Kesi ya Uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo 'CHADEMA' Tundu Antiphas Lissu iliendelea leo
Februari 9, 2026 Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es salaam.
Kumekuwapo na grafiki iliyotumia utambulisho wa The Chanzo ikiwa na kichwa cha habari kinachomnukuu Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Rugemeleza Nshala kikisema
"Dkt. Nshala asema, nimejiondoa kwenye kesi ya Lissu maana viongozi wenzangu wana maslahi binafsi katika hii kesi"
Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji uliofanywa na JamiiCheck umejiridhisha kuwa taarifa hiyo si ya kweli kwani kauli hiyo haijatolewa na Dkt. Nshala. Aidha kupitia utafutaji wa maneno muhimu imebainika kuwa grafiki hiyo haijachapishwa na The Chanzo bali imeghushiwa na wapotoshaji. Kupitia kurasa zake rasmi
The Chanzo imekanusha taarifa hiyo kuwa si ya kweli.
"Habari hii inayosambazwa katika majukwaa mbalimbali haijatolewa na The Chanzo, ni habari potofu."
Akizungumza na Waandishi wa Habari akiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam Februari 09, 2026 hakutoa kauli yoyote ya kujiondoa kwenye kesi hiyo bali alibainisha hoja tatu zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu mbele ya Mahakama.
Dkt. Nshala, alisema katika wasilisho lake Mahakamani, Lissu amewaeleza Majaji kuhusu mapito anayopitia gerezani ikiwemo uhuru na faragha ya kuzungumza na Mawakili na washauri wake wa sheria, kuzuiliwa kwa wanachama na viongozi wa CHADEMA wanaokwenda kumuona gerezani, sambamba na kucheleweshwa kwa kesi yake katika usikilizwaji kwani amekaa gerezani kwa siku zaidi ya 300 hadi sasa lakini kesi yake imesikilizwa kwa siku zisizozidi 15 hadi sasa