Dalili za chama chenye hatari ya kusambaratika | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dalili za chama chenye hatari ya kusambaratika

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by kilimasera, Mar 21, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Mar 21, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  CHAMA chochote cha kisiasa, au shughuli nyingine kama ilivyo kwa kundi lolote la binadamu, liwe kubwa au dogo likishakaa pamoja kwa muda mrefu na kuzoeana kupita kiasi hujisahau na kujikuta linapoteza dira na mwelekeo katika kuwaongoza wanachama, au wananchi.

  Aghalabu hujikuta likishughulika zaidi na magomvi na masuala madogo yasiyo na maana katika maisha ya wananchi. Na wakati mwingine huishia hata kuanza kutunga kuwepo kwa maadui wa urongo.

  Viongozi wa zamani wanapoondoka wale wanaoshika nyadhifa hizo ghafla huonekana ni pungufu na dhaifu kimaadili, au kiitikeli bali pia hata katika uwezo, ari na kasi yao ya kufanya maamuzi mbalimbali na yenye uzito mkubwa katika maisha ya kila siku ya wananchi kwa wakati unaotakikana na pale yanapofanyika haraka haraka, maamuzi hayo yanakuwa hayana ubora unaokubalika na wala hayafikii malengo yaliyowekwa kwa sababu huorojeshwa na kuchakachuliwa kiasi cha kukosa sura na picha ya awali iliyokuwepo..

  Chama au kundi kama hilo huathirika na gonjwa linaloitwa: 'ndivyotunavyofikiri' (groupthink) kama ulivyogunduliwa na guru wa menejimenti ya makundi ya watu, Prof. Irving Janis, sikuzote hudharau njia na fursa mbadala na hujikuta kikifanya maamuzi bomu na yaliyo na sura ya kufanya vyama na makundi mengine kuonekana si lolote si chochote.

  Ghafla chama huwa na viongozi ambao hata kama hawakusoma wanaojiona kuwa wana akili na wajanja kuliko mtu mwingine katika jamii husika. Na hawana sababu ya kumsikiliza yeyote yule. Huthubutu kutumia mifumo ya mawasiliano iliyopo, ikiwemo vyombo vya habari vya kitaifa na vile vya kichama kuugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo.

  Chama au kundi lolote linaweza kuugua ugonjwa wa 'ndivyotunavyofikiri' hasa pale wanaounda chama hicho au kundi hilo wnapokuwa wametoka kwenye mazingira yanayofanana na wamefinyangwafinyangwa au wote kulazimishwa kufikiri kwa namna moja na sawasawa kama sarufu ya shilingi mia toka nchi moja. Katika vikao mbalimbali 'wapenda chama' huwa kama vile wale kondoo kwenye kitabu cha Shamba la Wanyama. Nao hujenga tabia ya kuanza kulia 'bah-bah-bah' kila hoja inayokosoa chama au kundi husika, au kiongozi wake inapotolewa!

  Ugonjwa huu pia huwaathiri kwa kiasi kikubwa wale wanaoziba masikio ili wasisikie ukweli usiomezeka na kufumba macho wasione ukweli usiopendeza kwao. Hawajui na hawafatilii kwa makini yanayotokea nje ya chama na kwingine duniani. Huwa hawataki kabisa kusikiliza na kuelewa mawazo au fikra mpya au tofauti toka nje ya chama au kundi husika.

  Ni rahisi kujua kama chama au kundi linaugua ugonjwa wa 'ndivyotunavyofikiri' kwa sababu Prof. Javis ameelezea kuwepo kwa dalili kubwa kama nane hivi. Dalili hizo ni hizi zifuatazo:

  • Kujidanganya kuwa hakuna chama hicho kisichoweza kufanya na sio rahisi kushindwa na chama au kundi lingine la watu. Hili hujenga kujiamini, kiburi, jeuri na dharau kupita kiasi miongoni nwa viongozi na wafuasi wa chama, jambo ambalo husababisha viongozi na wafuasi hao kufanya utani,majaribio na mambo ya hatari yanayoweza kukigharimu chama na wanachama wake na wakati mwingine hata taifa zima. Na kinapoona kinashindwa huanza kujenga chuki na uadui dhidi ya kundi, au chama kingine kwa kuzusha kila aina ya uongo dhidi ya wapinzani wao;
  • Kuhalalisha kwa pamoja kiurahisi uamuzi wowote unaofanywa na chama au kundi husika bila kufanya tafakuti na tathmini ya kina juu ya uamuzi unaofanywa.

