Dogo akaja mikono mitupu!

Mtambuzi

Platinum Member
Oct 29, 2008
8,810
15,393
Ndio nilikuwa nimetia timu jijini Dar kwa mara ya pili mnamo mwaka 1989 baada ya mara kwanza kuja na kuchafua hali ya hewa nikiwa kwa kaka yangu na kupigwa patresheni kijijini. Safari hii nilifikia kwa mjomba angu ili kuona kama mjomba ataweza kunisaidia kuendelea na masomo ya kidato cha sita. Basi, nikawa nakaa kwa mjomba maeneo ya Temeke kata ya 14 nikiwa sina shughuli maalum ya kufanya. Hapo jirani na kwa mjomba kulikuwa na mzee mmoja Mshihiri mwenye duka.

Mzee huyo alikuwa na mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 12 wakati huo, ambaye alikuwa anasoma darasa la tano. Huyu mtoto alinizoea sana na mwisho akaniomba niwe namfundisha. Lakini fundishwa yake ilikuwa ya ajabu, kwani alichokuwa anataka ni kufanyiwa homework wanazopewa shuleni basi. Kila nikimfanyia homework akawa ananipa kitu kidogo kama shilingi 200 au 300. Nikawa mzee nimepata kibarua. Nikiona imepita wiki hajaleta homework namuuliza kulikoni, kama walimu wana malaria au vipi. Iliendelea hivyo mwisho nikawa namwambia anipe hela hata kama simfanyii homework.

Nilimwambia kwamba nasubiri kwenda Chuo Kikuu na kumwahidi kwamba, nikimaliza Chuo Kikuu nitakuwa Mbunge wa Temeke na kwa sababu yeye atakuwa mkubwa wakati huo, nilimwambia nitampa ukuu wa wilaya. Kwa sababu ya utoto na somo la Siasa halikuwa likipanda alikubali. Akaanza kuiba fedha nyingi dukani kwao na kuniletea. Dhambi eh, wakati mwingine! Nikiwa hapo Temeke nikaanza uhusiano na binti mmoja. Naye binti nikamwambia nasubiri kwenda Chuo Kikuu na kwamba, mambo yangu ni mazuri, vijihela vya chipsi kuku havinisumbui. Huyu binti aliniamini kwa sababu yule bwana mdogo wakati huo homework zilikuwa zimeongezeka na mshiko nao ukawa umeongezeka.Siku moja yule binti alinifuata akaniambia ana hamu sana ya chipsi na bia. Mzee mzima nilikuwa na kama shilingi mia tu mfukoni. Ilibidi nimwambie yule binti asubiri.

Nilikwenda hapo dukani kwao dogo na bahati nilimkuta. Nilimpiga signo na kumwita kando. Nilimwambia nina shida ya kufa na kupona, anitafutie shilingi 1,000. Dogo aliahidi kwamba, baada ya dakika ishirini angeniwezesha. Aliniambia baba yake akienda kuswali Insha tu, atashughulikia chapchap shida ya mwalimu wake wa tuisheni ya homework, yaani mimi.
Nilimwambia naenda kumsubiri baa ambayo anaijua, kwani tulikuwa tukienda hapo mara kadhaa kunywa soda. Nilimuuliza kama ana uhakika atapata, akasema niondoe hofu kabisa, ni lazima apate, basi nilimpitia demu wangu tukaenda pale baa. Nilipofika pale baa niliagiza bia kwa ‘mtoto' na chipsi. Kwa sababu wahudumu walikuwa kidogo wananijua hawakunidai kabla. Tukawa tunapiga darasa na 'mtoto' huku akijinoma chipsi, kuku na bia. ‘Mtoto' akamaliza msosi na bia, ikaagizwa bia ya pili, dogo hatokei.

Wasiwasi ukanishika, niliona ni vyema nifuatilie.
Ile nasimama, nikamwona dogo akiwa na baba yake na kaka yake fulani mnoko sana na Polisi aliyevaa sare. Nilihisi kama vile sipumui na sina mwili. Kabla sijapata muda wa kujiuliza, nilimsikia dogo akisema, ‘ni huyu hapa, huwa nampa kila siku.' Nilijua kila kitu kimekwenda ndivyo sivyo. Dogo alikuwa menaswa kwenye jaribio lake la kunasua ile elfu. Pale nilikuwa mtuhumiwa namba moja wa kumghilibu mtoto kujipatia mali, halafu hapo mezani chipsi, kuku na bia mbili zinahitaji kulipiwa. ‘Afande mchukue bwana, tapeli mkubwa.' Yule kaka yake dogo alisema. 'Bwana uko chini ya ulinzi kwa tuhuma za kumtuma mtoto kufanya uhalifu wa wizi dukani. Naomba tufuatane kwenda kituoni.' Alisema yule Polisi.

