Date::10/9/2008
Dk Hoseah ateuliwa kuingia katika 'Takukuru' ya kimataifa
Na Peter Edson
Mwananchi
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah ameteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Kimataifa la Mamlaka za Kupambana na Rushwa, uteuzi ulioanza rasmi mwezi huu.
Uteuzi huo ulifanywa kwenye mkutano mkuu wa tatu wa mwaka wa mamlaka hizo uliofanyika jijini Kiev, Ukraine kuanzi Oktoba 3 hadi 6 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa jana na Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani ilisema kuwa mkutano huo, ambao ulihudhuriwa na nchi 106 wanachama wa umoja huo na asasi 13 za kimataifa ulijadili na kuweka mikakati ya kuzuia na kupambana na rushwa mahali pa kazi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mbali na mikakati hiyo ya kupambana na rushwa, suala la kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka hizo ilikuwa moja ya ajenda ambayo ilijadiliwa kwenye mkutano huo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya kutathimini utendaji kazi wa Dk. Hoseah, mamlaka hizo kwa pamoja ziliridhia uteuzi wake wa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji katika shirikisho hilo.
Shirikisho hilo liliundwa mwaka 2006 kwa lengo la kuunganisha jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa kimataifa na makao makuu yake yapo katika mji wa Hongkong nchini China.
Novemba mwaka jana Dk. Hoseah alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Shirikisho la Mamlaka za Kupambana na Rushwa kwa Nchi za Mashariki mwa Afrika, ambazo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.