Dkt. Nasra: Serikali iweke wazi Mikataba yote ya Uwekezaji inayoingia na Nchi nyingine

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
617
1,541
Utata wa Diplomasia ya Uchumi, Usifubaze Mapambano ya Ulinzi wa Rasilimali Zetu Nchini.

{Uchambuzi wa Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2023/24}.

Utangulizi
Jumanne Mei 23, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stergomena Lawrence (Mb) amewasilisha bungeni Mpango wa makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo ikiwa na jumla kiasi cha Shilingi bilioni 247.9

Mpango huu utajadiliwa na kuidhinishwa na bunge kwa siku moja. Miongoni mwa majukumu yanayopaswa kuratibiwa na kuwepo kwenye mpango wa bajeti ni pamoja na; Kusimamia utekelezaji wa sera ya nje ya Taifa; Kuratibu masuala ya mahusiano kati ya Tanzania na nchi zingine, jumuiya na mashirikiano ya kimataifa; Kusimamia masuala ya mikataba na makubaliano ya kimataifa; Kuratibu masuala ya watanzania wanaoishi nje ya nchi; kuzisimamia taasisi za Serikali zilizo chini ya wizara.

Kutokana na majukumu haya ambayo yanagusa maslahi ya taifa, ACT Wazalendo kupitia Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Nasra Nassor Omar tumefanya uchambuzi wa hotuba ya mwaka huu kwa kuangalia; taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2022/23; hoja na msimamo ya Serikali juu masuala mbalimbali ndani ya wizara; Vipaumbele na mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Katika uchambuzi wetu tumeangalia maeneo matano (5) na kuyatolea mapendekezo ya namna bora ya kuyaendea. Kwa ujumla, tumeona hakuna mpango wa Serikali kuhusiana na changamoto zinazowakumba Watanzania wanaoishi nje hususani wanaokwenda kufanya kazi za kola ya bluu (wafanyakazi wa ndani, mahoteli) na shughuli za biashara ndogo ndogo.

Vilevile, kuwepo kwa hadaa ya diplomasia ya uchumi katika kubainisha na kuelewesha umma juu ya nafasi na maslahi ya Tanzania katika dhana ya diplomasia ya uchumi. Aidha, Serikali kutoweka mkazo na msisitizo katika kuratibu na kushawishi nchi rafiki kutufutia madeni au kuyapunguza ama kutuwekea masharti nafuu ya kuyalipa.

Maeneo matano (5) ya uchambuzi wa ACT Wazalendo kuhusu Mpango na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

1. Hasara za mikataba mibovu na mifumo ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji wa Kimataifa
Wizara ya Mambo ya Nje ina wajibu wa kuratibu na kusimamia mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa. Katika uratibu huo tumeshuhudia Tanzania ikisaini mikataba ya uwekezaji ya aina mbalimbali hususani mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili (Bilateral Investment Treaties_BITs) ambayo shabaha yake ni kuhamasisha na kulinda uwekezaji unaofanywa na nchi mojawapo ndani ya nchi nyingine (baina ya nchi hizo mbili).

Ingawa, tunatambua umuhimu na nafasi ya uwekezaji kwenye maendeleo ya uchumi wa taifa, hoja yetu kubwa kuhusu mikataba ya uwekezaji ya kimataifa ni kuongezeka kwa kasi kwa kesi, madai na fidia zinazopaswa kulipwa na Serikali ya Tanzania kwa Makampuni ya Kimataifa. Ambapo mikataba ya namna hii imekuwa ikitumika kama nyenzo ya unyonyaji na uporaji wa utajiri wa maliasili na nguvu za Watanzania kinyume na madai yanayopigiwa chapuo.

Wakati Serikali ikiaminisha na kuuambia umma wa Tanzania kuwa mikataba hii ni nyenzo ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) uzoefu na tafiti zinaonyesha hakuna uhusiano wa kisayansi (kitafiti) kati ya kuridhia na kuingia mikataba ya namna hii na kutiririka kwa uwekezaji. Hivyo, tunashawishika kusema kuwa mikataba mingi ya uwekezaji baina ya nchi mbili sio njia inayotumika na wawekezaji kufanya maaamuzi ya uwekezaji bali wanatumia kama nyenzo za kuzibana Serikali za nchi maskini zisiweze kutikisa maslahi yao (wawekezaji).

