuta hapa nchini ikiwemo upangaji wa bei kikomo za mafuta, na pia kusimamia bei hizo katika maeneo yote nchini.

Ni vizuri ikakumbukwa pia kwamba hata hivi karibuni, bei za mafuta katika soko la Tanzania zimekuwa zikishuka kufuata mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia kama ifuatavyo:
a) Bei ya petroli ilishuka toka kiwango cha juu zaidi, mwezi Septemba 2014, Shillingi 2,267 kufikia shillingi 1,898 kwa lita mwezi Januari 2016, hii ikiwa ni kupunguka kwa Shillingi 369 kwa lita.

b) Bei ya dizeli ilishuka toka kiwango cha juu zaidi, mwezi Aprili 2014, shillingi 2,149 kufikia shillingi 1,747 kwa lita mwezi Januari 2016, hii ikiwa ni kupunguka kwa shillingi 402 kwa lita.

c) Bei ya mafuta ya taa ilishuka toka kiwango cha juu Zaidi, mwezi Februari 2014 shillingi 2,069 kufikia shillingi 1,699 kwa lita mwezi Januari 2016. Hii ni sawa na punguzo la shillingi 370 kwa lita.

Punguzo hilo la bei limepatikana licha ya ongezeko la kodi ya Serikali la Shilingi 100 kwa lita ya mafuta na kushuka kwa thamani ya Shilingi ilishuka dhidi ya Dola ya Marekani ambapo katika mwaka 2015, thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ilishuka kwa asilimia 30 toka Shilingi 1,729 kwa Dola ya mwezi Januari 2015 kufikia Shilingi 2,254 kwa dola mwezi Agosti 2015 na baada ya hapo thamani ya Shilingi imepanda kufikia Shilingi 2,158 mwezi Disemba 2015.

4. UZINGATIAJI WA KANUNI KATIKA KUKOKOTOA BEI ZA MAFUTA
Kanuni ya kukokotoa bei za mafuta ni ya wazi, siyo siri, na huandaliwa kwa mchakato ambao ni shirikishi na huhusisha wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya Serikali, wafanyabiashara wa mafuta na pia wawakilishi wa watumiaji wa mafuta. Kanuni inaelekeza kuwa kabla EWURA haijafanya mabadiliko yoyote ni lazima utaratibu huu uzingatiwe, isipokuwa kwa maamuzi ambayo yanapitishwa na Serikali, hususan kodi na tozo mbali mbali. Kunapotokea mabadiliko ya kodi au tozo za Serikali, EWURA hufanya mabadiliko husika mara moja, baada ya kupata waraka husika kutoka Serikalini.


5. HITIMISHO
Kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei hapa nchini japo si wakati ule ule, kwamba yakishuka leo, kesho yanashuka hapa nchini.

Aidha kumekuwa na upotoshaji kwamba EWURA haishushi bei za mafuta kwa kuwa kushuka kwake kutaadhiri mapato yake. Ukweli ni kwamba tozo ya EWURA inatokana na lita za mafuta na si bei, kwa maana kwamba iwapo EWURA ingetaka mapato mengi, basi ingeongeza wingi wa lita za mafuta yanayoingia hapa nchini, na si kutegemea kupanda kwa bei. Hivyo basi kushuka au kupanda kwa bei hakuna uhusiano wowote na ongezeko la tozo kwa EWURA.

Imetolewa na Felix Ngamlagosi
Mkurugenzi Mkuu - EWURA
 
Hawa nao tangu Maseru astaafu wamebaki wapigaji tu....... haya watuekeze hiyo stock inayotajwa inauzwa lini?
Mbona hatuonagi unafuu wake?
 
Hawa wanatak kutuchezea,mkurugenzi ewura kama hawezi kazi step down
 
Kuna watu wengine aisee wanakula mishahara ya bure kabisa,mitambazi kama hii haina haja ya kuendelea kulipwa kupitia kodi zetu,itumbuliwe tu walahii
 
EWURA ni jipu linalohitaji kutumbuliwa haraka iwezekavyo....inawezekana wakawa wanashirikiana na wafanyabiashara wa mafuta kuwanyonya walalahoi........yamekaa pale ofisini yanashindana kuvimba matumbo tu...huku hazionekani.......wamekuwa watu wa kutoa matamko yasiyo na kichwa wala miguu....
 
