Kumekuwepo na taarifa zinazosambaa mtandaoni zikiihusisha Kampuni ya DP World kudhamini Ligi Kuu ya Soka la Wanaume Nchini Tanzania.
Taarifa hizi zililipotiwa pia Juni 24, 2023 kwenye Jukwaa la JamiiForums ambapo baadhi ya madai ilikuwa ni uwepo wa mpango wa TFF kuachana na wadhamini wa sasa ambao ni NBC.
Ukweli upoje?
Taarifa hizi zililipotiwa pia Juni 24, 2023 kwenye Jukwaa la JamiiForums ambapo baadhi ya madai ilikuwa ni uwepo wa mpango wa TFF kuachana na wadhamini wa sasa ambao ni NBC.
Ukweli upoje?
- Tunachokijua
- Juni 10, 2023, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Azimio la kuunga Mkono Mkataba wa Uwekezaji wa Bandari kati ya Tanzania na kampuni ya DP World ya Dubai.
Pendekezo hili lenye lengo la kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini lilisomwa na Waziri wa ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ambapo pamoja na mambo mengine alidai kuwa Serikali iliamua kutia saini ushirikiano ili kuongeza ufanisi Bandarini, ambapo ndio lango kuu la uchumi.
Mdhamini wa sasa wa ligi kuu ya Soka Tanzania Bara
Oktoba 6, 2021, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ilitia saini Mkataba wa kudhamini ligi hiyo baada ya kufikia makubaliano na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa udhamini wa kiasi cha Shillingi za Kitanzania bilioni 2.5.
Hafla hiyo fupi ya utiaji saini mkataba huo ilifanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency iliyopo Jijini Dar es Salaam ambapo viongozi wa pande zote mbili walikuwepo huku NBC ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Theobald Sabi aliyefuatana na wakurugenzi wengine wakati kwa upande wa TFF wao waliongozwa na Rais Wallace Karia.
Hivyo, hadi sasa mdhamini mkuu wa ligi kuu ya Tanzania bara ni Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).
Tetesi za DP World kudhamini ligi
Baada ya kupitishwa kwa azimio la uwekezaji wa Kampuni ya DP World kwenye Bandari ya Dar es Salaam, habari nyingi zinazohusisha kampuni tajwa zilianza kuibuka, ikiwemo hii ya kudhamini ligi kuu ya soka Tanzania Bara.
Mojawapo ya taarifa hizi inapatikana pia kwenye Jukwaa la JamiiForums, ambapo Juni 24, 2023, Mdau mmoja aliweka chapisho lake lenye kichwa cha habari "DP World Kudhamini Ligi Kuu Soka Tanzania Bara". Pamoja na madai mengine, andiko hili lilidokeza kuwa mpango wa kubadili nembo ya mdhamini mkuu kwenye jezi ya baadhi ya timu lilikuwa limekubaliwa.
Ukweli wa mambo ulivyo
JamiiForums imezungumza na Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amesema “Hapana, hata sijui lolote kuhusu suala hilo kiukweli.”
Pia, Afisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda athibitisha kutokuwepo kwa taarifa hizi kwenye ofisi yao. Amesema;
“Hatujapata taarifa kuhusu suala hilo, inawezekana wao (DP World) kama tetesi zilivyokuwa wanafikiria au wanajipanga kuja kwetu, wakija hapo ndipo tunaweza kutoa maelezo lakini kwa sasa hakuna kitu kama hicho.”
Hivyo, kwa kurejea taarifa rasmi za TFF pamoja na Bodi ya Ligi ambazo JamiiForums imezipata, Suala hili limethibitika kuwa sio la kweli.