Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Dk Ayub Rioba amestaafu baada ya muda wake kwisha.
Ameandika katika ukurasa wake wa Facebook:
Tarehe 19 Machi Rais Dkt. JPM aliniteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC. Alivyofariki JPM, nilipitia vita ngumu sana ya wale walioamini nilipaswa kutumbuliwa.
Ninamshukuru sana Dkt. JPM kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mkurugezi
Mkuu wa TBC. Ninamuombea kwa Mwenyezi Mungu apumzike kwa amani!
Lakini ninamshukuru sana Rais Dkt. SSH, siyo tu kwa kuninusuru wakati napigwa sana vita, bali kwa kuniteua tena mwaka 2024 kwa kipindi cha miaka miwili ya ziada. Ninaamini wagomvi wangu walipigwa na butwaa!
Kwa rekodi hiyo nimekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo. Hili silichukulii kama jambo jepesi, hasa katika mazingira ya utumbuaji tulioushuhudia kipindi cha Dkt. JPM na Dkt. SSH.
Ninamshukuru sana Rais Dkt. SSH kwa hilo na, kusema kweli, ninamtakia kila lakheri na mafanikio ktk uongozi wake mahiri.
Nimshukuru pia, kwa namna ya pekee, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa upendo na ushirikiano mkubwa aliouonesha kwa TBC kipindi chote nikiwa Mkurugenzi Mkuu TBC. Abarikiwe sana kwa kazi iliyotukuka anayoifanya Zanzibar.
Ninatumia fursa hii pia kuushukuru uongozi wa Wizara yetu nikianzia kwa Mhe Waziri (wakati ule) Dkt. Harrison Mwakyembe, ndugu Nape Nnauye, Prof Palamagamba Kabudi na sasa Paul Makonda. Shukrani hizi zinawaendea pia Manaibu Mawaziri wangu, wakiongozwa na Rafiki yangu wa siku nyingi na mtu makini, Mwana FA.
Aidha, ninawashukuru sana Makatibu Wakuu wote niliohudumu chini yao wakiwakilishwa na mwanafunzi wangu mahiri, Gerson Msigwa. Sina cha kuwalipa ila kuwaombea kila lakheri ktk uongozi wenu.
Sitatenda haki endapo sitawashukuru watendaji wote wa Serikali wa mihimili yote, likiwemo Bunge na Mahakama kwa ushirikiano mkubwa walionipa. Ninamtaja Profesa Ole Gabriel kwa namna ya kipekee kwa uzalendo na umakini wake. Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Kusiluka na Katibu Mkuu, Utumishi, Juma Mkomi, Mwenyezi Mungu awabariki sana. Miongozo yenu na upendo wenu kwa TBC siwezi kusahau.
Nitumie pia fursa hii kuishukuru sana Menejimenti ya viwango ya TBC kwa yote tuliyoyatekeleza pamoja kwa machozi, jasho na damu - japo sifa zote nilichukua mimi! Nitawakumbuka daima! Ninawasihi mtoe ushirikiano ule ule kwa Mkurugenzi Mkuu mpya atakayekuja.
Aidha napenda pia kuwashukuru sana wafanyakazi wenzangu wote kwa ushirikiano walionipa kwa miaka hii 10. Sina cha kuwalipa bali kumuomba Mwenyezi Mungu awajaze neema yake na kuwatimizia haja za mioyo yenu, kazini na ktk maisha yenu.
Vile vile, niwashukuru Watanzania wote kwa kutuunga mkono TBC ama kwa kufuatilia maudhui yetu au kwa kufanya biashara na sisi. Uzalendo wenu nitaukumbuka daima.
Nitaendelea kuikumbuka tarehe 19 Machi ambayo Rais Dkt. JPM aliniteua mwanzo na Rais Dkt. SSH akaniteua tena mwaka 2024. Lakini ni tarehe ambayo Rais Dkt. SSH, aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwangu mimi na Rais Dkt. SSH, tarehe 19 Machi inabaki kuwa tarehe muhimu kwetu binafsi na ktk historia ya Taifa yetu.