Dr. Slaa amtesa Katibu Mkuu CHADEMA, Vincent Mashinji

Chabruma

JF-Expert Member
Sep 19, 2013
5,660
1,777
Hakika Viatu vya Dr Slaa havijapata mvaaji

image.jpg


VIATU vya ukatibu mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alivyokuwa amevivaa Dk. Willbrod Slaa, vinatajwa kutomtosha Katibu Mkuu wa sasa wa chama hicho Dk. Vincent Mashinji. RAI linaripoti.

Dalili za Dk. Mashinji kuonekana kutoweza kwenda na kasi ya mtangulizi wake zinatajwa kuonekana mapema kabla ya kuteuliwa Machi 12, mwaka huu baada ya baadhi ya makada wenye ushawishi ndani ya chama hicho kutomkubali.

Baadhi ya makada waliokuwa wakimpinga Dk. Mashinji ambao baadhi yao ni wabunge wa Chadema walikuwa wakitaka kiti cha Katibu Mkuu kilichoachwa na Dk. Slaa miezi kadhaa kabla ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, kikaliwe na Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye.

Ushawishi wa kulifanikisha suala hilo ulishaanza kwa hoja kuwa Sumaye ni mwanasiasa mwenye uzoefu ambaye anaouwezo wa kuyafikia au hata kuyapita mafanikio ya Chadema ya Dk. Slaa ambaye alijiuzulu kwa hoja ya kutomuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.

Hata hivyo makada hao walishindwa nguvu na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe ambaye kwa usiri wa hali ya juu aliibuka na jina la Dk. Mashinji kwenye mkutano wa Baraza Kuu.

Ingawa Dk. Mashinji hakuwa na umaarufu wa kisiasa, wajumbe wengi wa Baraza Kuu waliomridhia waliamini anaouwezo wa kukifanyia chama hicho mambo makubwa kutokana na kuwa vigezo kadha wa kadha ikiwemo elimu na ujana.

Wakati Dk. Mashinji akisaka mwaka mmoja wa uongozi wake ndani ya chama hicho, tayari kumeanza kuibuka hoja za kumpinga moja kwa moja kwa madai kuwa ameshindwa kukanyaga baadhi ya mapito ya Dk. Slaa.

Makada waliobeba hoja hiyo wanaamini katika kipindi hiki ambacho chama na baadhi ya wanachama wake wanakamatwa na kufunguliwa kesi mbalimbali, Katibu Mkuu alipaswa kutoa matamko ambayo yangesaidia kutuliza hali ya kisiasa kama alivyokuwa akifanya Dk. Slaa.

Wakosoaji hao wamekuwa wakifikishiana malalamiko hayo kwa njia ya makundi yao ya mitandao ya kijamii yanayowajumuisha hasa WhatsApp.

Wanadai kuwa Katibu Mkuu wao hana meno, hana kauli nzito kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake na kwamba ameshindwa kuonesha uwezo wake wa kisiasa hasa akiwa kama Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini.

Moja ya mambo ambayo walalamikaji wanadai yalikuwa yaoneshe uwezo wa Dk. Mashinji ni sakata la Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwamba kiongozi wao huyo bila kuingilia uhuru wa Mahakama, alipaswa kutoa tamko zito lenye kuionya serikali.

Pia wanachama hao walienda mbali zaidi na kuhoji ukimya wa Dk. Mashinji katika kushughulikia matukio ambayo yalikuwa yanaisadia Chadema kujitangaza.

Janga la tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa wa Kagera na maeneo ya jirani, linatajwa kuwa moja ya masuala mbayo Dk. Mashinji ameshindwa kuyapa uzito uliostahili na badala yake kazi kubwa ilifanywa na Mwenyekiti wake na Lowassa ambaye anatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kuliko Katibu Mkuu wa chama hicho.

“Tumeona kesi za kina Lema, mpaka sasa Katibu hatoi matamko makali ambayo yataitia kiwewe serikali na kupunguza kuwaonea wanaChadema,”alisema.

ZIARA KANDA YA KATI

Hoja hiyo imeshika kasi zaidi sasa baada ya viongozi waandamizi wa Chadema, wakiongozwa na Mbowe kuanza ziara ya kikazi inayohusisha vikao vya ndani katika majimbo ya Kanda ya Kati (Dodoma, Morogoro na Singida), ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama kwa kanda hiyo uliofanyika jana.

