D-4 ni injini za petroli za Toyota zenye kutumia mfumo wa direct injection. Mitsubishi nao wana injini za aina hii ambazo wao huziita GDI (gasoline direct injection). Kwa kifupi injini hizi ni nzuri kwani zina nguvu zaidi na matumizi yake ya mafuta ni mazuri ukilinganisha na injini za aina nyingine zenye ukubwa (capacity) sawa. Tatizo la injini za D-4 ni kwamba zinataka mtumiaji awe makini sana na mafuta anayotumia kwenye gari lake, siyo kuweka petroli ili mradi ameweka petroli. Cha kuzingatia zaidi ni kutumia petroli yenye kiwango cha octane (samahani sijui Kiswahili chake) kinachoshauriwa na mtengenezaji. Petroli yenye kiwango cha octane chini ya kile kinachoshauriwa na mtengenezaji huweza kuleta matatizo ya kujaa kaboni (carbon) kwenye valvu na hii mara nyingi huleta matatizo mengi tu kutokana na umuhimu wa valvu katika injini. Kwa bahati mbaya sana, petroli inayopatikana sehemu nyingi za Tanzania haina ubora (kiwango cha juu cha octane na cha chini cha salfa) unaohitajika kwa injini za D-4.