  • Kudhani wao ni 'walokole' wacha-Mungu, 'wachache walioteuliwa', watakatifu na wenye haki zaidi kuliko raia wengine. Wanachama huamini katika uhalali wa imani au msimamo wao na hivyo hudharau haki na itikeli za mtazamo na msimamo wa wengine wakati wa kufanya maamuzi au jambo lolote linalohusu jamii au jumuiya nzima;
  • Hudhihaki vyama au makundi mengine katika jamii. Hisia za sisi ni kitu kimoja au huyu ni mwenzetu na wale ni maadui zetu hutawala na hivyo kusababisha kukosekana kwa matumizi yoyote ya akili, busara na hekima katika kushughulikia migogoro kwa njia sahihi na mujarabu.

  • Shinikizo kwa wanachama wanaohitilafiana na msimamo wa chama au kundi. Wanachama wote, wakiri au wasikiri hivyo, huwa wanapata shinikizo kubwa toka kwa wenzao kutotofautiana kabisa na misimamo na mitazamo ya chama au kundi husika. Hili hufanyika kwa sababu kila mtu wakati huo hujali nafsi, maslahi na nafasi yake na sio maslahi ya jamii husika au yale ya nchi na watu wake ;

  • Kujichuja katika hotuba, kauli na taarifa mbalimbali wao kwa wao wenyewe. Mashaka ambayo baadhi ya wanachama wanayo juu ya uamuzi au jambo lolote juu ya msimamo wa pamoja uliofikiwa (mathalani, kuilipa Dowans) huwa havipewi fursa na ni adimu kutokeza hadharani kwa namna ambayo itaonesha upinzani ndani ya kundi au chama husika;

  • Kujidanganya kuhusu juu ya wote kukubaliana jambo kwa pamoja. Fikra, misimamo, mitazamo na uamuzi wa wengi huchukuliwa kwamba ni watu wote kwa pamoja wamekubaliana. Aghalabu hili huwa si kweli. Kunakuwa na idadi kubwa ya wanachama wanaopinga lakini hunyamazishwa kwa njia moja au nyingine;

  • Walinzi wa mawazo na fikra wanaojichagua na kujipandikiza wenyewe ili viongozi wasipate habari mbaya. Watu wachache hujichukulia jukumu la kumlinda kiongozi na wafuasi wake wa karibu dhidi ya habari zozote mbaya au zinazotoa picha tofauti kabisa na ukweli ulivyo kama unavyoelezwa na habari za kupikwa, kupakuliwa na kuletwa mezani makusudi kutoa picha ya uongo na kweli kuhusu uamuzi au hali halisi ilivyo. Habari zozote zenye harufu mbaya au picha chafu huchujwa na hazifiki mbali. Hili hufanywa pia kwa kutumia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na chama na Serikali husika.

  • 'Ndivyotunavyofikiri' hutokea pale chama au kundi linapokuwa na umoja unaolazimishwa na pale panapohitajika pafanyike maamuzi makubwa ya kikundi au kichama au kiserikali au kitaifa.

  Shinikizo hili husababisha suala la ubora wa maamuzi kutozingatiwa kabisa na umoja wa chama na viongozi wake kupewa kipaumbele zaidi kuliko kitu kingine hata kama kwa kufanya hivyo ni wananchi wanaoumia .
  Maamuzi yanayofanywa wakati chama au kundi linaugua 'ndivyotunavyofikiri' huwa hayana uwezekano wa kufanikisha jambo lililokusudiwa hata kidogo. Huwa ni sawa na kazi ya zimamoto ambapo dereva hugonga magari mengine njiani; hufika kwenye moto bila maji na timu yote huwa ina usingizi au imelewa!