Athari za mikataba mingi ya uwekezaji wa kimataifa ni nyingi sana lakini katika uchambuzi wetu tumetaja kipengele cha mikataba kinachoruhusu wawekezaji wa nje kuishataki Serikali katika mahakama za kimataifa. Hii ni kutokana na uzoefu ukionyesha kuwa mifumo mbalimbali ya kimataifa ya utatuzi wa migogoro ya biashara na uwekezaji ikiwa na changamoto zinazopelekea mzigo mkubwa wa gharama za kesi na fidia, kukosekana kwa uwazi katika Mwenendo wa mashauri.

Aidha, athari kubwa zaidi ni kuminya uhuru wa nchi kujiamulia mambo yake kwenye matumizi ya rasilimali kwa kupunguzwa nguvu ya kudhibiti unyonyaji na uporaji wa rasilimali za nchi.

Katika uratibu unaofanywa na wizara ya mambo ya nje na baadaye wizara ya katiba na Sheria kuingia mikataba kwa miaka 17 (kuanzia 2005- 2022) Tanzania imesaini mikataba baina ya nchi mbili ipatayo 19.

Ndani ya miaka hiyo, kuna kesi zaidi ya 10 zilizofunguliwa na wawekezaji dhidi ya Serikali ya Tanzani katika Kituo cha kimataifa cha usuluhishi kesi za uwekezaji (ICSID). Kesi hizi zinaigharimu sana nchi yetu kutokana na mapengo yaliyopo kwenye mikataba iliyoingia. Baadhi ya mashauri yaliyofunguliwa na Madai yao tumeyaonyesha kama ifuatavyo;

i. Kampuni ya Winshear Gold Corp (ICSID Na.Kesi.ARB/20/25); Inapeleka madai ya Sh. bilioni 223.8 kwa kutumia makataba kati ya Canada na TZ. Kesi bado inaendelea.

ii. Kampuni ya Indiana Resources Ltd kupitia kampuni tanzu za Nachingwea U.K. Ltd, Ntaka Nickel Holding Ltd & Nachingwea naNickel Ltd (ICSID Case No. ARB/20/38) nayo inataka kiasi cha Sh. bilioni 218.3 MIUMBI. Kesi bado inaendelea inaendelea.

iii. Madai ya Shilingi trilioni 3.7 ($1.57bln) Kampuni ya Symbion Power Tanzania Ltd & wengine (ICSID kesi Na. ARB/19/17)

iv. Standard Chatered Bank (Hong Kong) Ltd (ICSID Case No.ARB/15/41); Mkataba wa Uwekezaji kati ya IPTL na Tanzania. Tanzania iliamuriwa kuilipa SCB-HK dola za Marekani milioni 185.45 (sawa na Sh. bilioni 438.5) pamoja na riba ya 2% kila baada ya miezi 6 kuanzia Septemba 1, 2018.

v. Kesi ya Standard Chartered Bank (Hong Kong) Ltd22 (ICSID Case No. ARB/10/20) Mkataba wa uwekezaji kati ya TANESCO na IPTL. TANESCO iliamuriwa kuilipa SCB–HK dola Marekani milioni 148.4 (sawa na bilioni 346) na riba ya 2% kila baada ya miezi 3 kuanzia Septemba 30, 2015.

Hizi ni baadhi ya keshi na madai yake pamoja na fidia kwa kesi zilizoamriwa. Orodha ni ndefu. Hivi karibu Novemba 2022 ndege aina ya Airbus A220 ya Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) ilishikiliwa nchini Uholanzi kutokana na mwekezaji kutoka Swedeni kushinda kesi dola 165 milioni (Sh.380 bilioni) dhidi ya Tanzania na kuishawishi Mahakama ya uholanzi kushikilia ndege hiyo kama kigezo cha kushinikiza malipo yake.

Katika mpango wa bajeti na mwelekeo wa Serikali juu ya sera ya mambo ya nje kwenye masuala ya uwekezaji, mikataba na makubaliano mbalimbali hakuna taarifa iliyoelezwa na Serikali mbele ya bunge na kwa umma.

Hofu na wasiwasi wetu ni kwamba kupitia vipengele hivi vya mfumo wa kimataifa wa usuluhishi wa migogoro kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya kesi ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya nchi yetu kwa miaka 15.

Kipekee wasiwasi wetu kuhusu mashauri yaliyopo kwenye vituo vya kimataifa ambayo yanaikamua nchi kulipa Kampuni hizo trilioni za shilingi sio tu kinatishia kupunguza uwezo wa Serikali kuwekeza kwenye huduma muhimu na ujenzi wa miundombinu bali hata juu ya uwezo wao wa kutunga sheria na sera, na kudhibiti uwekezaji kwa maslahi ya umma.

