Mkalukungone Mwamba
JF-Expert Member
- Aug 29, 2022
- 2,926
- 6,575
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na wananchi wa Mtaa wa Tabata, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, na kutoa ufafanuzi kuhusu hatua zinazochukuliwa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya mtaa huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Tabata, Gilbert Massawe, amesema Mamlaka imepanga kuboresha miundombinu ya maji kwa kuongeza ukubwa wa bomba kutoka inchi mbili hadi inchi sita.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza msukumo na upatikanaji wa maji katika mitaa ya Bandari, Mikumi, Albasti, Ubaya Ubaya na St. Mary ambayo kwa sasa inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wakazi na kuzidiwa kwa mtandao wa zamani wa maji.
“Tunaenda kutekeleza mradi huo ambao utakuwa suluhisho la kudumu la huduma ya maji katika maeneo hayo, ambayo kwa sasa yanakabiliwa na changamoto kutokana na miundombinu ya mtandao wa awali kuzidiwa kufuatia ongezeko la idadi ya wakazi,” alisema Massawe.
Aidha, Massawe amesema DAWASA inaendelea na hatua za kufunga pampu mpya katika Mtambo wa Ruvu Juu, ambazo zitasaidia kuongeza ufanisi wa msukumo na usambazaji wa maji katika eneo la Tabata na maeneo ya jirani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Tabata, Peter Joackim, amesema viongozi wa mtaa kwa kushirikiana na DAWASA tayari wametembelea maeneo mbalimbali yenye changamoto ya maji na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ya miundombinu.
Amesema kikao hicho kililenga kuwapatia wananchi mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa pamoja na mipango ya DAWASA ya kuboresha huduma ya maji katika Mtaa wa Tabata.
“Kikao cha leo kililenga kuwapatia wananchi mrejesho kuhusu hatua zilizochukuliwa na mipango ya DAWASA katika kuboresha huduma ya maji katika mtaa wetu wa Tabata,” alisema Joackim.
DAWASA pia imeeleza kuwa kwa mujibu wa ratiba ya huduma, mgao wa maji katika eneo hilo unatarajiwa kufanyika usiku wa leo, hivyo wananchi wanatarajiwa kupata huduma ya maji.
Mamlaka imesema wataalamu wake watakuwa katika maeneo hayo kufuatilia hali ya huduma na kutoa msaada pale utakapohitajika, huku ikiendelea na hatua za kuboresha miundombinu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika na ufanisi zaidi.