Licha ya CCM kukataa kukiri jambo ambalo ni kweli, CCM yenyewe imeutambua umakini wa Dk. Slaa, jambo ambalo limekifanya chama hiki kikongwe cha siasa kuingia kiwewe, badala ya kurekebisha mambo ambayo ni dhahiri kwamba yamekwenda mrama, badala yake, CCM inazidi kujichimbia kaburi miongoni mwa wananchi.
Ukweli ni kwamba wananchi wengi sana wameamka, na wametamka wazi wazi (mimi nikishuhudia) kwamba HAWATAIPA KURA CCM mwaka huu. Juzi nilikuwa Moshi Mjini, nikashuhudia akinamama - wajasiriamali, ukipenda kuwaita - wakijadiliana hadharani, tena kwa hoja nzito, kwamba wamechoka kuwaona viongozi wa CCM wakineemeka, mwaka hadi mwaka, wakati wao hali yao kiuchumi inazidi kuwa mbaya, tena wakipandishiwa ushuru kwenye masoko kila siku, sasa wanayakimbia masoko hayo. Wameamua kutafuta maeneo yasiyo rasmi kufanya biashara zao kwa kuwa ushuru wanaotozwa kwenye masoko ni mkubwa kuliko kipato chao.
CCM wametambua tishio kubwa dhidi yao kutoka kwa Dk. Slaa na wabunge wengi wa CHADEMA. Huu ndio msingi wa kesi isiyo na kichwa wala miguu, ya kwenda kudai fidia kwa Dk. Slaa, wakimchukua mamluki Mahimbo, ambaye anadaiwa kulipwa fedha nyingi kwa ajili ya KUJIABISHA hadharani. Hivi mwanaume anayejiheshimu anaweza kweli kutamka hadharani kwamba NIMEPORWA MKE na fulani? Ingekuwa mimi ningekaa kimya kuliko kujidhalilisha; UTU wa MTU haununuliwi, hata kwa shilingi bilioni moja!
Mahimbo anadai kuporwa mke. Hivi inawezekana mwanamke - tena mrembo, mwenye akili timamu kama Josephine - akakubali "kuporwa" kutoka kwa mumeme Mahimbo? Inaingia akilini kweli hii?
CCM wamekosea step. Badala ya wananchi kumchukia, sasa wanampenda zaidi. JK anajidhalilisha, kwani wananchi hawamwelewi. Wana-CCM wengi tu wamekiri - tena wengi wakiwa viongozi waandamizi - kwamba kesi ya madai dhidi ya Slaa ina msingi wa kisiasa, kwamba ni lengo la kumharibia.
Mimi nilidhani kuna mtu ambaye aliwaambia wananchi WASIICHAGUE CCM. Waliamua hata kabla Slaa hajatangazwa kugombea urais, na alipotangazwa rasmi, kwa wengi wa maskini hawa imekuwa ni majibu ya ndoto zao. Sikujua kwamba kila kona nchini, Kaskazini hadi Kusini, Mashariki hadi Magharibi, ni wimbo mmoja tu unaoimbwa - CHADEMA! Hata vyama vingine vya siasa havitajwi kwa mapenzi. Tembea mtaani kwako, wasalimie kwa alama ya vidole viwili - nembo ya CHADEMA - uone ni mikono mingapi itarudi kwako.
Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema: Upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM.
Viongozi wa CCM hawakumwelewa. Walidhani kwamba kutatokea baadhi ya watu, ndani ya CCM, wakajitokeza na kuleta upinzani. La hasha! Wapinzani wa kweli ndani ya CCM ni WANACHAMA WAKE, ambao sasa wamechoshwa na kila aina ya uonevu, majungu, vitimbi na ufisadi ndani ya CCM. Ile kauli ya "CCM ina wenyewe na wenyewe ndio sisi" ni mojawapo ya vitendo vya ufisadi ambavyo wana-CCM wamechoshwa navyo. Nenda kwenye Jimbo la Uchaguzi, Masasi, uone jinsi mgombea wa CCM, Mariam Kasembe, anavyohenyeshwa kwenye kampeni. Rudi hapa Kawe, uone jinsi Angela Kizigha anavyozomewa, tena na wana-CCM, wanaompa alama ya vidole viwili kila anapojaribu kwenda kuhutubia.
Mwanzo wa mwisho wa utawala wa CCM umefika. Kila kadri CCM wanavyozidi kumchafua Dk. Slaa na wagombea wengine wa CHADEMA, ndivyo wanavyozidi kumfagilia yeye pamoja na CHADEMA. Walivyoharibu (EPA, Richmond, Meremeta, Deep Green, n.k.), labda hawakufikiria kwamba wangekuja kulipa siku moja, tena wangekuja kulipa kwa KUONDOLEWA madarakani. Vyama vya upinzani havina kazi kubwa ya kujinadi, kwani tayari CCM imeshawafanyia kampeni miaka mingi iliyopita. Wananchi waliipa CCM mtihani wao wa mwisho, walipomchagua Kikwete kwa kura nyingi (Lina uhakika hili?), lakini AMEFELI mtihani huo!
Kadri CCM wanavyochafua - na kweli wamejichafulia, kuanzia kwenye kura za maoni ndani ya CCM - ndivyo wanachama wao wanavyochukia, na wameapa kupiga kura ya kisasi. Watanzania wengine wamesema HAWAYAONI hayo maisha bora waliyoahidiwa, na wanashangaa ari zaidi ni ya nini wakati kuna mafisadi ambao bado hawajahukumiwa; kasi zaidi ni ya nini wakati hata nusu ya ahadi za uchaguzi za 2005 hazijatekelezwa; na nguvu zaidi ni ya nini wakati umaskini umekithiri na unazidi kuwaangamiza vijana wanaoteketea kwa kukimbilia mijini (wengi wao wakipigwa, kuchomwa moto na kupoteza maisha yao, kwa kujihusisha na ubakaji), huku vijiji vikibakia na wazee, watoto na wanawake!
Ushindi ni dhahiri kwa Slaa na CHADEMA, kwa kuwa ufisadi umevuka mipaka. Wananchi wameona jinsi CCM wanavyotumbua pesa kwenye kampeni. Wamesema kama ni hongo watapokea, lakini kwa upande wa kura, CCM isahau kurejeshwa madarakani. Asilimia themanini (80%) ya viti vya ubunge vitakwenda upinzani, huku asilimia tisini (90%) ya viti vya udiwani vitakwenda upinzani. Slaa atashinda kwa asilimia sitini (60%), na hii ni kwa kuwa bado kuna 'wajinga' wanaopumbazwa, kwamba Kikwete bado ni "mtu wa watu"!
-> Mwana wa Haki
2010 HATUDANGANYIKI. CCM mnajidanganya!