Nilimsikia jana Radio 1 sijui anaitwa Kaguo anadai eti wananchi hawaelewi na wanapotoshwa na wao ewura ndio tu wanaojua tu mambo ya nishati. Lakini hata vijiswali vidogo alivyoulizwa na mwandishi vilimshinda kujibu. Hoja ni ndogo sana, kwamba mafuta yameshuka bei kote duniani lakini Tanzania hayashuki atueleze ni kwa nini. Maana yakipanda leo kesho yanapanda lakini sio kwenye kushuka!
Ndipo nikazidi kupata ushahidi kuwa siasa zinamaliza nchi maana hata wanaojiita wataalamu wanapokea 'maagizo' na wanatekeleza bila hata kufanya uchambuzi mdogo. Yaani wewe na ewura yako ndio mna uelewa kuzidi Watanzania milioni 50 na dunia nzima!?
 
Hawa ambacho huwa wananishangaza ni kuwa ikipanda huwa wanapandisha haraka sana na ikishuka wanaleta sababu zisizo na mashiko
 
Hakuna maaan yoyote unayodanganya wewe unaejiita mkurugenzi..kama mafuta yanachukua miezi miwili kutufikia kwa bei iliyoshuka kwa hesabu baada ya miezi miwili ijayo yakipanda ina maana haya ambayo waliagiza kwa bei ndogo hayatapungua bei na yale watakayoagiza kwa kipindi hicho bei juu yatapanda bei. Kwa hesabu ndogo hii Mafuta hayashuki bei kulingana na Soko la Dunia wewe endelea kusema sisi tunalalama na hatujui kitu..mpo hapo kwa masilahi yenu na wafanyabiashara wa mafuta..
 
Ewura ni jipu tena lililokwishawiva litumbuliwe tu! Yaani huyu director anatufanya sie hamnazo. Hebu shangaa hapa, ukienda Rwanda , Burundi na Uganda bei Za mafuta ziko chini na mafuta yao yanapita bandarini kwetu tena yanaposhuka kwenye world market na wao hawachelewi kushusha, hata Kenya wameshusha. Tumechoka kufanywa mburula na hawa wachumia tumbo, kama vp JPM aivunje ewura aipeleke tpdc au tra, hawa jamaa kwakweli jipu tena limekaa pabaya, nakuomba JPM litumbue kwani linatumaliza.
 
MAMLAKA ya Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei nchini.
Katika taarifa yake kwa umma, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema, licha ya kushuka kwa bei hizo za mafuta katika soko la dunia, hazitakuwa zikishuka kwa wakati huo huo nchini.
“Kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia kutaendelea kushusha bei hapa nchini japo si kwa wakati huo,” Ngamlagosi alisema.
Ngamlagosi alisema kumekuwa na upotoshaji kwamba Ewura haishushi bei za mafuta kwa kuwa kushuka kwake kutaathiri mapato yake, lakini ukweli ni kwamba tozo ya Mamlaka hii inatokana na lita za mafuta na si bei.
“Iwapo Ewura ingetaka mapato mengi, basi ingeongeza wingi wa lita za mafuta yanayoingia hapa nchini, na si kutegemea kupanda kwa bei. Hivyo basi kushuka au kupanda kwa bei hakuna uhusiano wowote na ongezeko la tozo kwa Ewura,” alieleza.
Alisema, Mamlaka hiyo itaendelea kutimiza wajibu wake kisheria katika sekta ndogo ya mafuta hapa nchini, ikiwemo upangaji bei kikomo za mafuta na kuzisimamia katika maeneo yote nchini.
Mkurugenzi huyo alisema kwa mwaka huu, bei ya petroli ilishuka toka kiwango cha juu zaidi, Septemba 2014, Sh 2,267 kufikia Sh 1,898 kwa lita ikiwa ni kupunguka kwa Sh 369 kwa lita. Bei ya dizeli ilishuka toka kiwango cha juu zaidi, Aprili 2014, ilipokuwa ikiuzwa Sh 2,149 na kufikia Sh 1,747 kwa lita Januari 2016, hii ikiwa ni kupungua kwa Sh 402 kwa lita.
 
Back
Top Bottom