Mwenyekiti Mbowe aliongoza timu iliyokwenda katika majimbo ya Mkoa wa Morogoro, akiambatana na Mjumbe wa Kamati Kuu Profesa Mwesiga Baregu, na kufanya mikutano katika majimbo ya Mlimba, Kilombero, Mikumi na Kilosa.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa (Tanganyika), Profesa Abdalla Safari aliongoza timu iliyokuwa mkoani Dodoma, akiambatana na Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalim, na kufanya ziara katika majimbo ya Kongwa na Mpwapwa, Chemba, Kondoa Kaskazini na Kondoa Kusini.

Wakati timu ya tatu iliongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika akiambatana na Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye ambao walitembelea majimbo ya Singida Mashariki, Singida Magharibi, Singida Mjini, Singida Kaskazini, Manyoni Mashariki na Manyoni Magharibi (Singida) na Bahi (Dodoma).

Katika ziara hiyo iliyoanza mwishoni mwa wiki, viongozi wakuu pamoja na Wajumbe wa Kamati Kuu waliambatana na wabunge ambao waligawanywa katika timu mbalimbali na kupangiwa majukumu kwenye kanda nane za upande wa Tanganyika, kati ya Kanda 10 za chama nchi nzima.

Watoa hoja wanaizungumzia ziara ya sasa kuwa ilipaswa Katibu Mkuu awe mstari wa mbele, lakini kwa sababu amekosa vionjo kama vya Dk. Slaa amelazimika kuwa nyuma ya Mwenyekiti na wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao ni Lowassa na Sumaye.

“Lakini hata sasa tunaona katika ziara zote wanaenda wajumbe wa Mkutano Mkuu na viongozi wengine waandamizi wa chama, yeye amebaki ofisini tu kwanini asitoke?,” waliuliza baadhi ya wanachama hao.

  1. MASHINJI AJIBU
Kutokana na madai hayo RAI lilizungumza na Dk. Mashinji ili kutolea ufafanuzi masuala hayo ambayo yameelekezwa kwake.

Akijibu hoja hizo kwanza Katibu Mkuu huyo wa Chadema, aliwatoa hofu wanachama wa chama hicho kutokana na ukimya wake, lakini pia aliwakumbusha kuzingatia hali halisi ya uhuru wa habari uliopo nchini kwa sasa.

Aidha, aliwaomba wanachama hao kutomlinganisha na mtu mwingine kwa sababu kila mtu ana karama yake na mtazamo wake katika uongozi

“Ili kujibu hoja yako kuna maswali mengi ambayo inabidi kujiuliza.. kipi cha msingi kati ya kutoa matamko 1,000 lakini waandishi wakashindwa kuandika au kureshape aina ya siasa unazotaka kuzifanya ili ufikie malengo ya siasa uzitakazo?.

“Katika hali hii iliyopo sasa mkuu wa nchi anaweza kupiga simu chumba cha habari na kumuuliza mhariri kwanini unaandika habari hiyo, au anaweza kuita vyombo vya habari na kurusha ‘live’ alafu akapiga marufuku kuandika habari zinazoongelewa na watu wengine, sasa tufanye siasa za aina gani?. haya ni maswali magumu. Itahitaji muda kutafakari kwa kina,” alisema.

Dk. Mashinji alifafanua zaidi kuwa kuna kitu kimoja katika maisha yake ambacho hapendi kukifanya ambacho ni kufanya kazi kwa kujilinganisha na mtu mwingine… “kwa sababu kila mtu amepewa karama yake na kila mtu ana mtazamo wake wa kutenda, hivyo ukipewa kazi unaangalia malengo mapana uliyonayo na kuangalia utayafikia vipi.

“Labda ulitakiwa kwenye vyombo vya habari, ila hawajui namna tukienda kwenye vyombo vya habari hatuandikwi, hivyo nadhani wangejua hili, haya maswali wangeyapatia majibu yake mapema,” alisema.

Hata hivyo alisema katika serikali ya awamu iliyopita kulikuwa na uhuru wa habari ndio maana Dk. Slaa, hata alipokuwa akipiga chafya alikuwa anaandikwa.

“Nisema kwamba unapoanza kazi yoyote kuna kasi, kuna watu wanakutathmini, sio jambo la kukaa muda wa saa 24 wakakufahamu, sasa hivi unaweza kuingia super market na watu wasitambue uwapo wako, ila kuna muda utafika na utashindwa hata kutoka mlangoni kwako, hivyo hili ni suala la muda tu.

