MTAZAMO
JF-Expert Member
- Feb 8, 2011
- 19,643
- 33,432
DALILI ZA KANISA LA AFRIKA KUELEKEA KWENYE KUJIUA.
Pd.TITUS AMIGU
Naona namna za dalili za kujitundika na kujininginiza. Kwa nini naona hivyo? Ni kwa sababu makosa yale mawili ya mwanzo ya watu wa Ulaya na Marekani tunayafanya yote; kosa linalotindikia kidogo ni lile la tatu. Lakini pamoja na hayo, makosa tunayoyafanya Afrika ni mengi zaidi ya hayo mawili waliyofanya wenzetu Ulaya na Marekani.
Najieleza. Kosa la kwanza la watu wa Ulaya na Marekani sasa ndilo limepamba moto, tunalifanya kwa bidii , tena bidii kubwa kabisa: kujenga “makanisa majengo” badala ya “kanisa watu”. Kosa la pili ndilo hilo tena, tunahangaika mno na mali, miradi, vitegauchumi eti ili tujitegemee kiasi hata waamini wengine kuona Kanisa halina maana kwa jinsi linavyowadai michango kila mahali na kila wakati. Kwenye jumuiya ndogo ndogo, wakipiga magoti kusali, wakiinuka tu, michango na harambee. Wakiingia kanisani mahubiri na ibada fupi kama “mkia wa mbuzi”, lakini mambo ya matangazo na harambee masaa kwa masaa.
Mahali pengine na wengine wanakasirikiana na kupeana adhabu za kunyimana sakramenti kwa kosa la kutotoa michango, au zaka na sadaka.
Lakini pamoja na makosa haya ni makosa yafuatayo manne, mosi, maaskofu na mapadre kuwaachia peke yao makatekista, pengine wasioandaliwa vizuri, kazi eti ndio wajenge msingi wa imani, mintarafu mafundisho ya ubatizo, kipaimara na ndoa.
Makatekista kwa kadiri ya uwezo wao wanafanya kitu lakini kwa kuwa wanachojenga huwa hafifu, Wakristo wanatindikiwa ubora na hivyo wakija watu wa makanisa mengine wanawafagia kana kwamba walikuwa vipepeo tu. Huwezi kujenga nyumba imara juu ya msingi dhaifu! Eti hapo tunashangaa kwa nini waamini wetu wanakuwa, ashkum si matusi, “changudoa wa imani” wakihama kutoka hapa na kwenda pale na hata mwishowe kugeuka maadui wetu wakali!
Pili, ni kuachilia vyama au vikundi vinavyowatoa watu kwenye imani ya kweli na kuwarudisha watu kwenye imani za jadi au kuwahamishia watu kwenye imani za dini zingine au makanisa mengine. Tunaachilia watu watufundishie watu wetu hofu za uchawi, mizimu, mapepo, majini, kufungwa na kufunguliwa, miti ya ukoo, laana, mikosi na kadhalika. Haya hayakupaswa kuwa mada zetu. Tulipaswa kupigia tarumbeta INJILI (HABARI NJEMA YA FURAHA) na mafundisho sahihi ya Kanisa Katoliki.
Eti hatuna habari Baba Mtakatifu Benedikto XVI alivyotuonya kwenye Mausia yake baada ya Sinodi ya Pili ya Afrika, tujitoe kwenye “KUJISAJILI KUWILI”, kwenye Ukristo na kwenye dini za jadi, katika AFRICAE MUNUS 93, mwaka 2009!
Tatu, ni kukazania Kanisa lijali sana mipaka ya nchi kana kwamba si Kanisa la ulimwengu. Kwa namna hii, nchi mbalimbali zinazidi kujitenga na zingine, hata matokeo yake tunakuwa na labda Kanisa la Kenya tu, ambapo mtu wa Uganda anaitwa na kutengwa kama mgeni; Kanisa la Tanzania tu, ambapo mtu wa Malawi anaitwa na kutengwa kama mgeni; Kanisa la Afrika ya Kusini tu, ambapo mtu wa Msumbiji anaitwa na kutengwa kama mgeni; Kanisa la Kameruni tu, ambapo mtu wa Demokrasia ya Kongo anaitwa na kutengwa kama mgeni; Kanisa la Nigeria tu, ambapo mtu wa Ghana anaitwa na kutengwa kama mgeni na kadhalika.
Matokeo ya jitihada hizi hasi, mtu wa nchi moja, kwa mfano, hawezi kuwa Askofu wa Kanisa Katoliki katika nchi nyingine hapa hapa duniani au hapa hapa Afrika. Inasikitisha, Kanisa linapotea kutoka maana ya neno “katoliki”, yaani “ya ulimwengu wote”.
Lakini vibaya zaidi ni kwamba baada ya ugonjwa huo kuanza, ubaguzi umeshaanza kuchanulia pahala pengine pia, sasa unaikamata mipaka ya makabila kiasi kwamba Mnubi hawezi kuwa Askofu kwa Wadinka; Muigbo hawezi kuwa Askofu kwa Wayoruba; Mshona hawezi kuwa Askofu kwa Wandebele; Mjaluo hawezi kuwa Askofu kwa Wakamba, labda Mmakua hawezi kuwa Askofu kwa Wasukuma na Mmakonde hawezi kuwa Askofu kwa Wanyakyusa.