  Iko mifano mingi ya 'ndivyotunavyofikiri' toka sehemu mbalimbali duniani. Mathalani, mojawapo ni lile la serikali ya Marekani kushindwa kutabiri kushambuliwa kwa nchi hiyo na Japani zaidi ya mika 60 iliyopita; Uvamizi wa Marekani huko Cuba ulioshindwa vibaya; na vita vya Marekani dhidi ya Vietnam kaskazini isiikomboe Vietnam Kusini. Maamuzi yote yaliyofanywa katika mazingira hayo yalisababisha nchi hiyo kushindwa na kujitia aibu kubwa duniani.

  Hivi karibuni, tumeona matukio ya Blair na Bush, kuziingiza Uingereza na Marekani katika vita dhidi ya Iraq kwa sababu ambazo hazikuwa za kweli na matokeo ya maamuzi hayo kwa nchi hizo na dunia kwa ujumla.

  Aidha, jinsi Waafrika walivyolazimishwa na nchi hizo za Uingereza na Marekani kukubali kujiunga na vita dhidi ya ugaidi na fedha chafu bila ya watu wa nchi husika kuachiwa kutoa maoni na misimamo yao juu ya jambo hilo. Matokeo yake yakiwa kupandwa mbegu za chuki dhidi ya Uislamu na Ukiristo Afrika na kwingineko. Si kwa kiasi kidogo kuwa haya yamechangia mapinduzi yanayoendelea leo katika nchi mbalimbali za Kiarabu duniani.

  Tumeona na bado tutaona zaidi 'ndivyotunavyofikiri' pia ikiathiri Umoja wa Afrika (AU) kuhusiana na Al Bashir wa Sudan; Mugabe wa Zimbabwe; wachocheaji mauaji ya Rwanda na Kenya na sasa Cote d'Ivoire. Kote huku kwa kiasi kikubwa maslahi ya wasionacho hayakuzingatiwa ila yale ya wale walioko madarakani na walichonacho tu.

  Huko nyuma wakati Watanzania wakidanganywa na kudhulumiwa na siasa za chama kimoja katika enzi za muasisi wa taifa hili, maamuzi kadhaa yaliyofanyika huko wahusika wakiugua 'ndivyotunavyofikiri' ni pamoja na Azimio la Arusha, Ujamaa na Kujitegemea, kuua serikali za mitaa, uanzishaji wa vijiji vya ujamaa, kuua matumizi ya lugha ya Kiswahili kama njia ya kufundishia, kuua vyama vya ushirika, kuua michezo shuleni, kuua matumizi ya lugha za kikabila katika magazeti na redio, uamuzi wa kuhamia Dodoma na maamuzi mengine mengi kama hayo.

  Kosa kubwa ambalo wanaharakati wa demokrasia ikwemo wanahabari wanalolifanya ni kukubali kulea Serikali zinazoendeleza tawala za usiri na uchinichini kama alivyosema tajiri maarufu na mchambuzi wa uchumi wa dunia, George Soros.

  Kiujumla kutokana na uoga na kutokujua nafasi yao kama mhimili pekee katika mihimili iliyopo unaoweza kupiga vita rushwa, wizi wa kura, ufisadi na kuwa na watu waovu kama viongozi vyombo vyetu vya habari na hususan televisheni na redio vimewaangusha Watanzania, na kwa bahati mbaya ni Watanzania wenyewe walioliruhusu hili kutokea.

  Aidha, kuruhusu mangimeza kama vile makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya na wakuu wa mashirika mbalimbali nchini kukokotwa na wanasiasa na vyama vya siasa kwa kiasi fulani kunatoa mwanya kuwa 'ndivyo tunavyofikiri' kushambulia taifa na kuua fursa yoyote ya nchi kuondokana na umaskini, maradhi na matatizo yake mengine.
   
 2. TUNTEMEKE

  TUNTEMEKE JF-Expert Member

  #2
  Mar 22, 2011
  Joined: Jun 15, 2009
  Messages: 4,582
  Likes Received: 55
  Trophy Points: 145
  Mkala yako haiana mvuto, too much polititics , hit to the point
   
Loading...