Wahudumu wa baa nao walikuwa wamefika wakitaka kulipwa chapaa zao. Nilimtazama yule demu wangu ambaye siku zote huwa anakunywa na kula chipsi kuku bila kujua kwamba, ni Juhudi za mfadhili dogo.
‘Tunamdai afande, tunaomba atulipe kwanza.' Mhudumu mmoja alisema. Nilijiuliza ni wakati gani radi huwa zinapiga bila mawingu ya mvua. Ni kwa nini isiwe wakati kama ule? 'Lipa bwana twende zetu.' Afande alifoka. Nilijifanya kupekua mifukoni na kusema, 'nimezisahau nyumbani.' Baba yake dogo alisema, ‘hujasahau chochote, ulikuwa ukisubiri kuletewa, ule na hawara yako. Mimi niwatafutie, nyie mbugie, tena bia! Hapana hiyo haikubaliki.'

Najua mnatamani kujua kilichotokea baadaye.(Umbeya tu!) Kwa taarifa yenu sikupelekwa Keko wala Ukonga, mambo yaliisha kimya kimya. Na kijijini sikurudishwa, nilipelekwa shule na baadae chuo na leo niko hapa JF.
 
Hapa leo sitanii, hawa wanangu King'asti, Cantalisia na na yule mwingine mwenye maneno mengi kama Chiriku..............Husninyo, mkisema lolote kwenye uzi huu, mtanitambua, ni bora msionekane kwenye anga hii................Nitawachapaaaa..........................LOL

Wallahi Sitanii, si mnanijua!
 
Ungeanza na kusema "Hadithi Hadithi hapo zamani 1989 palikuwa na mwalimu na mtoto mmoja ......" ningeelewa vizuri
 
Mtambuzi unatisha, usanii uliuanza mbali sana, sipate picha jinsi unvyopiga deal hapo ofisini kwako na kuzipiga ten percent za kodi za walalahoi! Loh!:A S embarassed:
 
Kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi heeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeh. Mtambuzi umenivunja mbavu zangu, yaani wewe chiboko. Nakumbuka siku moja nilikuwa kwenye dala dala bubu toka Ubungo - Posta. Daladala bubu ni zile ambazo mtu ana Noah yake yuko peke yake anafika Ubungo kisha anatangaza Posta 1,000.00 n.k

Kidogo nikazama JF nikakutana nauzi wa Mtambuzi. Yaani kwenye gari nilionekana kama kituko kwa jinsi nilivyokuwa nakenua meno bila watu kujua nini chanzo, kumbe Mtambuzi. Uzi wenyewe ulikuwa ule ulioenda kuzika Songea.
 
tehe! tehe! baba Ngina kumbe wewe ndo mwasisi wa uchakachuaji? yaani ulikuwa unachakachua homework za dogo? kisa hawala mkono uende kinywani,mbona hawa hukuwafanyia kareti za kichina na kuwalilia kama paka upate heshima?
 
Kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi kwikwi heeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeh. Mtambuzi umenivunja mbavu zangu, yaani wewe chiboko. Nakumbuka siku moja nilikuwa kwenye dala dala bubu toka Ubungo - Posta. Daladala bubu ni zile ambazo mtu ana Noah yake yuko peke yake anafika Ubungo kisha anatangaza Posta 1,000.00 n.k

Kidogo nikazama JF nikakutana nauzi wa Mtambuzi. Yaani kwenye gari nilionekana kama kituo kwa jinsi nilivyokuwa nakenua meno bila watu kujua nini chanzo, kumbe Mtambuzi. Uzi wenyewe ulikuwa ule ulioenda kuzika Songea.

Ule uzi wa Mazishi Songea ulikuwa ni kiboko mzee, yaani mzee mzima nikakalishwa kwenye kigoda kutambikiwa kwa sababu ya unzinzi! ile sitakuja kuisahau..............LOL
Lakini hii ya leo umeionaje.................... nilifedhehekaje!?
 
Huyu Baba yenu mbona mkali hivi ? Atapata wajukuu kweli huyu ! Hawa si ndiyo ma'baba wanaokaba hadi penati !
Hahahahaha!
Wala hana ukali wowote huyu,
Dawa yake ni kumpelekea mchumba Baunsa tu anatulia mwenyewe!
Anaijua vizuri shuhuli ya mabaunsa lol!
 
Back
Top Bottom