Lakini maana yake nini mambo haya yote? Maana yake ni moja tu: ule mwendo wa kuwa na Kanisa moja, takatifu, Katoliki na la mitume, unavunjika na ule mwendo wa Kanisa kuwa juu ya mipaka ya nchi na makabila (Efe 2:14-18) unamong’onyoka. Mimi nasema hiyo ni dalili mojawapo ya kujimaliza kwetu, kwani “Bandubandu humaliza gogo.” Si hivyo tu, Seminari nyingi, ndogo kwa kubwa, zinaanza kuwa za majimbo au za maeneo maalumu tu.
Katika mstari huu wa kuharibika mambo, wala haitakuwa ajabu konventi na monasteri nazo zikishambuliwa na virusi sawia. Kifupi, tunanyemelewa na hatari ya kuirefusha mizizi ya ubaguzi kikanda, kikabila, kijimbo, kiparokia na kadhalika. Hivi Kanisa la ulimwengu litakuwa linaimba wimbo wa kuwa Kanisa moja, takatifu, Katoliki na la mitume, wakati ukweli wake ni kinyume chake Kanisa linageuka kuwa la kitaifa, kikabila au kiparokia na kadhalika.
Zaidi ya hayo, Kanisa la ulimwengu litakuwa linajitangaza kusimamia kanuni moja ya imani, sakramenti sawa saba na teolojia iliyo juu ya mipaka yote, wakati wale wanaotakiwa washike vitu hivyo wameshajikatakata vifungu kama dagaa waliofiwa na mama zao. Lakini ukweli ni kwamba makanisa yakiwa makanisa ya nchi au ya makabila yatakwisha nguvu kama yanavyoendelea kiudhaifu makanisa ya Armenia, makanisa ya Urusi na kadhalika. Kwa nini basi hatusomi historia? Lakini, ndugu zanguni, historia ni mwalimu mkuu na ishara za nyakati si mapambo ya kwenye khanga!
Hivi hapa hata jirani zetu Waislamu hawezi kutufundisha kitu? Hatuwezi kuwasoma? Wenzetu, kutokana na dhana yao ya kuwa na UMMA MKUBWA, siku ya kiyama, hawathubutu kujigawagawa na kuchoreana mipaka ya kiimani kwa vigezo vya utaifa, rangi wala makabila. Hija ya Makka na Madina na uvaaji wa shuka zao mbili (ihram) wakati wa hija huwafanya wajisikie daima kuwa na Uislamu mmoja na wote kuwa ndugu. Ndiyo kisa ukikosana na Waislamu mahali fulani wote hujisikia umewakosea. Lakini kwetu kila mtu “kalumanyile”.
Kosa la nne na la mwisho katika mada hii ni waamini kujiweka nyuma katika kujifunza na kujua mafundisho ya Kanisa. Si waamini haba wasiofanya juhudi za kujisomea Biblia na mafundisho msingi ya Kanisa wakijiliwaza tu kwamba siyo wajibu wao namba moja isipokuwa kazi hiyo wenyewe ni makleri (maaskofu, mapadre na mashemasi) na watawa. Hii ni hatari nyororo itakayoliangamiza Kanisa na mwisho kuungamiza pakubwa Ukristo.
Hata wazazi huweza wasifanye lolote mintarafu kuwafundisha watoto wao imani nyumbani mwao, wakilalia mlango wazi kwamba watafundishwa wenyewe wakati wa mafundisho ya komunio ya kwanza au kipaimara. Wanasahau kuwakunja samaki wangali wabichi. Tuseme wengine hufurahia tu jina la kwamba familia ni kanisa la awali, wakati wanazembea kabisa wajibu unaoendana na jina hilo. Kujifunza na kujua mambo ya imani yetu si kazi ya makleri na watawa peke yao.
Kila mtu lazima ajifunze na aijue imani ya Kanisa Katoliki ili naye afanye mahali pake na wajibu wake wa kuikiri, kuiungama, kuipenda, kuitetea, kuilinda, kujivunia, kuistawisha na kuieneza.
Ili yasitupate yanayolipata Kanisa la Ulaya na Marekani, ilitupasa kupigiana sana kelele siku hizi kusudi tudumu kama Wakristo hai (2Tim 4:1-5). Kila Mkristo hai huonesha alama nne. Mosi, husali sala za jumuiya na binafsi. Pili, hupokea masakramenti ya Kanisa.
Tatu, hutimiza wajibu wake kwa Kanisa, kwa mfano, kulipa zaka na michango mingine. Na nne huwa na upendo kwa Mungu na jirani kwa maneno, kwa mawazo, kwa matendo na kwa kutimiza wajibu. Lakini ukweli wa kuuma ni kwamba mahali pengi waamini wanaogelea kwenye matatizo manne: mosi, kuishi katika uchumba sugu; pili, kubatizwa lakini kutokusali (wala kupokea masakramenti); tatu, kusali lakini kutotoa michango na nne, kutoa michango lakini kutokusali.
Kama makosa niliyoeleza katika makala haya hayatathibitiwi, sasa ndiyo tuna mifumo hasi inayotuelekeza kwenye kujiua. Dalili hizo si njema asilani. Ole wetu Kanisa tukijifikisha hapo! Labda hayo tunayafanya kwa sababu “tumelala nusu”.
Lakini kama hayo tunayafanya kwa akili na utashi wetu timamu basi, “MWANA KULITAFUTA, MWANA KULIPATA”.
Mzee wenu Pd. Titus Amigu.