e-Ardhi kurahisisha huduma za Ardhi Njombe

e-Ardhi kurahisisha huduma za Ardhi Njombe

Wizara ya Ardhi

Govt Institution
Joined
May 14, 2024
Posts
252
Reaction score
149
WhatsApp Image 2026-09-15 at 2.44.29 AM.jpeg

NJOMBE

Mfumo wa kidijiti wa e-Ardhi unatarajiwa kuwa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika upatikanaji huduma za ardhi, ikiwemo foleni, gharama na usumbufu wa kufuata huduma hizo katika ofisi za ardhi.

Hayo yameelezwa na wataalamu wa ardhi mkoani Njombe waliopewa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo, yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma za ardhi kwa wananchi kupitia teknolojia ya kidijiti.

Mmoja wa wataalamu walionufaika na mafunzo hayo, Benedict Nsaji, amesema mfumo wa e-Ardhi utasaidia kupunguza mlundikano wa wananchi katika ofisi za ardhi, kwa kuwa mteja ataweza kupata baadhi ya huduma akiwa mahali alipo bila kulazimika kufika mjini.

“Mfumo wa e-Ardhi utapunguza mlundikano wa wateja ofisini kwani mteja ataweza kupata huduma akiwa kwake, pia itampunguzia usumbufu na gharama za kuja mjini kwa ajili ya kupata huduma za ardhi,” amesema Nsaji.

Soma Pia: Huduma za ardhi Kigoma kunufaika na teknolojia ya mfumo wa e-Ardhi

Ameongeza kuwa mfumo huo utarahisisha pia utunzaji na upatikanaji wa nyaraka za ardhi, jambo ambalo awali lilikuwa changamoto kwa watoa huduma.

“Utunzaji wa nyaraka ulikuwa ni changamoto lakini kwa sasa imekuwa ni rahisi kwani nyaraka zote zinapatikana kwenye mfumo,” amesema.

Kwa upande wake, Happy Mkalawa, ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo, amesema mfumo huo utasaidia wananchi kupata huduma kwa wakati huku ukiimarisha uwajibikaji kwa watendaji wa sekta ya ardhi.

“Mfumo wa e-Ardhi utasaidia huduma kupatikana kwa wakati na kuchochea uwajibikaji kwa kuwa mfumo ni wa wazi na unaonesha kila hatua na zaidi unakukumbusha nyaraka muhimu za kuambatanisha,” amesema Mkalawa.

Mafunzo hayo yanatolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Njombe, yakiwa yameanza Septemba 14, 2026 katika ukumbi wa Hoteli ya Agreement, Njombe mjini.

Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wataalamu wa ardhi kutumia mfumo wa e-Ardhi katika kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi, hususan kwa kutumia njia za kidijiti.

Wataalamu walioshiriki mafunzo hayo wanatoka Halmashauri za Njombe Mji, Njombe Vijijini, Wanging’ombe, Ludewa, Makambako na Makete, pamoja na Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Njombe.
 
Back
Top Bottom