“Ukishasoma mazingira kama hayo hakuna haja ya kuwaweka watu kwenye wakati mgumu. Hali iliyopo sasa imemuacha kila mtu njia panda,”alisema.

Pamoja na mambo mengine alisema amekuwa akifanya vikao na wabunge wake mara kwa mara, lakini hawakumwambia chochote kuhusu ukimya wake.

Hoja hiyo ya Dk. Mashinji pia iliungwa mkono na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha The Greater Dar es Salaam na mtaalamu wa siasa za itikadi na propaganda, Tambwe Hiza, ambaye pamoja na mambo mengine aliwataka wanachama kumpa muda kiongozi huyo.

Alisema haoni tatizo kwa Katibu huyo kuwa kimya kwa sababu siasa za wakati huu ukijitokeza kuzungumza sana unaweza kukumbana na mkono wa sheria.

“Pamoja na ukimya wake namwona katika mambo ya msingi na muhimu anafanyia kazi, kwa sababu kumekuwa na kesi nyingi sana baada ya kutangaza operesheni Ukuta, na Katibu Mkuu amekuwa akiandaa mawakili wa kutosha kutetea wanachama, kumekuwa na ziara nyingi zilizofanywa na viongozi wakati wa Ukuta hata baada ya kuahirishwa kumekuwa na ziara zinazoendelea sasa ambapo viongozi wakuu na wajumbe wa Kamati Kuu wapo majimboni.

“Kwa upande wake anatimiza wajibu wake, nafikiri kwa sababu amechaguliwa Machi tu… wampe muda aweze kufanya kile ambacho wanachoweza kukiona.

“Ameshakwenda kufungua ofisi wilaya ya Kinondoni, amefanya kazi nyingi, amekwenda nje ya nchi kukutana na vyama marafiki wa chama chetu, ila ukweli ni kwamba watu wengi walizoea makelele ya Dk Slaa.

“Tukumbuke kuwa Dk. Slaa mwaka 2010 alikuwa mgombea urais na kabla ya hapo alikuwa mbunge, ila hata hakuwa na umaarufu ambao Lema au Lissu wanao sasa, kwa sababu hawa wamepata umaarufu kwa ubunge tu.

Hivyo tumpe nafasi, tusimchanganye na Dk. Slaa kwa sababu Dk. Mashinji anafanya siasa za kisomi hivyo muda ukifika utamsikia akiwaka vilevile,” alisema.

Chanzo Rai
 
Wenyewe wanaita wana katibu mkuu msomi alieacha siasa za uanaharakati!
 
Duh ila tanzania bwana mbona tunakuwa wagumu kuelewa sasa mlitaka mumsikie kivipi wakati shughuli za kisasa zimepigwa marufuku. alafu jamani katibu mkuu is not all about kuongea majukwaani ina majukumu mengi hasa ya kisera na kiutawala sasa labda mje na takwimu ni kivp amepwaya kulinganisha na majukumu aliyonayo na pia malengo aliyopewa na chama. alafu pia its too early kumjudge sahivi hata mwaka hajamaliza nashauri mumpe muda anavyozidi kugain pace na experience na uongozi wa chama kikubwa kama chadema with time i believe atakuwa a better choice kuliko mnavyomchukulia
 
Kaazi kwelikweli .........yaani wale waliokuwa wakikesha hapa kumtukana Dr.Slaa eti leo wanataka kuja kivingine kuonyesha alikuwa mtu muhimu saana na wapo ambao wanataka kukubaliana na huu upuuzi mpya ........

Katibu Mkuu Dr.Mashinji anawaumiza sana CCM ndio maana wanashindwa hata kupumua .........
 
Wadau, imedhihirika kuwa CHADEMA wamekuja na mbinu zile zile walizokuwa wanadai kuwa ni za CCM za kukodi malori kupeleka watu kwenye mikutano. Hayo yamejitokeza kwenye mkutano wa Dr Slaa uliofanyika huko Kahama mara baada ya babu Slaa kukosa watu wa kumpokea na kumshangilia hasa baada ya vijana wengi kutoridhishwa na maamuzi ya CC ya kumvua uanachama ZITTO KABWE. Imedhihirika pia kuwa hata huko Kigoma hali hiyo imejitokeza. Hii ni dhahiri kuwa CHADEMA sasa imeshakufa na tukio la kumvua uongozi ZITTO KABWE limekifanya chama hicho kukosa mvuto kwa vijana.

Nawasilisha.

Source: Gazeti la Hoja la Ijumaa, Desemba 6-12, 2013

 
Back
Top Bottom