Dk. Shein kufukuza mawaziri | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dk. Shein kufukuza mawaziri

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, May 29, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  May 29, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  [h=1][/h]

  [​IMG]
  Na Jabir Idrissa - Imechapwa 23 May 2012

  [​IMG][​IMG]
  MAWAZIRI watatu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliotuhumiwa ufisadi katika uuzaji na ukodishaji mali za serikali, huenda wakafukuzwa kazi kabla ya Oktoba mwaka huu, MwanaHALISI limeambiwa.


  Taarifa kutoka ndani ya serikali na vyama viwili vinavyounda serikali ya umoja wa kitaifa – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) – zinasema Rais Dk. Ali Mohamed Shein hana njia isipokuwa kuwafukuza mawaziri hao.

  Mawaziri waliotajwa katika vitendo vilivyotokea wakati wa uongozi wa Rais Amani Abeid Karume; na ikiwa ni siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ni Machano Othman Said, Mansour Yussuf Himid na Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini.


  Machano alikuwa akiongoza wizara ya mawasiliano na uchukuzi na Mansour wizara ya maji, ujenzi, nishati na ardhi. Dk. Mwinyihaji alikuwa waziri wa nchi ofisi ya rais, fedha na uchumi.


  Machano na Mansour wameliambia gazeti hili kuwa hawahusiki na kashfa hiyo. Dk. Mwinyihaji hakupatikana kutoa maelezo yoyote.


  Vyanzo vya taarifa vimesema rais asingependa kuvutana na Baraza la Wawakilishi, ambalo limetaka serikali iwachukulie hatua za kisheria watuhumiwa.


  Oktoba mwaka huu, serikali ya Dk. Shein inatarajiwa kulieleza baraza hatua ilizochukua dhidi ya watuhumiwa.


  Kamati teule ya baraza ilichunguza mazingira na mikataba katika ukodishaji/uuzaji jengo la kihistoria la Mambomsiige, lililopo Forodhani; kiwanja cha wizara ya miundombinu, eneo la Mtoni; na kiwanja cha Shirika la Utalii, jirani na jengo maarufu la Livingstone, mtaa wa Gulioni.


  Kulingana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongozwa na mwakilishi wa Chake Chake, Omar Ali Shehe (CUF), ikijumuisha mawaziri wawili wa zamani, utoaji wa raslimali hizo ulifanywa kwa bei ndogo kuliko thamani halisi ya mali zenyewe.


  Ripoti hiyo imesema, “Hapa inatubidi tuseme kwamba mawaziri wa wizara wamegeuka madalali… wizara haina bodi ya zabuni kwa ajili ya kuuza na kununua mali,” ripoti imesema.


  Uwanja wa wizara ya miundombinu na mawasiliano uliuzwa kwa mfanyabiashara Said Salim Bakhressa wa Coastal Ferries Ltd. Alipoulizwa alidai alipigiwa simu na Waziri Machano akimuarifu kuwepo kwa kiwanja cha serikali kinachouzwa.


  Ripoti inaonyesha kiwanja hicho kiliuzwa kwa bei ya Sh. 200 milioni bila ya kuwashirikisha viongozi wa wizara, akiwemo katibu mkuu.


  Zanzibar inatumia Sheria Na. 9 ya mwaka 2003 ya manunuzi ya serikali ambayo ilipitishwa na baraza la wawakilishi na kufanyiwa marekebisho mwaka 2005.


  Kwa upande mwingine, kamati inambana waziri Machano kwa kuvunja sheria kwa kuwa, kifungu cha 7(a) cha Sheria ya umilikiaji ardhi Na. 12 ya mwaka 1992 ya Zanzibar, kinampa mamlaka waziri anayehusika na ardhi.


  Ripoti hiyo ya zaidi ya kurasa 200 imesema uuzaji wa kiwanja umefanywa kwa kuzingatia maslahi binafsi na ni “…kinyume cha misingi ya utawala bora.”


  Waziri Machano ambaye sasa hana wizara maalum, anadai waliuza kiwanja hicho ili kupata fedha za kujenga ofisi za wizara baada ya kuidhinishwa na aliyekuwa rais wakati huo.


  Hata hivyo, kamati imesema imeshangazwa kwamba waziri ameshiriki kuuza uwanja harakaharaka, tena siku mbili tu kabla ya siku ya uchaguzi mkuu 2010.


