Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,319
- 15,808
Akifungua Mkutano wa wadau kukusanya maoni kuhusu Rasimu ya Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Sinza jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Leonard Akwilapo amesema, mpango huo unalenga kuongeza thamani ya ardhi, kuboresha mazingira ya makazi, kuimarisha miundombinu, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuifanya Sinza kuwa eneo la kisasa lenye ushindani mkubwa wa kiuchumi.
Amesisitiza kuwa, utekelezaji wa mpango huo utaongozwa na sheria, sera na taratibu za nchi huku haki za wamiliki wa ardhi zikiheshimiwa kikamilifu.
Pia soma ~ Mazungumzo ya kuhamisha Wananchi wa Sinza yasifanyike kwa mafungu hotelini, tushirikishwe na uwazi uwepo
"Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wa Sinza wanakuwa washiriki, wabia na wanufaika wakuu wa maendeleo yatakayozalishwa na Mpango huu, badala ya kuwa watazamaji wa maendeleo hayo." amesema
Kupitia mpango huo, wamiliki wa ardhi wataendelea kuwa sehemu ya maendeleo ya maeneo yao kwa kuchangia ardhi kwa pamoja ili kuwezesha upatikanaji wa miundombinu, huduma za jamii na maeneo ya maegesho, huku wakiendelea kunufaika na ongezeko la thamani ya ardhi na mali zao baada ya utekelezaji wa mpango.
“Lengo la Serikali si kuchukua ardhi za wananchi, bali kuweka mazingira yatakayowezesha matumizi bora zaidi ya ardhi, kuongeza thamani ya mali za wananchi, kuboresha ubora wa makazi na kuimarisha fursa za kiuchumi,” amesema.
Ametoa rai kwa wananchi wote kuwa waangalifu dhidi ya watu wanaoweza kutumia taarifa za Mpango huu kwa maslahi binafsi kwa kuwashawishi muuze ardhi zenu kwa bei zisizoendana na thamani yake ya baadaye.
‘’Ni muhimu kutambua kuwa eneo la Sinza linaendelea kuwa mojawapo ya maeneo yenye mvuto mkubwa wa uwekezaji katika Jiji la Dar es Salaam. Hivyo, wananchi wanapaswa kufanya maamuzi kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia maslahi yao ya muda mrefu’’ amesema.
Kwa upande wake Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo amesema, zoezi hilo lipo kwa nia njema ya maendeleo ya wananchi wa Sinza na kusisitiza zoezi hilo kufanyika kwa haraka haraka.
‘’Serikali haiwezi kuchukua hatua zozote za kuharibu maisha ya wananchi wake lengo la serikali ni kujenga ustawi wa watu wake’’ amesema Prof. Kitila Mkumbo.
Naye Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe. Lawrence Mlaki amesema kata ya Sinza ni moja ya kata 14 zilizopo kwenye manispaa yake na hali ya eneo hilo imebadilika sana kutokana na ujenzi wa maghorofa na maduka hivyo ipo haja ya kufanyiwa mabadiliko na mpango wa kuiboresha upya Sinza umekuja wakati muafaka.