Hivyo, ACT Wazalendo tunaitaka Serikali sio tu kupiga mapambio ya kuvutia uwekezaji iweke wazi mikataba yote ya uwekezaji inayoingia baina ya Tanzania na nchi nyingine.
Pili, tunatoa wito kwa Serikali kutathimini mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili kama ipo haja ya kuendelea nayo au kusitisha kabisa mikataba yenye vipengele vinavyopalilia uporaji wa rasilimali na unyonyaji wa nguvu kazi. Tatu, ni wakati wa kuamua nafasi yetu ya kuendelea kwenye vyombo vya kimataifa vya utatuzi wa migogoro ya kimataifa.

Mwisho, Wizara ya mambo ya nje kwa kushirikiana na wizara ya katiba na sheria inapaswa kuongeza umakini katika kubaini mapengo ya kisheria yanayotokana na uwekezaji yatakayoitia hasara zaidi nchi yetu.

2. Utata na hadaa za diplomasia ya uchumi kwa Tanzania
Katika hotuba za kila mwaka za mpango wa bajeti ya wizara ya fedha inataja sera ya mambo ya nje inayoongozwa na diplomasia ya uchumi. Ukiachilia utata wa uelewa wa pamoja baina ya viongozi, wanasiasa na wananchi wa kawaida.

Bado hakuna Mwongozo wa jumla kuhusu nini dhana yenyewe pamoja na sera kusema lengo ni kuhakikisha maslahi ya kiuchumi ya taifa katika kuamua mahusiano kati ya Tanzania na nchi zingine.

Ingawa kupitia uzoefu wa utekelezaji wake tangu miaka ya 1990 hadi sasa, mkanganyiko unatokana na dhana inayoelezwa na viongozi ambayo inakinzana na uhalisia wake kwa wananchi. Viongozi, wanaeleza kama diplomasia ya uchumi ni mkombozi wa kuliwezesha taifa kutumia mahusiano yake na nchi nyingine kujiletea maendeleo. Ili kutumia fursa hiyo kama taifa linapaswa kujitangaza kama ni sehemu salama kuvutia uwekezaji, kuweka mazingira mazuri ya kibiashara, safari za nje kwenye nchi zilizoendelea, kushiriki mijadala kwenye majukwaa ya kimataifa, kuingia makubaliano na mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Kwa kutazama sifa hizi na diplomasia ya uchumi ni dhahiri kuwa hii haiwezi kutoa uhakika wa kutumia mahusiano na nchi, taasisi, Mashirika mengine kujiletea maendeleo.

Kwa uzoefu wa miaka 30 tangu Tanzania iongozwe na sera ya nje yenye msingi wa diplomasia ya uchumi, ni wazi kuwa diplomasia ya uchumi ni Mradi wa kusimika na kuimarisha utengamano wa chumi za kiafrika kwenye uchumi wa mtaji wa kibepari wa kimataifa na mzunguko wa soko. Katika hali hii ni muhimu kama nchi kutafakari nafasi yetu kwenye uchumi wa dunia.

Nafasi yetu, bado ni kuzalisha na kutoa malighafi na nguvu kazi kwenye mtaji wa kimataifa na soko la dunia, hali hii haijabadilika tangu wakati tunatawaliwa na mkoloni. Sera ya diplomasia ya uchumi inaenda kukazia tu wajibu huo kwenye mlinganyo wa kibeberu, sisi tunakuwa wajibu wa uzalishaji na usambazaji wa malaghafi na mahitaji mengine kwa mataifa yanayonyanyuka na yaliyoendelea kitambo.

Aina hii ya mahusiano ya kimataifa inayobebwa na diplomasia ya uchumi sio mpya na wala haiwezi kutumika kama nyenzo ya kukabiliana za kutoendelea kwa nchi yetu.

Katika hoja ya kutaka mahusiano ya nje kwenye masuala ya uwekezaji na utatuzi wa migogoro ya kimataifa ya uwekezaji tumelezea namna mikataba mbalimbali inayotumia kama nyenzo ya kupora rasilimali huku ikizuia uwezo wa Serikali kuyadhibiti mataifa na makampuni yanayofanya hivyo.

Huu ni mfano wa dhahiri licha ya takwimu zinazotolewa za kuongezeka kwa idadi ya miradi ya uwekezaji, mitaji inayotiririshwa nchini bado kuna changamoto kubwa ambazo kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji, tunapata kiduchu.