  Ripoti pia inasema kamati ilipofuatilia mkataba wa uuzaji wa kiwanja hicho, ilipata mkataba kwenye karatasi zisizokuwa na nembo ya serikali wala muhuri wa wizara. “Utaratibu huu ni kinyume cha sheria,” imesema.


  Mwandishi wa habari hizi alimuuliza Waziri Machano iwapo anafikiria kujiuzulu kwa kutuhumiwa. Alisema hajafikiria kufanya hivyo. “Kila kitu kinajieleza. Mimi sikufanya kosa lolote. Wala sitajiuzulu,” ameeleza.


  Viongozi wa wizara hiyo walilaumiwa kwa kulidanganya baraza kwa kuomba kuidhinishiwa Sh. 100 milioni za kujenga jengo jipya la wizara ilhali wanajua kiwanja kilishauzwa katika bajeti ya 2009/10.


  Hata baada ya wizara kuidhinisha fedha hizo, ripoti imesema, ilitumia Sh. 49 milioni kubadilisha jengo la bohari ya Shirika la Meli Zanzibar kuwa ofisi za wizara.


  Kamati ilipendekeza waziri, katibu mkuu na watendaji waliohusika washitakiwe mahakamani na kiwanja kirudishwe serikalini.


  Dk. Mwinyihaji ametajwa kushiriki katika mpango wa kukodisha jengo la Mambomsiige kwa kampuni ya ASB Holdings Ltd., kwa dola 1.5 milioni kwa muda wa miaka 99 kwa ujenzi wa hoteli ya nyota tano. Ukodishaji huo umetajwa kutozingatia maslahi ya taifa.


  Kamati imesema Dk. Mwinyihaji alisema alitekeleza agizo la rais lililoandikwa kwa wino mwekundu. Hata hivyo, alikataa kuonyesha maandishi hayo akidai, “si sahihi kutoa siri ya serikali.”


  Aliieleza kamati kuwa alipokea agizo kuwa amepatikana mwekezaji wa kukodishwa jengo hilo kwa dola 1.5 milioni na malipo ya dola 10,000 kwa mwaka.


  Hata hivyo, kamati haikupata nyaraka za ukodishaji pamoja na maombi ya ukodishaji kiwanja cha Shirika la Utalii Zanzibar kwenye majalada ya ofisi ya Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati.


  Hata barua ya maombi ya mwekezaji kutaka kukodishwa jengo la Mambomsiige na lile la klabu ya Starehe, karibu nalo, havipo.


  Naibu katibu mkuu wa wizara hiyo alipohojiwa, alisema wizara haina nyaraka zozote zinazohusu maombi ya mwekezaji.


  Waziri Mansour pia aliikabidhi kamati dokezo la 11 Oktoba 2010 alilompelekea rais mstaafu (Karume) na dokezo la 13 Oktoba 2010 linalozungumzia mipango ya kukodisha majengo hayo.


  Kamati ilisema kuwa ilipata uthibitisho wa uamuzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa kupinga ukodishaji wa majengo hayo ambayo inayatambua kwa hadhi ya urithi wa kidunia yakiwa chini ya Mamlaka ya Uendelezaji wa Mji Mkongwe Zanzibar.


  Ripoti inaonyesha mamlaka ilitoa kibali Kumb. STCDA/4 VOL.III/426 cha Machi 2011 kuidhinisha kampuni ya ASB Holdings Ltd kukodishwa majengo hayo licha ya UNESCO na wananchi kupinga.


  Kamati imesema haikupata nyaraka za utoaji kiwanja cha Shirika la Utalii kilichopo pembeni mwa jengo la Livingstone, ambacho baada ya kuchunguza ilibaini alipewa mtu wa familia ya rais. Kuna taarifa kuwa aliyepewa alikiuza kwa Sh. 150 milioni muda mfupi baadaye.


  Waziri Mansour aliulizwa na kamati hiyo kama upo ushahidi wowote kuonyesha kulikuwa na maombi rasmi, lakini alikuwa na maneno tu.


  Alipoulizwa na MwanaHALISI anajisikiaje kuhusishwa na ukodishaji majengo na kutoa ardhi ya serikali, Mansour alisema hana la kusema; anasubiri serikali iseme.


  Alipoulizwa iwapo anafikiria kujiuzulu kuonyesha uwajibaki alisema, “Sina la kusema mpaka hapo serikali itakaposema.”   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  May 29, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  Kumbe hata Visiwani CCM ni Mafisadi pia
   
Loading...