PROFESA KYANDO
Member
- Jul 24, 2012
- 81
- 6
WAZIRI wa Fedha, Dk. William Mgimwa, amesema deni la taifa limezidi kukua. Amesema deni hilo limeongezeka hadi Sh bilioni 20,865 Juni, mwaka huu kutoka Sh bilioni 18,617 Juni mwaka jana.
Dk. Mgimwa, alitoa taarifa hiyo bungeni jana alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.
Wizara ya Fedha imeendelea kusimamia deni la taifa kwa kuzingatia mkakati wa kusimamia deni la taifa la mwaka 2002 pamoja na sheria ya mikopo, dhamana na misaada namba 30 ya mwaka 1974 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2004.
Hadi mwishoni mwa Juni mwaka 2012, deni la taifa lilikuwa Sh bilioni 20,865 ikilinganishwa na deni la Sh bilioni 18,617 Juni, mwaka jana ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 10.7.
Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 15,927.1 ni deni la nje na Sh bilioni 4,937.9 ni deni la ndani. Kati ya kiasi hicho cha deni la nje, Sh 12,644.6 ni deni la umma na kiasi kilichobaki cha Sh 3,282.5 ni deni la sekta binafsi.
Pia hadi kufikia Juni mwaka huu, deni la ndani la Serikali lilifikia Sh bilioni 4,937.9 ikilinganishwa na Sh bilioni 4,729 Juni, mwaka jana ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 4.2.
Wakati deni la taifa likikua, Dk. Mgimwa alisema mfumko wa bei nao umezidi kupaa kutoka asilimia 13 Julai mwaka jana hadi kufikia asilimia asilimia 17.4 Juni mwaka huu.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika wizara hiyo, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alitaka ufanyike ukaguzi maalum kubaini uhalali wa deni hilo.
Kwa mujibu wa Zitto, ukaguzi ukifanyika utawezesha kujulikana kama miradi iliyotekelezwa kupitia miradi hiyo inatekelezwa kama inavyotakiwa au kuna mazingira yenye utata.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, Dunstan Kitandula (CCM), alisema kuna haja Serikali ikadhibiti deni hilo la taifa kabla halijaongezeka zaidi.
Kitandula ambaye ni Mbunge wa Mkinga, alisema kuna haja pia Serikali ikaendelea kuwa na sera nzuri za bajeti na fedha kuepukana na madeni yasiyokuwa na maana.