ACT Wazalendo inaamini uzalendo wa rasilimali unapaswa kuongoza sera ya mambo ya nje ili kutumia fursa za mahusiano kwa maslahi ya umma badala ya maslahi ya makampuni, mataifa na watu binafsi. Hivyo, diplomasia ya ukombozi (liberation diplomacy) inapaswa kuwa ndio dira ya sera yetu ya mambo ya nje

3. Kutopewa kipaumbele kushughulikia mzigo mkubwa wa Deni la nje la Taifa
Kasi ya ukuaji wa deni la taifa nchini inatishia uwezo wetu wa kujihudumia, maendeleo ya watu na athari kwa mwenendo wa jumla wa uchumi wetu. Taarifa ya tathimini ya uchumi wa nchi yetu kwa mwezi Novemba mwaka jana 2022 iliyotolewa na Benki Kuu ya Taifa (BOT) inaonyesha kukua kwa kasi kwa deni la taifa. Takwimu zinaonyesha ndani ya mwaka mmoja kasi ya deni la taifa limeongezeka kwa Trilioni 27 kufikia Shilingi Trilioni 98.15 huku tukiona kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi umeendelea kukua kwa asilimia 4.5.

Taarifa zinaonyesha watu wanaotudai, Mashirika na nchi mbalimbali na mchanganuo wao. Hawa ni washirika ambao kwa namna moja wanaweza kushawishiwa kutufutia madeni (hususani yale yanayotokana na riba-ziada), kupunguziwa au kuwekewa masharti nafuu ya kuyalipa.

Wizara ya mambo ya nje inao wajibu wa kuwa na mkakati wa kushawishi nchi na wadau waliotukopesha kutufutia madeni au kutupatia nafuu ya madeni. Katika taarifa ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliyowasilishwa Bungeni tofauti na miaka mingine haijaeleza azma ya kutumia urafiki na mahusiano mema ya kimataifa katika kunusuru nchi yetu juu ya kasi kubwa ya ukuuaji wa deni la Serikali. ACT Wazalendo tunatoa wito kwa Serikali ni muhimu kutumia kuimarika kwa mahusiano katika ya nchi yetu na marafiki au taasisi mbalimbali katika kuzishawishi kutufutia madeni.

4. Vikwazo vya Watanzania wanaoishi nje (Diaspora) katika kuchangia maendeleo ya Taifa
Watanzania wanaoishi nje ya nchi wamekuwa wakiongezeka kila mwaka, lakini kuna changamoto kadhaa zinazozuia mchangao wao kwenye maendeleo ya nchi yetu. Miongoni mwa changamoto hizo ni suala la mikataba ya kazi kwa wanaoenda kufanya kazi la kola ya bluu. Idadi ya Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi hususani kazi za ndani, kwenye hoteli, migodini na shughuli za uvunaji wa misitu (informal sector) inazidi kuongezeka kila mwaka.

Lakini hakuna utaratibu mzuri wa kufuatilia, kuwalinda na kuwatambua Watanzania hao wanapokuwa huko. Mara kadhaa zimekuwa zikipatikana taarifa za kupitia unyanyasaji, ukatili wakati mwingine hata kupoteza maisha.

Aidha, kumekuwa na malalamiko juu ya suala la kisheria kuhusu hadhi ya uraia kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni ambao tayari wamepata uraia wa nchi hizo ikiwa bado wana uzalendo na nchi yao ya asili (Tanzania). Suala la hadhi ya uraia ni jambo la kisheria, nchi yetu bado haitambui uraia pacha, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu.

Athari za uamuzi na msimamo huu licha ya faida zake katika nyakati zilizopo inakuwa kikwazo katika kutumia dhana ya uzalendo kwenye kuvutia uwekezaji wenye maslahi mapana ya taifa.

Ingawa, takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa kiwango cha fedha zinazotumwa na Watanzania waliopo nje kuja nchini (remittances) kufikia kiasi cha Sh. trilioni 2.6 (dola za Marekani bilioni 1.1) kwa kipindi cha Januari hadi desemba 2022 ikilinganishwa na Sh. trilioni 1.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021. Bado mchango huu ni mdogo ukilinganishwa na nchi zingine za Afrika Mashariki hususani Kenya (Tsh.trilioni 8.4), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) (Tsh.trilioni 3.9), Uganda (Tsh.trilioni 2.5) kwa takwimu za mwaka 2022.

Changamoto zinazohusu fedha za kupokelewa kutoka kwa Watanzania waishio nje inahusisha sana masuala ya kibenki, mifumo ya miamala (kupokea na kutuma). Kuwepo kwa sheria za kama vile ya ugaidi, sheria ya utakatishaji wa fedha zinaathiri kwenye urahisi wa kutumia mifumo ya kidigitali kupokea fedha.

Aidha, suala la uraia pacha una athari kwenye uwekezaji, hususani kuvutia wazawa kuwekeza kwenye miradi ya kimakakati. Sheria za uwekezaji kama zilivyo kwa nchi nyingi haitoi nafuu kwa Diaspora kama raia wengine. Watapata nafuu sio kwa kigezo cha uraia wao bali vigezo vingine kama ilivyo kwa raia ambao hawana asili na Tanzania. Hivyo, ili linapelekea kuwekeza kwenye sekta isiyo na tija katika kusukuma maendeleo unaona wanaweka kwenye sekta ya nyumba na kupanda na maduka makubwa (shopping malls).

Changamoto hizi kwa muda mrefu zimekuwa ni kikwazo katika kutumia fursa ya Watanzania hawa kuiendeleza nchi yetu.
ACT Wazalendo tunatoa rai kwa Serikali ya Tanzania kuona haja ya kufanya mapitio ya sheria za nchi kuruhusu chaguo kwa Watanzania kuwa na uraia wa nchi mbili.

5. Kushikiliwa kwa Watanzania Nje ya Nchi kwa zaidi ya miaka 7
ACT Wazalendo hatujaridhishwa na ukimya wa Serikali kuhusu ushughulikiaji wa changamoto wanazopitia watanzania wanaofanya shughuli zao nje ya nchi hususani suala la Watanzania 37 waliowekwa kizuizini nchini Msumbuji tangu mwaka 2017.

Zipo taarifa za uhakika za kukamatwa kwa Watanzania 37 kati yao 24 walienda kufanya shughuli za uvuvi wakitokea Zanzibar na 13 kutoka Tanzania Bara ambao walienda kwa shughuli mbalimbali. Kwa upande wa Sakata la wavuvi, wavuvi hao walipatiwa vibali mapema mwezi Septemba 2017 kwa ajili ya kufanya shughuli za uvuvi kupitia Bahari ya Hindi.

Mwezi mmoja baadae, yaani Oktoba 2017 kulitokea machufuko Nchini Msumbiji, ndipo wavuvi 24 na Watanzania wengine (13) waliokuwa kwenye shughuli mbalimbali walikamatwa na kuwekwa magerezani. Hadi sasa zipo taarifa kuwa Watanzania 17 wamefariki wakiwa magerezani nchini Msumbiji na wengine kuendelea kushikiliwa bila msaada wowote.

Tulitoa tamko Machi 23, 2023 juu ya kadhia hii na kuitaka Serikali ichukue hatua za kufuatilia kwa karibu suala hili na kuhakikisha watanzania hawa wanarejeshwa nyumbani bila kuendelea kupata madhara zaidi. Majibu ya waziri mwenye dhamana alipoulizwa na vyombo vya habari alinukuliwa akisema sisi, ACT Wazalendo tumpelekee taarifa mezani kwake. Hii ni dalili ya kukwepa kuwajibika na kufanya mzaha juu ya maisha ya watu.

Pamoja na kuwepo kwa taarifa hizo kwa zaidi ya miaka kadhaa, ukimya wa Serikali unaibua simanzi, sintofamu na kushusha imani za ndugu, jamaa na marafiki juu ya hatima ya ndugu zao waliopo vizuizini.

ACT wazalendo tunaitaka Serikali kupitia wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria kufuatilia mashtaka yote yanayowakabili Watanzania waliopo nchini Msumbiji na Afrika ya Kusini na nchi nyingine kuhakikisha wanatendewa haki na wanarudishwa nyumbani.

Hitimisho
Mambo matano (5) tuliyoyabainisha kwenye uchambuzi wetu wa bajeti hii ya wizara mengine yanahitaji marekebisho ya kisera, sheria na hata katiba ya nchi. Mathalani suala la mjadala wa hadhi ya watanzania waishio nje wenye uraia wa nchi zingine.

Suala la mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili inavyotumika na Kampuni na nchi zenye nguvu kuibana Tanzania katika uvanaji na unufaikaji wa rasilimali zake, linapaswa kutazamwa kwa jicho la kizalendo zipo nchi nyingi zimefanya maamuzi magumu ya kujiondoa kwenye mikataba ya ukandamizaji kama vile Equador, Denimark, Venezuela, South Afrika, Brazil kutaja kwa uchache. Hivyo, sera ya nje inapaswa kuongozwa na kuvutia uwekezaji kwa kuimarisha ulinzi wa umma.

Imetolewa na; Imetolewa na;

Dr. Nasra Nassor Omar
Twitter: @drnasranassor
Waziri Kivuli Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Juni 9, 2023.

IMG-20230609-WA0012.jpg
 
Back
Top Bottom